Andiko La Ishirini Na Mbili Risala Ya Undugu

بِاسْمِهِ سُبْحَانَهُ

وَإنْ مِنْ شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ

Andiko hili limekusanya mada mbili: Mada ya kwanza inawalingania watu wa imani kuhusu undugu na mapenzi

Mada ya kwanza

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيْمِ

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِـحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُـمْ Qur’an, 49: 10

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيْمٌ Qur’an, 41: 34

وَالْكَاظِمِيْنَ الْغَيْظِ وَالْعَافِيْنَ عَنِ النَّاسِ وَاللهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِيْنَ Qur’an, 3: 134

Hakika kila lenye kupelekea kujipendelea na inda na inadi, na uhasidi, kwenye unafiki na mifarakano baina ya waislamu, na yanayoingiza ndani ya nafsi zao katika chuki na uhasidi na uadui, ni vitu vinavyokataliwa kabisa, pia vinakataliwa kwa uhalisia na kwa elimu, na kama hivyo ndivyo vinavyokataliwa na Uislamu, ambao ni wenye kubeba roho ya ubinadamu ulio mkubwa; ukiachilia kwamba uadui ni dhulma kubwa yenye kufisidi maisha ya mwanaadamu, kuanzia shakhsiya yake na maisha yake ya kijamii na kiroho, bali ni sumu kali inayofisidi maisha ya mwanaadamu kwa ujumla.

Hapa tutabainisha sura sita kuhusiana na ukweli huu:

Sura ya kwanza

Hakika uadui wa mwanaadamu kwa ndugu yake mwanaadamu ni dhulma katika uhalisia wake. Ewe ambaye moyo wako umejawa na chuki na uadui kwa ndugu yako muumini, ewe ambaye huna muruwa! Hebu fikiria laiti kwamba umo ndani ya jahazi au ndani ya nyumba na humo umo na watu wasiopungua tisa, walio safi dhidi ya makosa na baina yao mhalifu mmoja, na ukamuona mwenye kujaribu kulizamisha jahazi au kuivunja nyumba juu yenu, katika mazingira kama haya bila shaka utapiga mayowe kwa sauti yako yote kupinga tukio hilo la dhulma, kwani hakuna kanuni inayojuzisha kuzamisha jahazi hata kama ndani yake wamo maharamia madamu tu kati yao kuna mtu mwema.

Na kama ilivyo dhulma kuwa ni mbaya na fedheha, hivyo hivyo kujikusanyia uadui na chuki kwa muumini ambaye ni kiumbe wa Allah (s.w) na jahazi la kiungu, kwa kuwa tu anasifa ya kufanya kosa, wewe unapata shida na kudhurika dhidi yake, licha ya kwamba anasifa tisa nyingine nzima, bali ishirini nyingine, mfano Imani, Uislamu na ujirani mwema, hakika uadui na chuki ni vyenye kukupelekea kwenye raghba ya kutaka kulizamisha jahazi la uwepo wake, au kutia moto jengo la utambulisho wake, hii sio chochote ila ni chuki na uhasidi na dhulma na fedheha.

Sura ya pili

Uadui ni dhulma katika mtazamo wa kielimu, kwani uadui na mapenzi ni sifa mbili zenye kugongana, ni mfano wa mwangaza na kiza havikutani pamoja kwa uhakika wake kwa vyovyote ilivyo. Hivyo pale panapo kusanyika sifa za mapenzi na sababu zake zikawa ni zenye nguvu, hapo bila shaka mapenzi yataugeuza uadui katika sura isiyo ya uhakika, bali utageuka kuwa mapenzi na huruma, kwani muumini ni mwenye kumpenda na kumpendelea ndugu yake, na tendo lolote baya litakalotokea kwa ndugu yake litampelekea kuwa na huruma nae, na atakuwa anajaribu kumrekebisha kwa njia ya ulaini na upole, pasina ubabe wala matumizi ya nguvu. Imesimuliwa kutoka katika hadithi sahihi, “Sio halali kwa muislam kumhama ndugu yake muislamu zaidi ya siku tatu, wakikutana huyu anamkimbia huyu na huyu anamkimbia huyu, na mbora wao ni yule mwenye kuanza kusalimia”

Sahih Bukhari, Al-adab 57,62, Istidhaan 9, Muslim, mlango wa wema 23,25,26.

