Msingi Wa Tatu

Nini hekima ya Miiraji?

Jibu:

Hekima ya Miiraji ina hadhi ya juu sana kiasi kwamba fikira ya kibinadamu inashindwa kuitambua, na ina kina kirefu sana kiasi inashindikana kuifikia, nayo ni nyeti na nyororo sana kwa kiasi ni vigumu kwa akili pekee kuiona.

Lakini licha ya kutokuwa na uwezo wa kutambua hakika za hekima hii na kuzifahamu, inawezekana kutambua kuwepo kwake kwa ishara kama ifuatavyo:

Kwa ajili ya kudhihirisha nuru ya umoja wake Allah (s.w), na kudhihirika kwa upekee wake katika tabaka za viumbe, muumba wa viumbe na mola mlezi wa ulimwengu amemteua mtu mwenye sifa za kipekee kwenda Miiraji, ambaye ni kama uzi wa mawasiliano ya kinuru kati ya ukomo wa tabaka za wingi wa vilivyopo hadi katika chanzo cha umoja, akimfanya kuwa ni mlengwa wa mazungumzo yake, kwa niaba ya viumbe vyote, akimfundisha yeye na kwa kumtumia yeye, makusudio yake ya kiungu kwa niaba ya wenye utambuzi. Ili ashuhudie kwa macho yake uzuri wa ufundi wake na ukamilifu wa Uungu wake (Hali ya kuwa Bwana mlezi wa walimwengu) katika kioo cha viumbe vyake, na kuwashuhudisha wengine athari za uzuri na ukamilifu.

Kwa hiyo, madhali Bwana mola mlezi wa ulimwengu ana uzuri wa hali zote na ukamilifu wa hali zote – kwa ushahidi wa athari zake na alivyovitengeneza – na uzuri na ukamilifu ni vyenye kupendwa kwa dhati ya viwili hivyo, basi mmiliki wa  uzuri huo na ukamilifu ana mahaba yasiyo na ukomo ya uzuri wake na ukamilifu wake, na mahaba hayo yanadhihiri kwa sura tofauti na mitindo mingi katika vilivyotengenezwa, Allah (s.w) huelekeza mahaba yake kwa vitengenezwa vyake, kwa ayaonayo kwenye vitu hivyo katika athari ya uzuri wake na ukamilifu wake.

Na ilipokuwa kipenzi zaidi katika alivyovitengeneza na chenye hadhi ya juu mno kuliko vyote ni wenye uhai, na vipenzi zaidi kati ya wenye uhai ni wenye utambuzi – kwa kuzingatia mkusanyiko wa maandalizi – ni ndani ya mwanadamu – na mwanadamu kipenzi zaidi kwa hiyo ni yule mtu mmoja ambaye maandalizi yake yamekuwa wazi kikamilifu akadhihirisha kikamilifu vielelezo vya makamilifu yake (s.w), ambavyo vimeenea katika alivyovitengeneza na kudhihiri humo.

Na kama hivi, basi fundi wa vilivyopo kwa ajili ya kushuhudia aina zote za kudhihiri kwa mahaba yaliyotawanywa katika vilivyomo vyote, katika nukta moja, ndani ya kioo. Na kwa ajili ya kudhihirisha aina zote za uzuri wake – kwa siri ya upekee – amemteua ambaye ni tunda lenye nuru katika mti wa uumbaji na ambaye moyo wake unazingatiwa kuwa ni kokwa yenye uwezo wa kuhifadhi hakika za mti huo za kimsingi, akamteua kwa Miiraji, yeye ni kama kamba ya mawasiliano ya kinuru baina ya mbegu na tunda, yaani kutokea chanzo cha awali hadi kwenye ukomo, akionesha hali ya kupendwa kwa mtu huyo wa kipekee mbele ya viumbe, akampandisha katika hadhira yake, na akampa utukufu kwa kuona uzuri wake, na kumkirimu kwa kumwamrisha, na akamkabidhi jukumu la kufanya hekima takatifu aliyo nayo ienee kwa wengine.

