Muhtasari Wa Suala La Nane

Tulitaka katika (Suala la saba) kuulizia ufafanuzi wa suala la ufufuo katika ngazi nyingi, isipokuwa jibu la Muumba wetu kwa majina yake mazuri lilikuwa lenye kukidhi na kutosheleza sana limeleta yakini kabisa na kukinaisha kikamilifu likatutosheleza kiasi cha kutohitajia maelezo mengine yoyote. Huko tulichukua uthibitisho huo tu.

Ama katika Suala hili tutafupisha moja kati ya mamia ya matunda faida na tija zinazopatikana kwa (Kuamini Akhera). Kati yake ni ile inayohusu furaha ya mwanadamu Akhera na nyingine inahusu furaha yake duniani.

Ama ambayo furaha yake inahusu Akhera hakuna ufafanuzi mwingine baada ya ufafanuzi wa Qur’an, na ikarejewe hiyo Qur’an, ama inayohusu (Furaha ya dunia), Risale-i Nur inaifafanua, na hapa tutabainisha – kwa ufupi – baadhi ya natija tu baina ya mamia kati ya natija inayopatikana kwa (Kuamini Akhera) ili kumpa furaha mwanadamu katika maisha yake ya kibinafsi na kijamii.

Tunda la kwanza

Kama alivyo mwanadamu – tofauti na mnyama – ni mwenye mahusiano na nyumba yake, kadhalika ana mafungamano madhubuti na dunia. Na kama alivyo mwenye mafungamano na jamaa zake kwa mafungamano mbalimbali vilevile anayo nasaba ya kimaumbile na wanadamu wote. Na kama alivyo kwamba anapenda kubakia katika dunia ya kutoweka hakika anapenda sana kubakia katika nyumba yenye kubaki milele. Na kama anavyojitahidi daima kwa ajili ya usalama  wa tumbo lake katika chakula analazimika kwa maumbile yake – bali anajitahidi – kwa ajili ya usalama wa vyakula vya akili yake, moyo, roho yake na utu wake na kuvila katika meza pana upana wa dunia, bali yenye kuendelea hadi milele, kwa vile alivyo navyo miongoni mwa matarajio na mahitaji ambayo hayashibishwi ila na furaha ya milele. Niliyaambia mawazo yangu ya kufikirika enzi za utoto wangu: Unafadhilisha lipi kati ya mambo mawili? Kuishi umri wa furaha utakaodumu miaka elfu pamoja na ufalme wa dunia na utukufu wake kwa sharti kwamba mwisho wake uwe kutoweka kabisa, au kuishi katika uwepo wenye kubaki milele pamoja na maisha ya kawaida yenye taabu? Nikayaona yanataka (Maisha) ya pili na kukereka na ya kwanza kwa kusema: Hakika sipendi kutoweka bali kubakia japokuwa katika jahanamu!).

Maadam ladha zote za duniani hazishibishi mawazo ya kitaswira ambayo ni moja ya watumishi wa ainisho la mwanadamu, hapana budi kwamba hakika ya ainisho la mwanadamu lenye kujumuisha sana limefungamana kimaumbile na kubakia milele.

Kwa hiyo ni kiasi gani inakuwa (Kuamini na Akhera) ni hazina kubwa yenye kutosheleza na kukidhi kwa mwanadamu huyu ambaye ana mafungamano madhubuti na matakwa na matarajio haya yasiyoisha, naye hamiliki chochote isipokuwa sehemu ndogo ya Ikhtiyari al-Juz’iy (Sehemu ndogo sana ya hiari), na anagaagaa katika ufukara wa hali zote! na kiasi gani imani hii inakuwa ni mhimili wa furaha inayotafutwa na ladha inayotakiwa? na kiasi gani inakuwa ya kurejewa, mahali pa kupata msaada na maliwazo kwake mbele ya majonzi ya kidunia yasiyodhibitika? lau mtu huyu angejitolea uhai wake wote ili apate kufanikiwa matunda na faida hizi ingekuwa bado ni kitu kidogo sana!

Tunda la pili

Linaekea katika maisha binafsi ya mwanadamu

Hakika kinachomtia wasiwasi mwanadamu daima na kutibua maisha yake ni kufikiria kwake daima juu ya hatima yake, na namna atakavyoingia kaburini, kama ilivyomalizikia hatima ya wapendwa wake na jamaa zake. Basi dhana ya huyu mwanadamu masikini –ambaye anajitolea mhanga maisha yake kwa ajili ya rafiki mpenzi – na kujenga kwake picha kwamba maelfu bali mamilioni kwa mamilioni katika ndugu zake wanadamu wanaishia katika kutoweka nako ni umauti – huo utengano wa milele ambao hakuna kukutana baada yake – picha ya mawazoni ya namna hii itamuonjesha maumivu makali yenye kutabiri maumivu ya jahanamu. Wakati mwanadamu huyu akisumbuka na adhabu yenye kuumiza itokanayo na mawazo hayo, (Kuamini Akhera) kunakuja kufungua busara yake na kuondoa kifuniko kwenye macho yake kwa kumwambia: (Tazama) basi anaangalia kwa nuru ya imani, tahamaki anavuna ladha ya kina inayotabiri ladha ya pepo, kwa anayoshuhudia katika kuokoka kwa wapenzi wake na wote kukomboka na kifo cha moja kwa moja na kutoweka na kuoza na kupotea na kutokana na kubakia kwao milele katika ulimwengu wa nuru ya milele wakingojea ujio wake kwao. Tunafupisha kwa haya ambapo Risale-i Nur imeelezea natija hii pamoja na hoja zake.

Tunda la tatu

Lenye kuelekea katika mahusiano ya mwanadamu

Hakika makamo ya juu ya mwanadamu na kuwazidi kwake viumbe hai wengine na kupambanuka nao hakika ni kwa sababu ya sifa zake na maandalizi yake ya kimaumbile yenye kujumuisha, uja wake wa jumla, na kwa sababu ya upana wa maduara ya uwepo wake, kwa hiyo mwanadamu ambaye amejihusisha na muda wa sasa tu na kujivua na muda uliopita, wenye kukatwa mawasiliano na mustakabali – na hali ya kuwa zama hizo hazipo ni mfu na zenye giza kwa mujibu wa matazamo wake –  mwanadamu huyu anachuma tabia za murua, mapenzi na udugu wa kibinadamu kwa msingi wa muda wake wa sasa ulio finyu, na zinakuwa maalumu kwake kwa mujibu wa vipimo vyake vidogo, huelekeza mapenzi kwa baba yake, ndugu yake, mke wake au mama yake na huwahudumia kwa mujibu wa vipimo hivyo finyu kana kwamba yeye hawajui tangu hapo kabla na hatowaona huko mustakabali, hatapanda abadani katika ngazi ya ukweli katika utambuzi wa fadhila, wala nafasi ya ikhlasi katika urafiki, wala katika ngazi ya mapenzi yaliyotakasika na vyenye kutibua mapenzi, wala heshima iliyoepukana na lengo (binafsi); kwa sababu upana wa tabia hizo na makamilifu yake umepungua na kuwa mdogo kwa kiwango hicho hicho, na wakati huo mwanadamu anaporomoka katika ngazi ya chini ya mnyama duni kabisa kiakili.