Ama sababu za uadui na bughudha zinaposhinda na kuchukua nafasi moyoni, katika hali kama hii mapenzi yanageuka na kuwa ya uongo na kuvaa guo la kujidai na kusingizia. Tambua ewe dhalimu! Ni dhulma ilioje muumini kubeba uadui na chuki dhidi ya ndugu yake. Ikiwa mfano wewe utazipa ukubwa au kuzitukuza changarawe ndogo na kuziona ni bora kuliko Alkaaba tukufu, au ni bora kuliko Jabal Al-uhud, bila shaka utakuwa unafanya ujinga mkubwa, ni kama hivyo ikiwa utakuza makosa madogo yanayofanywa na ndugu yako muumini, ukayapa uzito mkubwa kuliko hata imani yake, ambayo ni mfano wa Al-kaaba kwa ubora, na makosa yale ukayafanya ni makubwa kuliko Uislamu wake, ambao ni kama Mlima wa Uhud kwa utukufu. Kupendelea kwako makosa madogo madogo yanayotendwa na ndugu yako muumini, juu ya sifa yake ya Uislamu na matendo mazuri hiyo ni dhulma kwa kila mwenye akili bora.

Hakika imani juu ya itikadi moja, ni yenye kuita bila ya shaka kwenye kuunganisha nyoyo za waumini na kuwa sawa na moyo mmoja tu. Na umoja wa kiakida ni wenye kupeleka umoja wa kijamii. Hakika unahisi kuwepo mahusiano pamoja na yule unayeishi pamoja nae mahala pamoja, na kuwepo mahusiano ya kiurafiki, ukiwa unafanya kazi nae chini ya uongozi mmoja, au unahisi mahusiano ya kiudugu kwa kuwepo pamoja katika mji mmoja, vipi ikiwa ni kwa sababu ya kiimani, ambayo inakupulizia nuru na hisia bora zenye kukuonyesha mahusiano ya umoja kwenye maeneo mengi, na makubaliano na kukamatana na kamba za udugu zilizo nyingi zenye kufikia majina ya Allah matukufu, ni kamba zinazokupelekea kujua kuwa Mola wenu ni mmoja, mfalme wenu ni mmoja, muabudiwa wenu ni mmoja, na mfano wa haya mengi hadi kufikia elfu, na baadae mkatambua kuwa Mtume wenu ni mmoja, dini yenu ni moja, kibla chenu ni kimoja, hadi kufikia mia, baadae mkajikuta ni wenye kuishi mji mmoja, nchi moja na mfano wa haya moja moja hadi kufikia kumi.

Ikiwa kuna kiwango kama hichi cha mahusiano yenye kupelekea umoja na  mapenzi  na udugu, na ni yenye nguvu za kiroho ya kuunganisha sehemu zote za ulimwengu zilizo nyingi, je, atakuwaje yule mwenye kwenda kinyume navyo akakamatana na vijisababu dhaifu mfano wa nyumba ya buibui, sababu ambazo ni zenye kujenga unafiki, chuki na uadui? Na kuujaza moyo wake uadui, na chuki za kweli dhidi ya ndugu yake muumini! Je, hii sio khiyana dhidi ya sifa bora za kuunganisha? Na kudogosha sababu za mapenzi? Je, sio dhulma dhidi ya sifa zenye kujenga udugu? Ama ukiwa moyo wako haujafa wala haujazimika nuru yake hebu zingatia haya vizuri.

Sura ya tatu

Hakika aya tukufu:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى Qur’an, 6:164

ni yenye kutufunza uadilifu, kwa maana mtu haijuzu kumtia adabu mwenzake kwa kosa la mwingine, na utaiona Qur’an na rejea nyingine za sheria, pamoja na adabu za watu wa ukweli na hekima wenye kukutanabahisha kwamba; kuficha uadui dhidi ya muumini na kuwa na chuki nae ni dhulma kubwa mno, kwani ni sawa na kuzikataa sifa zote nzuri ambazo anasifikana nazo muumini kwa kosa moja alilolitenda, pamoja na kueneza uadui kwa jamaa zake kwa sababu ya sifa moja inayokuchukiza, hii ni dhulma kubwa, kama ilivyosifiwa na Qur’an kwa undani kabisa:

إِنَّ الْإِنْسَانَ لَظَلُومٌ Qur’an, 14:34

baada ya haya kuna nafasi ndani ya nafsi ya kujidai kuwa umo katika haki?

