Mng’ao Wa Ishirini Na Moja Unahusu ikhlasi

Mng’ao huu ulikuwa ni suala la nne katika maswala saba ya ukumbusho wa kumi na saba katika (mng’ao wa kumi na saba), isipokuwa umekuwa ni nukta ya pili, katika (mng’ao wa ishirini). Kulingana na maudhui yake – ikhlasi – na kwa msingi wa hali yake ya nuru umekuwa ni (Mng’ao wa ishirini na moja) ukaingia katika kitabu cha (Ming’ao).

[Mng’ao huu kwa uchache unasomwa kila siku kumi na tano]

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ

وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ Qur’an, 8:46.

وَقُومُواْ لِلّهِ قَانِتِينَ Qur’an, 2:238.

قَدْ أَفْلَحَ مَن زَكَّاهَا ۞ وَقَدْ خَابَ مَن دَسَّاهَا Qur’an, 91:9-10.

وَلاَ تَشْتَرُواْ بِآيَاتِي ثَمَناً قَلِيلاً Qur’an, 2:41

Enyi ndugu wa Akhera! Na enyi Sahiba zangu katika huduma ya Qur’an! Jueni – nanyi mnajua – kuwa ikhlasi katika matendo na hasa yale matendo ya kiakhera, ndio msingi muhimu, nguvu kuu kabisa, mwombezi mtarajiwa zaidi, ngome thabiti zaidi, njia fupi zaidi kwenda kwenye hakika, dua njema zaidi ya kimaanawi, njia tukufu zaidi ya makusudio, jambo la hadhi ya juu zaidi na uja ulio safi zaidi. Maadamu katika ikhlasi kuna nuru zenye kumulika, na nguvu madhubuti nyingi mfano wa sifa hizi maalum. Na maadamu hisani ya kiungu imeweka kwenye mabega yetu jukumu takatifu zito, na huduma ya jumla tukufu, ni jukumu la imani na huduma ya Qur’an, na sisi tuko katika upeo wa uchache udhaifu na ufakiri na tunawakabili maadui wagumu na dhiki kali, na zinatuzingira bidaa na mambo ya upotevu ambayo yanashambulia vikali katika enzi hizi ngumu, hatuna makimbilio isipokuwa kwa kujitolea kila tukiwezacho katika jitihada na nguvu ili tufanikiwe kwa ikhlasi. Sisi tunalazimika kuwa nayo. Bali tumekalifishwa hasa, na tunahitajia sana kuimarisha ikhlasi katika dhati zetu, kwa sababu ikiwa hatutafanikiwa kuipata yatatupotea baadhi ya tuliyoyachuma katika huduma takatifu – hadi sasa – na huduma yetu isingedumu wala kuendelea, kisha tutahesabiwa hesabu ngumu, ambapo tutakuwa katika ambao wanaojumuishwa na katazo la kiungu na hofisho lake kali katika kauli yake:

وَلاَ تَشْتَرُواْ بِآيَاتِي ثَمَناً قَلِيلاً

kwa kuwa tumenyongesha ikhlasi tukaharibu furaha ya milele kwa ajili ya tamaa duni za kidunia za kuchukiza zenye madhara zenye kutibua zisizo na manufaa wala faida yoyote, kwa ajili ya kuridhisha manufaa binafsi ya kisehemu yaliyo duni, mfano kuiajabia nafsi na ria. Na vilevile tunakuwa katika wale wenye kukiuka haki za ndugu zetu katika huduma hii na wenye kuchupa mwongozo wa huduma ya Qur’an. Na katika ambao wamekuwa na adabu mbaya hawakuheshimu utakatifu wa hakika za kiimani na hadhi yake ukweli wa kuziheshimu.

Basi enyi ndugu zangu! Hakika mambo muhimu ya kheri na njia tukufu za wema, zinapingwa na vizuizi na vipingamizi vingi vya kudhuru. Mashetani wanafanya bidii na kujitahidi wenyewe pamoja na wahudumu wa Da’wah hiyo takatifu, kwa hiyo inatakikana kuegemea kwenye ikhlasi na kutulia kwa hiyo ikhlasi ili kukinga vizuizi hivyo na kuwazuia hao Shetani. Basi epukeni – enyi ndugu zangu – sababu ambazo zinaharibu ikhlasi na kuitia ufa kama mnavyojiepusha na nge na nyoka. Hakuna kuiamini nafsi yenye kuamrisha wala kuitegemea katu, kama ilivyokuja katika Qur’an tukufu katika ulimi wa sayyidina Yusuf (a.s).

وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي إِنَّ النَّفْسَ لأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلاَّ مَا رَحِمَ رَبِّيَ Qur’an, 12:53.

ubinafsi usiwahadaeni kabisa na ghururi wala nafsi yenye kuamrisha maovu abadani.

Na ili kufikia katika kufanikiwa ikhlasi na kuihifadhi, na kukinga vizuizi na kuviondosha, jaalieni kanuni zifuatazo kuwa ni kiongozi chenu:

Kanuni yenu ya kwanza:

Kutafuta radhi za Allah (s.w) katika amali zenu. Akiridhia yeye (s.w), basi hakuna thamani kwa kukengeuka kwa ulimwengu wote na hakuna umuhimu wowote. Na kama akikubali yeye (s.w) hakuna taathira katika kukataa kwa watu wote. Yeye (s.w) akitaka na hekima yake ikalihitajia baada ya kuridhia na kuikubali amali, atawajaalia watu wanaikubali na kuiridhia, hata kama hamkuitaka nyinyi, kwa hiyo inapasa kujaalia radhi ya Allah (s.w) peke yake na sio kingine ndio kusudio la msingi katika huduma hii. Huduma ya imani na Qur’an.

Kanuni yenu ya pili:

Kutowakosoa ndugu zenu wanaofanya katika huduma hii ya Qur’an, na kutochochea hisia za husuda kwa kujifaharisha na kujikweza. Kwa sababu kama ilivyo hakuna kuhusudiana katika mwili wa mwanaadamu kati ya mikono miwili, wala hakuna kukosoana kati ya macho mawili, wala ulimi haulipingi sikio, wala moyo hauoni aibu ya roho, kila kimoja kati yao hukamilisha upungufu wa mwenziwe na kusitiri kasoro yake na kujitahidi kwa ajili ya kukidhi haja zake, na kusaidia katika huduma zake. Na kama sio hivyo uhai wa mwili huo ungezimika, na roho ingetoweka na mwili ungechanika. Na kama ilivyo hakuna husuda baina ya meno ya mashine na visanduku, wala hayatanguliani yenyewe kwa baadhi yake wala hayayadhibiti mengine wala kuyasukuma kwa kutofanya kazi kwa kukosoa na kujeruhi na kufuatilia aibu na kasoro, wala hayadhoofishi shauku yake ya kujitahidi, bali kila moja kati yao humsaidia mwenziwe kwa nguvu zote alizo nazo kwa kuelekeza harakati za meno na masanduku katika lengo lake linalotarajiwa, basi vyote huenda katika sababu iliyofanya vitu hivyo viwepo, kwa ushirikiano timamu na kuafikiana kikamilifu kwa namna ambayo kama kitaingilia kati kitu kigeni au kudhibiti jambo hilo – japo kwa kiasi cha atomu – kiwanda kingetetereka na kusibiwa na uharibifu na mwenye kiwanda kwa nafasi yake atatenganisha sehemu zake na kukiharibu kiwanda kwa ujumla kutokea kwenye msingi.

Basi enyi wanafunzi wa Risale-i Nur na enyi wahudumu wa Qur’an! Sisi sote ni sehemu na viungo katika haiba ya kimaanawi inayostahiki kupewa jina la: Mtu kamili. Na sisi sote ni sawa na meno na masanduku ya mashine inayofuma furaha ya milele katika maisha ya milele. Sisi ni wahudumu wafanya kazi katika jahazi ya kiungu inayokwenda na Umma wa Muhammad (s.a.w) katika ufukwe wa salama nao ni Dar es salaam (Makazi ya Amani).

Nasi kwa hiyo tuna haja kubwa mno bali tunalazimika kuungana na kushirikiana kiukamilifu na kufuzu kwa siri ya ikhlasi ambayo inaandaa nguvu ya kimaanawi kwa kiasi cha elfu moja mia moja na kumi na moja (1111) inayotokana na moja-moja nne. Ndiyo, kama hazijaungana (alifu) tatu zitabaki kuwa thamani yake ni tatu tu, ama zikiungana na kushirikiana kwa siri ya kihesabu, zitavuna thamani ya mia moja na kumi na moja (111), na hali ni vivyo hivyo katika nne (nne) zinapoandikwa kila (4) peke yake mbali na nyinginezo hakika jumla yake (16) ama nambari hizo zikiungana na kuafikiana kwa siri ya udugu na umoja wa lengo na jukumu moja katika msitari mmoja wakati huo zitavuna thamani ya elfu nne mia nne na arobaini na nne (4444) na nguvu yake. Kuna shuhuda na matukio ya kihistoria mengi sana yamethibitisha kwamba watu kumi na sita katika waliounga udugu, waliungana, waliojitolea mhanga kwa siri ya ikhlasi iliyotimia, nguvu yao ya kimaanawi na thamani yao inavuka watu elfu nne. Ama hekima ya siri hii ni kwamba kila mtu kati ya watu kumi walioafikiana kwa hakika anaweza kuona kwa msaada wa ndugu zake wengine na kusikia kwa masikio yao. Yaani hakika kila mmoja kati yao anakuwa na nguvu ya kimaanawi na thamani ambayo kana kwamba anaangalia kwa macho ishirini au anafikiri kwa akili kumi na anasikia kwa masikio ishirini na anafanya kwa mikono ishirini.

