Nyongeza Ya Andiko La Kumi Na Tisa Na Neno La Thelathini Na Moja

Muujiza Wa Kupasuka Kwa Mwezi

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمنِ الرَّحِيمِ

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ *وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ Qur’an, 54:1-2.

Hakika ya wanafalsafa wa kimaada, na wanaowaiga kiupofu, wanataka kufuta na kufunika muujiza wa kupasuka kwa mwezi wenye kung’ara kama mwezi wa badri, wanaamsha dhana potofu kuhusu jambo hilo, kwa kuwa wanasema: (Ingekuwa kupasuka kwa Mwezi kumetokea kweli ulimwengu ungejua hilo, na vitabu vyote vya historia vingelitaja jambo hilo!).

Jibu:

Hakika kupasuka kwa mwezi ni muujiza wa kuthibitisha kwa utume, umetokea mbele ya wale ambao walisikia da’wah na kuikanusha, na ilitokea usiku, katika wakati ambapo umeenea mghafala, na limedhihirishwa kwa muda mfupi, ukiachilia mbali kutofautiana Matlai na kuwepo kwa mawingu na mfano wa hivyo katika vizuizi mbali mbali vinavyozuilia mwezi kuonekana. Hali ya kujua kwamba kazi za kufuatilia anga na nyenzo za ustaarabu wakati huo havikuwa vimeenea, kwa hiyo hailazimu kuona watu wote kupasuka kwa mwezi, kila mahali, na hailazimu vilevile kuingia katika vitabu vya historia.

Sasa sikiliza nukta tano tu kati ya nyingi kati ya hizo, zitatokomeza kwa idhini ya Allah (s.w) mawingu ya dhana ambazo zimegubika uso wa muujiza huu wa dhahiri:

Nukta ya kwanza:

Hakika ukaidi wa makafiri katika zama hizo ni wenye kujulikana na ni mashuhuri kwa historia, wakati Qur’an ilivyotangaza:

وَانشَقَّ الْقَمَرُ Qur’an, 54:1.

Na Mwangwi wake kufika angani, hakuthubutu yeyote katika makafiri, na hali ya kuwa wao wanapinga Qur’an, kuikadhibisha aya hii tukufu. Yaani kukanusha kutokea kwa tukio hilo. Kwa sababu isingekuwa tukio limetokea kiuhalisia wakati huo, na halikuwa limethibiti kwa hao makafiri, wangejitokeza kwa nguvu ili kubatilisha madai ya utume, na kumkadhibisha Mtume (s.a.w). Wakati ambapo vitabu vya historia na sira havikunakili chochote katika kauli za makafiri kuhusu kukanusha kwao kutokea kwa kupasuka mwezi, isipokuwa yale yaliyobainishwa na aya:

 وَيَقُولُوا سِحْرٌمُّسْتَمِرٌّ Qur’an 54:2.

Nayo kwamba wale walioshuhudia muujiza katika makafiri walisema: Huu ni uchawi tumeni watu waende kwa watu wa mbali mkatazame je, waliona hilo au hapana?. Na asubuhi ilipofika misafara kutoka Yemen iliwasili na mingineyo wakawauliza, wakawaeleza: Kwamba wao wameona mithili ya hivyo. Wakasema: “Hakika Uchawi wa yatima wa Abu Talib umefika mbinguni!”.

At-Tirmidhy, Tafsirul Qur’an 54. Ahmad bin Hambal, Al-Musnad 3/165. At-twabary, Jamiul Bayan 27/84-85. Al- Qurtuby, Al-Jamiul Ahkam Al Qur’an 17/126. Al-Bayhaqy, Dalailu Al-Nubuwat 2/268, Al-Suyuuty, Al-Khaswaisul Kubra 1/209.