Tambua hakika ufisadi ambao chanzo chake kikuu, ni uadui na bughudha,  ni kitu kikubwa katika macho ya wengi mfano wa mchanga, na hivyo hivyo ndivyo ilivyo shari, ni kubwa lakini haina uzito na wala haisambai kwa mwingine, isipokuwa ile anayojifunza mtu toka kwa watu wa shari. Lakini kwenye kheri (Al-bir) na ihsani ambavyo ni sababu kuu za mapenzi na upole, ni mfano wa nuru (mwangaza), ambao daima kazi yake kung’arisha kilicho karibu na kwengine (mbali), na ndiyo tunajikuta katika mifano mizuri “Rafiki wa rafiki yako ni rafiki yako”, pia utakuta watu wanasema “Kwa sababu ya uliyemzoea unamkirimu mwingine”.

Ewe ulie katika dhulma! ikiwa unataka haki, basi hii hapa, hivyo kubeba kwako uadui kwa jamaa wa mtu unaechukia sifa yake moja, ni kinyume na uhakika wa mambo.

Sura ya nne

Hakika uadui wako dhidi ya ndugu yako muumini ni dhulma ya wazi, kwa maisha yake binafsi, ukitaka kutambua haya hebu soma misingi ifuatayo:

Msingi wa mwanzo: Unapotambua kwamba uko katika haki, kwenye mwenendo wako au fikra zako, hapo utaweza kusema ya kuwa “Hakika mwenendo wangu ni wa haki au ni bora”. Lakini haijuzu kusema “Hakika haki ni mwenendo wangu mie peke yangu”, kwani haiwezekani kabisa fikra zako pungufu kuwa ni kipimo na hukumu juu ya njia nyingine, zamani amesema mshairi: 

“Jicho la kuridhia jambo halioni kosa na jicho la kuchukia jambo linaibua makosa”.

Ni ubeti wa Abdillah ibn Mua’wiyat bin Abdillah ibn Ja’far ibn abi twalib (adabu Dunya wa Diyn, uk

Msingi wa pili: “Ni juu yako kusema ukweli kwa kila unachokizungumza, lakini sio juu yako kueneza kila la kweli, ni juu yako vile vile kusadikisha kila unalolizungumza, lakini sio sahihi kusema kila ukweli”.

Kwani anayekuwa kwenye nia isiyo ya kweli mfano wako wewe anaweza kusababisha kuinua hisia za mpinzani kwa nasaha zake akapata kinyume cha makusudio.

Msingi wa tatu: Ukitaka kumfanyia mtu uadui, kwanza fanyia uadui uadui uliomo ndani ya moyo wako, na jitahidi kuzima moto, na ng’oa kabisa mizizi yake, jaribu kupambana na adui yako mkubwa na mwenye madhara makubwa kwako, hiyo ni nafsi yako baina ya kifua chako, pigana na matamanio yake, fanya vyema katika kuitengeneza, wala usimfanyie uadui ndugu yako kwa ajili yake. Ama ikiwa unataka uadui hivyo fanyia uadui makafiri na wazandiki, hao ni wengi sana, tambua hakika sifa ya mapenzi yenyewe inapendwa na yenye kustahiki hivyo, kama ilivyo sifa ya uadui inastahiki uadui kabla ya kitu chengine.

Ama ukitaka kumshinda adui yako, ondosha baya lake kwa zuri, kwa kufanya hivyo utazima moto wa uhasama, ama ukiondoa ubaya kwa ubaya, uhasama utaongezeka, hata kama ataonekana ameshindwa kinje nje, lakini moyo wake utajawa na chuki na hasira juu yako na utaendelea, lakini kukabili baya kwa zuri kutampelekea kujuta na anaweza kugeuka na kuwa rafiki yako kipenzi. Hakika muumini anatakiwa daima kuwa mkarimu, na unaemkirimu daima unammiliki na unamfanya kuwa ni ndugu yako, hata kama atakuwa muovu, bali atakuwa karimu kwa imani, amesema mshairi:

“Unapomkirimu karimu utammiliki na ukimkirimu muovu atatovuka’’

Beti ya Al-Mutanabbi. Angalia (Al u’rfu twayyib fii sharhi diwani Abi twayyib 387 Dar-ul-Qalam, Beirut).

