Suala La Sita

Suala hili ni ishara kwa muhtasari ya hoja moja tu kati ya maelfu ya hoja za jumla juu ya (Kumwamini Allah (s.w)) na ambayo imeelezwa pamoja na hoja zake za kukinaisha katika sehemu nyingi za Risale-i Nur.

Lilinijia kundi katika wanafunzi wa sekondari huko (Kastamonu) wakisema “Tujulishe Muumba wetu kwa sababu walimu wetu hawatuelezi habari za Mungu!”.

Nikawaambia: “Kila somo katika masomo mnayosoma daima linaelezea kuhusu Allah (s.w), na kumjulisha Muumba Mkarimu kwa lugha yake maalum. Basi sikilizeni masomo hayo na sio walimu”.

Kwa mfano:

Lingekuwapo duka la madawa kubwa, katika kila chupa kati ya chupa zake kumewekwa madawa kwa vipimo nyeti na kwa kiasi madhubuti; kama linavyotuonesha kwamba nyuma yake kuna mtaalamu wa madawa mwenye busara, na mkemia mahiri, vivyo hivyo duka la madawa la tufe la ardhi ambalo linajumuisha zaidi ya sampuli mia nne elfu za vilivyo hai ikiwemo mimea na wanyama, na kila moja kati ya hizo kwa hakika ni sawa na chupa ya madawa ya kikemia madhubuti, na chupa ya mchanganyiko ya kiuhai ya ajabu. Basi duka hili kubwa la madawa linamuonesha hata kipofu mfamasia wake mwingi wa hekima mtukufu, na kumtambulisha Muumba wake mkarimu kwa kiwango cha ukamilifu, mpangilio na ukubwa wake, kwa kulinganisha na duka lile la madawa liliopo sokoni, kulingana na vipimo vya  (Elimu ya tiba) mnayoisoma.

Na kwa mfano:

Kama kiwanda cha ajabu kinavyofuma maelfu ya bidhaa anuwai za kufumwa, na vitambaa mbalimbali, kutokana na maada rahisi mno, kinatuonesha pasi na shaka kwamba nyuma yake kuna mhandisi makanika mahiri, na kumtambulisha kwetu; kadhalika mashine hii ya kiungu itembeayo inayoitwa tufe la ardhi, na kiwanda hiki cha kiungu ambacho ndani yake kuna mamia ya maelfu ya viwanda vikuu, na katika kila kimoja kati ya hivyo kuna maelfu ya viwanda bora, kinatujulisha bila ya shaka fundi wake na mmiliki wake kulingana na vipimo vya (Elimu ya makanika) mnayoisoma, kinamtambulisha kwa kiwango cha ukamilifu wa kiwanda hiki cha kiungu, na ukubwa wake kwa kulinganisha na kile kiwanda cha mwanadamu.

Na kwa mfano:

Kama vile stoo au ghala la vyakula na riziki, na duka kubwa la vyakula lililowekwa kutoka – kila upande – sampuli elfu moja ya bidhaa za vyakula, na kupambanuliwa kila moja dhidi ya nyingine, na kupangwa safu katika mahali pake maalum, linavyotuonesha kwamba lina mmiliki na mwendeshaji; kadhalika ghala hili la Mwingi wa rehema kwa ajili ya vyakula ambavyo vinaenda kila mwaka masafa ya miaka ishirini na nne elfu, katika mpangilio madhubuti maridadi, na ambalo linakusanya ndani yake mamia ya maelfu katika aina za viumbe ambao kila mmoja anahitaji aina maalum ya chakula. Na ambalo linapita katika majira manne linakuja na majira ya machipuo kama lori lililosheheni maelfu ya aina za vyakula tofauti, linavileta kwa viumbe masikini ambao majira ya baridi vyakula vyao vilikwisha. Hilo ndio tufe la Ardhi na jahazi la Subuhana ambalo linajumuisha maelfu ya sampuli za bidhaa na zana na makopo ya vyakula. Ghala na bohari hii ya kiungu – inaonesha – kulingana na vipimo vya (Elimu ya lishe na biashara) mnayoisoma – mwenyewe mmiliki wake na msarifu wake kwa kiwango cha ukubwa wa ghala hili, kwa kulinganisha na ghala lile lililotengenezwa na mwanadamu na inamtambulisha kwetu na kutuelekeza tumpende.