Naam, kama hakika kuegemeana kwa uhakika, na kuungana kikamilifu kunatokana na (ikhlasi), ni mhimili ambao manufaa yasiyokoma yanazunguka katika mhimili hio, Vile vile hilo ni shikizo kubwa, na nguzo yenye nguvu kwa ajili ya kisimamo kuelekea khofu nyingi, bali mbele ya umauti, kwa sababu umauti haupokonyi isipokuwa roho moja tu, Basi ambaye ameshikamana na ndugu zake kwa siri ya undugu wa ikhlasi katika mambo yanayoambatana na akhera na katika njia ya kuridhisha Allah (s.w), anabeba roho kwa idadi ya ndugu zake, basi anakutana na mauti hali ya kutabassam na kusema: Na zisalimike roho zangu nyingine na zibakie zenye kunusuriwa, hakika hizo zinanidumishia maisha ya kimaanawy kwa kuvuna kwake thawabu kwa ajili yangu daima. Basi mimi kwa hiyo sijafa. Na anasalimisha roho yake na hali ya kuwa mtulivu wa jicho, na ulimi wa hali yake inasema: Mimi ninaishi kwa roho hizo kwa upande wa thawabu wala sifi isipokuwa kwa upande wa dhambi na makosa. (Mtunzi)

Kanuni yenu ya tatu:

Jueni kwamba nguvu yenu nyote ipo kwenye ikhlasi na haki.

Naam, hakika nguvu iko kwenye haki na ikhlasi, hata watu wa batili wanapata nguvu kwa uthabiti na ikhlasi wanaoonyesha katika batili yao. Naam, hakika huduma yetu hii katika njia ya Imani na Qur’an yenyewe katika dhati yake ni dalili kuwa nguvu ipo katika haki na Ikhlasi. Basi kitu kidogo katika ikhlasi katika njia ya huduma hii kinathibitisha madai yetu haya na kinakuwa ni dalili juu yake. Hiyo ni: Kwa sababu yale tuliyoyafanya katika zaidi ya miaka ishirini katika mji wangu

Inakusudiwa mji wa (Van) kusini mashariki ya Uturuki.

na katika Istanbul miongoni mwa hudumu katika njia ya Dini na Elimu za Kisharia, tumefanya pamoja nanyi kwa maradufu zake mara mia moja hapa

Inakusudiwa kijiji cha (Barla) katika magharibi ya Uturuki alipelekwa uhamishoni huko mwaka 1926.

ndani ya miaka minane. Kwa kujua kwamba wale ambao walikuwa wananisaidia huko walikuwa wengi mara mia moja bali mara elfu kuliko wanaonisaidia mimi hapa. Hakika ya huduma zetu hapa katika miaka minane pamoja na kuwa mimi ni mpweke mgeni shabihi ya asiyejua kusoma

Inakusudiwa ubaya wa mwandiko.

na chini ya uangalizi wa maafisa wasio na insafu na katika kero zao zimetupatia kwa fadhila za Allah nguvu ya kimaanawi imedhihirisha taufiki na kufuzu kwa mara mia moja maradufu kuliko ilivyokuwa kipindi kilichotangulia, kwa ajili hiyo imetokea kwangu ukinaifu ulio timia kwamba taufiki hii ya kiungu sio kwa sababu nyingine isipokuwa ni kutokana na usafi wa ikhlasi yenu. Na mimi nakiri kwamba nyinyi mmeniokoa kwa ikhlasi yenu timamu – kwa kiasi fulani – kutokana na ria, huo ugonjwa mbaya ambao unauchezea nafsi chini ya pazia la umashuhuri na kuvuma. Tunamwomba Allah akupeni nyote taufiki katika ikhlasi kamili na mnivute mimi katika ikhlasi hiyo pamoja nanyi.