Uhalisia ni shahidi wa kwamba:“Unapomwita mtu fisadi kwa kauli yako: “Hakika wewe ni mwema na mtu bora” pengine kwa kauli hii atengenee, na kinyume chake unapomwita mtu mwema  “Wewe ni muovu na mbaya”, pengine aharibike na kupotea, hebu soma kauli yake Allah (s.w):

وَإِذَا مَرُّوا بَاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا Qur’an, 25: 72

وَإِنْ تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللهَ غَفُورٌ رَحِيْمٌ Qur’an, 64: 14

Na mfano wa aya kama hizi tukufu, hakika ndani yake yamo mafanikio, taufiki, furaha na utulivu. Msingi wa nne: Hakika mwenye kujaza moyo wake chuki na uadui, dhidi ya ndugu yake muumini huyo ni mwenye kuidhulumu nafsi yake kwanza, kabla ya kuwa ni mwenye kumdhulumu ndugu yake, na kuchupa mipaka ya rehema za Allah (s.w), kwani anakuwa ameitumbukiza nafsi yake kwa dhiki na uadui kwenye adhabu kali, na anaipa adhabu kila aonapo neema imemteremkia hasimu yake na anaungulika kwa machungu kwa khofu dhidi yake. Uadui unapochipuka kwa sababu ya uhasidi unafuatiliwa na adhabu kali, kwani uhasidi ni wenye mateso makubwa kwa hasidi, kuliko kwa mwenye kuhusudiwa, ama hasidi anachomwa sana na moto wa uhasidi wake. Ama anayehusudiwa hakimsibu kitu au pengine madhara hafifu tu.

Ama tiba ya husuda ni kama hivi: Hasidi atambue maafa mwishoni wa uhasidi wake, azingatie hayo, atambue kwamba yale aliyonayo yule anayemfanyia husuda katika vitu vya kidunia kama vile mali, nguvu au cheo, hivi ni vitu vya kupita tu, na faida zake ni ndogo, na mashaka yake ni makubwa, ama ikiwa husuda ni kwa ajili ya mambo ya kiakhera, asili ni kwamba hakuna husuda, hata kama mshipa wa husuda utasimama katika vitu hivi. Hasidi atakuwa ima ni mwenye kujionesha, hivyo amali zake zitaanguka, au atabaki na dhana mbaya kwa anayemhusudu hivyo atamdhulumu.

Hakika hasidi katika uhasidi wake anakasirikia qudura ya Allah (s.w), kwani anakuwa ni mwenye kuhuzunika kwa kuja fadhila na rehema za Allah (s.w) kwa anayehusudiwa, na anafurahishwa pindipo misiba itamshukia, ni kana kwamba anakosoa qudura za Allah (s.w) au kupinga rehema zake zilizo pana, na inaeleweka kuwa kukosoa qudura za Allah (s.w) ni sawa mwenye kujipiga (kichwa chake) na jabali, na mwenye kupinga rehema za Allah (s.w) anaharamishiwa nazo.

Je, ni katika insafu moyo wa muumini kujaa husuda na chuki kwa mwaka mzima dhidi ya ndugu yake, kwa vitu vidogo vidogo visivyo na uzito, visivyostahiki uadui hata wa siku moja?! Wala hapaswi mtu kunasibisha uovu unaotoka kwa ndugu yake kwake peke yake kwani:

Kwanza:

Qudura ya Allah (s.w) ina nafasi kwenye kila kitu, hivyo pokea nafasi ya qudura hii kwa kuridhia na kuikubali.

 Pili:

Hakika shetani na nafsi yenye kuamrisha maovu, ni vyenye nafasi, na ukiondosha vitu hivi viwili haitabakia mbele yako isipokuwa  huruma kwa ndugu yako muumini badala ya uadui, na utamuona kama ameghilibiwa na nafsi yake na shetani, na utatarajia kwake majuto na kumuona anarudi katika njia sahihi. 