Tutaitazama hekima hii ya kiungu kupitia mifano miwili:

Mfano wa Kwanza:

Nao ni yale tuliyoyabainisha kwa upambanuzi katika (Neno la kumi na moja) kama ifuatavyo:

Ikiwa itakuwepo hazina nyingi mno za mfalme zenye ujazo wa aina zisizo na hesabu za johari za thamani na almasi za kipekee, na zikawa na ufundi wa hali ya juu katika maajabu ya kiufundi, naye ana maarifa mapana kwa sanaa mbali mbali za ajabu zisizohesabika, na ujuzi kamili kuzungukia vyote hivyo, na uoni wenye kuenea juu ya elimu za ajabu zisizo na mpaka, na elimu kamili juu ya vitu hivyo. Hapana shaka kwamba mfalme huyo mwenye maajabu na fani pana atataka kufungua maonesho ya jumla, ataonesha humo bidhaa zake za thamani – kwa kuwa kila mwenye uzuri na ukamilifu anataka kushuhudia na kuonesha uzuri wake na ukamilifu wake – na hii ili aelekeze macho ya wakazi katika kuona adhama ya ufalme wake na awashuhudishe mmemetuko wa utajiri na yaliyofurutu ada ya ufundi wake na maajabu ya maarifa yake, hiyo ili ashuhudie uzuri wake na ukamilifu wake wa kimaanawy kwa pande mbili:

Upande:

Kwa uoni wake mkali madhubuti, na

Mwingine:

Kwa uoni wa wengine.

Kwa msingi wa hekima hii, mfalme huyu kwa vyovyote ataanza kusimamisha kasri kubwa pana ya haiba, na kuigawanya kwa ustadi katika duru na tabaka na vigawanyo vikubwa, hali ya kupamba kila sehemu kwa johari na mapambo ya hazina zake mbali mbali na kuiweka uzuri wa kiwango cha juu kinachofanywa na mkono wa ufundi wake na maridadi zaidi, akipangilia kwa mipangilio madhubuti zaidi ya sanaa yake na hekima yake. Na baada ya hapo atatandika meza pana zilizoamirishwa, kwa kinachowiana na kila kundi, akiandaa kwa meza hizo karamu ya wageni ya jumla ya ukarimu yenye kusheheni sampuli za neema zake na aina za vyakula vyake vitamu.

Kisha anawaita raia wake katika karamu hii ya ukarimu, na kushuhudia makamilifu yake ya ajabu, na mmoja wao anamjaalia kuwa ni mtume kati yake na wao, na anamwita kwake, hali akipita kutoka kwenye tabaka za chini mno hadi za juu yake, na kumwendesha duru hadi duru, na tabaka juu ya tabaka, akimshuhudisha vituo vya kazi ya ufundi huo wa ajabu na ghala za kuhifadhia mavuno yanayopatikana duniani, hadi anamfikisha katika duru yake maalum, na anampa utukufu wa kumkubalia katika hadhara yake, akimdhihirishia dhati yake yenye kheri nyingi, ambayo ndio asili ya makamilifu yake yote. Na kumjulisha makamilifu yake ya kidhati na kumwongoza katika hakika za kasri. Na kumtunuku jukumu la Mwelekezi kiongozi wa watazamaji na kumtuma kwao ili awajulishe wakazi, mtengenezaji wa kasri, kwa yaliomo katika kasri ikiwemo nguzo za nakshi na maajabu ya ufundi wake. Na kumjulisha alama zilizomo kwenye nakshi na ishara zilizomo kwenye kazi za ufundi, na kuwatambulisha wenye kuingia kwenye kasri, ni nini haya marembo yaliyopangiliwa na nakshi zilizowekwa kwa vipimo? na vipi kwamba hizo zinajulisha makamilifu ya mmiliki wa kasri na ufundi wake? na awaongoze katika adabu za kutembea na kutazama na kuwafundisha taratibu rasmi za kuhudhuria mbele ya mfalme mkuu ambaye haonekani. Yote hayo kulingana na yanayomridhisha na anayoyataka.

Na kama hivi – na Allah (s.w) ana mfano wa juu – hakika fundi mtukufu, Mfalme wa azali na milele, ametaka kuona na kuonesha uzuri wake wa hali zote, na makamilifu yake ya hali zote, akajenga kasri hili la ulimwengu kwa namna ya uzuri mno uwavyo, kiasi kwamba kila kilichomo ndani yake kinataja makamilifu yake, kwa ndimi nyingi, na kujulisha uzuri wake kwa ishara nyingi, hata kwamba viumbe vinadhihirisha kwa kila kilichomo ndani yake, na ngapi katika hazina za kimaanawy zimefichwa ndani ya kila jina miongoni mwa majina ya Allah mazuri, na ngapi katika yenye upole yenye kujificha ndani ya kila anuani takatifu!. Bali huku kujulisha kwake kuna uwazi uliofanya sanaa zote na elimu pamoja na kanuni zake zote, zinashindwa kufikia yaliyomo kwenye kitabu cha ulimwengu, katika dalili za ajabu tangu zama za Adamu (a.s), hali ya kujua kwamba kitabu hicho hakijaweka wazi bado moja ya kumi ya maana ya majina na makamilifu ya kiungu.