Lakini (Kuamini Akhera) hakuji kwa mwanadamu huyu kwa ajili ya kumuokoa na kumpa msaada hadi inabadilisha muda huo finyu – ambao ni kama kaburi – kuwa muda mpana mkunjufu sana kiasi inajumuisha muda uliopita na mustakabali kwa pamoja na kumuonesha uwepo mpana kwa upana wa dunia, bali kwa wasaa unaotandawaa kutoka azali hadi milele. Na hapo mwanadamu huyu atafanya heshima kwa mazazi wake na kumtukuza kwa ukomo wa ubaba unaoendelea hadi katika nyumba ya furaha na ulimwengu wa roho – na atamsaidia ndugu yake – kwa tafakuri hiyo – kwa udugu unaoendelea hadi milele na atampenda mkewe na kusuhubiana naye na kumsaidia kwa sababu kwake yeye ni sahiba mzuri sana wa maisha hadi peponi, hafanyi duara hili pana la uhai – na huduma muhimu zilizomo – kuwa ni njia ya kuendea mambo duni ya kidunia wala malengo yake madogo madogo na manufaa yake duni. Hivyo hupata urafiki uliotimia, utambuzi safi wa fadhila na ikhlasi iliyotimia, katika mahusiano yake na huduma zake, na makamilifu na tabia zake njema zinaanza kupanda na kuwa juu kwa kiwango hicho hicho na utu wake unakuwa juu  na kila mmoja kwa mujibu wa daraja yake.

Mwanadamu huyo ambaye hakuwa mwenye kupanda katika ngazi ya kinega katika kuonja kwake maisha – sasa amekuwa – kwa fadhila ya kuamini Akhera – ni mgeni mheshimiwa duniani, kiumbe mwenye furaha, na kiumbe wa kipekee humo duniani anashika nafasi ya juu kuliko wanyama wote, bali anakuwa kiumbe mpendwa zaidi na mja aliyetukuzwa sana mbele ya mlezi na mfalme wa ulimwengu.

Tumetosheka na kiasi hiki katika kubainisha natija hii kwani Risale-i Nur imezibainisha kwa hoja na dalili mbali mbali.

Faida ya nne ambayo inaangalia katika maisha ya kijamii

Ni ile ambayo (Mwale wa tisa) umeibainisha na muhtasari wake ni: Kwamba (Watoto) ambao wanawakilisha robo ya wanadamu hawawezi kuishi maisha ya mwanadamu mnyoofu mwenye silka za kiutu ila kwa kuamini Akhera. Kwani bila ya imani hii wangelazimika kuishi maisha yaliyojaa ubaya, migongano na majonzi ya kuumiza. Hawapati raha wala maliwazo na michezo yao, kwa sababu umauti ambao unawasibu watoto wenzao wanao wazunguka unaathiri mno katika nafsi ya kila mtoto, na katika hisia zake ndogo laini, na katika moyo wake ambao kwenye mustakabali utakuwa na matarajio na matakwa yake mengi, na katika roho yake ambayo haiwezi kuhimili hivyo itasibiwa na wasiwasi na kutahayari, hata maisha yake na akili yake kuwa ni nyenzo za mateso kwake, michezo anayojisitiri ndani yake haimpi manufaa yoyote wala kuyapatia majibu maswali yake na tahayari yake, isipokuwa mwongozo wa imani ya (Kuamini Akhera) unamfanya kuisemesha nafsi yake kwa kusema:

“Hakika rafiki yangu – au ndugu yangu ambaye amefariki, hivi sasa amekuwa ndege katika ndege wa peponi, yeye ana maliwazo zaidi kuliko sisi na kufurahia matembezi huko peponi. Na hakika mama yangu – japo amefariki – ila yeye amekwenda katika rehema pana ya mwingi wa rehema na atanikumbatia tena katika kifua chake cha upendo mwingi huko peponi, basi namwona mzazi huyo mwenye huruma”. Na kwa hivi anaweza kuishi kwa utulivu maisha ambayo yanamstahiki mwanadamu.

Vilevile (Wazee) ambao wanawakilisha robo ya wanadamu, hakika wao hawapati maliwazo kwa kuzimika kwa maisha yao hivi karibuni, na kuingia kwao chini ya udongo, hali ya kuwa dunia nzuri tamu imeshafunga milango yake mbele yao isipokuwa kwa (Kuamini Akhera). Kwani bila ya imani hii wazazi hao wenye kuheshimiwa wenye huruma, na kina mama hao wenye kujitolea muhanga, wenye huruma nyingi wangeteseka na balaa baada ya balaa, na wangekuwa katika hali ya kinafsi dhalili mno na katika wasiwasi mzito wa moyo, na dunia ingekuwa finyu kwao kama jela, na maisha yenyewe yangekuwa ni adhabu ya kudumu isiyowezekana.

Wakati ambapo imani ya Akhera inawanong’oneza kwa kusema: “Wazee msihuzunike na wala msijali sana, kwani mnao ujana wa kudumu milele na hapana budi ujana huo utakuja na kwamba maisha angavu ya furaha na umri mrefu wenye kuendelea milele unakungojeeni, na mtakutana na watoto zenu na ndugu zenu ambao mmewakosa, na mema yenu yote yamehifadhiwa na mtachukua thawabu zake.” na kama hivi (Imani ya Akhera) inatoa maliwazo na furaha kwao, kwa namna ambayo kama mmoja wao atabebeshwa mizigo ya uzee mara mia moja angeubeba kwa kustahamili na kwa kusubiri akingojea yatakayofuatia katika maisha ya kiakhera yenye furaha.

Na kadhalika (Vijana) ambao wanawakilisha theluthi ya wanadamu, huenda wasisikilize sauti ya akili zao za uthubutu. Matakwa yao na matamanio yao yanachemka, nao ni wenye kuzidiwa na hisia na mihemko yao, vijana hawa wakiikosa (Imani ya Akhera) na kama hawakukumbuka adhabu ya jahanamu, hakika mali, heshima za watu na raha za wanyonge, na heshima ya wazee vinakuwa kwenye hatari, kwani huenda mmoja wao anaweza kuharibu furaha ya nyumba yenye amani na starehe kwa ajili ya ladha wa kupita, na kwa hivyo akaonja matokeo ya ubaya wa jambo lake – adhabu ya miaka mingi katika jela kama hizi na kuporomoka na kuwa kama mnyama wa mwitu.