Tatu:

Juu yako kuzingatia kwamba katika jambo hili kuna mapungufu ya nafsi yako, ima utakuwa huyaoni au hupendelei kuyaona.

Ondosha sifa hii pamoja na sifa mbili zilizotangulia, utaona zimebakia sifa nyingine chache, na ukikabiliana nazo  kwa hima na bidii na kwa msamaha, utaepukana  na kufanya dhulma na utaacha kumuudhi mtu, ama ukiyakabili makosa yake kwa ukali kwa mambo madogo ya kidunia kana kwamba unabaki humo milele na kwa uadui wa kudumu, bila shaka utaingia kwenye wasifu huu

ظَلُومًا جَهُولًا

utakuwa ni sawa na yule myahudi aliyetumia mali nyingi kwa ajili ya kukata kipande kidogo cha kigae kisichokuwa na faida bali ni jiwe la barafu lilioyayuka akidhania kuwa ni kipande cha almasi.

Kama hivi tumejaribu kukubainishia kwa ufupi mbele yako mambo yenye kusababisha madhara kutokana na uadui kwa mtu binafsi. Na ukiwa ni mwenye kuipenda nafsi yako kikweli kweli, usiache fursa ya kukiingiza kitendo kibaya ndani ya moyo, mpaka kikakita humo, msikilize Hafidh Al-shirazi anavyosema maneno yenye hekima:

دُنْيَانَه مَتَاعِيسْتِي كِه اَرْزَدْ بَنِـزَاعِي

“Hakika dunia yote haistahiki kuwa kitu cha kugombania”

Ikiwa dunia kubwa na vilivyomo ndani yake ni upuuzi kiasi hiki, vipi kuhusu sehemu ndogo ndani yake. Msikilize tena anavyosema:

أسَايِشِ دُوكَيْتِي تَفْسِيرِ اِين دُو حَرْفَسْت

بَا دُوسِـتَانْ مُـرُوَّتْ شمَنَـانْ مُـدَارَا

“Kupata furaha na salama katika limwengu zote mbili (dunia na akhera) huwekwa wazi na vitu viwili: Kuishi vyema na marafiki kwa muruwa na insafu, na kuishi na maadui kwa msamaha na usafi”.

Ukisema: Hilo siliwezi kwani uadui umenijaa moyoni, upo ndani ya fitra yangu na sina mbadala wala chaguo, achilia kuwa wamenijeruhi hisia zangu wameniudhi wala siwezi kuwasemehe.

Jawabu: Tabia mbaya hata kama haikuleta athari na hukumu yake au haikutendewa kwa mujibu wa muktadha wake, kama vile kusengenya, na akatambua mwenye kufanya hayo udhaifu wake, hapo hapana kosa wala hapatatokea madhara, ukiwa tu humiliki khiyari juu ya mambo yako, wala huwezi kuondokana na uadui, hakika hisia zako kuwa ni mwenye sifa kama hii, na ukajua kuwa hauko katika haki, hivyo viwili vitakuokoa kwa idhini ya Allah (s.w) dhidi ya shari za uadui uliomo ndani ya nafsi yako, hilo linaingia katika majuto ya ndani ya nafsi na toba iliyojificha, na istighfari iliyo ndani yake. Na sisi hatukuandika haya isipokuwa ni kwa ajili ya istighifari ya kiroho, ili muumini asije akachanganyisha baina ya haki na batili na akamfanya hasimu wake asie na makosa kuwa ni dhalimu.

Kuna jambo lililonitokezea na lenye mazingatio: Siku moja nilimuona mtu mwenye elimu kiasi akimtia dosari mwanachuoni hadi kufikia kumkufurisha, kwa sababu za kisiasa, na wakati huo huo nilimsikia akimsifu mnafiki anayewafikiana naye kwenye rai ya kisiasa, niliumizwa mno na tukio lile nikasema:

أَعُوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ وَالسِّيَاسَةِ

Na hapo ikawa ndiyo mwanzo wangu wa kuachana na maisha ya kisiasa.