Kama hivi basi fundi mwenye utukufu, uzuri na ukamilifu ambaye amesimamisha kasri hii ya ajabu ikiwa ni maonesho ya kuona uzuri na ukamilifu wake wa kimaanawy na kuonesha, hekima yake inahitajia kumjulisha mmoja wa wenye utambuzi katika Ardhi maana ya aya za kasri hilo, ili maana yake yasibakie kuwa ni mchezo yasiyo na manufaa kwao. Na ampandishe katika ulimwengu wa juu ambao ni vyanzo vya maajabu yaliyomo kwenye kasri hilo, na hazina za mavuno yaliyomo. Na kumnyanyua hadi daraja ya juu iliyo juu ya viumbe wake wote na kumpa utukufu wa kukaribia hadhara yake na kumtembeza katika limwengu za akhera akimkalifisha majukumu ili awe mwalimu kwa waja wake wote. Hali ya kuwalingania kwenye ufalme wa Uungu wake. Akiwafikishia kazi za mambo ya kuridhiwa na Uungu wake. Akiwafasiria aya zake za kimaumbile kwenye kasri. Na mifano kama hiyo ya majukumu mengine ambayo Allah (s.w) hubainisha kwayo kwa walimwengu wote, fadhila za mteule na ukubwa wa cheo chake kwa nishani alizomvika za miujiza, na awafundishe kwa Qur’an tukufu kwamba yeye ni mfikishaji mkweli na mkalimani mwaminifu.

Na kama hivi, tumebainisha hekima chache za Miiraji kati ya hekima zake nyingi, na hiyo kwa mwanga wa mfano huu, na ni juu yako kupimia hekima zilizobaki kwa mfano wake.

Mfano wa pili:

Mtu mjuzi akitunga kitabu cha muujiza ambapo kila ukurasa wa kitabu hicho umesheheni hakika za yaliyomo kwenye vitabu mia moja, kila mstari wa kitabu hicho unabeba maana nyororo ya yaliomo kwenye kurasa mia moja, na kila neno lake linabeba hakika zilizomo kwenye mistari mia moja, na kila herufi yake inaelezea maana ya yaliomo kwenye maneno mia moja. Maana yote ya kitabu hicho na hakika zake zote vimekuwa, vinaashiria katika makamilifu ya kimaanawy ya mwandishi huyo wa ajabu wa muujiza na vinaelekea upande wa makamilifu hayo.

Jambo likiwa hivi, hapana shaka basi kwamba huyo mwandishi wa muujiza hakiwachi kitabu chake hiki cha muujiza bila faida na wala hafungi milango ya hazina hii isiyomalizika, bali ni muhali kuiacha bure bila lengo nyuma yake. Kwa hiyo atawaelimisha watu maalum maana ya kitabu hicho, ili kisibakie kitabu hicho cha thamani chenye kupuuzwa bila maana, na ili yadhihiri makamilifu yake yaliyojificha, na kupata njia yake kuelekea kwenye ukamilifu, na kushuhudisha uzuri wake wa kimaanawy ushuhudiwe ili apendwe na kupendezeshwa mwenyewe, yaani atamjulisha mmoja misamiati ya kitabu hicho, kwa maana yake yote na hakika zake akimsomesha somo kwa somo kutokea ukurasa wa mwanzo humo hadi ukurasa wa mwisho. Hadi amtunuku shahada juu ya hilo.

Na kama hivi, mtia sura mzuri (s.w), ambaye ameandika viumbe hivi kudhihirisha makamilifu yake, na kuweka wazi uzuri wake na hakika za majina yake matakatifu, ameviandika kwa uandishi wa ajabu, hakuna ajabu zaidi ya hiyo, kwani vyote vilivyomo bila ya mpaka katika pande zilizopo, vinajulisha juu ya majina yake mazuri na sifa zake tukufu na makamilifu yake ya hali zote na kuyaelezea.

Na katika yanayojulikana, kwamba kitabu, vyovyote kitakavyokuwa, kama hakijulikani maana yake, kitapeperuka kama vumbi lenye kutawanywa, na thamani yake itaporomoka hadi kwenye kutokuwepo. Basi vipi kitabu kama hiki ambacho kila herufi ndani yake inabeba maelfu ya maana? Katu thamani yake haiwezi kuporomoka na haiwezi kupeperuka kama vumbi katu! Mwandishi wa kitabu hicho cha muujiza kwa vyovyote atakifundisha na kujulisha sehemu yake, kulingana na utayari wa kila kundi, ambaye mwenye uoni  enevu zaidi na utambuzi jumuishi zaidi na utayari mkamilifu zaidi.