Lakini ikiwa (Imani ya Akhera) itampa msaada basi ni haraka sana anarejesha akili yake na kuiambia nafsi yake kwa kusema:

“Licha ya polisi wa serikali na wapelelezi wake hawawezi kuniona kwa kuwa niko kwenye kificho hakika malaika wa mfalme mkuu mwenye utukufu ambaye anamiliki jela ya jahanamu ni ile jela kuu ya kudumu wananisajilia maovu yangu, kwa hiyo mimi siko huru mwenye kuachiliwa kamba, bali mimi ni mgeni anayepita mwenye jukumu, na nitakuwa – hakuna namna – katika siku fulani dhaifu na mzee kama wao”. Yatajitokeza matone ya rehema, upole na huruma – wakati huo – kutoka katika kina cha moyo wake na atahisi kuwaheshimu wale ambao aliotaka kukiuka haki zao kwa udhalimu. Na kwa kuwa Risale-i Nur imefafanua maana hii tunafupisha kwa kiasi hiki.

Na kadhalika (Wagonjwa na wenye kudhulumiwa na wenye misiba mithili yetu na mafukara na wafungwa) ambao wamehukumiwa adhabu kali, wote hao wanawakilisha sehemu muhimu sana ya wanadamu, kama (Kuamini Akhera) hakukuwasaidia na kama hawakuliwazika nayo basi kifo wanachokiona mbele yao daima kutokana na maradhi waliyonayo, na hakika udhalilishaji ambao wanauona kutoka kwa madhalimu – bila ya kuweza kuwalipizia kisasi wala kuokoa heshima yao kutoka katika makucha yao – hakika kukata tamaa kuchungu kunakotokana na upotevu  na  majanga yaliyosibu mali na watoto wao, na hakika dhiki kali inayotokana na maumivu na mateso ya jela kwa miaka mingi matokeo ya ladha fupi kabisa haimalizi  dakika au saa kadhaa, yote hayo yaifanya dunia – bila shaka – kuwa ni jela kubwa kwa hawa waliofikwa na majanga na kufanya maisha yenyewe ni adhabu iumizayo kwao!

Lakini imani ya Akhera haiwapi msaada wa pole na maliwazo ila haraka wanakunjuka nyoyo zao na wanavuta pumzi wakiwa na faraja kutokana na dhiki, kukata tamaa, wasiwasi, babaiko na usongo wa kisasi inayowaondolea kwa ujumla au kiasi kidogo kila mmoja kulingana na ngazi za imani yake.

Hata inayumkinika kwangu kusema: Kwamba isingekuwa imani ya Akhera ambayo imenipa mimi na ndugu zangu katika msiba wetu wakutisha na huku kuingia kwetu jela – pasipo na dhambi yoyote tuliyoitenda – ingekuwa kuhimili uchungu wa siku moja katika siku za mateso ni kama umauti wenyewe, na msiba huu ungetusukuma katika kuacha maisha na kuyasusa. Lakini shukrani kwa Allah (s.w) – bila idadi wala mpaka – kwa kunifanya kustahamili maumivu mengi kutokana na ndugu zangu ambao ni wapenzi zaidi kwangu kuliko nafsi yangu na kustahamili upotevu wa maelfu ya Risale-i Nur ambayo ni tukufu zaidi kuliko macho yangu, na ninastahamili kukosa vingi katika vitabu vikubwa vya  kupendeza vyenye thamani na ninastahamili huzuni na majonzi yote haya kwa imani hiyo ya Akhera, licha ya kuwa nisingeweza kustahamili idhilali yoyote na kushinikizwa na yeyote vyovyote awavyo, basi mimi nina kuapieni – mpate kutulia – hakika nuru ya imani ya Akhera na nguvu yake vimenipa subira, ushupavu kupozwa, liwazo, ugumu na shauku ya kufuzu thawabu ya jihadi kubwa katika mtihani huu kwa kiasi kwamba nina hesabu nafsi yangu kuwa katika madarasa yote ni kheri tupu na uzuri. Ni haki kuitwa (Madrasa ya Yusuf) kama nilivyolieleza hilo mwanzoni mwa risala hii na lau isingekuwa maradhi ambayo yalikuwa yakinisumbua wakati mwingine na kama si shida za ukongwe ningefanya jitihada zaidi ili nipate masomo yangu kwenye madrasa hii pamoja na utulivu wa moyo nilio nao. Kwa hali zote tumetoka kwenye maudhui nataraji masamaha kwa nyongeza hii.

Kadhalika hakika (Nyumba ya kila mwanadamu) ni dunia yake ndogo bali ni pepo yake ndogo, kama haikuwa (Imani ya Akhera) mwamuzi na mtawala wa furaha ya nyumba hii, kila mmoja katika watu wa nyumba hiyo mgogoro wenye kuumiza, na mateso makali katika mahusiano ya wao kwa wao kwa kiwango cha ngazi za upole wake na mapenzi yake kwao, basi itageuka pepo hiyo na kuwa ni jahimu isiyowezekana, na anaweza kuilewesha akili yake kwa pumbao na usafihi wa muda mfupi, katika hili anakuwa mithili yake ni mithili ya mbuni anapomwona mwindaji huficha kichwa chake mchangani ili yule mwindaji asimuone na hali ya kuwa anashindwa kukimbia na kuruka, naye vilevile anazamisha kichwa chake katika ghafla ili umauti kutoweka na utengano visimwone, akipuuza utambuzi wake kwa muda kwa upumbavu na kana kwamba amepata tiba ya kinachomsumbua!

Kwa mfano mama – ambaye anajitolea mhanga kwa ajili ya mwanawe – kila anapoona mwanawe anaingia katika hatari hutetemeka kwa kumhuzunikia na kumhofia mwanawe. Na watoto kadhalika pale wanaposhindwa kuwaokoa wazazi wao na ndugu zao kutoka katika misiba isiyokatika, huwa kwenye wasiwasi ya kudumu na wanahisi hofu ya kuendelea. Kwa kupimia hili basi maisha ya familia ambayo yanadhaniwa kuwa ni maisha ya furaha, hukosa furaha yake katika dunia hii yenye migogoro yenye kutoweka ambapo haitoi mafungamano kati ya watu, wala uhusiano wa undugu kati yao – ndani ya maisha mafupi sana – urafiki wa hakika, utambuzi wa fadhila wa dhati na ikhlasi kamili, na huduma na mapenzi yalio safi, bali tabia zina kuwa ndogo na kusinyaa kwa kulingana na ufupi wa uhai wenyewe na pengine hudondoka na kukosekana jumla.

Lakini Imani ya (Kuamini Akhera) haiingii katika nyumba hiyo hata inanawirisha maeneo yake moja kwa moja na kuangaza, kwa sababu uhusiano wa undugu, upole na mapenzi ambayo yanawafunganisha wakati huo hayapimwi ndani ya muda mfupi sana, bali hupimwa kulingana na mahusiano yanayoendelea hadi katika kubaki na kudumu kwao mlele huko Akhera na furaha ya milele – wakati huo – kila mmoja atafanya heshima ya dhati kwa wengine na kuwaelekezea mahaba safi na kudhihirisha upole wa kweli na kuonesha urafiki mwema, bila ya kuangalia mapungufu. Hapo tabia hupanda na kuwa juu na furaha ya kibinadamu ya kweli inaanza kustawi katika nyumba hiyo.

