Muhtasari Wa Suala La Pili

Kama risala ya (Mwongozo kwa vijana) ilivyofafanua ufafanuzi mzuri kwamba umauti hakuna pa kukimbilia kamwe, na kwamba kuja kwake ni kwa yakini zaidi kuliko yakini ya kuja kwa usiku wa mchana huu, na kufuatia kwa majira ya baridi baada majira haya ya mapukutiko. Na kama jela hii ilivyo ni nyumba ya wageni ya muda mfupi haiwi tupu ila inajazwa tena upya, basi dunia vivyo hivyo ni kama hoteli, na kama nyumba ya mafikio na misafara ambayo imejengwa kwenye njia ya misafara ya haraka.

Umauti ambao unaondosha wakazi wa kila mji mara mia moja na kuwasukuma makaburini, hapana budi kuwa unakusudia kitu zaidi kuliko maisha haya ya kutoweka na chenye hadhi ya juu kuliko maisha hayo.

Risale-i Nur imefumbua fumbo la hakika hii ya kushangaza na kuweka wazi na muhtasari wake ni:

Kwa kuwa umauti hayauliwi, na mlango wa umauti haufungwi, hakika jambo kuu kabisa litakaloshughulisha akili ya mwanadamu na kufanya kuwa ni shida kubwa kwake ni kuokoka kutoka katika mkono wa mnyongaji huyu wa umauti na kukomboka kutokana na jela ya pekee ya kaburi.

Risale-i Nur imethibitishwa kwa kukinaisha kabisa – kwa heri itokanayo kwenye nuru ya Qur’an – kwamba shida hii ina tiba na muhtasari wake ni kuwa:

Umauti ima ni kunyongwa kwa milele na kutoweka kabisa ambako kunamsibu mtu na wapenzi wake na ndugu zake wa karibu wote, au kuruhusiwa kutokana na kazi kwa ajili ya kwenda kwenye ulimwengu mwingine ulio bora zaidi na hati ya kusafiria ya kuingia katika kasri za furaha kwa shahada na hati ya imani. Ama kaburi ni jela ya pekee yenye giza na lindi lenye kina kirefu au ni mlango kwenda katika mabustani ya kudumu milele na mahali pa wageni penye nuru baada ya kuruhusiwa kutoka katika jela ya dunia.

Hakika Risala ya (mwongozo wa vijana) imethibitisha hakika hii kwa mfano nao: Hakika kumewekwa katika uwanja wa jela hii milingoti ya vitanzi ikiegemea kwenye ukuta, nyuma yake kuna afisi kubwa inatunuku zawadi za ukarimu watu wote washiriki. Na sisi wafungwa mia tano tunangojea zamu yetu tuitwe kwenye medani hiyo, tutaitwa huko mmoja mmoja tumependa au tumekataa, hakuna kuokoka! Ima kila mmoja wetu ataambiwa “Njoo upokee amri ya kunyongwa kwako na panda kitanzini” au: “Pokea amri ya jela ya pekee ya milele na uingie kwenye mlango huu ulio wazi” au patasemwa: “Furaha yako! umeshinda tikiti inayokupa faida ya mamilioni ya lira za dhahabu haya chukua”.

Basi haya sisi hapa tunashuhudia matangazo ya ulinganio huu umeenea huku na kule na tunaona watu wanapanda kwenye vinyongeo kwa zamu na kati yao wapo wanaoshuka, na miongoni mwao wapo wanaoifanya kuwa ni ngazi ili kufika katika afisi ya zawadi iliyo nyuma yake, na tumeshakuwa katika yakini ya kukinaisha kwa yale yanayoendelea katika afisi ile – kana kwamba tunaiona kwa macho – kwa kuegemea kwenye yale wanayoyasema maafisa wakuu wa afisi hiyo katika simulizi za kweli zisizokubali shaka.

Makundi mawili yameingia kwenye jela yetu – wakati huu – mojawapo linabeba zana za muziki na chupa za mvinyo pamoja na halua nje yake ni asali na ndani yake kuna sumu, wameziweka mashetani wa kibinadamu na wanatuletea na kutushawishi kuvitumia.