Na kwa ajili ya kudurusisha mfano wa kitabu hiki na kukielimisha kiujumla na yenye kukusanya hakika zake zote, hekima inahitajia mwendo na kupita katika upeo wa hadhi ya juu, yaani inalazimu kushuhudia na mwendo kuanzia tangu mwisho wa tabaka za vilivyomo vingi, ambao ndio mwanzo wa kurasa za kitabu hiki, na kukomea katika duru ya upekee ambao ndio ukomo wa kurasa zake.

Na kama hivi, unaweza kushuhudia kitu katika hekima za hadhi ya juu ya Miiraji katika mwanga wa mfano huu.

Na sasa tunamgeukia kafiri ambaye yupo katika nafasi ya kusikiliza, na tusikilize yanayotembea moyoni mwake ili tushuhudie ni hatua gani ambayo amechanganyikiwa nayo.

Yanayopita kwenye mawazo ni kuwa moyo wake unasema: Nimeanza kupiga hatua katika njia ya imani, lakini kuna mishkeli mitatu na magumu matatu siwezi kuitatua na kuifahamu!

Kwanza:

Kwa nini hii Miiraji tukufu imefanywa mahususi kwa Muhammad (s.a.w).

Pili:

Vipi awe nabii huyu mtukufu (s.a.w) kuwa ni mbegu ya hivi viumbe? Mnaposema: Hakika ya viumbe vimeumbwa kutokana na nuru yake na wakati huo huo yeye ndiye tunda la mwisho kabisa katika matunda ya viumbe na mwenye nuru zaidi! Maneno haya yanafidisha nini?.

Tatu:

Mnasema katika mliyotangulia kuyabainisha: Hakika kupanda Miiraji katika ulimwengu wa juu, hakika ilikuwa ni kwa ajili ya kushuhudia maeneo ya kazi na viwanda msingi kwa athari zilizomo ulimwenguni, na kwa ajili ya kuona hazina na ghala ya matokeo ya matendo, maneno haya yana maana gani?

Mushkeli wa kwanza

Jibu:

Hakika mushkeli wenu huu wa kwanza, umetatuliwa kwa upambanuzi katika maneno ya thelathini na tatu ndani ya kitabu (Maneno), isipokuwa sisi hapa tutaashiria kwa ufupi tu kwa sura ya faharisi ya muhtasari ya makamilifu ya Mtume (s.a.w), na dalili za unabii wake, na kwamba yeye ndiye Mstahiki wa Miiraji hii tukufu.

Kwanza:

Hakika vitabu vitakatifu, Taurati, Injili na Zaburi vina bishara za unabii wa Mtume Mtukufu (s.a.w), na ishara kwa hilo, pamoja na kukutana na upotoshaji katika zama zote, na katika zama zetu hizi Mwanazuoni mhakiki Husein Al-Jisri ametoa bishara mia moja na kumi na kuzithibitisha katika kitabu chake kinachoitwa (Al-Risalat al-Hamiidiyya).

Pili:

Imethibiti kihistoria na kupokewa kwa masimulizi sahihi,  bishara nyingi walizobashiri makuhani mfano wa makuhani wawili mashuhuri: Shikki na Sateeh. Muda mfupi kabla ya kupewa utume mtume (s.a.w) na wamepasha habari kuwa yeye ni nabii wa zama za mwisho.

Tatu:

Kilichotokea usiku wa kuzaliwa kwake (s.a.w) kama kuanguka masanamu ndani ya Al-Kaaba na kupasuka vibaraza vya kisra na mfano wa hayo katika mamia ya Irhaasati na ya kufurutu ada mashuhuri katika vitabu vya historia.

Nne:

Kutoka maji kati ya vidole vyake vitukufu na kulinywesha jeshi kwa maji hayo, na kunung’unika kwa shina kavu lililokuwa katika msikiti wa Mtume (s.a.w) kwa ajili ya kutengana nalo na kutoa sauti ya kilio mbele ya kundi kubwa la masahaba watukufu, na kupasuka kwa mwezi kama ilivyoeleza aya tukufu:

وَانشَقَّ الْقَمَرُ Qur’an, 54:1.

Na mfano wa hiyo katika miujiza yenye kuthibiti mbele ya wanazuoni wenye kuhakiki na ambayo inafikia elfu imethibitishwa na vitabu vya Sira na historia.

Tano:

Wameafikiana maadui na wapenzi kwa lisilo na shaka ndani yake kwamba tabia njema anazojipamba nazo nabii Muhammad (s.a.w) ni katika daraja za juu sana, na mambo mazuri aliyosifika nayo katika da’wa yake ni katika ngazi za juu sana, hayo yanashuhudiwa na kuishi kwake na watu na mwenendo wake, na kwamba sharia yake maridadi inajumuisha mambo mazuri yaliyo kamilika mno, hayo yanashuhudiwa na tabia njema katika dini yake nyoofu.