Na kwa mfano:

Lau ikiwa jeshi kubwa katika kikosi chake kuna aina mia nne elfu za mataifa mbalimbali kila aina ina chakula chake pekee tofauti na aina nyingine, na silaha inayoitumia ni tofauti na silaha ya kundi lingine, na mavazi inayovaa yanatofautiana na mavazi ya kundi lingine, na mtindo wa mazoezi yake na mafunzo yake ni mbali na wa kundi lingine, na muda wa kazi na kipindi cha kupumzika sio muda wa kundi lingine, basi kiongozi wa jeshi hili ambaye peke yake anawapa riziki tofauti, silaha mbali mbali, mavazi tofauti bila ya kumsahau yeyote kati yao wala kuchanganya wala kubabaika ni kiongozi hasa mwenye maajabu bila shaka yoyote; kama kambi hii ya ajabu inavyotuonesha kwa uwazi kiongozi huyo wa kufurutu ada bali inatuelekeza kumpenda kwa heshima zote na kupendezwa; hali kadhalika kambi ya Ardhi katika kila majira ya machipuo inaandikisha upya jeshi kubwa la Subuhana likiundwa na aina mia nne elfu za mataifa ya mimea na wanyama na kuipa kila aina mavazi yake, riziki zake, silaha zake, mazoezi yake na ruhusa zake maalum kutoka kwa kiongozi mkuu mmoja wa pekee mtukufu bila kusahau aina yoyote wala kuchanganya wala kubabaika katika ukomo wa ukamilifu na upeo wa mpangilio. Basi kambi hii kunjufu pana sana ya majira ya machipuo yenye kutandawaa juu ya uso wa Ardhi inaonesha – kwa wenye akili na busara – mtawala wa Ardhi kulingana na (Elimu za kijeshi) mlezi wake na mwendeshaji wake na kiongozi wake mtakatifu sana na mtukufu na kuwajulisha kwa kiwango cha ukamilifu wa kambi hii ya kifahari na kiasi cha ukubwa wake kwa kulinganisha na kambi ile iliyotajwa, bali inaelekeza kumpenda mmiliki wake (s.w) kwa kumsifu, kumtukuza na kumtakasa.

Kwa mfano:

Fikiria kwamba mamilioni ya taa za umeme zinatembea katika mji wa ajabu bila kuisha mafuta yake wala kuzimika. Je, hazioneshi – kwa mshangao na heshima – kwamba yupo mhandisi bingwa na mtaalamu wa umeme mwerevu mno wa kiwanda cha kufua umeme na wa taa hizo? basi taa za nyota zinazoning’inia katika dari ya kasiri la Ardhi ambazo ni kubwa kuliko tufe la Ardhi yenyewe kwa mara elfu nyingi kulingana na elimu ya falaki na zinakimbia upesi kuliko mfyatuko wa kombora, bila ya kupotosha mpangilio wake au kugongana na wenzake kabisa na bila ya kuzimika, wala kuisha kwa mafuta kulingana na mnayoyasoma katika (Elimu ya falaki). Taa hizi zinaashiria kwa vidole vya nuru katika uwezo wa Muumba wake usio na mpaka. Jua letu kwa mfano ambalo ni kubwa kwa mara milioni kuliko tufe letu la Ardhi na la zamani kuliko ardhi kwa miaka milioni, sio ila ni taa ya daima na jiko lenye kuendelea katika nyumba ya wageni ya mwingi wa rehema. Basi kwa ajili ya kudumisha kuwaka kwake kila siku inalazimu mafuta mithili ya bahari za ardhi, na mkaa kwa kadiri ya milima yake, na kuni kwa kiasi cha maradufu kwa maradufu ya ukubwa wa ardhi, lakini ambaye analiwasha – na kuwasha nyota zote mfano wake bila mafuta wala mkaa wala zeti na bila ya kuzimika na kulikimbiza kwa kasi kubwa kwa pamoja bila kugongana, hakika ni uwezo usio na ukomo na ufalme mkubwa usio na mipaka. Basi ulimwengu huu mkubwa na taa zilizomo zenye kuangaza, na kandili zenye kuning’inia unabainisha kwa uwazi – kwa mujibu wa vipimo vya elimu ya umeme – mfalme wa maonesho haya na tamasha kubwa, na unamtambulisha mnawirishaji wake na mwendeshaji wake wa ajabu na mtengenezaji wake mtukufu, kwa ushahidi wa hizi nyota zenye kumemetuka, na kuelekeza kumpenda kwa wote kwa kumsifu, kumtakasa na kumtukuza, bali inawapeleka kwenda kumwabudu (s.w).

