Mng’ao Wa Ishirini Ikhlasi

بِسْمِ اللهِ الَّرحْمنِ الَّرحِيْمِ

إِنَّا أَنْزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ  فَاعْبُدِ اللهَ مُخْلِصًا لَهُ الدِّيْنَ ۞أَلَا للهِ الدِّيْنُ الْخَالِصُ (Qur’an, 39: 2 – 3)

Na Mtume (s.a.w) amesema:

هَلَكَ النَّاسُ إِلَّا الْعَالِمُونَ وَهَلَكَ الْعَالِمُونَ إِلَّا الْعَامِلُونَ وَهَلَكَ الْعَامِلُونَ إِلَّا الْمُخْلِصُونَ وَالْمُخْلِصُونَ عَلَى خَطَرٍ عَظِيْمٍ (Kashf al-khafaa (2796))

Aya hii tukufu na hadithi ya Mtume (s.a.w) zinatuonesha umuhimu wa ikhlasi katika Uislamu na upeo wa ukubwa wake na kuwa ni msingi ambao mambo ya dini hutegemea, na baina ya vipengele vingi katika ikhlasi tutazungumzia hapa kwa ufupi nukta tano.

Nukta ya kwanza

Swali muhimu na lenye kushangaza:

Kwa nini wanahitilafiana watu wa dini na maulamaa na watu wa tarika za kisufi nao ni watu wa haki na maafikiano na mapenzi kwa mashindano na msongamano, na wakati huo huo wanawafikiana watu wa dunia na mighafiliko, bali watu wa upotofu na unafiki wanakubaliana pasina ugomvi wala husuda baina yao, pamoja ya kuwa maafikiano ni sifa ya watu wa kweli, ama khitilafu ni zenye kwenda pamoja na unafiki na mifarakano. Vipi imebadilisha haki na batili mahala pake, ikawa haki iko kwa watu wapotofu na batili ikawa kwa watu wa kweli?

Jawabu:

Tutabainisha sababu saba katika sababu nyingi juu ya suala hili lenye kuumiza na lenye kupoteza usingizi wa wenye ari na mapenzi (ya dini yao).

Sababu ya kwanza:

Hakika khitilafu ya watu wa haki haitokani na kupotea kwa ukweli, kama ilivyo maafikiano ya watu wenye mghafiliko hakutokani na kuegemea kwao katika ukweli, bali wadhifa wa watu wa dunia na siasa na wasomi na mfano wa wao katika tabaka za kijamii ni wenye kubainika wazi, kila pote na kundi na jumuiya ni yenye kazi maalumu inayoshughulika nayo, na ujira wanaopata wa kimaada kwa ajili ya huduma zao na kuendeleza maisha yao, pia hivyo ni vitu vilivyo wazi, kama ilivyo ujira wanaoupata wa kimaanawi mfano wa cheo, umashuhuri, ni vitu vilivyo wazi na kupambanuka.

Tahadhari: Kuelekewa na watu hakutafutwi, bali hupewa, kuelekewa huko kukitokea kusifurahiwe. Kama mtu ataona raha kwa kule kuelekewa na watu basi amekwisha poteza ikhlasi na kuangukia kwenye ria. Ama kutafuta umashuhuri na kusikika ambako kunajumuisha kuvuta watu na kutaka wa kuelekee sio ujira wala thawabu, bali ni lawama na adhabu ndivyo vinavyofuatia kutokana na kukosekana kwa ikhlasi. Naam, hakika kuelekewa na watu haipaswi kukusudiwa, kwa sababu ladha chache iliyomo inadhuru ikhlasi ambayo ni roho ya amali njema, kisha haiendelei mpaka katika mlango wa kaburi. Ukiachilia mbali kule kuzalisha sura yenye kuumiza ambayo huwa nyuma ya kaburi miongoni mwa adhabu za kaburi. Hivyo haifai kutaka kuelekewa na watu na kutafuta kuridhiwa nao. Na wasikilize hili wenye kuabudu umashuhuri, na wenye kutaka kwa shauku kuvuna ridhaa za watu. (Mwandishi)

Kwa hivyo hakuna kinacholeta ushindani, au mgomvi, au hasadi baina yao, wala hakuna kinachopelekea midahalo na mijadala, kwa hivyo utawaona ni wenye umakini katika kuwafikiana hata wawe ni wenye kufuata njia ya upotofu kiasi gani.

          Ama watu wa dini na elimu na watu wa tasawuf, kazi ya kila mmoja wao ni yenye kuelekea kwenye jamii, na ujira wao wa akhera hauko wazi, kama ilivyo hadhi na daraja zao katika jamii, na kuelekewa na watu na kuridhiwa hakupo wazi pia. Wako wengine wengi ambao watakaokuwa daraja moja, mikono mingi inaweza kukunjuka kwenye ujira mmoja wa kimaada au wa kiroho, na hapa ndipo mahala panapozuka mizozo na zahama na mashindano na husuda na choyo, na makubaliano kugeuka unafiki na maafikiano kuwa ni khitilafu na mfarakano.

Hakika maradhi haya hayapoi isipokuwa kwa dawa ya ikhlasi iliyo bora, nayo ni mtu kupata utukufu wa kuifanyia kazi aya:

إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللهِ (Qur’an, 10: 72)

kwa kupendelea haki na uongofu dhidi ya kufuata nafsi na matamanio, pamoja na kuithibitisha haki mbele ya mapenzi ya nafsi, na atekeleze kauli yake Allah (s.w):

وَمَا عَلَى الرَّسُوْلِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِيْنُ (Qur’an, 24: 54)

kwa kuacha kutafuta malipo yawe ya kimaada au ya kiroho kutoka kwa watu

Hapana budi kufanya tabia ya “ITHAR” (kupendelea wema kwa wengine) ambayo ni tabia waliyojipamba nayo masahaba watukufu (r.a) na wakapata sifa ya Qur’an tukufu usawa wa macho. Na kuichukulia kuwa mwongozo elekezi. Na hii maana yake ni kuwafadhilisha wengine kuliko nafsi yake mtu wakati wa kupokea zawadi na sadaka, na kutokubali kitu kuwa malipo ya anachofanya mtu, katika huduma kwa ajili ya dini, bali asiombe kwa moyo. Na kama akipata vitu mfano wa hivi na avihesabu kuwa ni hisani ya kiungu tu, pasi na kubakia chini ya takrima ya watu. Kwani haitakikani kuombwa kitu duniani kulipia huduma zinazotolewa kwa ajili ya dini, ili ikhlasi isije ikapotea.