Sita:

Tumeashiria katika ishara ya pili ya (Neno la kumi) kwamba Mtume mtukufu (s.a.w) ndiye ambaye aliyeonesha kiwango cha juu sana cha uja na chenye hadhi ya juu kabisa katika utumishi mtukufu katika dini yake kwa kuitikia utashi wa Allah (s.w) katika kudhihiri kwa Uungu wake kwa muktadha wa hekima.

Ni kama hivyo, iko wazi – yeye ni mjulishaji mtukufu zaidi juu ya uzuri katika ukamilifu wa hali zote wa Muumba wa ulimwengu na mtambulishaji bora zaidi aliyeitikia utashi wa Allah (s.w) katika kudhihirisha uzuri huo kupitia mjumbe kama hekima na hakika vinavyohitajia hilo.

Na kwamba yeye yuko hivyo – kama inavyoshuhudiwa – mjulishaji mtukufu zaidi juu ya ukamilifu wa ufundi wake katika uzuri wa hali zote wa Mtengenezaji wa Ulimwengu, na kwa ulingano mtukufu zaidi na sauti yenye mvuto zaidi, akaitikia utashi wa Allah (s.w) katika kuleta macho kuangalia ukamilifu wa ufundi wake na kuutangaza.

Na kwamba vivyo hivyo – kwa dharura – yeye ni mkamilifu zaidi aliyetangaza kuliko wote ngazi zote za Tawhiid, akaitikia utashi wa Bwana mlezi wa walimwengu katika kutangaza upekee katika tabaka za wingi wa viumbe.

Na yeye yuko hivyo – kwa ulazima – ni kioo chenye kuonesha zaidi na kisafi mno kwa kuakisi mazuri ya uzuri wa Mmiliki wa ulimwengu na yaliyo laini ya uzuri wake uliotakasika na upungufu – kama zinavyoashiria hilo athari zake za kupendeza – na yeye ndiye mbora aliye mpenda na kumpendezesha, akitikia utashi wake (s.w) katika kuona uzuri huo mtakatifu na kumwonesha kwa kulingana na hakika na hekima.

Na kwamba yeye yuko hivyo – kwa uwazi – ni mkuu zaidi ambaye ametambulisha yaliyoko kwenye hazina za ghaibu ya fundi wa ulimwengu huu, hazina hizo zilizojaa maajabu mno ya miujiza na johari za thamani mno, na yeye ni mbora aliyetangaza hayo na kuyasifia, akaitikia utashi wake, katika kudhihirisha hazina hizo zenye kufichwa.

Na kwamba yeye yuko hivyo – kwa uwazi – ni mwelekezi mkuu wa Qur’an tukufu kwa majini na wanadamu bali kwa wenye roho na malaika, na mtukufu aliyebainisha maana za athari za mtengenezaji wa viumbe hivi ambavyo amevipamba kwa mapambo mazuri sana na kuwaweka humo wenye Utambuzi katika viumbe vyake ili watazame vema na kutafakari na kuzingatia, akaitikia utashi wake (s.w) katika kubainisha maana ya athari hizo na makadirio ya thamani yake kwa watu wa fikra na kushuhudia.

Na kwamba yuko hivyo – kwa uwazi – ni mbora zaidi aliyefunua hakika za Qur’an kuhusu maana ya makusudio katika mageuzo ya viumbe na shabaha yake, na mkamilifu zaidi aliyefumbua fumbo la vilivyokuwepo. Nayo ni maswali magumu matatu: Nani wewe? Unatoka wapi? Na unakwenda wapi? akaitikia utashi wake (s.w) katika kufumbua talasimu (fumbo) hilo lililofumbwa kwa wenye utambuzi kupitia mjumbe.

Na kwamba yeye yuko hivyo – kwa uwazi – ni mkamilifu aliyebainisha makusudio ya kiungu kwa Qur’an tukufu na mbora aliyeweka wazi njia katika anayoyaridhia mola mlezi wa walimwengu, akaitikia Utashi wake (s.w) katika kutambulisha analolitaka kutoka kwa wenye utambuzi na anayoyaridhia kwao  kwa kupitia mjumbe, baada ya kuwa amejitambulisha kwao kwa kazi zake zote alizotengeneza za ajabu na kuzipendesha kwao kwa neema ghali alizowaenezea.

