Suala La Tatu

Nalo ni tukio lenye mazingatio limetangulia kutajwa katika (Mwongozo kwa vijana) kwa upambanuzi, na muhtasari wake ni:

Katika moja ya siku za Idi ya jamhuri nikiwa nimekaa mbele ya dirisha la jela ya (Eski şehir) ambayo ni mkabala na shule ya kati ya wasichana, wanafunzi wake chipukizi walikuwa wakicheza katika uwanja wa shule kwa furaha sana, ikaonekana kwangu ghafla katika kioo cha kimaanawy ikajionesha kwangu hali yao itakayokuwa baada ya miaka hamsini. Nikaona: Kwamba kiasi cha mabinti hamsini katika jumla ya wanao karibia wanafunzi sitini wanageuka udongo na kuadhibiwa kaburini na kwamba kumi kati yao wamegeuka kuwa ni vikongwe wabaya waliofikia umri wa miaka sabini na themanini, nimeshuhudia nyuso zao na uzuri wao kuharibika, wanateseka na maumivu kutokana na mitazamo ya kukirihisha kutoka kwa wale ambao walikuwa wanategemea kutoka kwao kuvutiwa na kupendezwa ni kwa kuwa hawakulinda heshima yao siku za ujana wao. Naam, hili nililiona kwa yakini nikalia juu ya hali yao yenye kuumiza kilio kikubwa kilichowazindua baadhi ya wenzangu jela wakanijia haraka wakiniuliza.

Nikawaambia: “Niacheni sasa na hali yangu, nendeni niacheni”

Ndiyo, nilichokiona ni hakika na sio mawazo ya kufikirika, kama kitakavyo kuja kiangazi hiki na mapukutiko na majira ya baridi hakika kilichopo nyuma ya kiangazi hiki cha ujana na nyuma ya majira ya mapukutiko ya uzee ni majira ya baridi ya kaburi na barazakhi. Lau ingeyumkinika kuonesha matukio fulani ya baada ya miaka hamsini ya mustakabali kama inavyoyumkinika hivyo kwa matukio ya miaka hamsini iliyopita – kwa kifaa kama kifaa cha sinema – na kuhudhurishwa matukio ya watu wa upotevu na hali zao katika mustakabali hivyo wangekirihika na kuumia na kulia kilio kichungu kwa hayo wanayoyafurahia hivi sasa na kuburudika nayo katika mambo yaliyoharamishwa.

Na nilipokuwa nimezama katika kutafakari, na kugeukia yanayoonekana katika kioo cha kimaanawy yaliyohudhurishwa mbele yangu katika jela ya (Eskişehir), ikasimama mbele yangu haiba ya kimaanawy kana kwamba inawakilisha shetani wa kibinadamu na kulingania kwenye usafihi na kuchuuza upotevu akiniambia: “Tunataka kustarehe na starehe zote za maisha na kuwastarehesha wengine kwayo tuache na hali yetu na jiepushe nasi”.

Nikamjibu kwa kusema: “Maadamu unajitupa katika mikono ya upotevu na usafihi kwa ajili ya starehe ndogo hali ya kusahau umauti na bila kuyajali, kwa hiyo tambua kuwa: Hakika (wakati uliopita) wote – kwa mujibu wa upotevu wako – umekufa umeteketea na kutokomea katika kutokuwepo, ni eneo kubwa la makaburi la kuogofya, mizoga imeoza na athari zimechakaa, kwa hivyo ikwa una gao la akili au ukiwa una moyo wenye kutweta uhai, hakika maumivu yanayotokana – kwa mujibu wa upotevu wako – na umauti wa milele, na kutokana na aina ya utengano usiokuwa na mipaka kwa ndugu na wapenzi wako wasiohesabika yanaondoa starehe hiyo ndogo yenye kulewesha ambayo unaionja katika kipindi kifupi mno.

Na kama ilivyo (Muda uliopita) haupo kulingana na wewe, (Mustakabali) pia kwako haupo na hii ni kwa kutokuamini kwako, bali ni uwanda wa kutisha wenye giza mfu. Hakuna yeyote kati ya waliopo masikini atakuja na kudhihiri katika uwepo – kupitia muda uliopo – isipokuwa mnyongaji wa umauti atamkamata na kumtupa kwenye kukosekana. Na wewe kwa kuwa umefungamana na nyakati hizo – kwa kulingana na akili yako – hakika mustakabali unamimina katika kichwa chako chenye kukufuru mvua ya balaa ya machungu yenye kuumiza na shaka kubwa na migongano mikali hadi kufanya starehe zako zote ndogo za kisafihi ni athari baada ya kuwa ni zenye kuonekana.