 Kwa hiyo umma japo ni juu yake kudhamini maisha ya watu hawa, kama inavyostahiki kupewa zaka pia, isipokuwa hawa watendaji hawaombi watu chochote na pengine hupewa zawadi, na hata kama watapewa vitu, wasivichukue kwa ajili ya kufanya kwao shughuli za dini kilicho bora ni kuwapendelea wengine wenye kustahiki zaidi kuliko nafsi yake mtu, na kuridhia vile alivyogaiwa na Allah (s.w) katika riziki na kukinai kwavyo, ili mtu apate sifa ya Qur’an tukufu:

وَيُؤْثِرُونَ عَلَى أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهْمْ خَصَاصَةٌ (Qur’an, 59: 9)

na hapo atakuwa ameipata ikhlasi na kuokoa nafsi yake kutokana na shari za maangamizo haya ya hatari. (Mwandishi)

akidiriki yakini kwamba mapenzi ya watu juu ya maneno yake, taathira yake nzuri kwao na kupata mwelekeo wao kwake, ni mambo yenye kusimamiwa na Allah (s.w) na ni kwa sababu ya ihsani yake na fadhila zake pekee, na wala hayaingii hayo katika wadhifa wake uliomo kwenye ujumla wa kufikisha (Al-balaghu) tu, bali yeye asili sio mukalafu wa hayo. Na hakika aliyewafikishwa na Allah (s.w) kwa haya tuliyoyazungumza hivi punde tu atapata ladha ya ikhlasi, na kinyume chake atapitwa na kheri nyingi.

Sababu ya pili:

Hakika makubaliano ya watu wapotofu yanatokana na udhalili wao, lakini khitilafu za watu waongofu zinatokana na utukufu wao, kwa kuwa watu wa dunia na upotofu walioghafilika hawategemei haki wala uhakika ni dhaifu na dhalili, wanahisi kuwepo haja muhimu ya kuwapatia nguvu na wanakamatana kwa nguvu zao zote kwa kupata msaada kwa wengine na kukubaliana nao, na huwa wanalinda makubaliano haya hata yakiwa ni yenye kuwaongoza kwenye upotofu, kana kwamba ni wenye kutenda hasa katika kusaidiana juu ya batili, na wanatenda hayo ya upotofu kwa nafsi moja, na wanaonyesha uthabiti na ari juu ya kufuru yao, na wanawafikiana katika unafiki wao, kwa hali hii wanafikia malengo yao kwani ikhlasi ya dhati japo kwenye mambo ya shari haiendi ovyo ovyo na haiwi bila ya mafanikio kwani yeyote anayemuomba Allah (s.w) jambo kikweli kweli Allah (s.w) atampa jambo hilo.

Naam, “mwenye kutafuta na kujitahidi hupata” kanuni katika kanuni za hakika ina kiasi cha ukunjufu na kuenea kujumuisha maslaki yetu pia. (Mwandishi)

Ama watu wa uongofu na elimu na watu wa tarika kwa kuwa wao huegemea kwenye haki na ukweli na kwamba kila mmoja wao wakati wa nyendo zake kwenye njia ya haki anakuwa hapana anachokitarajia ila ni kupata radhi za Allah (s.w) na anatulia kwake kwa utulivu mkubwa, na anapata utulivu wa kiroho kwenye mwenendo wake huo, na kila anapohisi udhaifu anarejea kwa mola wake na sio kwa watu, na anatafuta nguvu kutoka kwa Allah (s.w) pekee na anapoona khitilafu kinyume na njia aliyonayo yeye, hivyo utamuona haoneshi hisia au hamu ya kushirikiana na wengine, bali haoni haja ya kuwafikiana na wale waliohitilafiana nao kinje nje. Na inapokuwa ghururi na kujipendelea mtu nafsi yake, mtu hudhania kwamba yeye pekee ndiye aliye kwenye haki na wengine wote wapo kwenye batili, hapa ndipo panapotokea khitilafu na mashindano badala ya makubaliano na mapenzi, hivyo anakosa ikhlasi na amali zake zinaanguka na kupeperuka.

Kinga pekee ya haya ni katika vipengele tisa vifuatavyo:

  1. Matendo bora yenye kujenga, nayo ni mtu kutenda kwa mujibu wa mapenzi yake kwenye njia anayoiamini, bila ya kufikiria uadui kwa wengeni au kuwadogesha kwa kuwadharau, kwa maana nyingine asishughulike nao kabisa.
  2. Juu yake ni kukamatana na kamba ya umoja yenye kufunganisha njia mbali mbali katika Uislamu kwa aina yoyote ile ambayo itakuwa ni sababu ya kuwa ni chemchem ya mapenzi na njia ya udugu na maafikiano baina yao.
  3. Kuchukua tabia ya insafu kama kiongozi: Nayo ni kila mwenye kufuata njia ya haki huweza kusema “Njia yangu ndiyo njia ya haki na ni bora na nzuri pasina kuingilia njia za wenzake lakini haijuzu kwake kusema: Haki ni katika njia yangu pekee au ubora na uzuri ni katika njia yangu pekee”. Jambo ambalo ni lenye kupelekea kuzibatilisha njia nyingine na kuziona ni zenye ufisadi.
  4. Kutambua kwamba kuwa na makubaliano na watu wa haki ni njia moja wapo ya kupata taufiki ya Allah (s.w) na ni moja ya chemchem za utukufu wa Kiislam.
  5. Kuhifadhi haki na uadilifu na kutengeneza mtu wa kiroho kwa kuwa na makubaliano na watu wa haki na kusimama dhidi ya watu wapotofu na batili ambao wamekuwa ni wenye kufanya mashambulizi mazito dhidi ya mtu wa kiroho mwenye nguvu, kwani watu wa batili wana mtu wa kiroho mwenye nguvu kwa sura ya wingi kwa ajili ya kupiga vita mtu wa haki, hivyo ni lazima  watu wa haki kudiriki kwamba juhudi za mtu binafsi awe na nguvu kiasi gani ni lazima kushindwa.
  6. Kwa ajili ya kuokoa haki kutoka kwenye mikono ya batili.
  7. Kuacha ghururi ya nafsi na matamanio yake.
  8. Kuacha kinachofikiriwa kwa makosa kuwa ni utukufu na ubora.

9. Kuacha mambo yanayopelekea uhasidi, ushindani, na hisia za kujipendelea zisizo na msingi.

Kwa vipengele hivi tisa vinapelekea ikhlasi na vinamfanya mwanaadamu kutekeleza wadhifa wake vizuri na kwa sura inayotakiwa.

Imethibiti katika hadithi sahihi kuwa wenye kushika dini hasa katika Wakristo mwisho wataafikiana na watakuwa pamoja na watu wa Qur’an katika kupambana na adui wao wa pamoja mpagani. Hivyo watu wa Imani na hakika katika wakati wetu huu hawana haja ya kuwafikiana wao kwa wao peke yao, bali wanatakiwa wawafikiane hata na watu wa kiroho wenye kushika hasa miongoni mwa Wakristo, waache kwa wakati maalum kila kinachochochea khitilafu na mabishano katika kumsukuma adui wao wa pamoja mpagani mwenye kufanya uadui. (Mwandishi)

Sababu ya tatu:

Khitilafu ya watu wa haki haitokani na udhaifu wa kukosekana hima, kama ilivyo maafikiano ya watu wapotofu haitokani na hima ya hali ya juu, lakini khitilafu ya watu waongofu inatokana na matumizi mabaya ya hima na kuchupa mipaka, vilevile makubaliano ya watu wapotofu chanzo chake ni udhaifu na ajizi vinavyotokana na kukosekana hima.

Na kinachowapelekea watu waongofu kuyaelekea matumizi mabaya ya hima na kufikia khitilafu na ghururi na uhasidi, ni yale matarajio makubwa ya kupata thawabu za Akhera, jambo ambalo ni sifa yenye kupendeza, na kutafuta ziada ya thawabu pasina ukinaifu na kuweka jambo hilo ndani ya nafsi, jambo  hili linampelekea mwenye pupa ya kutafuta thawabu kufikia mjadala na mizozano na ndugu yake wa ukweli ambae anahitajia mno mapenzi yake na msaada wake na udugu wake na kukamatana mikono kama mfano kusema: “Wacha mimi nipate thawabu hizi na niwaongoze mimi watu hao na wanisikilize maneno yangu mimi pekee, na mfano wa hayo kwenye kujitafutia mtu thawabu kwa nafsi yake, au aseme kwa nini wanafunzi wangu wanakwenda kwa fulani na fulani, kwa nini wanafunzi wangu hawafikii idadi fulani na wala hawaongezeki, hivyo utakuta uchoyo ndani ya nafsi yake kupitia mazungumzo kama haya ya ndani kwa ndani, ni fursa njema ya kujivimbisha kichwa, hivyo inampeleka kidogo kidogo kujichafua kwa sifa mbaya na hii ndiyo hali ya kupendelea cheo, inayompelekea kukosa ikhlasi na kumfungia milango yake, na kumfungukia milango ya ria kwa upana wake.

Kinga pekee ya kosa hili kubwa na jeraha hili kubwa na maradhi haya ya kiroho mazito ni: kutambua kwamba radhi za Allah (s.w) hazipatikani ila kwa ikhlasi. Hakika radhi za Allah (s.w) sio kwa kuwa na wafuasi wengi au kuwa na mafanikio na taufiki katika kazi, kwani kuwa na wafuasi wengi au taufiki katika kazi ni jambo linalosimamiwa na Allah (s.w) kwa fadhila zake na ukarimu wake wala haulizwi lakini Allah (s.w) anampa anayemtaka.

Pengine neno moja tu linaweza kuwa ni sababu ya kuepukana na moto na kuwa ni sababu ya kupata radhi za Allah (s.w), na pengine kumuokoa mtu mmoja inaweza kuwa ni sababu ya kupata radhi za Allah (s.w) kwa kiwango cha kuongoa watu elfu kwa hivyo haipaswi kuchukuliwa idadi kuwa ni kigezo.

Hakika ikhlasi katika amali na kuhimiza haki hujulikana kwa ukweli wa raghba au hamu katika kuwafaidisha Waislamu kwa ujumla, kutoka chanzo chochote cha faida, na kutoka kwa mtu yeyote, ama mtazamo pekee kwamba masomo na maelekezo ni kutoka kwangu mie pekee ili kupata mafanikio na thawabu za Akhera ni hila za kinafsi na ujanja wa uchoyo.

Ewe mwenye kutaka ziada za thawabu wala hatosheki na amali za kiakhera alizozifanya!