Na yeye yuko hivyo – kwa uwazi – ni mtukufu zaidi aliyetimiza jukumu la utume kwa Qur’an tukufu, na kuitekeleza kikamilifu, katika ngazi ya hadhi ya juu na sura fasaha zaidi na mtindo mzuri zaidi, akaitikia Utashi wa Bwana Mlezi wa walimwengu,  katika kugeuza uso wa mwanadamu huyu kutoka kwenye wingi na kwenda kwenye umoja na kutoka katika chenye kutoweka na kwenda kwenye cha kubaki, ni mwanadamu huyo ambaye Allah (s.w) amemuumba kuwa ni tunda la ulimwengu wote na kumpa matayarisho yenye kuenea ulimwenguni kote na akamuandaa kwa ajili ya uja wa kiujumla na akampa mtihani na hisia zenye kuelekea kwenye wingi na dunia.

Na kwa kuwa kwamba watukufu zaidi kati ya vilivyomo ni wenye uhai, na wabora zaidi kati ya walio hai ni wenye utambuzi, na watukufu zaidi kati ya  wenye utambuzi ni binadamu wa kweli wakamilifu, kwa hiyo yule ambaye ametekeleza katika wanadamu wenye kutukuzwa majukumu yale yaliyotajwa huko nyuma na kuyapa haki yake, hapana shaka kwamba huyo atapandishwa – Miiraji tukufu – atakuwa mkabala wa pinde mbili – au karibu zaidi, na atagonga mlango wa furaha ya milele na atafungua hazina za rehema kunjufu, na ataona hakika za imani ya ghaibu kuona kwa kushuhudia, na nani atakuwa huyo kama si huyo Nabii mkarimu (s.a.w)?.

Saba:

Mwenye kuzingatia ataona katika hivi vilivyotengenezwa vilivyotawanywa katika ulimwengu kwamba ndani yake kuna utendaji wa uzuri katika ukomo wa uzuri, na tendo la upambaji katika ukomo wa kupendeza, basi ni jambo la dhahiri kwamba mfano wa upendezeshaji huu na upambaji huu vinajulisha kuwepo utashi wa kupendezesha na kukusudia kupamba kwa fundi wa hivyo vilivyotengenezwa. utashi huo mkali unajulisha kwa vyovyote kuwepo kwa utashi wenye nguvu wa hadhi ya juu, na mahaba matakatifu kwa fundi huyo kwa ufundi wake.

Kwa hiyo ni katika yaliyo wazi kuwa kiumbe mpendwa kabisa mbele ya muumba mkarimu ambaye anapenda vitu vyake alivyovitengeneza ni yule anayesifika kwa jumla ya sifa hizo, na anayedhihirisha katika dhati yake sifa laini za ufundi kikamilifu, na anayezitambua na kuzitambulisha, na anayependezesha nafsi yake na kutambulisha – kwa mshangao na kuthamini – uzuri wa vilivyotengenezwa vinginevyo.

Basi nani ambaye amejaalia mbingu na Ardhi inagonga sauti ya mwangwi (Subhanallah, Maashaallah, Allahu Akbar) katika dhikiri za kushangaa kwa kupendezwa na tasbihi na takbira kwa yule anayepangilia vilivyotengenezwa kutokana na sifa za pekee zinazovipamba na mazuri ya kuvipendezesha na yalio nyororo na makamilifu yanayovinawirisha? Na ni nani ambaye ametetemesha kwa naghama za Qur’an tukufu ikavutika bara na bahari kuielekea katika shauku kubwa  kutokana na kuhisi uzuri na kuthamini katika kutafakari na kuitangaza, katika dhikiri na tahalili? Ni ipi itakayo kuwa hiyo dhati yenye kubarikiwa kama siyo Muhammad mwaminifu (s.a.w)?.

Na basi mfano wa nabii huyu mtukufu (s.a.w) ambaye katika kitanga cha mema yake huongezwa mfano wa waliofanya umma wake katika mambo mema kwa siri ya: (Sababu ni kama mtendaji). Na ambaye inaongezwa katika makamilifu yake ya kimaanawy swala ambazo umma wote unazitekeleza. Na ambaye humiminwa kwake rehema ya kiungu na mahaba yake ambayo hayapingwi na mpaka wowote, ukiachilia mbali anayoyapata katika matunda ya majukumu ya utume wake aliyoyatekeleza katika thawabu kubwa ya kimaanawy. Naam, Mfano wa nabii huyu mtukufu (s.a.w) hapana shaka kwamba kwenda kwake peponi, na kwenye Sidrat al-Muntaha, na katika kiti cha enzi kitukufu, basi na kuwa ukaribu wa upinde na mshale au karibu zaidi, hakika ni ndio ukweli wenyewe, na hakika yenyewe halisi, na hekima tupu.

Mushkeli wa pili

Ewe uliyekaa katika nafasi ya kusikiliza! hakika hii uliyoifanya kuwa ni mushkeli yenyewe ina kina kirefu, nayo ni ya juu yenye hadhi kiasi akili haiifikii, bali haiikaribii, na pamoja na hivyo huonekana kwa nuru ya imani.