Na kwa mfano:

Lau kingekuwapo kitabu katika kila mstari wa kitabu hicho kimeandikwa kitabu kwa hati makini na kuandikwa katika kila neno miongoni mwa maneno yake sura ya Qur’an, na masuala yake yote yakawa na maana ya kina, na yote yanaungana mkono, basi kitabu hiki cha ajabu bila shaka kinabainisha umahiri wa mwandishi wake wa hali ya juu, na uwezo wa mwandishi wake uliokamilika. Yaani mfano wa kitabu hiki kinamtambulisha mwandishi na msanifu wake utambulisho ulio wazi kama ulivyo mchana, na unabainisha ukamilifu wake na uweza wake na unachochea kupendezwa na kuheshimu mbele ya wenye kukitazama kiasi hawana la kusema mbele yake ila kukariri: (Tabarakallah, Subhanallah, Mashaallah!) katika maneno ya kusifia uzuri na kupendezwa; vivyo hivyo kitabu hiki kikubwa cha ulimwengu katika ukurasa mmoja wa kitabu hicho ambao ni uso wa ardhi na jozi moja ya sahifa yake nayo ni majira ya machipuo huandikwa aina za vitabu tofauti mia tatu elfu ambazo ni makundi ya wanyama na mimea kila moja ni sawa na kitabu, vyote hivyo vinaandikwa kwa pamoja na vikiwa vimeingiliana pasi na kuchanganyika, kukosea au kusahau, na katika ukomo wa mpangilio na ukamilifu, bali huandikwa kasida kamili ya kupendeza katika neno moja kama mti, na katika kila nukta kama mbegu huandikwa faharisi ya kitabu kamili. Kama linavyo shuhudiwa hili na lilivyo kiuhalisia mbele yetu linatuonesha kwa misisitizo kwamba nyuma yake kuna kalamu inayotiririka inayoandika, ni wajibu wenu sasa kukadiria kiasi cha kujulisha kwa kitabu cha ulimwengu kikubwa ambacho katika kila neno lake kuna maana lundo na hekima tofauti, na kiasi cha kujulisha kwa Qur’an hii kubwa mno iliyopata umbo ambayo ni ulimwengu, Muumba wake (s.w) na mwandishi wake (s.w) kwa kulinganisha na kile kitabu kilichotajwa katika mfano. Na hii kwa muktadha wa mnachosoma katika (Elimu ya hekima ya vitu) au (Sanaa ya usomaji na uandishi) na muichukue kwa kipimo kikubwa zaidi, na kwa mtazamo mpana katika ulimwengu huu mkubwa. Na kwa hivyo mtafahamu ni vipi kinamtambulisha Muumba mtukufu kwa (Allah akbar), na vipi kinafundisha kutakasa kwa (Subhanallah) na vipi humpendezesha Allah (s.w) kwetu kwa kusifu (Alhamdulillah).