Elewa hakika Allah (s.w) alituma Mitume wake watukufu na watu hawakuamini ila wachache, na licha ya hivyo hawakukosa thawabu za utume mtukufu kamili bila mapungufu. Sio kutangulia au kupata fadhila ni kwa sababu ya kuwa na wingi wa wafuasi, bali kunatokana na kupata hadhi na radhi za Allah (s.w), Je, ni nani wewe mwenye pupa ya kutaka watu wote wakusikilize, na ukasahau wajibu wako na ukawa ni mwenye kuingilia shaani za Allah (s.w) na kudura zake. Tambua hakika watu kuamini maneno yako na kukubali mlinganio wako na kukusanyika mbele yako, hayo ni kwa fadhila za Allah (s.w) anampa amtakaye, hivyo usiishughulishe nafsi yako kwa yale ambayo yanamhusu Allah (s.w) katika kudura na maelekezo, lakini kusanya hima yako kufanya yale uliyotakiwa na yaliyo wajibu.

Hakika kusikiliza haki na ukweli, na kupata thawabu kwa mzungumzaji wa mambo hayo si kwa mwanaadamu peke yake, bali Allah (s.w) ni mwenye viumbe vyenye hisia, wa kiroho, na malaika waliojaza ulimwengu na kuimarisha, ikiwa unataka ziada za thawabu za akhera kamatana na ikhlasi na ifanye kuwa ni msingi wa amali zako, na jaalia radhi za Allah (s.w) peke yake ndiyo lengo lako na mafanikio ya amali zako, ili wahuike watu kwa neno hilo zuri lililotamkwa kwa midomo yako na lienee angani kwa ikhlasi na nia safi, na kuwafikia viumbe mbali mbali visivyo na idadi ili uweze kupata thawabu zilizo nyingi, kwa mfano utakaposema (Alhamdulillahi) utaandikiwa kwa amri ya Allah (s.w) kwa kutamka neno hilo mamilioni ya shukrani ndogo ndogo na kubwa kubwa angani. Hakika Allah (s.w) ameumba masikio yasio na idadi na yote yanasikia maneno hayo yaliyo mazuri bila ya upuuzi wala israfu katika amri za Allah (s.w), na ikhlasi na nia ya kweli itakapoingiza uhai kwenye maneno haya yalioenea kwenye chembe chembe za anga hakika yataingia kwenye masikio ya viumbe hivyo vya kiroho katika hali ya ladha nzuri na kama ladha ya tunda zuri, lakini ikiwa radhi za Allah (s.w), na ikhlasi havikuingiza uhai ndani ya maneno hayo, basi hayatasikilizwa bali yatakimbiwa na yatabaki thawabu zake kwa kutamkwa tu na mdomo, basi na wasikilize haya wale wanaosoma Qur’an na wanapata shida kwa kutokuwa na sauti zilizo nzuri hivyo kukosa wasikilizaji.

Sababu ya nne:

Khitilafu za watu waongofu na kuwepo husuda baina yao havitokani na kukosa fikra njema kuhusu mwisho wao na wala sio mitazamo finyu, kama pia maafikiano mema baina ya watu wapotofu hayatokani na wasiwasi juu ya mwisho wao au ubora na uzuri wa mitazamo yao, bali kushindwa kwa watu waongofu katika kuthibiti na kubaki kwenye njia, na uchache wa Ikhlasi kwenye amali inawaharamishia kupata raha za sifa za daraja ya juu, kwa hivyo wanaporomoka kwenye shimo la khitilafu, licha ya kuuendea uongofu kwa akili na nyoyo zenye kung’arisha mwisho wao, na wanachota katika haki na uhakika wa mambo, na hawaegemei katika matamanio yao ya nafsi kwa hisia zao juu ya kuona mwisho.

Ama watu wapotofu kwa ghururi ya nafsi na matamanio na hisia za matamanio na mitazamo mifupi ya mustakabali wa Akhera inawafanya wafadhilishe raha za dunia kulikoni mbele ya Akhera, hivyo utaona ni wenye kuwafikiana baina yao kwa umadhubuti kabisa na wanakusanyika kwa ajili ya kupata manufaa ya dunia na starehe za karibu.

Hakika watumwa wa nafsi, wapumbavu miongoni mwa watu wenye mioyo iliyokufa na wenye kutangatanga na matamanio ya chini kabisa daima ni wenye kukusanyika na kuwafikiana baina yao, kwa ajili ya manufaa ya haraka ya kidunia. Wakati ambao wanatakiwa watu waongofu kuwa na maafikiano ya ukweli, na umoja ulio kamili, na kujitolea kwenye matunda, na mshikamano wa nguvu baina yao, kwani wao ni wenye kuelekea kwa nuru ya akili zao na miangaza ya nyoyo zao, kwenye kuvuna ukamilifu na matunda ya akhera ya hapo baadaye, lakini kwa kukosa kujiepusha na ghururi na kiburi, na kuchupa mipaka, wanapoteza chemchemu iliyo kubwa na yenye utajiri na yenye kuwapa nguvu nayo sio nyingine ila ni kuwafikiana kwa kila hali, na kama hivyo inapotea Ikhlasi kwa kuvunjika vunjika na zinaharibika amali za akhera na kwenda vibaya, na inakuwa vigumu kupata radhi za Allah (s.w). Na kinga ya maradhi haya mazito ni kujifaharisha kwa kuwa pamoja na wenye kufuata njia kwa minhaji ya haki, na kufungamana nao kwa kamba ya mapenzi kwa kutekeleza hadithi tukufu

الْحُبُّ فِي اللهِ

(Tazama Abu Daud na Musnad Ahmad bin Hanbal, Al-musnad 5/146; Attayalisy, uk 50, 100; Ibn Abi shybah, Musannif  6/170,172,7/80.)

kisha kuwa nyuma yao na kuacha utukufu wa uongozi kwao, na kuacha kushangazwa na nafsi na ghururi kwa kufikiria msingi wa kwamba kila mwenye kuongoza njia ya kheri kwa vyovyote alivyo ni bora kuliko yeye, ili imrahisishie njia ya ikhlasi, na kuwa na elimu kwamba dirhamu moja iliyopatikana kwenye amali iliyo na ikhlasi kwa ajili ya Allah (s.w) ni bora kuliko kilo nyingi za amali zisizo na ikhlasi, na kubakia katika daraja ya ufuasi pasina kuhangaika kupokea majukumu, ambayo ni mara chache mtu anaweza kuepukana na hatari, na kwa mambo haya inapatikana kinga na tiba dhidi ya maradhi haya na kumnyanyua mtu kwenye ikhlasi, na anakuwa mtu ni muumini wa kweli aliyetekeleza amali za akhera kwa ubora na ukamilifu.