Sura ya tano

Sura hii inabainisha madhara makubwa yanayopatikana na kuyasibu maisha ya kijamii, ikiwa ni sababu ya inda, khitilafu na mifarakano. Pakisemwa: Kuna hadithi inayosema kwamba,

اخْتِلَافُ أُمَّتِي رَحْمَةٌ (Imam Nawawi, Sharhu sahiih al-Muslim 11/91; Qurtubiy, Al-jamiu’ li ahkam-al-Qur’an Kareem 4/159; Suyutiy, tadriib al-Raawy 2/175.)

na khitilafu ni zenye kupelekea mifarakano na vikundi na mtu kukamatana na rai yake tu, na maradhi haya ya khitilafu ni rehema kwa watu madhaifu, kwani zinawaokoa wao dhidi ya wachache walio madhalimu wenye  nguvu, na ambao ikiwa watafikia makubaliano kwenye mji au kijiji itapelekea makandamizo dhidi ya wanyonge madhaifu, ama mifarakano na khitilafu zikiwa baina ya wenye nguvu, wadhaifu na wanyonge itakuwa ni faraja kwao na kuokoka dhidi yao. Vilevile ukweli unadhihiri bayana kwenye migongano ya kifikra, na kwenye mazungumzo na tofauti za akili.

Jawabu: Tunasema jawabu la swali la kwanza ni kama hivi: Khitilafu iliyokuja katika hadithi ni ile khitilafu njema (chanya) yenye mafanikio, na maana yake, ni kuwa kila mmoja anapaswa kuonesha ubora na usahihi wa njia yake na mtazamo wake anaoufuata, bila ya  kujaribu kuvunja au kutia dosari njia za wengine, bali harakati zake ni kwa ajili ya kukamilisha mapungufu na kusawazisha kwa mujibu wa uwezo wake, ama khitilafu mbaya (hasi), ni ile inayompelekea kila mmoja kuharibu njia ya mwenzake na kuivunja, na hii inatokana na chuki, choyo, na uadui, na aina hii ya khitilafu ni yenye kukataliwa kabisa kabisa katika mtazamo wa hadithi, kwani wenye kukhitilafiana ni watu wasioweza kufanya jambo lolote jema la kujenga. Ama jawabu la swali la pili: Tunasema ya kuwa: Ikiwa mifarakano na kugawana makundi kwa ajili ya haki, inawezekana kuwa ni makimbilio ya watu wa haki, lakini tunayo yashuhudia kutokana na mifarakano ni kwa sababu ya malengo ya kibinafsi na kwa matamanio ya nafsi yenye kuamrisha maovu, ni makimbilio ya wenye nia mbovu bali makimbilio ya madhalimu, hakika dhulma imo wazi kwenye matendo yao, hata kama shetani atamfikia mmoja wao kwa ajili ya msaada na kumuwafiki kwenye rai yake, atampongeza na kumshukuru, ama akiwa katika safu ya upinzani mwanaadamu kama malaika atamlaani na kumtupilia mbali.

Ama jawabu la swali la tatu tunasema: Migongano ya rai na mijadala ya kifikra kwa ajili ya haki, na katika kufikia ukweli inakuwa ni pale penye khitilafu za njia licha ya kukubaliana katika misingi na malengo. Aina hii ya khitilafu inaweza kuleta huduma nzuri katika kuigundua haki na kudhihirisha pembe au zawiya zake zote kwa sura iliyo wazi na nzuri, ama mijadala na tafiti katika kutafuta haki ikiwa ni kwa ajili ya malengo ya kibinafsi na kujikweza na kujipandisha daraja na kushibisha matamanio ya kifirauni na kutafuta umashuhuri, katika hali hii ukweli hautong’ara kabisa, bali utazalisha fitina, na hupati kupitia watu kama hao maafikiano katika makusudio wala malengo, bali hakuna katika dunia nukta ndogo ya maafikiano ya fikra zao, kwani hawako kwa ajili ya haki, utaona ni wenye kuchupa mipaka jambo linalopelekea mipasuko isiyoweza kutibika, na ulimwengu wa Kiislamu leo ni shahidi wa haya.