Madhumuni haya yamebainishwa katika Risale-i Nur hapa tumetosheka kwa yaliyotangulia.

Na kadhalika kila (Mji) kwa dhati yake ni nyumba pana kwa wakazi wake. (Imani ya Akhera) isipokuwa ni yenye kutawalia watu wa familia hii kubwa, itawatawalia chuki, manufaa binafsi, hila, ubinafsi, kujikalifu, ria, rushwa na hadaa badala ya misingi ya tabia njema ambazo ni ikhlasi, murua, fadhila, mahaba, kujitolea muhanga na radhi ya Allah (s.w) na thawabu Akhera. Na maana za ugaidi na fujo na ushenzi ni vyenye kutawala na kuendesha chini ya jina la mfumo,  usalama, na ubinadamu ambayo wanayadhihirisha, na wakati huo maisha ya mji huo yanashika alama na watoto wanasifika kwa ubaya na uzembe na vijana wanasifika kwa ulevi na uhuni na wenye nguvu watasifika na dhuluma na ukiukaji na wazee watasifika kwa kilio na manung’uniko.

Na kwa kulinganishia hili (Miji) kwa ukamilifu wake si kingine bali ni nyumba pana sana. Na taifa ni nyumba ya familia ya umma. Kama (Imani ya Akhera) ikitawalia katika nyumba hizi, fadhila hufunuka na kuwa wazi, na heshima ya kubadilishana itadhihiri na huruma ya kweli, na mahaba ya dhati bila badala, na kusaidiana pamoja na huduma ya kweli bila hila, na kutangamana na hisani bila ya ria, na fadhila na heshima bila ya kiburi, na fadhila nyengine zitaenea ambapo Imani ya Akhera itanong’ona kwa watoto kwa kuwaambia: “Acheni ubaya na uzembe kwa sababu mbele yenu kuna pepo yenye neema basi msijishughulishe nafsi zenu mbali na hiyo kwa michezo”. Inamakinisha tabia kwao kwa mwongozo wa Qur’an tukufu.

Na inawasemesha vijana kwamba: “Mbele yenu kuna moto wa jahanamu komeni ulevi na uhuni”. Na kuwafanya wazinduke na kumsemesha dhalimu: “Tahadhari hakika adhabu kali itakuthibitikia” hapo humkomesha na udhalimu na kumfanya kutosheka na uadilifu, na kuwasemesha wazee: “Furahini kwani mbele yenu kuna ujana wa kudumu wenye mng’ao, na furaha ya akhera ya daima yenye kubaki inawangojeeni ni ya thamani zaidi kuliko mlizozikosa katika aina za furaha na ni ya juu zaidi kuliko hizo basi njooni mjitahidi kupata mafanikio hayo”. Hapo hugeuza kilio chao kuwa ni sherehe na furaha.

Kulinganishia hili (Imani ya Akhera) inabainisha taathira yake nzuri na kutuma mionzi ya nuru yake katika kila kundi, sehemu yake na jumla yake, enevu yake na mahsusi yake, chache yake na nyingi yake.

Na wasikilize kwa makini Wataalamu wa elimu jamii na wa tabia miongoni mwa wadau wa mambo ya mwanadamu!

Yakilinganishwa tuliyoyataja huko nyuma katika faida za kuamini Akhera itafahamika wazi na kwa namna ya kukinaisha kwamba mhimili wa furaha katika makazi mawili na katika maisha yote hayo mawili si vyovyote isipokuwa ni Imani peke yake.

Hakika yamekuja katika (Neno la ishirini na nane) na katika Risale-i Nur nyingine majibu yenye nguvu mno kujibu utata wa kipuuzi kuhusu: (Ufufuo wa kimwili), (Kufufuliwa mwili) tunatosheka nayo ila hapa tutaashiria kwa ufupi sana: Hivyo tunasema:

Mengi ya majina mzuri ya kiungu yanadhihirika katika hali ya kimwili ni kioo chake jumuishi zaidi, na kwamba makusudio ya mbali ya kiungu katika kuumba viumbe yanadhihirika katika hali ya kimwili, ni kituo tajiri mno cha makusudio na yenye kutenda kazi zaidi, na kwamba nyingi ya aina mbali mbali za hisani za Mola mlezi na neema zake enevu hubainika katika hali ya kimwili, na kwamba aghalabu ya mbegu za dua anazoziomba mwanadamu kwa ulimi wa haja zake, na misingi mingi ya shukurani na himidi zinazopelekwa kutoka kwake na kwenda kwa Muumba wake Mwenye kurehemu zinatokana na hali ya kimwili, na kokwa zenye kuzidia zaidi kuwa katika aina mbalimbali  katika ulimwengu wa kimaanawy na kiroho pia zimo katika hali ya kimwili.

Basi kwa kupimia hili: Hakika hali ya kimwili ina misingi inajikita ndani yake mamia ya hakika za jumla, kwa hiyo Muumba Mkarimu hukithirisha na kuongezea hali ya kimwili katika uso wa dunia ili hakika hizo zilizoelezwa zipate kudhihiri, hutunuku viumbe uwepo kwa kasi mno na kwa nguvu ya ajabu, msafara baada ya msafara ikivituma katika huu ulimwengu wa maonesho, kisha hukomesha huduma zake na baada yake hutuma viumbe wengine kwa mfululizo. Na kama hivi anajaalia mashine ya viumbe katika kazi na shughuli ya kudumu, ikifuma mazao ya kimwili juu ya ardhi ikijaalia ardhi kuwa ni shamba la Akhera na kitalu cha pepo hata Allah (s.w) ili kulituliza tumbo la mwanadamu la (kimwili) na kulifanya kuwa katika shukurani na kuridhia husikia dua lake inaloliomba kwa ulimi wa hali kwa ajili ya kubaki kwake na anaijibu kwa hakika, kwa vyakula anavyoumba visivyojulikana idadi, vitamu na vimetengenezwa vyema, na kwa kufanya neema za thamani sana ziwepo kwa mamia ya maelfu ya sampuli, jambo ambalo lina dhihirisha kwa uwazi na bila shaka kwamba aghalabu ya aina za ladha za kimaada zenye kuhisiwa peponi hakika ni za kimwili. Na kwamba neema kuu ya furaha ya milele wanayoitafuta viumbe wote na kuliwazika nazo ni za kimwili pia.