Na kama hivi hakika kila elimu miongoni mwa elimu nyingi mno inajulisha juu ya Muumba wa ulimwengu (s.w) – kwa kulinganisha na yaliyotangulia – na inamtambulisha kwetu (s.w) kwa majina yake yaliyo mazuri na kutuelimisha kwa sifa zake tukufu na makamilifu yake. Na hii ni kwa yale iliyonayo miongoni mwa vipimo vikunjufu na vioo maalum na macho makali yenye kuona na mitazamo yenye mazingatio.

Nikawaambia wanafunzi wale vijana: Hekima ya kukariri kwa Qur’an tukufu.

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ

na

رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ

Hakika ni kwa ajili ya kuelekeza katika hakika hii iliyotajwa, na kufundisha hoja hii ya wazi ya Tawhid, na kwa ajili ya kututambulisha Muumba wetu mtukufu (s.w).

Wakasema: Shukurani kwa mola wetu Muumba bila mpaka, juu ya somo hili ambalo lenyewe ni hakika ya hali ya juu.Allah akulipe malipo yaliyo bora na akuridhie.

Hakika mwanadamu ni mashine yenye uhai, huumia kwa maelfu ya aina ya maumivu na kupata ladha kwa maelfu ya aina za ladha, pamoja na kuwa yuko katika ukomo wa kutojiweza, ana maadui wasio na mpaka sawa ni wa kimaada au wa kimaanawy, na pamoja na kuwa yupo katika ufukara, ana matakwa ya ndani na ya nje yasiyohesabika; ni kiumbe masikini anayepata maumivu ya mapigo ya kutoweka na utengano kwa kuendelea. Na pamoja na yote haya anapata kwa kujinasibisha na mfalme mtukufu kwa imani na uja maegemeo yenye nguvu, na ngome kubwa anayojihami nayo katika kuwazuia maadui wake wote, na humo pia anapata pa kuomba msaada anaomba kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake na kujibu matakwa yake na matarajio yake yote. Kama kila mmoja anavyojinasibu kwa bwana wake na kujifaharisha kwa utukufu wa kujinasibisha naye na anajienzi kwa nafasi ya cheo chake kwake, vivyo hivyo kujinasibu kwa binadamu – kwa imani – kwa mweza ambaye uweza wake hauna ukomo, na kwa mfalme mwingi wa rehema mwenye rehema kunjufu, na kuingia katika uja wake utiifu na shukurani, hubadili muda wa umri na umauti kutokana na kunyongwa kwa milele kuwa tikiti ya kupita na ruhusa ya kwenda kwenye ulimwengu wa kudumu! Ni juu yenu kukadiria ni kiasi gani mwanadamu anakuwa mwenye kupata ladha ya uja mbele ya Bwana wake, na kuneemeka na imani ambayo anaiona moyoni mwake, na mwenye kufurahi kwa nuru za Uislamu, na mwenye kujifaharisha kwa Bwana wake Mweza Mwingi wa rehema akiwa mwenye kumshukuru kwa neema ya imani na Uislamu.

Kama nilivyowaambia hayo ndugu zangu wanafunzi ndivyo ninavyo waambi vilevile wafungwa: Hakika aliyemtambua Allah na kumtii ni mwenye furaha japo akiwa katika giza la jela. Na mwenye kughafilika naye na kumsahau ni mwenye mateso japo akiwa kwenye kasri kubwa. Mdhulumiwa siko moja alipiga kelele na kusema mbele ya madhalimu hali akipanda kizimba cha kunyongwa akiwa mwenye furaha akasema:

“Hakika mimi siishii katika kutoweka wala sinyongwi, bali ninaachiliwa huru kutoka katika jela ya dunia kwenda katika furaha ya milele, lakini ninakuoneni kuwa nyinyi ndio mmehukumiwa kifo cha milele kwa vile mnavyoona kuwa umauti ni kutoweka na kukosekana. Kwa hiyo nafsi yangu imeshalipa kisasi kwenu” akasalimisha roho yake akiwa ameridhia akikariri:

لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيْمُ الْحَكِيْمُ

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.