Mnajua kwamba Imamu ali (r.a) na sheikh Alkaylany (q.s) wameelekea kwenu na wametazama kwa jicho la upole, kutilia umuhimu na kuliwaza katika karama zao za ajabu, na wanazibariki huduma zenu kimaana. Isiwaingie shaka kwamba kuelekea huko na kugeuka huko na maliwazo hayo sio kwa sababu yoyote ila kwa kiasi mlicho nacho cha ikhlasi. Ikiwa mtaiharibu ikhlasi hii kwa makusudi, kwa hiyo mtastahiki makofi yao. Kumbukeni daima (Makofi ya upole na rehema) ambayo yapo katika (Mng’ao wa Kumi). Ikiwa mnataka wabakie hawa wabora wawili maustdhi na wasaidizi wa kimaanawi kwenu basi chukueni ikhlasi iliyotimia kwa kutekeleza kwenu aya tukufu:

وَيُؤْثِرُونَ عَلَى أَنفُسِهِمْ Qur’an, 59:9.

Yaani ni juu yenu kuwafadhilisha ndugu zenu kuliko nafsi zenu katika ngazi, vyeo, takrima na kuelekewa, hata katika manufaa ya kimaada ambayo nafsi inayafukuzia na kupata raha kwayo. Bali hata katika manufaa yale ambayo ni masafi yaliyotakata vyema kama kufundisha hakika za Imani kwa wengine msitazamie kadri muwezavyo kutimiza hilo kwa mikono yenu bali ridhieni na tulieni yatimie hayo kwa mikono ya wasio kuwa nyinyi ili isipenye kujistaajabia katika nafsi zenu. Na pengine itakuwa kwa mmoja wenu kutazamia kufuzu thawabu peke yake, akajitahidi kubainisha jambo muhimu katika imani yeye mwenyewe, na pamoja ya kuwa hili halina dhambi ndani yake wala madhara linaweza kutibua usafi wa ikhlasi kati yenu.

Kanuni yenu ya nne:

Ni kuona fahari hali ya kuwa wenye kushukuru kwa sifa za pekee za ndugu zenu. Na kuzisawiri katika nafsi zenu. Na kuhesabu fadhila zao katika dhati zenu.

Kuna istilahi zinazozunguka kati ya watu wa tasaufi mfano: (Al-fanaa fii Al Sheikh) (Al-fanaa Fii Al-rasuul) na mimi sio m-sufi, lakini (Al-fanaa Fii Al-Ikhwan) ni kanuni nzuri inawiana na maslaki yetu na njia yetu kwa utimilifu. Yaani atoweke kila mmoja ndani ya mwingine, yaani kila ndugu asahau hisia zake za kinafsi na aishi kifikra pamoja na sifa za ndugu zake na fadhila zao. Kwa kuwa msingi wa maslaki yetu ni (Undugu) kwa ajili ya Allah, na kwamba mahusiano yanayotuunganisha ni udugu wa kweli, na sio uhusiano wa baba na mtoto wala uhusiano wa shekh na muridi. Na ikilazimu basi ni uhusiano na mwalimu. Na maadamu maslaki yetu ni (Alkahliliyya) basi mashrabu yetu ni (Alkhullat). Na Alkhullat inahitajia rafiki mkweli, na rafiki mwenye kujitoa muhanga, na ndugu jasiri mwenye ghera. Na msingi mkuu wa huu ukhullat ni ikhlasi kamili. Basi mwenye kufanya upungufu katika hilo miongoni mwenu ameporomoka kutoka katika mnara wa juu wa ukhullat na huenda akaanguka katika bonde lenye kina kirefu, kwani hakuna mahali pa kati kati. Naam, hakika njia ni mbili, basi atakayetutenga sisi sasa hivi katika maslaki ya ikhlasi iliyo timamu – nayo ndio njia kuu ya Qur’an tukufu – huenda akawa katika ambao wanatumikia Ulahidi (Ukanaji Mungu), maadui wa Qur’an bila kutambua.

Basi ambao wameingia medani ya huduma ya Qur’an tukufu iliyo takatifu kupitia (Risale-i Nur) hawaporomoki kwa idhini ya Allah katika mfano wa lindi hilo, bali wataipa nguvu nuru ikhlasi na imani.

Enyi ndugu zangu katika kuhudumia Qur’an!