Je, inayumkinika na kuingia akilini na je, upo uwezekano katu Mweza wa kila kitu Mwenye kurehemu mjuzi wa kila kitu mkarimu kukubali daima dua ya ulimi wa hali wa tumbo rahisi kwa ajili ya kubakia kwake, na kuliitikia kwa kusudio na kimatendo hasa – bila ya kuingia kwa sadifu – kwa vyakula vya kimaada vyenye kuhisika anavyoliumbia katika ukomo wa ufundi na muujiza kwa kufanya hivyo huliridhisha tumbo, kisha Allah (s.w) asikubali dua za jumla na dua zisizo kuwa na ukomo ambazo huombwa na tumbo kubwa la wanadamu na maumbile yake ya asili, na asiwape ladha tele za kimwili huko Akhera zile ambazo kimaumbile wanaliwazika nayo bali wanaitarajia katika maisha ya umilele? na je inayumkinika asijibu maombi hayo kimatendo na asitekeleze ufufuo wa kimwili?! na asimridhishe mwanadamu huyu – ambaye ni natija ya viumbe na khalifa wa Ardhi na mja aliyetukuzwa na kupewa heshima sana – kuridhika kwa milele? Kamwe kisha kamwe! Hili ni muhali katika muhali mia moja bali ni batili kijumla kwani ni vipi asikie king’ong’o cha nzi wala asisikie radi za mbingu na vipi atachunga maandalizi ya askari wa kawaida wala asijali jeshi kubwa! basi ametakasika Allah (s.w) na hayo kutakasika kukubwa.

Naam, hakika uwazi unaokinaisha wa aya tukufu:

وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ Qur’an, 43:71.

unabainisha kwamba zaidi ya anacholiwazika nacho mwanadamu katika tamu za kimaada zenye kuhisika – na ambazo huonjwa mifano yake duniani –  ataviona na kuvionja kwa sura yake inayolingana na hali ya peponi. Na kwamba thawabu ya yanayofanywa na ulimi, jicho, sikio, na viungo vingine katika shukurani ya dhati na ibada za dhati zitatunukiwa ladha hizo za kimwili zinazohusiana nazo. Basi ufafanuzi wa Qur’an tukufu kwa ladha za kimwili ni wazi upeo wa uwazi kiasi haiwezi kuchukua taawili (Tafsiri ya undani) yoyote inayogeuza kutoka katika maana ya dhahiri, bali inakataa kutokukubali maana ya kiudhahiri.

Na kama hivi matunda ya imani ya Akhera na natija zake yanadhihirisha kwamba mfano wa namna inavyojulisha hakika ya tumbo la mwanadamu na mahitaji yake ujulisho wa kukinaisha juu ya kuwepo kwa vyakula, basi hakika ya mwanadamu na makamilifu yake na haja zake za kimaumbile na matarajio yake ya milele na hakika zake na maandalizi yake vinahitajia natija na faida zilizotajwa za kuamini Akhera, na vinajulisha kwa kukinaisha juu ya Akhera, pepo na ladha zake za kimaada na kuhisiwa na kubakia milele, na vinashuhudia kuthibiti kwake. Na kwamba hakika ya makamilifu ya huu ulimwengu  na aya zake za kimaumbile zenye hekima na hakika zake zote zilizofungamana na hakika za kiutu zinajulisha kwa kukinaisha pia juu ya kuwepo kwa Akhera na juu ya kuthibiti kwake na kushuhudia ushahidi wa ukweli juu ya ujio wa ufufuo na kufunguka kwa milango ya pepo na moto. Na kwa kuwa Risale-i Nur imelithibitisha suala hili kwa namna ya kupendeza na kwa hoja zenye nguvu mno bila ya kubakisha vumbi la utata na hasa (Neno la kumi) na la (Ishirini na nane) – pamoja na vituo vyake viwili – na la (Ishirini na tisa) na (Mwale wa tisa) na (Risalat al-Munajaat) kwa hiyo tutatosheka nayo.

Hakika ya ufafanuzi wa Qur’an tukufu katika yahusuyo jahanamu uko wazi mno haukuacha nafasi ya ufafanuzi mwingine wowote, ila tutabainisha kwa muhtasari sana yanayotoa baadhi ya utata duni katika nukta mbili, tukielekeza maelezo yake katika Risale-i Nur:

Nukta ya kwanza

Hakika kufikiria na kuhofia jahanamu hakuondoshi ladha ya matunda ya imani yaliyotajwa, kwa kuwa rehema ya Mola mlezi iliyo kunjufu humnong’oneza huyo mwenye kuhofia: “Njoo kwangu chini yako kuna mlango wa toba ingia kupitia mlango huo”. Hakika kuwepo kwa jahanamu sio kwa ajili ya kutisha bali ni kwa ajili ya kukujulisha ladha za pepo kwa maarifa kamili na ili kukuonjesha hiyo pepo kikamilifu na kukulipizia kisasi wewe na kwa viumbe wasio na mpaka katika waliovunja haki za wote na kuzikiuka, na ili kuwafurahisha hao wote kwa hili na kuingiza furaha kwao.

Basi ewe mwenye kuzama katika upotevu – na asiyeweza kutoka humo – kuwepo kwa jahanamu ni bora zaidi kwako kuliko kutokuwepo milele kwani katika kuwepo kwake kuna aina ya rehema hata kwa makafiri wenyewe, kwa sababu mwanadamu – na wanyama wenye kuzaliwa – hustarehe kwa kustarehe kwa ndugu zake na wanawe na wapenzi wake na kufurahika – kwa upande fulani – kwa furaha yao. Basi ewe kafiri! Ima wewe utaanguka kwenye shimo la kutokuwepo – kwa kuzingatia upotevu wako – au utauingia moto wa jahanamu. Na ilivyo kuwa kutokuwepo ni shari tupu kwa hivyo kunyongwa moja kwa moja kwa wapendwa wako wote na wale unaofurahi kwa kufurahi kwao katika ndugu, wazazi na kizazi chako, kutaunguza roho yako na kuuadhibu moyo wako na kuiumiza hakika yako ya utu zaidi kuliko adhabu ya jahanamu kwa mara elfu, kwa sababu kama kusinge kuwapo jahanamu, basi na hata pepo isingekuwapo vilevile, kila kitu kwa hiyo kinadondoka kwa ukafiri wako kwenda katika kutokuwepo. Lakini ukiingia jahanamu na ukabaki ndani ya uwepo hakika wapenzi wako na ndugu zako ima watapata raha peponi au watakuwa ndani ya duara za uwepo chini ya rehema za Allah (s.w). Basi huna pa kukimbilia ila ukubali uwepo wa jahanamu kwani uadui dhidi ya uwepo wake – na kuikataa – yaani ni kujitenga katika kukosekana kutupu, ambako ni kuteketeza furaha ya wapenzi wote na marafiki na kuwafanya watoweke!

Naam, hakika jahanamu ni makazi ya uwepo inatekeleza jukumu la mahakama ya Mwingi wa Hekima Mtukufu na uadilifu wake, na ni mahali pa kutisha mno ndani ya duara la uwepo ambao ni kheri tupu, zidisha juu ya hilo, ina majukumu mengine na huduma tukufu na hekima tofauti zinazohusu ulimwengu wa kubakia. Hayo ni makazi yenye utukufu na haiba kwa wengi ya wenye uhai mfano wa malaika wa adhabu.