Lakini punde tu utakapo tupilia mbali njia ya upotevu na kuacha mwenendo wa usafihi kwa kuingia katika ngome ya imani ya uhakikisho, kwa hali ya kunyooka juu yake hata uone kwa nuru ya imani kwamba wakati huo uliopita kitambo sana sio kuwa haupo na wala sio mazikoni panapoozesha na kuteketeza kila kitu bali ni ulimwengu wa kinuru hasa ambao unageuka kuwa ni mustakabali, nao ni uwanda wa kungojelea roho zilizobaki zenye kutazamia ufufuo kwa kuingia katika Firdausi ya furaha ya milele iliyoandaliwa kwao; kwa hiyo inakuonjesha na hali ya kuwa ukingali duniani – ladha ya pepo ya kimaanawy kwa kadiri ya kiwango cha imani yako. Kama ulivyo mustakabali sio wenye kuumiza wala kutia dhiki wala sio mahali pa upweke wala sio bonde la giza la kuogofya bali huo kwa nuru ya imani ni mafikio ya furaha za milele za mwingi wa rehema mwenye kurehemu mwenye utukufu na ukarimu, ambaye rehema yake imekienea kila kitu na ukarimu wake umezungukia kila kitu. Kama Allah (s.w) alivyotandika majira ya machipuo na mapukutiko kuwa ni meza mbili zilizojaa aina mbalimbali za neema na vyakula, basi amekunjua (s.w) meza za dhifa zake za fahari katika kasiri hizo ndefu na amefungua maonesho ya hisani yake na neema zake zenye kuenea huko na watu wanatiwa shauku kuzielekea bali wanapelekwa huko.

Naam, hivi ndivyo aonavyo muumini katika kioo cha kiimani – kila mmoja kulingana na daraja yake – na anayo nafasi ya kuhisi kitu katika ladha za hizo neema za kudumu. Kwa hivyo, ladha ya hakika safi ambayo haitibuliwi na maumivu hakika iko kwenye imani tu na kwa imani peke yake inayumkinika kuipata.

Na kuna maelfu ya matunda matamu ya kiimani katika dunia hii na maelfu ya matokeo na faida isipokuwa sisi tutabainisha moja kati ya hizo kwa mfano:

Jenga taswira – kwamba mtoto wako wa pekee unayempenda sana amelala kitandani ana machungu ya kukaribia umauti, na wewe umezama katika fikra ya kukata tamaa yenye uchungu na kuumia maumivu makali sana kutokana na kufariki kwake kwa milele kwenye maumivu. Jenga taswira –  ukiwa katika hali hiyo ya kukatisha tamaa – tahamaki daktari bingwa – kama Hidhiri au Luqman – anakuja na kumnywesha mtoto dawa yenye kupambana na sumu ghafla anafungua macho yake kwa furaha kufurahikia maisha na ameokoka kutokana na umauti. Furaha yako unadhani itakuwaje.?

Hali ni vivyohivyo kwa wale mamilioni ya waliozikwa katika makaburi ya muda uliopita unaowapenda – kama mtoto huyu – mapenzi makubwa na kufungamana nao kwa mahusiano. Wakati ambo wao wanakaribia kuteketezwa na kutoweka katika uwepo katika makaburi ya muda ulio pita – kwa mtazamo wako – tahamaki hakika ya imani inamulika nuru kupitia dirisha la moyo – kama alivyofanya Luqman Al-hakim kwa yule mtoto – katika eneo lile pana la makaburi ambalo linadhaniwa kuwa ndio kituo cha kunyongea. Na ghafla wafu wako wima wakiwa hai kwa nuru ile – katika ulimwengu wa Barazakhi – wananadi kwa ulimi wa hali: (Sisi sio wafu na hatutakufa kamwe na tutakutana hivi karibuni).

Naam, kama uponaji wa mtoto uletavyo furaha na shangwe visivyo na mpaka baada ya kukata tamaa, mambo ni hivyohivyo hapa katika yanayotufanya tuwe na yakini kuwa imani – kwa kuleta kwake furaha hii katika dunia yetu hii – inathibitisha kwamba hakika yake ni mbegu inabeba katika uchangamfu kama ingechukua umbo ingemea juu yake pepo maalum kwa kila muumini na ingekuwa kwake mti wa tuba.

Hivi ndivyo nilimwambia yule shetani mkaidi, isipokuwa alinishupalia kwa kusema: (Tuache tuishi japo kama wanyama, tukighafilika na yanayoenda katika mazingira yetu katika mambo haya makini, na tupitishe maisha yetu kwa ladha ya upuuzi na burudani ya mchezo).

Nikamjibu: Hakika wewe hulinganishwi na mnyama, na hutokuwa mithili yake, kwa kuwa mnyama hana kinachomfikirisha muda uliopita na mustakabali. Mnyama haoni maumivu na masikitiko kwa yale yaliopita wala haimjii dhiki wala kuhofia mustakabali kwa hiyo anapata ladha yake kamili hivyo anamshukuru Muumba wake mkarimu. Bali hata mnyama aliyeandaliwa kwa ajili ya kuchinjwa hahisi isipokuwa maumivu ya kisu kikipita kwenye koromeo lake, kwa haraka hisia hii huondoka, basi anaokoka na maumivu hayo.