Sababu ya tano:

Hakika khitilafu za watu wa haki, na kukosa kuwafikiana baina yao hakutokani na udhaifu wao, kama vile makubaliano ya uhakika ya watu wapotofu hayatokani na nguvu zao, lakini kukosekana makubaliano baina ya watu wa haki ni yenye kutokana na hisia kwamba hawana haja ya kuwa na nguvu, kutokana na kuwepo na chemchem kamili inayowapa nguvu, ama watu wa upotofu na mghafiliko ni kwamba maafikiano yao ni yenye kutokana na udhaifu na ajizi, kwani hawakuti kwenye nafsi  zao chemchem yoyote ya kuwapatia nguvu, kwa maana hiyo haja kubwa ya kuwa na nguvu inawafanya wawafikiane kwa nguvu zote. Ama udhaifu wa hisia za wenye nguvu wa kutokuwa na haja ya kuwa na makubaliano, ndiyo inafanya makubaliano yao kuwa dhaifu, simba mwituni hawahisi haja ya kuwa na makubaliano, tofauti na mbwa mwitu, hivyo simba huishi maisha ya kipekee, ama wengine nyati, swala, na punda milia wanaishi pamoja kwa kuwaogopa simba na mbwa mwitu. Hii ni kwamba jumuiya za madhaifu

Hakika kinachotia nguvu madai yetu haya ni kuwa vyama vyenye nguvu zaidi Ulaya na vyenye athari sana kwenye jamii na kwa upande mwingine ni imara zaidi, ni vyama vya wanawake, – na hii ni jinsia nyororo – ndani ya  marekani ambayo inadai haki na uhuru wa mwanamke. Na  kadhalika vyama vya wa ARMANI ambao wao ni wachache mno na dhaifu kati ya mataifa, isipokuwa wanaonesha kujitoa muhanga na ushupavu wa hali ya juu. (Mwandishi)

na mtu wa kiroho (ndani ya nafsi) ni mwenye kumathilisha nguvu, ama jumuiya za wenye nguvu na mtu wao wa kiroho (ndani ya nafsi) anamathilisha udhaifu. Kwenye Qur’an kuna ishara nzuri ya mfano huu na siri, nayo ni kuegemezwa kitendo

“قَالَ”

yaani amesema, na hapa kimekuja kitendo kwa umbo la kiume na wanaohutubiwa ni wanawake

licha kuwa uke ni wenye udhaifu

“وَقَالَ نِسْوَةٌ فِي الْمَدِيْنَةِ”

na wakati huo huo kimekuja kitendo

“قَالَتْ”

kwa umbo la kike katika kauli yake Allah (s.w)

“قاَلَتْ الْأَعْرَابُ” 

na hali ya kuwa hili ni kundi la wanaume, na hii ni ishara kwamba kundi lile la wanawake na udhaifu wao, wanapata nguvu na kupata aina fulani ya ujanadume, ndiyo pakahitajika kuhutubiwa kwa umbo la uume, na ndiyo kitendo kikachukua umbile la

قَالَ

  katika hali ya kupendeza kabisa, ama wale wanaume mabedui wenye nguvu imekuwa kundi lao ni dhaifu kwa sababu ya kupata sifa fulani ya kike kwa ule wasiwasi, hadhari, upole ndiyo umbile la kitendo kikaja umbile lenye kufaa

“قَالَتْ الْأَعْرَابُ”

Hakika watu wenye kueneza haki hawaoni kuwepo haja ya kusaidiana na kuwa pamoja na wengine, kwa sababu ya yale wanayoyabeba ndani ya vifua vyao katika imani nzito, na yenye kuwapa nguvu na kuwapa tawakuli na kujisalimisha kwa Allah (s.w), hata iwe ni wenye kuhitajia wengine basi hawatowapokea kwa nguvu zote. Ama wale waliojaalia dunia kuwa ndiyo lengo lao, na kwa sababu ya kughafilika kwao na nguvu za uhakika, wanakutia ndani ya nafsi zao udhaifu na ajizi katika kufanikisha mambo ya kidunia, hivyo wanajikuta ni wenye haja kubwa ya kupata wa kuwaongezea nguvu, hivyo hukubaliana kihali na mali na kwa mihanga na kujitolea.

Kwa kuwa watu wa haki hawazingatii vyema nguvu zitokanazo na makubaliano, na wala hawazijali, hivyo daima wanaishia kwenye matokeo mabaya nayo ni khitilafu, wakati ambao watu wa batili na upotofu kwa kuhisi kwao kwa sababu ya ajizi yao na udhaifu wao kwa yaliyomo ndani ya makubaliano ambayo ni nguvu kubwa, wamepata njia madhubuti ya kuwafikisha kwenye malengo yao, hakika haya ndiyo maafikiano.

Hakika njia ya kuepukana na hali hii thakili yenye kuumiza, na kuondokana na maradhi haya ya kuangamiza, maradhi ya kuhitilafiana, ambayo yamewagubika watu wa haki, ni kuacha makatazo ya Allah (s.w) kama yalivyokuja katika aya tukufu:

وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيْحُكُمْ Qur’an, 8:46

Na kufuata maamrisho ya kiungu kama yalivyokuja katika aya tukufu:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَى Qur’an, 5:2

Hizi ni kanuni mbili za kuzitendea kazi katika maisha ya kijamii, na elimu juu ya hasara zinazosababishwa na khitilafu na madhara yake makubwa kwa Waislam na Uislamu, na kiasi gani huwafungulia njia watu wa upotofu kunyoosha mikono yao juu ya watu wa haki, na kuingia kwenye safu za kiimani kwa kujitolea, na kwa hisia za kuwa na ajizi kamili na udhaifu kamili, na kwa kujificha ili kuepukana na ria ili kufikia daraja ya ikhlasi.