Nukta ya pili:

Wamesema wengi wa wakubwa wa Elimu ya Al-Kalam, mfano wa Saad Attaftazaany kuwa: (Kupasuka kwa mwezi ni Mutawatir, mfano wa kumiminika maji kati ya vidole vyake vitukufu (s.a.w) na kunywa jeshi maji hayo, na mfano wa kulia kwa shina kutokana na kutengana kwake na Mtume (s.a.w) ambalo alikuwa akiegemea wakati wa hutuba, na kusikia kilio chake kundi la masahaba, yaani tukio wamelinakili kundi kubwa kutoka kwa kundi kubwa ni muhali kulingana kwao juu ya uongo. Tukio ni la mutawatir kwa namna ya kukinaisha kama kudhihiri kwa nyota kabla ya miaka elfu na kama kuwepo kwa kisiwa cha Serandib ambacho hatujakiona.

Na kama hivi unaona kwamba kuamsha shaka kuhusu suala hili la kukinaisha na mfano wake katika masuala yaliyoshuhudiwa kwa macho dhahiri hakika ni upumbavu na uzuzu, kwani inatosha katika matukio hayo kwamba hayo ni katika yamkini na wala sio muhali. Kwa kujua kwamba kupasuka kwa mwezi ni yamkini kama kupasuka kwa Mlima kwa volkeno.

Nukta ya tatu:

Hakika muujiza huja kwa ajili ya kuthibitisha madai ya utume, na sio kuwalazimisha kuamini kwa njia ya kuwakinaisha wakanushaji. Kwa hiyo inalazimu kuudhihirisha kwa wale waliosikia madai ya utume, kinachowafikisha katika kukinai na kutulia juu ya ukweli wa utume. Ama kuudhihirisha mahali pote, au kuudhihirisha kwa namna ya waziwazi kiasi watu watalazimika kukubali na kutii, hilo linakinzana na hekima ya Mwingi wa hekima mwenye utukufu, na ni tofauti vilevile na siri ya kulazimisha kwa kiungu. Kwa sababu siri ya kulazimisha kwa kiungu kunahitajia kufungua uwanja mbele ya akili bila kuinyang’anya hiari.

Angekuwa muumba mkarimu ameacha muujiza wa kupasuka kwa mwezi umebaki kwa muda wa saa mbili, na kuudhihirisha kwa ulimwengu wote na kuingia ndani ya historia kama wanavyoutaka wanafalsafa, makafiri wangekuwa wanasema hakika hilo ni tukio la kifalaki la kawaida, na isingekuwa hoja ya ukweli wa Mtume (s.a.w), wala muujiza unao muhusu mtume mtukufu (s.a.w). Au ungekuwa ni muujiza wa wazi unaolazimisha akili kuamini na kuinyang’nya hiari, na wakati huo zitakuwa sawa roho za chini kama mkaa duni mfano wa Abu Jahli, na roho za juu safi kama Almasi mfano wa Abu bakr Al-Siddiq (r.a), yaani ingekuwa inapotea siri ya kulazimishwa ya kiungu.

Na kwa ajili ya hili muujiza ulitokea kipindi kifupi sana, na usiku, na wakati mghafala unaenea, na ikawa tofauti za matalai na mawingu na mfano wa hayo ni vizuizi vya watu kuuona. Na haukuingia ndani ya vitabu vya historia.

Nukta ya nne:

Hakika ya muujiza huu uliotokea wakati wa usiku, na kipindi kifupi tu, na katika wakati wa mghafala, hawauoni watu wote bila shaka kila mahali. Bali hata ungedhihiri kwa baadhi yao, wasinge sadiki macho yao, na kama angesadiki, hakika ya tukio kama hili limepokewa kutoka kwa mtu mmoja lisingekuwa na thamani katika historia.

Wanazuoni wahakiki wamejibu yaliyozidishwa katika mapokezi ya muujiza kwamba mwezi baada ya kupasuka kwake uliteremka Ardhini! Wamesema: Pengine baadhi ya wanafiki wameiingiza ziada hii ili waangushe thamani ya mapokeo na kudhalilisha hadhi yake.

Kisha katika wakati huo mawingu ya ujinga yalikuwa yanagubika katika mbingu ya Uingereza, na wakati unakaribia magharibi huko Hispania, na Marekani ikiwa katika hali ya mchana kweupe, na asubuhi imeingia huko China na Japani. Na kwengineko kulikuwa na vizuizi vya kuoneka muujiza huu mkubwa, hauonekani huko.