Nukta ya pili

Hakika ya kuwepo kwa jahanamu na adhabu yake kali hakupingani – kabisa – na rehema isiyokuwa na mpaka wala uadilifu wa hakika, wala hekima yenye kipimo ambayo haina israfu ndani yake, bali hakika ya rehema, uadilifu na hekima vinataka uwepo wa jahanamu na vinauhitajia, kwa sababu kumuua mnyama aliyeshambulia wanyama mia moja au kuteremsha adhabu kwa dhalimu ambaye amevunja heshima za elfu moja ya watu wasio na hatia, ni huruma kwa mara elfu maradufu kwa waliodhulumiwa kupitia uadilifu. Na hakika ya kumsamehe dhalimu huyo kutokana na adhabu au kumuachia na kumwacha yule mnyama mwitu akiwa huru kuna dhuluma mbaya na kutokuwa na huruma kwa mamia ya masikini kwa mamia ya maradufu, mkabala na huruma isiyokuwa mahali pake. Na mfano wa hili pia kafiri kabisa – ambaye anaingia jela ya jahanamu – kwani yeye kwa ukafiri wake anakanusha haki za majina ya kiungu yaliyo mazuri, yaani anazikiuka haki hizo na kwa kukadhibisha kwake ushahidi wa vilivyomo – vyenye kushuhudia majina hayo – anakiuka haki zao pia,  na kwa kukanusha kwake majukumu matukufu ya viumbe – nazo ni tasbihi zake kwa majina –  na anakiuka haki zake na kwa kupinga kwake aina za ibada ambazo wanazitekeleza waja kukabiliana na kudhihiri kwa ulezi na uungu wa Allah (s.w) – nalo ndio lengo la kuumbwa kwake na sababu katika sababu za kuwepo na kubakia kwake – anakiuka vibaya sana haki za viumbe wote,  kwa hiyo ukafiri ni jinai kubwa na dhuluma mbaya ubaya wake unavuka mipaka yote ya msamaha kwa hiyo inathibiti kwake hofisho la aya tukufu:

إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ Qur’an, 4:48.

Bali kutomtupa mtu kama huyu katika jahanamu kwa kumuhurumia ni jambo linalopingana na huruma yenyewe moja kwa moja katika haki za hizi idadi kubwa za halaiki na viumbe ambavyo haki zao zimevunjwa.

Na kama hivyo kama wanavyotaka wenye madai kuwepo kwa jahanamu, hakika enzi ya utukufu wa Allah (s.w) na adhama ya ukamilifu wake (s.w) vinaitaka kwa yakini.

Naam, mpumbavu au mwovu, asi akimwambia mtawala mtukufu wa nchi: “Wewe huwezi kunitupa jela na hutaweza hilo kamwe” kwa kukiuka mpaka wake na utukufu wa mtawala huyo na adhama yake, hapana budi kuwa mtawala huyo ataanzisha jela kwa ajili ya huyo safihi mkiukaji hata kama kusingekuwa katika nchi hiyo kuna jela. Vivyo hivyo mambo kwa kafiri halisi basi yeye kwa ukafiri wake anakiuka vikali enzi ya utukufu wake (s.w), na kwa kukanusha kwake anapinga adhama ya uweza wake na kwa kukiuka kwake anagusa ukamilifu wa ulezi wake wa kiungu, kusingekuwepo hata hizo sababu zenye kupasisha na hizo nyudhuru nyingi na hekima nyingi na majukumu mengi kwa jahanamu na kwa kuwepo kwake, hakika kuumba jahanamu kwa ajili ya mfano wa hawa makafiri na kuwatupia humo ni katika hali ya enzi na utukufu huo. Kisha hali ya ukafiri yenyewe inafahamisha jahanamu kwa sababu kama ilivyo hali ya imani ikiundika mwili inaweza kujenga kwa ladha zake na neema za uzuri wake pepo maalum kwenye dhamira ya mwanadamu na moyo wake, ni pepo ndogo inaashiria na kupasha habari kuhusu pepo ya kudumu milele wanayoingojea huko Akhera, vivyo hivyo ukafiri –  na hasa hasa ukafiri halisi – unafiki na kuritadi yapo maumivu na mateso ya kutisha kwa namna ambayo kama yangefanyika mwili na kujikita katika nafsi ya mwenye nayo ingemtengenezea jahanamu yake maalum ambayo inaashiria yale atakayo yafikia huko Akhera katika jahanamu ambayo ni kali zaidi kitisho na kwa mateso. Tumethibitisha hili kwa dalili za kukinaisha kwenye Risale-i Nur na imeashiriwa pia mwanzoni mwa suala hili.

Na kwa kuwa hii dunia ni shamba la Akhera, hakika ndogo ambazo huzaa matunda na kuweka mashuke Akhera, basi mbegu hii yenye sumu (Ukafiri) inaashiria kwenye pembe hii kwenye ule mti wa Zaqqum na kusema: “Mimi ni shina la mti ule na johari yake, basi atakayenibeba moyoni mwake katika wenye kusibiwa na majanga nitamzalia matunda ya kielelezo maalum kutoka katika mti ule uliolaaniwa”.

Na kwa kuwa ukafiri ni kukiuka haki zisizokuwa na mpaka, na ukiukaji wenye kufedhehesha, kwa hiyo ukafiri ni jinai isiyokuwa na mpaka, kwa hiyo unamfanya mwenye nao kuwa anastahiki adhabu isiyokuwa na mpaka. Ikiwa kuua ambako hutokea katika dakika moja tu humfanya muuaji aonje adhabu ya miaka kumi na tano (Muda unao karibia dakika milioni nane) na huo unazingatiwa kuwa unaafikiana na uadilifu wa kibinadamu, hesabu yake ni yenye kufaa masilahi ya umma na haki zake, hakuna makosa kwamba dakika moja ya ukafiri halisi – kwa kuuzingatia ukafiri ni mauaji elfu – kwa hiyo ikikabiliwa kwa adhabu inayokaribia mamilioni ya dakika kulingana na uadilifu huo wa kibinadamu basi anayemaliza mwaka mmoja kamili katika umri wake katika ukafiri kwa hiyo anastahiki adhabu ya dakika trilioni mbili na themanini na nane bilioni yaani anakuwa ni mstahiki wa:

خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا Qur’an, 4:169.

Hivyo, hakika mtindo wa kimuujiza wa Qur’an tukufu katika kubainisha kwake pepo na moto na yaliyomo katika (Risale-i Nur) – ambayo ni neema kutokana nayo na tafsiri yake – katika hoja kuhusu kuwepo kwake hazikuacha nafasi ya ufafanuzi mwingine wowote basi aya nyingi mno mfano:

وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّار Qur’an, 3:191.

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا

إِنَّهَا سَاءتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا Qur’an, 25:65-66.