Sababu ya sita:

Hakika khitilafu baina ya watu wa haki haitokani na kukosa hamasa, au ushujaa na wala sio kwa kuanguka hima na kukosekana ghera na umoja, kama ilivyo maafikiano baina ya watu wa mghafiliko na upotofu, ambao ni wenye kutafuta mambo ya kidunia, hayatokani na ushujaa au kuwa na ghera na hima ya juu, lakini watu wa haki wameelekeza mitazamo yao katika thawabu za akhera zaidi, hivyo wakaeneza ushujaa wao na hima zao kwenye masuala mengi muhimu, na kutokana na kwamba hawatumii muda wao mwingi, ambao ndiyo rasilimali yao ya kweli kwenye suala maalumu moja pekee, hivyo hawafikii maafikiano yao kwa umadhubuti pamoja na wenye kufuata njia ya haki, kwa kuwa masuala ni mengi na nyanja nazo ni nyingi mno.

Ama watu wa dunia walioghafilika kutokana na kuwa macho yao yanaelekea kwenye maisha ya kidunia pekee, nayo hiyo dunia ni lengo lao kubwa na mwisho wa elimu yao, bado utawaona ni wenye kushikamana nayo kwa kamba madhubuti, na kwa hisia zote walizonazo na kwa roho na moyo. Hivyo mtu yeyote atakae nyanyua mkono wa msaada watakamatana naye kwa nguvu, na wanatupa wakati wenye thamani sana kwenye kadhia za kidunia ambazo kwa hakika sio zenye faida mbele ya watu wa haki, mfano wao ni sawa na yule sonara Myahudi mwendawazimu aliyenunua kipande cha kioo kisicho na thamani kwa thamani ya mawe ya vitu yenye thamani kubwa, hakika kununua kitu kwa thamani kubwa, kuelekeza hisia zote kwake, bila shaka ni jambo lenye kupelekea mafanikio makubwa hata ikiwa ni katika njia ya batili kwani ndani mnakuwa na ikhlasi kubwa.

Na kama hivi ndivyo watu wa batili wanavyowashinda watu wa haki, hupoteza watu wa haki ikhlasi, wakaporomoka kwenye shimo la udhalili, kujidai na ria, wakabakia ni wenye kufuatafuata na kujisogeza kwa watu wa dunia waliopoteza kila maana ya ushujaa na ghera na hima ya juu.

Enyi watu haki! Enyi watu wa sheria na ukweli na tarika, enyi waenezaji wa haki kwa ajili ya haki! Fanyeni kwa ajili ya kuondosha maradhi haya ya kutisha, maradhi ya khitilafu kwa kujifundisha adabu za Al-furqan tukufu nayo ni kauli yake Allah (s.w):

وَإِذَا مَرُّوا بِالَّلغْوِ مَرُّوا كِرَامًا Qur’an, 25:72

Sameheni makosa ya ndugu zenu na sameheni kasoro zao, na fumbeni macho yenu dhidi ya aibu baina yenu, wekeni pembeni mijadala yenu ya ndani. Hakika maadui wenu wa nje wanakushambulieni kila pembe, fanyeni kuwaokoa ndugu zenu wa haki dhidi ya kuporomoka katika udhalili kuwa ni wajibu wenu mkuu wa akhera na wa aula kupewa kipao mbele, tendeni kwa mujibu zinavyo kuamrisheni aya nyingi tukufu na hadithi tukufu, katika kuleta udugu na mapenzi na kusaidiana, na shikamaneni kwa hisia zenu zote na kamba ya maafikiano na ndugu zenu katika dini, na minhaji (misingi) ya haki kwa nguvu zaidi ya zile wanazoshikamana nazo watu wa batili na dunia na mghafiliko, jihadharini daima kukwama kwenye nyavu za khitilafu, na wala asiseme mmoja wenu “nitatumia wakati wangu wenye thamani katika kusoma nyiradi na dhikiri na kuleta mazingatio, badala ya kuutumia kwenye mambo madogo madogo” na akatoka nje ya uwanja ikawa ni njia ya kudharau maafikiano na umoja, ikawa ni sababu ya kudhoofisha kundi la Waislam, hakika mambo mnayoyadhani kuwa ni madogo na mepesi, pengine kwa upande mwingine ni makubwa mno na muhimu katika jihadi hii ya kiroho, kama vile mpiganaji kubakia daima akilinda mipaka ya Kiislam na katika masharti muhimu kwa saa moja katika wakati inaweza kuwa ni mfano wa mwaka mzima katika ibada, hakika siku yako moja yenye thamani ambayo unaitumia katika masuala madogo katika masuala ya jihadi ya kiroho, hasa katika wakati mgumu kama huu ambao watu wa haki wameshindwa juu ya mambo yao, nasema kwamba hakika siku yako moja yaweza kuwa sawa na hukumu ya saa moja ya kubakia mpiganaji yule yaani thawabu zake ni nyingi, bali yaweza kuwa siku yako moja ni sawa na siku elfu, hasa ikiwa amali ipo kwa ajili ya Allah (s.w) na katika njia yake, na wala haitazamwi amali kwa sababu ya udogo au kwa ukubwa wake na wala kwa sababu ya hadhi yake bora au ya chini, chembe ndogo katika njia ya radhi za Allah (s.w), na ikhlasi zinakuwa sawa na nyota zenye kumeremeta angani, ukweli wa njia hauchukuliwi kama kigezo lakini kinachozingatiwa ni matokeo na malengo, na kwamba Allah (s.w) ameridhia, hakika msingi wa amali ni ikhlasi, na masuala haya hayatakuwa masuala madogo bali ni makubwa na makubwa sana.