Na sisi hapa tutajaribu kukaribisha kitu kwenye fahamu katika hakika hiyo ya juu kwa baadhi ya mifano, ambayo inasaidia hilo, nayo ni kama ifuatavyo: Vikiangaliwa hivi viumbe kwa mtazamo wa hekima, vinadhihiri kana kwamba ni mti mkubwa na katika maana yake, kama ulivyo mti una matawi, majani, maua na matunda, basi katika ulimwengu wa chini, ambao ni upande wa mti wa uumbaji, inashuhudiwa vilevile kwamba chembe chembe ni sawa na matawi yake, na mimea na miti ni sawa na majani yake, na wanyama kana kwamba ni maua yake, na watu kana kwamba ni matunda yake. Basi kanuni ya kiungu inayopita kwa miti inalazimu kupita vilevile katika mti huu mkubwa, na hii kwa muktadha wa jina la Allah (s.w), (Al-Hakiim). Kwa hiyo kulingana na hekima ni kuwa mti huu wa uumbaji unatokana vile vile na mbegu, na iwe hiyo mbegu ni yenye kukusanya vielelezo na misingi ya limwengu nyinginezo ukiachilia mbali kubeba kwake ulimwengu wa kimwili; kwa sababu mbegu ya kiasili ya viumbe inayokusanya maelfu ya limwengu na chanzo chake haiyumkiniki kuwa ni maada isiyo na uhai katu. Na kwa kuwa hakuna mti usio kuwa na mti wa aina za viumbe ulioutangulia, basi hakika maana na nuru ambayo ni sawa na chanzo na mbegu yake imekuwa mwili kwa tunda katika mti wa viumbe na kuvikwa mavazi ya tunda, na hii ni kwa sababu mbegu haiwi tupu bila nguo daima, kwa hiyo madhali haikuvaa vazi la tunda mwanzoni mwa uumbaji, italivaa mwishoni.

Na madhali mwanadamu ni hilo tunda, na kwamba bora ya matunda ya sampuli ya wanadamu na mwenye nuru zaidi na mzuri zaidi mkuu na mtukufu zaidi na mpole zaidi na mwenye manufaa zaidi ni Muhammad (s.a.w), kama ilivyotangulia kuthibitishwa, ambaye ameleta mtazamo wa jumla ya viumbe kwa fadhila zake, na ambaye amedhibiti nusu ya mtazamo wa nusu ya Ardhi na moja ya tano ya wanadamu katika dhati yake iliyobarikiwa na kukusanya mitazamo ya walimwengu katika mazuri yake ya kimaanawy kwa mahaba, kutukuzana na kupendezwa, hapana budi kwamba nuru ambayo ni mbegu ya kuundika kwa viumbe itakuwa mwili katika dhati yake (s.a.w) na itadhihiri kwa sura ya tunda la hitimisho.

Ewe msikilizaji! usiweke mbali uumbaji wa viumbe hivi vya ajabu vikubwa kutokana na kiini cha kisehemu cha mwanadamu. Hakika Mweza mwenye utukufu ambaye anaumba mti mkubwa wa msonobari, kana kwamba ni ulimwengu kwa dhati yake, kutokana na kokwa yake ndogo, vipi asiumbe, au ashindwe kuumba viumbe kutokana na nuru ya Muhammad (s.a.w)?.

Naam, hakika mti wa viumbe unashabihiana na mti wa Tuba wa peponi, shina lake na mizizi yake imekwenda mbali kwenye ulimwengu wa juu, na matawi yake na matunda yake yako chini chini kuelekea ulimwengu wa chini, kwa hiyo kuna uzi wenye uhusiano wa kinuru kuanzia katika kituo cha tunda chini hadi katika kituo cha kokwa ya asili.

Kwa hiyo Miiraji ya Mtume ni sura na mfuniko wa uzi wa uhusiano huo wa kinuru, ambapo mtume mtukufu (s.a.w) amefungua njia hiyo na kupanda humo kwa uwalii wake, na amerejea kwa utume wake, na kuacha mlango ukiwa wazi, ili waupite mawalii wa umati wake ambao wanamfuata kwa kupita kwa roho na moyo, hivyo kupanda katika njia hiyo ya kinuru chini ya vivuli vya Miiraji ya kiutume, na kupanda humo hadi katika makamo ya juu kila mmoja kulingana na utayari wake na upokeaji wake.