Na kauli bora ni: Ikiwa mwenendo wa muumini na harakati zake, ni zenye kwenda sambamba na mafunzo bora yatokanayo na hadithi tukufu:

الْحُبُّ فِي اللهِ وَالْبُغْضُ فِي اللهِ (Abu Daud, Sunnat 2; Ahmad ibn Hambal, Al-Musnad  5/146; Al-Bazar, Al-Musnad  9/ 461. Musnad ya Attwayalasiy 101; Ibn Abi Shaybat, Al-Musnaf  6/170, 172, 7/80.)

Na kuhukumia kwa amri za Allah (s.w) katika kila jambo, hivyo unafiki na mipasukano ndiyo vitakavyochukua nafasi, hakika yule asiyeongoka kwa misingi hii bila shaka atakuwa ni mwenye kutenda dhulma wakati ambao anataka uadilifu. Tukio lenye mazingatio: Katika vita vimoja baina ya waislamu na makafiri, alikuwa Imamu Sayyidna Ali (r.a) akipigana na mmoja wa wapiganaji wa kishirikina, na Imamu akamshinda na kumpiga, na alipokuwa anataka kummaliza, yule adui alimtemea mate usoni mwake, Sayyidna Ali alimwachia na kwenda zake, yule mshirikina alistaajabu sana kwa tendo lile la Sayyidna Ali na akamuuliza, unakwenda wapi? Akasema Sayyidna Ali: Nilikuwa napigana nawe kwa ajili ya Allah (s.w), lakini ulipofanya ulichokifanya, nilikhofia nikikuuwa nitakuwa nimekuuwa kwa sababu ya kulipizia kisasi, ndiyo maana nikakuacha kwa ajili ya Allah (s.w). Akasema yule kafiri: Tendo langu lilipaswa kuamsha hasira zako na kukuharakiza kuniua, na madamu munafuata dini iliyo na msamaha kama huu, hakika hii ni dini ya haki.

(Al-Mathnawiy al-Ruumi, Tarjama ya Alkafafiy juzuu ya 1, uk 443.)

Kisa kingine: Kiongozi mmoja wa Kiislamu alimvua madaraka kadhi mmoja wa makadhi wake, baada ya kumuona ni mkali na mwenye ghadhabu katika kutoa hukumu ya kumkata mkono mwizi, haipaswi kwa mwenye kutekeleza hukumu za Allah (s.w), kuwa na chochote cha kibinafsi kwa mwenye kuhukumiwa bali anaweza kuwa na huruma kwa kuwa hii ni nafsi, lakini huruma isiyompelekea kuacha kutekeleza hukumu ya haki, lakini kwa sababu nafsi yake (yule kadhi) ilichanganyika na jambo hilo na ni kinyume na uadilifu ndiyo akamuondoa katika ukadhi.

Maradhi Ya Kijamii Ya Hatari Na Hali Mbaya Yameusibu Umma Wa Kiislamu yanafanya Moyo Usononeke Kwayo

Makabila makubwa yaliyo nyuma yanadiriki vya kutosha maana ya hatari inayowakabili, utawaona ni wenye kupinga khitilafu za ndani, na wanajaribu kusahau uadui wao wakati wa adui wa nje anapowavamia.

Wakati makabila hayo yanatambua kisawasawa maslahi yao ya kijamii, kwa nini wale wanaosimamia huduma na masuala ya waislamu na kuulingania wasisahau uadui wao mdogo usio na msingi, wenye kusababisha kutengeneza njia za uvamizi wa adui dhidi yao, na maadui wamejipanga na wanawajia kwa kila pembe, hali hii ya kuporomoka yenye kutisha na khiyana ndiyo iliyouzunguka Uislamu na waislamu.

Kwa mnasaba huu tunatoa mfano huu wenye mazingatio:

Kulikuwa na makabila mawili ya ukoo wa “Hasnani”, walikuwa na visasi vya kumwagana damu baina yao, mpaka wakapotea kwa visasi hivyo watu wasiopungua hamsini, lakini mara tu adui wa nje alipowavamia kutoka kabila la “Sibkani”, walishikamana na kusaidiana na kusahau moja kwa moja khitilafu zao mpaka wafanikiwe kuzuia uadui huo.