Eh! rehema na huruma iliyoje ya Allah (s.w) ukubwa wake uliyoje kwa kudhihiri katika kuficha ghaibu na kusitiri misiba na mabalaa na hasa kwa wanyama.

Lakini ewe mwanadamu kimekwishatoka kitu katika muda wako uliopita na mustakabali wako katika ghaibu kwa hukumu ya akili uliyo nayo, wewe umenyimwa kabisa yale wanayoneemeka nayo wanyama katika raha na utulivu kwa kuteremshwa pazia la ghaibu mbele yao, majuto na masikitiko yatokanayo na yaliyopita na aina ya utengano wenye kuumiza na hofu zitokanazo na mustakabali vinaondosha starehe yako ndogo na kutokomeza na kukutosa katika ngazi ya chini mno kuliko mnyama kwa upande wa starehe. Madhali hakika ni hivi, si juu yako kwa hiyo isipokuwa kujiweka mbali na akili yako na kuitupa nje na uihesabu nafsi yako kuwa ni mnyama uokoke, au uinawirishe akili yako kwa nuru ya imani na usikilize sauti tamu ya Qur’an tukufu uwe juu zaidi kuliko mnyama ukivuna ladha safi tohara na hali ukingali katika dunia hii yenye kutoweka.

Nikamshinda kwa hoja hii lakini alipinga na kusema: (Kwa uchache tutaishi mfano wa makafiri wa kigeni)

Nikamwambia kumjibu: (Hutakuwa hata mfano wa hao makafiri wa kigeni, kwa sababu wao wakimkanusha nabii mmoja wao wanaamini manabii wengine. Na hata kama hawamjui yeyote katika manabii wanaweza wakawa na imani ya Allah (s.w). Na kama hawakuwa na imani hii vilevile huenda wanacho cha kuwafikisha katika ukamilifu katika huluka njema na tabia za kiutu. Ama ikiwa Mwislamu atamkanusha nabii wa mwisho (s.a.w), na kukanusha dini ambayo hakuna dini nyingine isiyo kuwa hiyo ya haki na kujumuisha mambo yote na kuasi kutoka katika duara la uongofu wake na kuweka shingo yake nje yake, hatamridhia nabii mwingine bali hatoikubali imani ya Allah (s.w) kwa sababu hakujua manabii wengine na wala kupata uongofu wa kumwamini Allah (s.w), isipokuwa kwa kupitia kwake (s.a.w) na kwa kufikisha, kuelekeza na mwongozo wake. Kwa hiyo hakibaki chochote kati ya hivyo moyoni mwake isipokuwa kwa kumuamini yeye (s.a.w). Hii ndiyo sababu watu walikuwa tokea zama za kitambo sana katika dini nyingine wanaingia katika Uislamu makundi kwa makundi, wakati ambapo haikutokea kuwa Mwislamu mmoja  akawa Yahudi wa kweli au Mmajusi wala Mnasara, na huenda akawa kafiri mharibifu wa imani na mwenendo mwenye kudhuru nchi na waja).

Na kwa hivi nilisimamisha hoja juu ya mkaidi yule ya kwamba hawezi kushabihiana hata na makafiri wa kigeni. Na alipokuwa hakupata cha kuegemea alirudi nyuma na kukengeukia kwenye jahanamu na ubaya ulioje wa mafikio.

Basi enyi ndugu zangu mliokusanyika katika madrasa hii ya Yusuf! Madhali hakika ndiyo hii, na Risale-i Nur imeeneza nuru yake – na haijaacha kuwa – tungu miaka ishirini ikiwa inavunja ukaidi wa wapingaji na kuwafanya kuwa hawana budi kuamini, basi juu yetu kushikamana na imani na njia iliyonyooka nyepesi yenye manufaa iliyo salama kwetu na mustakabali wetu na Akhera yetu na nchi yetu na uma wetu. Hii ni kwamba tusipoteze wakati wetu katika yasiyo na maana katika mawazo ya kufikirika na matarajio duni, bali tuuhuishe kwa kusoma sura tuzijuazo katika Qur’an tukufu nyakati za usiku na mchana, na kwa kujifundisha maana zake kutokana kwa ndugu zetu wenye kuzitendea kazi, na kulipa swala za faradhi zilizotupita na kwa kuvuna tabia njema kutoka miongoni mwetu, huenda Allah (s.w) akatujaalia kuwa katika wanaopandikiza katika jela hii miche ili itokee kuwa ni miti yenye kunufaisha, na tujibidiishe kwa juhudi ili maafisa wa jela wawe walimu waelekezi wakiwaandaa watu kwenda peponi kutoka katika madrasa hii ya Yusuf, na waangalizi wazuri wakisimamia kuwaelekeza vizuri na siyo maaskari wa mateso dhidi ya wahalifu wauaji.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.