          Na tumetangulia kuthibitisha kwamba fundi mtukufu ameanzisha viumbe hivi na kuvipamba kana kwamba ni kasri la ajabu kwa ajili ya makusudio na shabaha tukufu, basi Mtume Mtukufu (s.a.w) ambaye yeye ndiye Mhimili wa makusudio hayo, na ndio uwanja wake, hapana budi kuwa ndio mahali pa uangalizi wake (s.w) kabla ya kuumba viumbe, na awe ni wa kwanza aliyepata udhihirisho wake (s.w), kwa hiyo yeye ni wa kwanza kimaana na wa mwisho kwa uwepo.

Na kwa kuwa Mtume Mtukufu (s.a.w) ni mkamilifu zaidi wa matunda ya uumbaji na uwanja wa thamani ya matunda yote, na mhimili wa kudhihiri kwa makusudio yote, inalazimu iwe nuru yake ndio ya kwanza iliyopata udhihirisho wa uumbaji.

Mushkeli wa tatu

Hakika hii ina wasaa kiasi cha kutoweza akili zetu za kibinadamu zilizo finyu kuweza kuifahamu, lakini tunaweza kuitazama kutokea mbali.

Naam, hakika mashine za kimaanawy za ulimwengu wa chini, na kanuni zake za kiujumla, hakika ziko katika ulimwengu wa juu. Na kwamba matokeo ya matendo yasiyokuwa na mpaka katika viumbe ambavyo vinaishi ardhini, na hivyo vyenyewe kwa dhati yake ni mkusanyiko wa kazi zilizotengenezwa, na vivyo hivyo matunda ya matendo ambayo wanayatenda majini na watu, vyote hivyo hupatikana katika limwengu za juu vilevile. Hata ishara za Qur’an tukufu na muktadha wa jina la Allah “Al-Hakiim” na hekima inayoingia katika viumbe, pamoja na shahidi za mapokezi mengi na alama zisizo na mipaka, zinajulisha kwamba matendo mema huchukua sura ya matunda ya peponi na matendo maovu huchukua umbo kwa sura ya zaqqumi ya jahanamu.

Naam, hakika vilivyomo vingi vimeenea juu ya uso wa Ardhi ueneaji mkubwa, na mitindo ya uumbaji imetanzuka kwa kiasi kikubwa, kwa kiasi kwamba makundi ya viumbe na sampuli za vilivyotengenezwa ambavyo hubadilika na kwa vitu hivyo ardhi hujazwa na kuachwa tupu yanapita sana vilivyotengenezwa vilivyoenea katika ulimwengu wote.

Na kama hivi, vyanzo vya wingi huu na vijisehemu na madini yake ya msingi, hapana budi kuwa ni kanuni za kiujumla, na midhihirisho ya kiujumla ya majina mazuri, kwa kiasi kwamba mandhari ya kanuni hizo za kiujumla na midhihirisho hiyo ya kiujumla na majina hayo yenye kuzungukia kila kitu, ni mbingu,  ambazo ni rahisi (sio changamani) na ni safi kwa kiasi fulani na ambayo kila moja kati ya hizo ni katika nafasi sawa na Arshi ya ulimwengu, na dari yake, na kituo cha usarifu. Hata moja ya limwengu hizo ni pepo ya Maawa ambayo ipo mbele ya Sidrat al-Muntaha. Mpashaji wa kweli amepasha habari (s.a.w) ambayo maana yake: Hakika tasbihati na tahmidati ambazo zinatajwa ardhini hufanyika mwili kwa sura ya matunda ya peponi.

Ibnu Hiban, As-Swahih 3/109. Al Mustadrak 1/680. Al-Bayhaq, As-Sunanul Kubra 6/207. Abuu Ya’ala, Al-Musnad 4/165.

Basi nukta hizi tatu zinatubainishia kwamba hazina za yaliomo ardhini katika matokeo na matunda yapatikanayo kwa hakika yapo huko, na kwamba mavuno yake yanaelekea na kupelekwa huko. Usiseme – ewe msikilizaji – vipi inakuwa “Alhamdulillah“ ambayo ninaitamka hewani iwe ni tunda peponi? Kwa sababu wewe unapotamka neno zuri na hali ya kuwa uko macho mchana inaweza kuonekana kwako katika njozi kwa sura ya tufaha tamu na unalila. Na vilevile maneno yako mabaya mchana unaweza kuyameza ndotoni kikiwa ni kitu kichungu cha kumezwa kwa taabu. Ukimsengenya mtu yeyote unatahamaki kuwa unalazimishwa kumla maiti!.

Kwa hiyo maneno yako mazuri au mabaya ambayo unayatamka katika ulimwengu wa dunia ambao ni ulimwengu wa kulala, utayala katika ulimwengu wa Akhera ambao ni ulimwengu wa kuwa macho, na kama hivi haitakiwi kukanusha kula kwako huku.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.