Andiko la Kumi na tano Kutoka mwale wa kumi na saba

فَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ {Qur’an 99:7-8}

Aya hii inaonesha udhihirisho kamili mno wa jina tukufu la Al-hafiidh mlinzi na muhifadhi wa kila kitu. Kama unataka uthibitisho kuhusu ukweli huu wa Quran yenye hekima zote, tazama kurasa za kitabu cha ulimwengu, ambacho kimeandikwa katika mtindo wa kitabu kilicho wazi, utaona kiwango cha juu kabisa cha kudhihirisha jina tukufu la Al-hafiidh, na mambo mengi yenye kulingana na ukweli mkuu katika ulimwengu huu.

Kwa mfano, hebu chukua mbegu za miti mbali mbali kwa ujazo wa kiganja chako, maua, na mimea, halafu zika mbegu hizo, ambazo ni kama mifano midogo midogo ya maua tofauti, mti, mimea yote, vyote hivyo ni tofauti na aina mbali mbali, ndani ya giza la ardhi tupu isiyo na uhai, halafu mwagilia rasha rasha za maji yasiyo na uzito wowote, na yasiyoweza kupambanua chochote na kwenda popote unapoyamwagilia.

Sasa, hebu njoo kwenye majira ya machipuo, mandhari ya ufufuo kwa kila mwaka, tazama! Na chunguza kwa makini, wakati wa majira ya machipuo, wakati ambapo radi ambayo ni mfano wa malaika Israfiil anavyoita mvua kama vile anapuliza baragumu lake kwa sauti kubwa, akipasha habari njema ya pumzi ya maisha inayopuliziwa ndani ya mbegu zilizozikwa chini ya ardhi; utaona kwamba chini ya udhihirisho wa jina tukufu la Al-hafiidh, mbegu ambazo zinafanana na zote zikiwa zimechanganywa pamoja, zinaafikiana kikamilifu na bila makosa na amri ya uumbaji kutoka kwa Muumbaji Mwingi wa hekima, zinaafikiana sawa sawa kabisa kiasi kwamba katika kukua kwake, utambuzi wa wazi kabisa, uono wa ndani, madhumuni, utashi, ujuzi, ukamilifu, na busara vinakuwa dhahiri, kwani unaona kwamba mbegu hizo, ambazo zote zinafanana, zinajitenga na kujipambanua kutokana na wenzake.

Kwa mfano mbegu hii ndogo kabisa, imekuwa mtini, imeanza kueneza neema za Mwingi wa hekima Muumba juu ya vichwa vyetu, inazigawanya, na kuzieneza kwetu kwa mikono yake na mbegu hizi mbili ambazo kwa muonekano ziko sawa zimezaa maua yaitwayo maua ya jua na pansi yamejipamba kwa ajili yetu, yanatabasamu nyusoni mwetu, yanatufanya tuyapende, na aina hii ya mbegu imezaa matunda mazuri, ilikuwa miche, kisha matunda yenye kuchochea hamu yetu ya kula kwa ladha zake tamu, kunukia, na sampuli zake, yanajitoa muhanga kwa ajili ya wateja wake kiasi kwamba yanaweza kupanda kutoka katika kiwango cha maisha ya mmea na kuwa katika kiwango cha maisha ya mnyama, na kuendelea au unaweza kuleta mifano mingine zaidi kwa maana hii, mbegu zilizoendelea kwa namna hiyo ambapo gao moja tu limekuwa kama bustani iliyojazwa miti na maua mbalimbali, hakukupatikana kosa la aina yeyote kati yake, zinabainisha maana ya aya:

فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَى مِنْ فُطُورٍ {Qur’an 67:3}

Kupitia udhihirisho na kutangaza jina la Al-hafiidh, kila mbegu inatunza na kuonesha wasifu uliorithiwa kutokana na wazazi na asili yake, bila kuchanganya wala dosari yoyote.

Kwa hiyo, hii ni ishara ya hakika kabisa kwamba Mwenye kuhifadhi anatenda kazi za maajabu kama hizi ataonesha tangazo kuu juu ya uhifadhi wake katika ufufuo wa wafu na hukumu ya mwisho.

Naam, kudhihirisha uhifadhi ambao hauna makosa na kutokuwa na dosari kutokea katika kiwango kama hichi, hali ndogo mno ya mpito ya muda mfupi sana ni ushahidi wa kukinaisha, kwamba matendo, kazi, maneno, na amali njema na amali mbaya za mtu, matendo ya mshika amana na khalifa wa Allah (sw) Ardhini ambayo yana athari ya kudumu na umuhimu mkubwa yanahifadhiwa kwa muhtasari na yatakuja kuhesabiwa.

Hivi mwanadamu anadhani ataachwa kufanya atakavyo? Allah (sw) Apishe mbali! mwanadamu amewekewa hatima ya milele. na kwa ajili ya furaha ya kudumu na majonzi ya kuendelea ataitwa kwenye hisabu kwa matendo yake yote aliyoyafanya, dogo au kubwa mengi au machache atapokea ima thawabu au adhabu.

Kwa hiyo, ushahidi wa uhifadhi wa hali ya juu na ukweli wa aya iliyotajwa mwanzoni, ni mkubwa kuliko kiasi cha kuhesabika, hayo tuliyoyaonesha katika suala hili ni kama tone katika bahari, ni nukta moja ya vumbi katika mlima.

سُبْحَانَكَ لاَ عِلْمَ لَنَا اِلاَّ مَا عَلَّمْتَنَا اِنَّكَ اَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

Utakatifu ni Wako! hatuna ujuzi ila ule uliotufundisha, hakika Wewe ni Mjuzi wa kila kitu Mwingi wa hekima.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.