Na aghalabu wa alilokuwa mtume (s.a.w) akilirudia rudia katika dua zake kila wakati, na Manabii (a.s) na watu wa hakika kama: “Tuepushe na moto”.. “Tuokoe na moto”.. “Tukomboe na moto” ambalo kwao imepata ukinaifu kamili kwa msingi wa wahy ulioshuhudiwa, yote hayo yametubainishia kuwa kadhia kubwa sana ya mwanadamu juu ya Ardhi hakika sio nyingine isipokuwa ni kuokoka kutokana na moto, na kwamba hakika kuu zaidi na ya kushangaza mno katika hakika za viumbe, bali muhimu zaidi sio nyingine bali ni (Jahanamu) ambayo wanaishuhudia baadhi ya hao wenye kuhakiki na watu wa ushahidi na ufunuo, na wengine wanaona ndimi zenye kuwaka na giza jeusi na baadhi yao wanasikia mrindimo wa kuwaka kwake na kufoka kwake basi wanapiga kelele kutokana na kishindo chake: “Tuepushe na adhabu ya moto”.

Naam, hakika ya kukabiliana kwa kheri na shari katika ulimwengu huu, ladha na maumivu, nuru na giza, joto na baridi, uzuri na ubaya, uongofu na upotevu, na kuingiliana kati yao hakika hilo ni kwa hekima kubwa kwani kama kusingekuwapo shari isingefahamika kheri, na kusingewapo maumivu ladha isingefahamika, na mwanga bila giza sambamba nao haidhihiri uzuri wake, na viwango vya joto huthibiti kwa kuwepo kwa baridi, na inakuwa hakika moja ya uzuri elfu moja katika hakika kwa kuwepo kwa ubaya, bali huvuna maelfu ya aina za uzuri na ngazi za uzuri. Na nyingi ya ladha za peponi hujificha kwa kutokuwepo kwa jahanamu. Basi kwa kupimia hili inayumkinika kujulikana kila kitu kwa upande wa dhidi yake, na kwa kuwepo kwa dhidi inayumkinika hakika moja kutoa matunda ya hakika nyingi.

Kwa kuwa vilivyomo hivi vyenye kuchanganyika vinamiminika kumiminika kutoka makazi ya kutoweka kwenda katimka makazi ya kubakia, hapana budi kwamba kheri, ladha, nuru, uzuri, imani na mifano ya hayo kumiminika kuelekea peponi na inadondoka shari, maumivu, giza, ubaya, ukafiri na mifano ya hayo katika mambo ya kudhuru kwa jahanamu. Humimina mifereji ya viumbe hivi vyenye kugongana daima kuelekea katika birika hizo mbili na kutulia tuli kwenye viwili hivyo mwishoni mwa safari.

Kwa kadiri hii tunatosheka na tunaelekeza katika yaliyokuja katika (Neno la ishirini na tisa) katika nukta za mfano.

Enyi wenzangu katika masomo katika madarasa hii ya Yusuf!

Hakika njia nyepesi ya kuokoka na jela ya milele ya kutisha (Jahanamu) hakika ipo katika kutumia kwetu fursa ya kubakia kwetu kwenye jela ya kidunia, hii ambayo imefupisha mikono yetu kutenda madhambi mengi ikatuokoa nayo. Kwa hiyo basi sio juu yetu ila kufanya istighfari (kuomba msamaha) na kutubia dhambi tulizozifanya katika siku zilizotangulia pamoja nakutekeleza faradhi, ili tugeuze kila saa moja katika saa za jela hii kwa hukumu ya siku moja ya ibada, hivyo hii kwetu ni fursa bora kwetu ili kuokoka kutokana na jela ya milele na kwa ajili ya kuingia kwetu pepo yenye nuru. Na kama tukiikosa fursa hii Akhera yetu itazama katika mikasa kama ilivyo hali ya dunia yetu na itathibiti kwetu kauli yake Allah (s.w):

خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ Qur’an, 22:11.

Sauti za takbira ya Idi al-Adh’ha mubarak zilikuwa zikipaa juu wakati mada hii ikiandikwa, mawazo yakanipeleka ya kwamba moja ya tano ya wanadamu wanakariri: (Allah Akbar), na kwamba zaidi ya Waislamu mia tatu milioni wanakariri kwa pamoja, kana kwamba sauti ya (Allah Akbar) inakuwa juu kwa ukubwa wa tufe la Ardhi na kwa upana wake kwa hiyo ardhi inazisikilizisha ndugu zake sayari nyingine neno hili takatifu katika pande za mbingu. Na kuna zaidi ya mahujaji ishirini elfu katika Arafa na Idd kwa pamoja wanakariri mwangwi wa aliyoyasema mtume mtukufu (s.a.w) na kuyaamrisha kabla ya miaka elfu moja na mia tatu pamoja na jamaa na swahaba wema. Nikahisi hisia kamili bali nimekinai kikamilifu kwamba miangwi hiyo, sauti na kukariri hakika ni uja mpana wa kijumla unakabiliana na kudhihiri kwa ulezi wa kiungu wa jumla kwa utukufu wa (Mola Mlezi wa Ardhi) na (Mola Mlezi wa walimwengu).

Kisha nikaiuliza nafsi yangu: Je, ukoje uhusiano baina ya Akhera na neno hili takatifu (Allah Akbar)? Nikakumbuka haraka kwamba neno hili pamoja na maneno mazuri yenye kubakia yalio mema: (subahanallah, walhamadulillah, walaailaha illa Allah) na mfano wa hayo katika maneno ya alama za Kiislamu hukumbusha – bila shaka – Akhera sawa kwa sura ya kisehemu au kiujumla na yanaashiria kuthibiti kwake. Hakika upande mmojawapo wa maana ya (Allah Akbar) ni: Hakika ya uweza wa Allah na ujuzi wake ni juu ya kila kitu na ni kubwa na tukufu kuliko kila kitu, basi hakitatoka kitu chochote kiwacho katika duara la ujuzi wake na hakitakimbia usarifu na uweza wake, na hakitamponyoka kamwe, basi yeye (s.w) ni mkuu kuliko kila mkubwa tunayemuhofia na kumtukuza. Yaani ni mkuu kuliko kuleta ufufuo katika uwepo ambao tunauona kuwa ni mkubwa – na mkuu kuliko kutuokoa kwetu kutoka katika kutokuwepo na mkuu kuliko kutupa kwetu furaha ya milele. Yeye ni mkuu kuliko kila kitu ambacho tunakistaajabia na kuliko kitu chochote kilicho nje ya akili yetu ambapo Allah (s.w) anasema:

مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ Qur’an, 31:28.