Hakika sababu kuu ya kuchuma ikhlasi na nyenzo kubwa kabisa yenye kuathiri ya kuihifadhi ni (Mafungamano ya umauti). Kama ilivyo urefu wa matumaini unaondoa makali ya ikhlasi na kuiharibu na kupelekea katika kuipenda Dunia na ria, basi hakika (Mafungamano ya umauti) yanaweka mbali ria, na kumfanya mwenye kufungamana nayo anafanikiwa kuipata ikhlasi. Kwani inamkomboa kutokana na vitimbi vya nafsi yenye kuamrisha maovu na hii ni kwa kukumbuka kifo chake na kwa kuzingatia kutoweka kwa dunia na kuondoka kwake. Na kwa hakika watu wa tasawuf na watu wa hakika ya kimatendo wamejifanyia (Mafungamano ya umauti) kuwa ni msingi katika njia ya mwenendo wao, na hii ni kwa kile walichojifunza kutoka katika aya tukufu

كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ Qur’an, 3:185.

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ Qur’an, 39:30.

Kwa mafungamano hayo wakaondoa dhana ya kubakia na njozi ya umilele ambayo inazalisha urefu wa matumaini ambapo wamezijaalia kwa mawazo ya kufikirika na wakaziletea taswira nafsi zao kuwa zimekufa. Basi hivi sasa wanaoshwa na sasa wanawekwa kwenye kaburi na wanapotafakari kwa sura hii nafsi yenye kuamrisha maovu inaathirika zaidi kwa mawazo haya yenye kufikirika kwa hiyo kidogo kidogo inaachana na matumaini yake mapana. Mafungamano haya kwa hiyo yana faida nyingi na manufaa mbalimbali. Na inatosha kwamba hadithi tukufu inatuongoza katika hilo kwa kauli yake: (Fanyeni wingi wa kumkumbuka mvunjae ladha).

Tirmidhy, sifa za kiama 26, zuhd 4; Al-nasai, al-janaiz 3; Ahmad bin Hanbal, Almusnadi 2/292.

Na kwa vile maslaki yetu ni hakika ya kielimu na sio tarika ya kisufi, hatuoni nafsi zetu kuwa zenye kulazimika kama wao katika kuvaana na mafungamano hayo kwa mawazo ya kufikirika. Ukiachilia mbali kwamba njia hii haiwiani na njia ya hakika. Kwani kutafakari hatima sio kwa kuuleta mustakabali kuja kipindi cha sasa kwa mawazo ya kufikirika, bali kwenda kifikra kutokea sasa hadi mustakabali, na kushuhudia mustakabali kupitia muda wa sasa uliopo kama ilivyo hakika, basi hapana haja ya mawazo ya kufikirika wala hailazimu kufanya hivyo. Kwani mwanadamu anaweza kushuhudia jeneza lake hali ya kuwa ni tunda lililobebwa juu ya mti wa umri wake mfupi, na anapojaribu kugeuza mtazamo wake kidogo haoni umauti wake peke yake, bali anaona vilevile umauti wa zama zake, mpaka anapotembea kwa macho yake zaidi ataona umauti wa dunia na kuteketea kwake, na hapo inafunguka njia ya ikhlasi kamili mbele yake.

Na sababu ya pili katika kufanikisha ikhlasi ni:

Mtu kuvuna uhadhiri na utulivu kwa imani ya uhakikisho na kwa ming’ao yenye kupatikana katika (Kutafakari kiimani katika viumbe). Kuchunguza huku kunampeleka mwenye kuwa nako katika kumtambua muumba (s.w); hapo humiminika utulivu katika moyo. Ni kweli kwamba kung’aa kwa aina hii ya kuchunguza katika fikira ya mwanadamu kunamfanya daima afikirie uhadhiri wa muumba mwingi wa rehema (s.w) na kumwona yeye, yaani yeye yupo hadhiri na anamtazama yeye daima; wakati huo basi hamgeukii mwingine na wala haombi kutoka kwa mwingine. Kwa kuwa kutazama na kumgeukia asiyekuwa yeye kunapotosha adabu ya kuwa hadhiri na utulivu wa moyo. Na kwa hivi mtu anaokoka na ria, na kuipata ikhlasi kwa idhini ya Allah (s.w).

Na kwa kila hali katika hili (mazingatio) kuna daraja nyingi na ngazi nyingi. Na fungu la kila mtu ni lile analovuna, na faida yake anayofaidika ni kutokana na ukubalifu wake na uwezo wako.

Tunatosheka kwa kiasi hiki na tunaelekeza katika Risale-i Nur ambapo imeeleza mengi katika hakika kuhusu kuokoka na ria na kufaulu ikhlasi.