Sababu ya saba:

Hakika khitilafu za watu wa haki na ukweli na ushindani wao hazitokani na ghera (wivu) uliopo baina yao na wala pupa ya takataka za kidunia, na kwa upande mwingine makubaliano ya watu wa dunia na mghafala, sio kwa sababu ya utukufu wao na ushujaa wao, lakini watu wa haki na ukweli wameshindwa kuhifadhi fadhila na ubora wanaoupata kutokana na kushikamana kwao na ukweli, hivyo wakashindwa kubakia na kuwa thabiti, kutokana na ushindani msafi na mbora katika njia ya haki, imepelekea kuachia fursa kwa wenye kujipenyeza kufanya hivyo katika uwanja huu, kwa maana hii wakawa wametia dosari sifa hii bora, na wakatumbukia kwenye dimbwi la khitilafu, kwa sababu ya husuda, ikapelekea kujidhuru wao wenyewe na kudhuru makundi ya Uislamu kwa ujumla wake.

          Ama watu wa upotofu na mghafiliko, kutokana na mapungufu yao ya murua na ajizi yao na udhalili wao, hakika wamenyoosha mikono yao na wakaungana na kufanya umoja wa kweli pamoja na watu wa aina yoyote ile, hata watu wa chini kabisa, kwa lengo tu la kutopoteza manufaa wanayoyakimbilia nyuma yake, wala hawawakasirishi marafiki na viongozi wao ambao wamekuwa wanafuata amri zao hadi kufikia kuwafanyia ibada kwa ajili yao. Hivyo wamekuwa wakishirikiana na kila yule ambae anakubaliana nao katika amri zao vizuri. Pia wakakusanyika na kila aliyekuwa anakusanyika kwa ajili ya manufaa kwa hali yoyote ile, ndiyo wakafikia malengo waliyokuwa wakiyakimbilia, kwa sababu ya hima na bidii katika masuala haya.

Enyi watu wa haki na ukweli! Enyi watu mliotiwa mtihani wa khitilafu! Hakika mmeipoteza ikhlasi katika wakati huu mzito, na wala hamkuzifanya radhi za Allah (s.w) kuwa ni lengo la harakati zenu, hivyo mkaandaa njia ya kuporomoka, na mkawaonjesha watu wa haki machungu ya udhalili na udhaifu. Tambueni hakika haifai kuwa na husuda wala ushindani wala ghera, katika mambo ya dini na akhera, hakika katika ukweli hakuna mambo haya, kwani chanzo cha husuda na ushindani ni vyenye kutokana na kuwepo mikono mingi kwenye jambo moja na kukusanyika macho mengi mahala pamoja, na kutamani matumbo mengi chakula kimoja, hivyo kugeuka mazungumzo na mashindano, kuwa ni ugomvi na husuda, na kama ilivyokuwa dunia finyu na ya mpito na wala haishibishi hamu za wanaadamu na mahitajio yao mengi, na kwamba watu wengi wanaangamia kwa jambo moja, hivyo matokeo yake ni kuporomoka ndani ya shimo la husuda na ushindani, ama akhera ni pana na kwa kila muumini ni pepo upana wake ni baina ya mbingu na dunia na masafa yake ni mwendo wa miaka mia tano

Swali muhimu lililokuja kutokea upande muhimu sana: Vipi akili zetu fupi za kidunia zitaweza kufahamu yaliyopokelewa kuwa, muumini atapewa pepo upana wake ni miaka mia tano? Jibu: Kama ilivyokuwa hapa duniani kila mtu ana dunia yake ya muda maalum, mhimili wake ni uhai wake anastarehe kwayo atakavyo kwa milango yake ya fahamu ya dhahiri na ndani, hata anaweza kusema kuwa jua ni taa yangu na nyota ni kandili (taa za chemli) kuwepo kwa viumbe wengine na vyenye roho hakuzuwii umiliki wake huu, bali wanaimarisha dunia yao maalum na kuipendezesha, kadhalika mambo yalivyo peponi, pamoja na tofauti kubwa, basi kila muumini ukiachilia mbali kuwa na bustani yake maalumu yenye jumla ya maelfu ya kasri na Hurul-ayni ana pepo maalumu yenye upana wa miaka mia tano katika pepo ya jumla, anastarehe kwayo starehe inayolingana na kudumu milele kwa vile milango yake ya fahamu inavyo funuka na kukunjuka kulingana na daraja ya kila muumini, kuwepo kwa wengine pamoja naye hakupunguzi chochote katika kuneemeka, kuburudika na kumiliki kwake bali huimarisha pepo yake maalumu iliyo pana na kuipamba. Naam, basi kama mwanaadamu anavyostarehe duniani kwa kinywa, sikio, jicho, na vionjo vyake vingine hisia zake zote kwa umbali wa saa moja anayotumia kwenye bustani, au umbali wa siku moja anayoitumia katika utalii, au katika mwendo wa mwezi kamili kwenye milki ya kifalme au kwenye mwaka mmoja katika umri wake akijichangamsha katika matembezi na msafara, vivyo hivyo huko peponi, milango ya fahamu ya  kuonja na kunusa katika ufalme huo wa kudumu milele katika masafa ya mwaka mmoja kiasi alichokuwa akistarehe hapa katika uhai huu wenye kutoweka kwenye saa moja kwenye bustani ya wimbo, na milango ya fahamu ya kuona na kusikia inastarehe katika ufalme huo wa kudumu milele uliyojaa mapambo kutoka mbali na kuelekea mbali ya maeneo yake katika safari ambayo kitambo chake ni miaka mia tano kwa starehe inayowiana na umilele wake anavyostarehe navyo duniani ikiwa pamoja na misafara, matembezi, na utalii anaotumia mwanaadamu mwaka mmoja, basi kila muumini atapata kulingana na daraja yake kutokana na matendo yake aliyotenda duniani na kulingana na uwiano na aina ya mema yake, hisia zake zitafunguka na milango yake ya fahamu itakunjuka, hisia na milango hiyo ya fahamu itastarehe huko peponi kulingana na kudumu kwake milele. (Mwandishi)