Basi uwazi wa aya hii tukufu unabainisha kwamba kukusanya na kutawanya (ufufuo) kwa wanadamu wote ni rahisi kwa uweza wa kiungu kama kufanya nafsi moja iwepo, basi hakuna ajabu kupita katika maneno ya mithali kauli ya mwanadamu: (Allah Akbar, Allah Akbar) kila aonapo kitu kikubwa au msiba mkubwa au lengo kubwa, akiiliwaza nafsi yake kwa kauli hiyo na akifanya nguvu kubwa anayoegemea kutokana na neno hili kubwa. Naam, hakika neno hili pamoja na wenzake: (Subhanallah, walhamdulillah) ni faharisi za ibada zote na mbegu na muhtasari wake (kama ilivyokuja katika (Neno la kumi na tisa)). Hivyo kukariri kwa maneno haya – na hizo ni hakika kuu tatu katika swala na katika dhikiri zake – hakika ni kwa ajili ya kutia nguvu maana ya swala, kuipa kina na kuiimarisha. Nayo ni jawabu la kukinaisha la maswali yanayotokana na kustaajabia, ladha na haiba ambayo yanayokuwa nafsini mwa mwanadamu wakati akishuhudia ulimwengu na kuona yanayomwamsha hisia na kumfanya atahayari na yanayompeleka katika kushukuru na ambayo ni uwanja wa adhama na kiburi katika mambo ya ajabu, mazuri, makuu, mengi na yale ambayo ni juu ya aliyoyazoea.

Naam, hakika askari anaingia katika hadhara ya mfalme na diwani yake (Makazi ya mfalme) siku ya Iddi kwa mfano wa kuingia kwake kiongozi mkuu, wakati ambao nyakati nyengine mfalme wake anamtambua kwa cheo cha kamanda na katika makamo yake – kama ilivyokuja mwishoni mwa (Neno la ishirini na sita) – basi kila mtu pia katika haji anaanza kumtambua mola wake wa haki (s.w) kwa jina la (Rabbil Ardhi wa Rabbil Alamiin) ujuzi unaofanana sana na inavyokuwa utambuzi wa mawalii wema. Na kila ngazi ya ukuu inapofunguka na adhama ya kiungu ndani ya roho yake hujibu kwa (Allah Akbar), kwa sababu ya maswali yanayomtawala yanayojirudia yenye msisitizo na kuleta tahayuri, basi (Allah Akbar) ni jawabu la kukinaisha kwa vitimbi vya hila za Shetani kama ilivyokuja katika (Mng’ao wa kumi na tatu). Naam, basi kama lilivyo neno hili (Allah Akbar) linajibu swali letu kuhusu Akhera majibu mafupi na yenye nguvu katika wakati huohuo, basi hakika fungu la maneno (Alhamdulillah) nalo pia linakumbusha ufufuo na kuuhitajia. Ambapo linatwambia: (Maana yangu haitimii bila ya Akhera) kwa sababu maana yangu yanafidisha kuwa: (Kila himidi au shukurani inayotoka kwa yeyote Mwenye kuhimidi na kutuka juu ya yeyote Mwenye kuhimidiwa awaye, kuanzia tangu azali hadi milele, ni mahususi kwake yeye (s.w)), na kwa kuwa furaha ya milele ndio asili ya neema zote na kilele chake, na ndio inayogeuza neema kuwa neema za hakika hazigeuki wala kuondoka, nayo ndio ambayo inayookoa wenye utambuzi kutokana na masaibu ya kutokuwepo na kuwakomboa nayo, kwa hiyo hayo peke yake yanaweza kukabili maana yangu ya kiujumla.

Naam, hakika ya kurudia kila muumini kila siku baada ya swala kwa vile inavyoamuru sharia zaidi ya mara mia moja na hamsini (Alhamdulillah) kwa uchache, na ambalo linafidisha hamdi na thanai na shukurani kunjufu inaendelea kutokea azali hadi milele hakika hiyo ni thamani anailipa kwa kutanguliza kwa ajili ya kupata furaha ya milele peponi, kwani haiyumkiniki kuyafunga maana ya hamdi katika neema za dunia fupi za kutoweka zenye kutibuliwa kwa machungu wala haiyumkiniki kuwa yenye kuishia juu yake. Bali hata lau ungezingatia katika hizo neema zenyewe utaziona kuwa sio isipokuwa ni nyenzo za neema za milele za kudumu zinazostahiki shukurani juu yake.

Ama neno (Subhanallah) hakika linamaanisha: Kumtakasa Allah (s.w) na kumtukuza kutokana na kila mshirika na kutenda upungufu na kasoro na dhuluma na kushindwa na ukatili na uhitaji na hila, na kila kinachohalifu ukamilifu wake na uzuri wake na utukufu wake. Na maana hii inakumbusha furaha ya milele na kujulisha juu ya Akhera ambayo ni mhimili wa adhama yake (s.w), utukufu wake na ukamilifu wake. Na pia inaashiria yale yaliyomo katika makazi hayo miongoni mwa pepo ya neema na kuijulisha. Na kama sio hivyo isingekuwa huko kuna furaha ya milele hakika vidole vya tuhuma vingeelekea kwenye adhama yake (s.w), ukamilifu wake, utukufu wake, uzuri wake na rehema zake, basi hapo vingepatwa na upungufu na kasoro, ametukuka Allah (s.w) na hayo kutukuka kukubwa. Yaani hakika ya Akhera haina shaka, kwani hiyo Akhera ni mahitajio ya ufalme wa Allah, ukamilifu wake, utukufu wake, uzuri wake na rehema yake (s.w).

Na kama hivi hakika ya maneno haya matakatifu matatu pamoja na (Bismillah) na

(لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ)

na baki ya maneno yenye kubarikiwa, kila moja kati yao ni mbegu katika mbegu za nguzo za kiimani na kila moja kati ya hizo ni muhutasari wa hakika za nguzo za kiimani na hakika za Qur’an.

Na kama yalivyo haya maneno matatu ni kokwa za swala na mbegu zake hizo basi ni kokwa za Qur’an pia. Kama unavyoshuhudia mwanzoni mwa baadhi ya sura za dhahiri ambapo zinafungua zikiwa kana kwamba ni johari yenye kung’aa mwanzoni mwake. Nazo ni hazina za hakika na misingi madhubuti za juzuu za Risale-i Nur ambazo zinaanza kwa vipawa vya Tasbihati, nazo pia ni nyiradi za Twarika ya Muhammad hutajwa mwishoni mwa swala ndani ya duara pana mno la uwalii wa Muhammad na uja wa Muhammad, kwa kiasi kwamba katika kila swala kuna zaidi ya mia moja milioni waumini katika mzingo huo mkubwa wa dhikiri wanarudia rudia kwa pamoja mara thelathini na tatu (Subahanallah) na mara thelathini na tatu  (Alhamdulillah) na mara thelathini na tatu (Allah Akbar). Basi hapana budi kwamba unatambua kiasi cha umuhimu wa kusoma maneno hayo matatu yenye baraka. Ambayo ni mbegu za Qur’an na Imani na swala na ni muhutasari wake. Na kiasi cha thawabu za kuyarudiarudia kwa mara thelathini na tatu baada ya swala ndani ya huo mzingo mpana.

Na kama hivi kama kwamba (Suala la kwanza) katika Risala hii lilikuwa somo muhimu sana katika swala, hakika mwisho huu wa Risala – bila hiari yangu – ni somo muhimu kuhusu Adhkari za swala! na Alhamdulillah kwa neema zake.

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيْمُ الْحَكِيْمُYou May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.