Ukijua hili basi zingatia maneno ya anayesema: “Historia ya Uingereza, China, Japani Marekani na mfano wa nchi hizo haitaji tukio hili, kwa hiyo halikutokea!”. Mzaha gani huu. Ehe, kuangamia kuwe kwa wale wanaokula makombo ya Ulaya.

Nukta ya tano:

Kupasuka kwa mwezi sio tukio lililotokea lenyewe, kwa misingi ya sababu za kiasili na kwa njia ya sadfa! Bali amelifanya litokee Muumba Mwingi wa hekima, Bwana Mlezi wa jua na mwezi, ni tukio lililofurutu ada ya kanuni za kimaumbile, ili kusadikisha utume wa mtume wake mpendwa (s.a.w), na kutangaza ukweli wa madai ya da’wa yake, akalidhihirisha (s.w) kulingana na hekima yake na kwa hitajio la siri ya kuongoza na kulazimisha na hekima ya kufikisha ujumbe, na ili asimamishe hoja kwa amtakaye katika wenye kulishuhudia hilo, wakati ambapo amelificha, kwa hitajio la hekima yake (s.w) na utashi wake, kwa wale ambao haikuwafikia da’wa ya nabii wake (s.a.w) katika wakazi wa maeneo mbali mbali ya ulimwengu, na akawazuia kuliona kwa mawingu na kwa tofauti za Matlai na kutokuchomoza kwa mwezi, au kuchomoza kwa jua katika baadhi ya nchi na kuangaza kwa mchana katika nchi nyingine, na kuzama kwa jua katika nyinginezo, na sababu nyingine mfano wa hizo ambazo zinapelekea kuzuilika kuonekana kwa kupasuka kwa mwezi.

Muujiza huu ungedhihirishwa kwa watu wote ulimwenguni, ima kwamba ungekuwa unadhihiri kwao ikiwa ni matokeo ya ishara ya mtume mtukufu (s.a.w) na kudhihirisha kwa muujiza wa unabii wake, na wakati huo utafika katika udhahiri mno, yaani watu wote watalazimika kusadiki, yaani itanyang’anywa kwao hiari, na hapo siri ya taklifa itapotea. Wakati ambapo Imani inahifadhi uhuru wa akili katika hiari wala haiipokonyi, au litadhihiri kwao kama tukio la mbingu tu, na wakati huo uhusiano wake na utume wa Muhammad utakatika na hautabakia na upekee mahususi.

Muhtasari:

Hakika kupasuka kwa mwezi hakuna shaka ndani yake. Hakika kumethibitishwa kwa namna ya kukinaisha. Hapa tutaashiria kutokea kwake kwa hoja sita za kukinaisha

Yaani kuna hoja sita za kukinaisha juu ya kutokea kwa kupasuka kwa mwezi katika namna sita katika Ijmai. Lakini kwa masikitiko katika makamo haya hatukutimiza haki yake katika somo hili imebaki kwa ufupi. (Mtunzi)

kati ya nyingi miongoni mwake, Nazo: kukubaliana kwa masahaba watukufu kwa pamoja (r.a) nao ni waadilifu na kuwafikiana kwa wanazuoni wahakiki miongoni mwa wafasiri katika kufasiri kwao:

وَانشَقَّ الْقَمَرُ Qur’an, 64:1.

Na kunakili wanazuoni wote wa hadithi walio wa kweli katika mapokezi yao kutokea kwake kwa isinadi nyingi na kwa njia lukuki.

Tunataja hadithi tatu ambazo ni muttafaq:

Kutoka kwa Abdallah bin Masud (r.a) amesema: Mwezi ulipasuka wakati wa Mtume wa Allah (s.a.w) vipande viwili Mtume (s.a.w) akasema: “Shuhudieni” (Muttafaq Alayhi).