Enyi waumini munaelewa makundi ya maadui ni mangapi yamejipanga kuvamia kundi la imani? Ni yenye kuzidi mia. Wanawazunguka Waislamu na Uislamu kila pembe, wakati ambao waislam wanatakiwa wawe wameshikamana, kuzuia uadui wa moja kati ya makundi hayo, wao kila mmoja yuko mbali pembeni kwa maslahi ya kibinafsi, kana kwamba ni mwenye kufungulia adui milango aweze kuingia kwenye ngome za waislam zilizo na amani. Je, hili ni sawa kwa umma wa Kiislamu?

Ukitaka kuorodhesha makundi dhidi ya Uislamu kuanzia watu wa upotofu mpaka kumalizia ulimwengu wa makafiri na misiba ya kidunia, utawakuta hawapungui sabini, wote hao utawakuta ni wenye kukukabaseni na wanataka kukuangamizeni. Nanyi hamna khiyari mbele yao isipokuwa silaha madhubuti kali na handaki imara, na ngome imara, nayo ni udugu wa Kiislamu.

Amka ewe muislamu! Tambua msukosuko dhidi ya ngome ya Uislamu kwa hoja nyepesi, na sababu zisizo za msingi, ni kinyume na maslahi ya Uislamu. Tanabahi kwa hilo!

Imepokewa katika hadithi yenye maana hii: Al-dajjali na Al-sufiyani na mfano wao ni miongoni mwa  watu wenye kukamatana na wanafiki na watadhihiri zama za mwisho, na watahamasisha mipasuko baina ya watu na waislamu, na watafaidika nao kwa kupenda kwao dunia, na wataeneza vita na mauaji, na watautawalia umma wa Kiislamu na kuufanya mateka. Enyi waislamu! ikiwa ni kweli mnataka maisha mazuri, na mnakataa kuwa mateka na madhalili na kudogoshwa, hivyo amkeni kutoka usingizini mwenu, na rejeeni kwenye njia, ingieni kwenye ngome madhubuti tukufu

إنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ Qur’an, 49:10

na kuweni makini dhidi ya mikono ya madhalimu, ambao wanafaidika na khitilafu zenu za ndani. Kama hamkuwa makini mtashindwa kulinda haki zenu, na hamtaweza hata kuhifadhi maisha yenu, ni wazi kwamba mtoto mdogo anaweza kuwapiga mashujaa wawili wenye kupigana, na kijiwe kidogo ni muhimu katika kunyanyua uzito wa mizani au kuupunguza hata kama patakuwa na majabali mawili yenye uzito sawa.

Enyi watu wa imani! Nguvu zenu zinakwenda na upepo, kwa sababu ya matamanio yenu ya kibinafsi, na migawanyiko, nguvu ndogo zinaweza kukuonjesheni idhilali na maangamizo, ama mukiwa mumeshikama kikweli na mila za Uislamu mtashinda, hebu kamataneni na uongofu wa hadithi ya Mtume (s.a.w):

الْمُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِ كَالْبُنْيَانِ يَشُدُّ بعْضُه بَعْضًا (Bukhari, Swalat 88; Muslim, Al-bir 65.)

kwa msingi huu pekee mtaweza kusalimika na idhlali ya kidunia na kuokoka na shida za akhera. 

Sura ya sita

Ikhlasi ni njia muhimu ya kujiepusha na kujiokoa dhidi ya adhabu. Inadi na uadui ni vitu vyenye kutikisa maisha ya muumini ya kiroho, na kusababisha adha dhidi ya usalama wa ubudiyah wa mja kwa mola wake, kwa kupotea ikhlasi, kwani mtu mwenye taasubi ya rai yake na kundi lake daima anatarajia kumshinda adui yake, hata ikiwa ni katika amali za kheri atakazozifanya, kwa maana hiyo hapati tawfiki kamili kwa amali yoyote ile kwa ajili ya Allah (s.w), vile vile hapati tawfiki ya uadilifu, kwani daima anakuwa pamoja na wale wanaowafikiana na rai yake, hukumu zake, na miamala yake dhidi ya wengine, kwa hali kama hii ndivyo inavyopotea misingi mikuu inayojenga kheri “Ikhlasi na Uadilifu”, kwa uhasama na uadui. 

Mlango huu ni mrefu lakini tutatoshelezeka na haya tu.You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.