 Ama kundi la pili mikononi mwao kuna vitabu vya malezi na vipeperushi vya kitabia pamoja na vyakula vizuri na vinywaji vya baraka, wanatuletea vikiwa zawadi kwetu, na wanatueleza kwa kuafikiana na kwa utulivu kamili na yakini iliyotimia:

Hakika ambacho kundi la kwanza inatoa katika vyakula si lolote isipokuwa ni mtihani na majaribio mkivikubali na kuviridhia hatima yenu itakuwa kama inavyodhihiri mbele yenu katika vinyongeo. Ama mkiridhia zawadi zetu – ambazo tunakuleteeni kwa jina la mtawala wa nchi hii na kwa amri yake – na mkasoma maelekezo yaliyomo na dhikiri kwenye vitabu hivyo mtaokoka na kunyongwa na mtapokea tikiti ya zawadi kutoka afisi ile ili mpate kufanikiwa faida kubwa, zawadi kutoka kwa mfalme, ukarimu na fadhila kutoka kwake. Sadikini tunayokwambieni na muitakidi kwa kina kana kwamba mnayaona kwenye mwanga wa mchana. Lakini hadharini na halua hizo zilizotiwa ladha ya asali – za haramu au zenye kutia shaka – ikiwa mtakula katika hizo matumbo yenu yatapata maumivu makali kutokana na athari ya sumu, mtasumbuliwa kutokana nazo maumivu hadi kupanda kwenu kwenye vinyongeo. Na kama hivyo kama ulivyo mfano huu kadari ya kiungu itawatunuku waumini ambao wametumia umri wao kwa utiifu na amali zao kuhitimishwa kwa mema atawatunuku hazina za milele hazikatiki baada ya kukoma kwa uhai wao wa kidunia, ama wale ambao waliopitiliza katika upotevu na ufuska bila ya kurejea kwa mola wao watanyongwa moja kwa moja (kwa wasioamini Akhera) au kuwekwa katika jela ya pekee yenye giza ya milele (kwa mwenye kuendelea katika upotevu wake na usafihi wake pamoja na kuamini kwake kwa kubakia kwa roho) hawa watapokea maamuzi ya mateso yao ya milele kwa yakini inayofikia tisini na tisa kwa mia. Naam, habari hii ya kweli wanaielezea mia moja na ishirini na nne elfu katika manabii (a.s).

Amesema Abudharri (r.a) “Nilisema: Ewe mjumbe wa Allah ni ngapi ukamilifu wa hesabu ya Manabii? Akasema laki moja na ishirini na nne elfu, Mitume Mursali katika hiyo ni mia tatu na kumi na tano kundi kubwa”. (Ahmad bin Hanbali, Al-Musnad 5/265. Ibn Hiban, As-Sahih 2/177, At-Tabarani, Al-Muujamul Kabiir 8/217. Al-Hakim, Al-Mustadrak 2/ 652. Ibn Saad, At-Tabaqaat al-kubraa 1/23-54).

Na mbele yao kukiwa na miujiza inayowasadikisha na wanaelezea zaidi ya mia moja na ishirini na nne milioni katika mawalii mwenyezi mungu atukuze siri zao wenye kufuata nyayo za manabii (a.s) na wenye kusadikishwa kwa yale waliyoyaeleza kwa kufunuliwa na maonjo, na wanaelezea hilo pia wasiohesabika katika Maulamaa wenye kuhakiki

Hakika ya mmoja ya hao wanazuoni wahakiki ni: Risale-i Nur ambayo imewatia lijamu wanafalsafa wakaidi wa kimaada na kuwahemeza wakanaji wakubwa kwa uasi, miaka yote ishirini iliyopita, na haijaacha kuwa ni yenye kusimama kwa wayo na muundi katika medani ya changamoto na makabiliano. Nayo inapatikana kwa wote. Kila mmoja anao wasaa wa kuisoma bila ya kuishinda. (Mtunzi)