Na kutoka kwa Anas (r.a): Kwamba watu wa Makka walimwomba mjumbe wa Allah (s.a.w) awaonyeshe muujiza akawaonyesha kupasuka kwa mwezi. (Muttafaq Alayhi).

Na kutoka kwa Ibn Abbas (r.a): Hakika mwezi ulipasuka katika zama za Mtume (s.a.w) (Muttafaq Alayhi).

Rejea: Musnad Imam Ahmad 1/377, 413, 447, 456, 3/207, 220, 275, 278, 4/81 na ameipokea Attayalisy, kwa namba 295, 1891, 1960. Na Tafsir ya Ibn Kathir (6/469) ili kujua tawatur ya tukio.

Na kushuhudia watu wa Kashf na Ilhamu katika mawalii wa kweli wema. Na kusadiki viongozi wa elimu ya Al-Kalamu wabobezi pamoja na kutofautiana kwa maslaki zao na masharibu (vyanzo) zao. na kukubali kwa umma ambao haukubaliani kwa pamoja juu ya upotevu kama hadithi tukufu ilivyoeleza juu ya hilo.

Amesema Mtume (s.a.w): “Umma wangu haungani juu ya upotevu”

(Kashfu Al-Khafaa 2/350. Abu Daud, Al-fitan na Al-Malahim 1. At-Tirmidhy, Al-fitan 7. Ibn Majah Al-Fitan 7. Ad-Daramiy, Al-Muqadimat 8. Ahmad bin Hambali, Al-musnad 6/396.

Yote hayo yanabainisha kupasuka kwa mwezi na kuuthibitisha kwa namna ya kukinaisha mfano wa jua katika ufasaha wake.

Kwa ufupi

Somo lilikuwa hadi hapa kwa jina la uhakiki wa kisayansi, ili kumlazimisha adui. Ama baada ya hili maneno yatakuwa kwa jina la hakika na kwa ajili ya imani. Uchambuzi wa kisayansi umetamka hivi. Ama hakika tunasema: Hakika mwisho wa diwani ya utume (s.a.w) na yeye ni mwezi wenye kuangaza wa mbingu ya utume, uwalii wa utumishi wake ni wa hadhi ya juu hadi katika daraja kuwa mpendwa, ukadhihirisha karama kubwa na muujiza mkuu kwa Miiraji. Yaani kwa kutembea kwa mwili wa kiardhi katika anga za mbingu za juu, na kumtambulisha kwa wakazi wa Mbingu, kwa muujiza huo ulithibitisha uwalii wake mkubwa kwa Allah (s.w) na kupendwa kwake kwa dhati na hadhi yake ya juu kwa wakazi wa mbingu na hadhara ya juu. Hali kadhalika Allah (s.w) alipasua mwezi uliotundikwa Mbinguni na wenye kufungamana na Ardhi kwa ishara kutoka kwa mja wake akiwa Ardhini, akadhihirisha Muujiza wake huu, kuthibitisha utume wa huyo Mja mpendwa, Mpaka akawa (s.a.w) kama vipande viwili vyenye kutoa nuru kwa mwezi, alipaishwa hadi katika anga za makamilifu kwa mbawa mbili za uwalii na utume za nuru, hata akafika ukaribu wa pinde mbili au karibu zaidi na akawa ni fahari ya wakazi wa Mbingu kama alivyo kuwa ni fahari kwa wakazi wa Ardhi.

.عَلَيْهِ وَعَلَى آلِهِ وَصَحْبِهِ الصَّلَاةُ وَالتَّسْلِيْمَاتُ مِلْءَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتِ

سُبْحَانَكَ لاَ عِلْمَ لَنَا إِلاَّ مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

اَللَّهُمَ بِحَقِّ مَنْ انْشَقَّ الْقَمَرُبِإِشَارَتِهِ اجْعَلْ قَلْبِي وَقُلُوْبَ طَلَبَةِ رَسَائِلِ النَّوْرِ الصًّادِقِيْنَ كَالْقَمَرِ فِي مُقَابَلَةِ شَمْسِ الْقُرْآنِ..آمِيْــنَ..آمِيْــنَ.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.