Tutabainisha kwa muhtasari baadhi ya sababu nyingi ambazo zinaharibu ikhlasi na kuizuia na kuelekeza kwenye ria na kusukuma kuelekea huko.

Kizuizi cha kwanza cha ikhlasi

Hasadi inayotokana na manufaa ya kimaada. Hasadi hii huharibu ikhlasi hatua kwa hatua, bali inavuruga matokeo ya amali, bali inakosesha hata yale manufaa ya kimaada vilevile.

Naam, umma huu daima umebeba heshima na kuthamini kwa wanaotenda kwa bidii kwa ajili ya hakika na Akhera, na umewanyooshea mkono wa msaada kiukweli, na hii ni kwa nia ya kushirikiana nao katika amali na huduma za kweli za ikhlasi kwa ajili ya Allah (s.w). Ukawapa zawadi na sadaka ili kutekeleza haja zao za kimaada na ili wasishughulike nazo na kuwa mbali na huduma zao tukufu; Wakadhihirisha heshima waliyokuwa nayo kwa ajili ya watendaji katika njia ya Allah; isipokuwa misaada hii na manufaa hayapaswi kutafutwa katu, bali yatolewe hiba tu. Yasiombwe hata kwa ulimi wa hali kama vile yule anayeyangojea kimoyo. Bali yatolewe kwa namna isiyotegemewa na kama si hivyo ikhlasi ya mtu itaharibika na kutenguka, na anakaribia kuingia ndani ya makatazo ya kiungu katika kauli yake (s.w): 

وَلاَ تَشْتَرُواْ بِآيَاتِي ثَمَناً قَلِيلاً

na hivyo kudondosha sehemu ya amali yake. Basi kuyataka manufaa haya ya kimaada na kuyatazamia kwa msukumo unaotokana na ufadhilishaji wa nafsi yenye kuamrisha maovu na pupa yake ya kuvuna manufaa kwa ajili ya dhati yake, kunachochea mshipa wa husuda na kutikisa hisia zake mbele ya ndugu yake wa hakika na sahibu yake mwenye ikhlasi katika huduma ya kiimani, basi anaharibu ikhlasi yake na kupoteza utakatifu wa da’wa yake kwa Allah na kuchukua hatua yenye kukimbiza kwa watu wa hakika, bali anakosa manufaa ya kimaada vilevile. Na kwa kila hali basi suala hili ni refu.

Nitataja yanayozidisha siri ya ikhlasi na kudumisha maafikiano ya kweli kati ya ndugu zangu wa kweli. Nitaeleza ndani ya mifano miwili:

Mfano wa kwanza wa kudumisha ikhlasi:

Watu wa Dunia wamejifanyia (Kushirikiana katika mali) ni kanuni wanayoongozwa nayo kwa ajili ya kupata utajiri mkubwa au nguvu kubwa, bali wamejifanyia wale ambao wana taathira katika mambo ya kijamii – katika watu au makundi na baadhi ya wanasiasa – kanuni hii kuwa ni kiongozi wao. Na wamefanikiwa matokeo ya kufuata kwao kanuni hii nguvu kubwa na wakanufaika nayo manufaa makubwa, licha ya yaliyomo katika madhara na matumizi mabaya, na hii ni kwa sababu ainisho la kushirikiana halibadiliki kwa maovu na madhara yaliomo, kwa kuwa kila mtu – kwa mujibu wa kanuni hii – anajihesabu nafsi yake ni sawa na mmiliki wa mali yote. Na hii ni kwa upande wa ushiriki wake katika mali na usimamizi wake, japokuwa hawezi kunufaika na mali yote. Na kwa kila hali kanuni hii ikiingia katika amali za kiakhera itakuwa ni mhimili wa manufaa matukufu bila maovu wala madhara. Kwa sababu mali zote hizo za kiakhera zinabeba siri ya kuingia kwa utimilifu wake katika hozi ya kila mmoja miongoni mwa watu wale wenye kushirikiana katika hizo, bila ya upungufu wala kukatwa sehemu sehemu.

Na tufahamu hili kwa mfano:

Watu watano wameshirikiana katika kuwasha taa ya mafuta. Ikatokea kwa mmoja wao kuleta mafuta, na kwa mwingine kuleta utambi, na kwa wa tatu kuleta chupa, na kwa wa nne taa yenyewe, na kwa wa tano pakiti ya kibiriti. Basi walipowasha taa kila mmoja kati yao akawa ni mmiliki wa taa kamili. Ingekuwa kila mmoja kati ya wale walioshirikiana ana kioo kikubwa kilichotundikwa ukutani, basi taa kamili ingeakisi katika kioo chake – pamoja na yaliyo chumbani – bila ya kugawika vijisehemu wala kupungua.