na Mujitahidina na Masidikina ambao wamethibitisha madai yao na kusadikisha kwao kwa akili na fikira kwa dalili zenye nguvu na hoja zenye kukinaisha wakaelezea kwa yakini waliyoyaeleza wapekee hao kutokana na makundi hayo maili.  Basi hayo makundi makubwa matatu na mijumuiko mingi katika watu wa kweli na hakika – nao ni viongozi wa utu na majua ya ubinadamu na miezi yake – wote wanaelezea hakika hiyo kwa makubaliano ya pamoja na kwa tawaturi. Hasara iliyoje kwa asiyetilia umuhimu amri zao wala hapiti njia iliyonyooka yenye kupelekea katika furaha ya milele kwa maelekezo yao wala kujali matokeo yake ya kuumiza – nayo kwa yakini inafikia tisini na tisa katika mia – katika wakati ambao hapiti katika njia ambayo ina uwezekano moja wa hatari na kwa kuegemea mwelezaji mmoja, bali atabadilisha njia nyingine japo ikiwa ndefu.

Hawa ni mfano wa mlevi mwovu zuzu anayezugika kujali ming’ato ya mbu na kuachana na mashambulizi ya wanyama wakali wenye kumshambulia kwa kuwa amepoteza moyo na akili yake na kuharibu roho yake na kuteketeza utu wake kwa sababu yeye pamoja na taarifa za kweli zinazotokana na hao wapasha habari ambao wasio na idadi, ameacha njia fupi na nyepesi zaidi inayopelekea kwenye kufaulu kwa hakika pepo na furaha ya milele, na kuchagua njia ndefu kuliko hiyo na yenye taabu na dhiki zaidi na ambayo inampelekea katika jela ya jahanamu na mateso ya milele kwa lazima.

Wakati ambapo mwanadamu – kama tulivyosema – hapiti njia fupi duniani yenye uwezekano mmoja katika mia wa hatari au yenye jela ya mwezi mmoja na kwa maneno ya mpasha habari mmoja na anaweza akawa ni muongo. Bali anafadhilisha njia nyengine japokuwa ni ndefu au haina manufaa kwa sababu tu ya kutokuwa na madhara.

Kwa kuwa ukweli wa mambo ndio huu basi inatakikana kwetu sisi changamano la wenye kupewa mtihani wa jela tukubali kwa ridhaa yote na furaha zawadi za kundi la pili ili tulipe kisasi kwa nafsi zetu kutokana na msiba wa jela kama ilivyokuwa ladha ya dakika moja katika kulipiza kisasi na starehe ya dakika chache au saa katika usafihi zimetusukuma kuingia jela baadhi yetu wanaishi humo miaka kumi na tano au mwaka mmoja au miwili au miaka mitatu kutokea kuhukumiwa. Kwa hiyo basi juu yetu – bila ya hiari ya jela – tubadili kwa kukubali kwetu zawadi za kundi la pili, saa hizi chache kuwa ni siku za ibada kama hizo, na kubadili miaka miwili au mitatu ya kuadhibiwa kwetu kuwa katika miaka ishirini na thelathini ya umri wa milele. Na kubadili kwa miaka ishirini na thelathini ya kukaa kwetu jela kuwa mamilioni ya miaka ya kudumu milele. Hapo basi hukumu zilizotolewa dhidi yetu zitakuwa ni njia ya kuokoka na jela ya jahanamu. Na wakati huo maisha yetu ya Akhera yatatabasamu na furaha baada ya kilio na majonzi ya dunia yetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumelipiza kisasi kwa nafsi zetu kutokana na mateso hayo na kwa haki kabisa tutakuwa tumedhihirisha kuwa jela ni madarasa ya kimalezi ya kurekebisha tabia.

Basi na washuhudie wakuu na watawala wa jela, hakika wale ambao waliowadhania kuwa ni waovu wauaji na kuwadhania kuwa ni masafihi wenye kukhalifu utaratibu wamekuwa ni wanafunzi wa madrasa ya kimalezi yenye kubarikiwa wanajifunza humo adabu nzuri na tabia iliyonyooka na kuwa raia wema kwa nchi na waja, basi na wamshukuru sana Mola wao.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.