na kwa kila mmoja humo ni kupata Hurul-ayni na kasri elfu sabini, na hivyo huko hakuhitaji husuda wala ushindani, haya yanatuelekeza kwamba hakuna husuda wala ugomvi katika amali njema yenye kupelekea akhera, kwa maana hakuna haja ya ugomvi na husuda, na mwenye kufanya husuda huyo ni mwenye kujionyesha, kwa maana ni sawa na mwenye kutafuta ngawira za kidunia chini ya pazia la dini, na anatafuta manufaa kwa jina la amali njema, au ni mjinga hajui ni upi mwelekeo wa amali njema, wala hajatambua bado kwamba ikhlasi ndiyo roho ya amali njema na ndiyo msingi wake, anatuhumu upana wa rehema za Allah (s.w) kama kwamba sio pana, na anaanza kwa uhasidi na mashindano yaliyojaa ndani ya nafsi yake kwa aina ya uadui kwa waja wa Allah (s.w) na vipenzi vyake mawalii wake wema na wa kweli.

Hapa nitaonesha mfano mmoja wa tukio unaotilia mkazo ukweli huu; Kulikuwa na mmoja wa rafiki zetu waliopita alikuwa na uadui na mtu mmoja maalum, na aliposifiwa mtu huyo mbele yake kwenye kikao na kusemwa; Hakika huyu mtu mwema ni kipenzi cha Allah (s.w), hatukuona kwa kauli hii chochote cha shida kwa sifa aliyopewa adui wake, lakini mmoja wao alipomtaja “Hakika huyu ni mtu ana nguvu na ni shujaa” alikuja juu na kuvimba mishipa ya husuda na ghera, tukamwambia: “Ewe fulani hakika daraja ya mapenzi (uwalii) kwa Allah (s.w) na taqwa, ni katika daraja bora na kubwa akhera na wala havina kigezo, hauwi sawa mchanga na nyota. Sisi tumeshuhudia kutajwa daraja hii hakukushughulisha kabisa, lakini palipotajwa nguvu za misuli, ambazo hata ng’ombe na ushujaa wanaoumiliki simba vimetiribua uhasidi kwako”. Akajibu: “Hakika sote tumekuwa na malengo mamoja katika hii dunia, nguvu na ushujaa na mfano wake ni wasila zenye kutufikisha kwenye malengo ya kidunia, na kwa sababu ya haya ndiyo nimehisi ushindani na husuda, ama daraja ya akhera hakuna mipaka, na pengine aliyekuwa adui wangu duniani awe rafiki yangu mkubwa akhera”.

Enyi watu wa haki na njia! Hakika kuihudumikia haki siyo jambo jepesi, bali ni mfano wa kubeba hazina iliyo kubwa na nzito sana, na kuisimamia kuihifadhi, na wale ambao wanaoibeba mabegani mwao, wanatoa bishara njema kwa mikono ya wenye nguvu kuwataka msaada wao na wanaifurahia sana, ni wajibu kupokewa hao kwa mapenzi ya kweli, na kutazamwa nguvu zao na taathira zao na msaada wao zaidi kuliko nafsi zao, na kupokewa kwa fahari inayowastahikia, hakika hao ni ndugu wa kweli wakuheshimiwa waliojitolea. Na kama wajibu unawastahikia haya yote kwa nini watazamwe kama mahasidi, achilia mbali husuda na ghera, mpaka ikaharibika ikhlasi kwa sababu ya hali hii, na zikawa amali zenu majukumu yenu kwenye kapu la tuhuma la waovu, ikapelekea wao kukuekeni kwenye nafasi isiyo yenu, na wakakufananisheni na wenye kula dunia kupitia dini, na wakakusanya maisha yao kwenye pazia la elimu ya haki, na wakakufanyeni sawa na wenye kupigania na kuwa na pupa la takataka za dunia na mfano wa haya katika tuhuma za dhuluma.

Tiba pekee ya maradhi haya ni kuishutumu mtu nafsi yake, na kuelekea upande wa rafiki yake kwenye njia sahihi, na kutokwenda kinyume na misingi ya insafu na kutafuta haki, kama walivyo ridhia wanachuoni wa adabu na mijadala, ambayo imo ndani yake: “Anapotaka mtu kudhihirisha haki kwenye ulimi wake pasina mwingine kwenye mijadala, akafurahia hilo na akaridhika kuwa mwenzake yuko katika batili, huyo ni dhalimu hana insafu”, achilia kwamba ni mwenye kudhurika kwa matokeo hayo, kwani anakuwa hajajifunza kitu kipya kutokana na mjadala ule, kwa kudhihiri haki kwa ulimi wake, bali pengine inaweza kumpeleka kwenye ghururi na kudhurika, lakini laiti haki ingalidhihiri kupitia ulimi wa hasimu yake, asingelidhurika kwa lolote wala isingalimletea ghururi bali angalijifunza jambo jipya, hakika mwenye kutafuta haki mwenye insafu anaiporomosha nafsi yake kwa ajili ya haki, na anapoiona kwa hasimu yake anairidhia na anaifurahia.

Laiti watu wa dini na haki na tarika na elimu wangalifanya hili ni msingi mkuu, na dira yao katika maisha yao na amali zao hakika wangalifikia ikhlasi kwa idhini ya Allah (s.w) na wangalifanikiwa katika amali zao za akhera, na wangaliokoka kwa rehema za Allah (s.w) na fadhila zake dhidi ya msiba huu mkubwa uliowafika na kuwazunguka kila upande.

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيْمُ الْحَكِيْمُ

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.