Na vivyo hivyo katika kushirikiana katika mambo ya kiakhera kwa siri ya ikhlasi, na kushikamana kwa siri ya udugu, na kuunganisha jitihada kwa siri ya kujiunga pamoja; Ambapo jumla ya amali za washiriki na jumla ya nuru inayochomoza kutokana na amali hizo zitaingia kwa ukamilifu wake katika daftari la amali za kila mmoja miongoni mwao. Na hili ni jambo lenye kushuhudiwa na lenye uhalisia baina ya watu wa hakika. Nalo ni katika yanayohitajiwa na ukunjufu wa rehema ya Allah (s.w) na ukarimu wake wa hali zote.

Basi enyi ndugu zangu! Nataraji manufaa ya kimaada yasije kuwapeleka katika Husuda baina yenu Inshaallah (s.w). Isipokuwa mnaweza kuhadaika kama walivyo hadaika baadhi ya watu wa tarika za kisufi, katika mlango wa manufaa ya kiakhera. Iko wapi thawabu ya mtu binafsi na ya sehemu ndogo katika ile thawabu kubwa inayotokana na anga la kushirikiana katika amali zilizoelezwa kwenye mfano uliotangulia, na iko wapi nuru ya sehemu ndogo katika nuru ile yenye kuangaza.

Mfano wa pili wa kudumisha ikhlasi:

Watu wa viwanda na watu wa kazi mbali mbali hupata uzalishaji mwingi na utajiri mkubwa ikiwa ni matokeo ya wao kufuata kanuni ya (kushirikiana katika ufundi na umahiri) na huu hapa mfano:

Watu kumi katika watengenezaji wa sindano za kushonea walifanya kazi kila mmoja akiwa peke yake. Matokeo yakawa sindano tatu kwa kila mmoja kati yao kwa siku moja. Kisha watu hawa waliafikiana kwa mujibu wa kanuni ya (Kuunganisha jitihada na mgawanyo wa kazi) mmoja wao akaleta chuma na mwingine alileta moto na mwingine alishughulika na kutoboa sindano na mwingine kuiingiza kwenye moto na mwingine akaanza kuweka makali. Na kama hivi wakati wa mmoja wao haukuondoka bure, ambapo kila mmoja kati yao alijihusisha na kazi maalum na kuitimiza kwa haraka, kwa sababu kwanza ni kazi rahisi ya kijisehemu na pili kwa ajili ya kupata kwake uzoefu na umahiri katika kazi hiyo. Na walipogawana mavuno ya juhudi yao waliona kwamba fungu la kila mmoja kati yao katika siku moja ni sindano mia tatu badala ya sindano tatu. Tukio hili likawa ni wimbo wanaouimba watu wa viwanda na kazi, ambao wanaitia katika kuunganisha juhudi na mgawanyo wa kazi.

Basi enyi ndugu zangu! Maadam hupatikana mfano wa faida hizi kubwa zikiwa matokeo ya kuungana na kuafikiana katika mambo ya kidunia na katika maada rundo, basi vipi itakuwa thawabu ya matendo ya kiakhera na ya kinuru! Na vipi itakuwa thawabu inayojiakisi kutoka katika amali za kundi lote kwa fadhili ya kiungu katika kioo cha kila mmoja katika kundi hilo! Amali zile ambazo hazihitajii kuzikata mafungu wala kugawanyika. Basi ni juu yenu kukadiria faida hiyo kubwa. Hakika mfano wa faida hii kubwa haiachiliwi ipite kwa hasadi na kutokuwa na ikhlasi!

Kizuizi cha pili cha ikhlasi:

Kutoa kile ambacho u – mimi wa nafsi yenye kuamrisha maovu kinachezea na kutaka utukufu unaotoka katika daraja na hadhi, inayoelekewa na macho, na kupenda kukabiliwa na watu na kutafuta kuelekea kwao kwa msukumo unaotokana na kupenda umashuhuri na kutangazika sauti kunakotokana na kutazamia cheo na kukipenda. Basi kama ulivyokuwa huu ni ugonjwa mzito wa kiroho, ni mlango wa (Shiriki iliyojificha) ambayo ni ria na kuistaajabia nafsi kunakobomoa ikhlasi.

Enyi ndugu zangu! Maslaki yetu yalivyokuwa ni katika kuhudumia Qur’an tukufu yakijengwa juu ya hakika na udugu, na kwamba siri ya udugu ni katika kuitowesha mtu haiba yake ndani ya haiba ya ndugu zake

Naam, hakika ya mwenye kufaulu ni yule ambaye anayeitupa haiba yake, na kuyayusha ubinafsi wake ambao ni kama kipande cha barafu kwenye kauthari (mto wa pepo) wa Qur’an tukufu ili apate birika hilo. (Mtunzi).

na kuwatanguliza wao juu ya nafsi yake, haitakikani mfano wa husuda hii inayotokana na kupenda cheo kutuathiri, kwani jambo hilo linaenda kinyume kabisa na maslaki yetu. Kwa sababu maadamu karama na utukufu wa ndugu wote unarudi kwa kila ndugu katika kundi, basi haiyumkiniki kutolewa mhanga ngazi hiyo ya juu na karama ya juu na utukufu wa kimaanawi wa hadhi ya juu ya kundi zima, kwa ajili ya umashuhuri wa kijisehemu na utukufu wa kibinafsi unaotokana na u-mimi na husuda. Basi mimi nina mategemeo na ninatumai kwamba hilo lipo mbali kabisa kila umbali na wanafunzi wa Risale-i Nur.

Naam, hakika nyoyo za wanafunzi wa Nur na akili zao na roho zao haziporomoki katika mfano wa mambo haya ya chini, isipokuwa hakuna yeyote isipokuwa anabeba nafsi yenye kuamrisha maovu, yanaweza kupita mambo na hisia za kinafsi katika mishipa na kuambatana na neva na kupitisha maamuzi licha ya akili, moyo na roho. Basi kwa kutegemea kile ambacho (Risale-i Nur) inakiacha katika athari kwenu, basi siituhumu mioyo yenu, akili zenu na roho zenu. Isipokuwa nafsi, utashi, hisia na dhana huweza kuhadaiwa; kwa ajili hiyo inawajieni tahadhari na tanbihi mara nyingine kwa ukali na ugumu. Basi ukali huo unaelekezwa katika nafsi, matamanio, hisia na dhana, basi kuweni na tahadhari daima.

Naam, maslaki yetu ingekuwa ni tarika mahususi na usheikh, kwa hiyo ingekuwa makamo moja, au idadi ndogo kati yake, na katika makamo hayo wangekuwapo wafaao wengi kwa makamo hayo. Na wakati huo ingeyumkinika kutokea ushindani na U-mimi ndani ya nafsi. Lakini maslaki yetu ni udugu na si vinginevyo. Basi asidai ndugu ubaba kwa ndugu yake, na wala asijivike vazi la (Murshid) mwelekezi kwake. Hapa makamo katika udugu ni yenye uwanja mpana mkunjufu, hakuna nafasi ndani yake ya kusongana na kushindana, na ikiwa hapana budi ndugu ni msaidizi wa ndugu yake ni mkamilishaji wa kazi yake, na msaidizi wake.

  Na katika yanayojulisha kuwa katika maslaki ambazo zina ubaba na uelekezi na uustadhi kuna matokeo ya hatari yenye kuangamiza yanatokana na ushindani na hasadi kwa kupupia thawabu na kutazamia kunyanyuka kwa hima, nasema kuwa dalili ya hilo ni huko kuhitilafiana na magomvi yanayozunguka katikati ya sifa pambanuzi tukufu na manufaa makubwa ambayo wanavinjari nayo watu wa tarika za kisufi, na ambayo yamewapelekea katika matokeo mabaya zimekuwa nguvu zao za hadhi kubwa hazina uthabiti mbele ya vimbunga vya bidaa.

Kizuizi cha tatu cha ikhlasi:

Ni hofu na tamaa. Tunaelekeza katika risala ya (hujuma sita) .

Irejewe sehemu ya sita kutoka andiko la tisa katika mkusanyiko wa (Al-Maktubat).

Ambapo kumeshereheshwa kizuizi hiki pamoja na vizuizi vingine kwa uwazi kamili.

Tunamuomba Allah Ar-Rahman, Al-Rahiim aliyetakasika tukitaka shufaa kwa majina yote mazuri atuwafikishe kwenye ikhlasi iliyotimia. Amin.

اَلّلهُمَّ بِحَقِّ سُوْرَةُ الْإِخْلَاصِ اجْعَلْنَا مِنْ عِبَادِكَ الْمُخْلِصِيْنَ الْمُخْلَصِيْنَ. آمين.. آمين

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلُّمْتَنَا إِنَّكُ أَنْتَ الْعَلِيْمُ الْحَكِيْمُ Qur’an, 2:32.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.