“BAADHI YA MARADHI NI NEEMA YA KIUNGU”

Tiba ya Tano

Kutoka katika Ujumbe kwa Wagonjwa

Ewe uliyepatwa na maradhi! Kwa uzoefu, nimekuwa na rai kwa wakati huu kuwa kwa baadhi ya watu, maradhi ni neema ya kiungu, zawadi ya Mwingi wa Rehema. Ingawa sikuwa mwenye kuistahiki, kwa miaka minane au tisa iliyopita kuna vijana wengi wamenijia kwa sababu ya maradhi yao, ili kuniomba dua zangu, nikagundua kuwa wote walishaanza kuifikiria akhera zaidi kuliko vijana wengine. Hawakuwa na ulevi wa ujana na wamekana kwa kiasi fulani utashi wa kinyama na kutokuwa wasikivu. Hivyo niliwazingatia na kuwakumbusha kuwa maradhi yao yalikuwa neema ya kiungu ndani ya mipaka yenye kustahamilika. Niliwaambia: “Ndugu yangu! Siko kinyume na maradhi yako haya, sikusikitikii kwa ajili ya maradhi hayo ili nikuombee dua. Jaribu kustahamili mpaka maradhi yakuzindue kikamilifu, na baada tu ya maradhi kutenda kazi yake, Muumbaji Mwingi wa hekima, atakurudishia afya yako, akipenda.

Pia, nilikuwa nikiwaambia: “Kwenye balaa la afya njema, baadhi yenu huangukia kwenye kughafilika, wanaacha swala tano za kila siku, hawafikirii kaburi, na wanamsahau Allah (s.w). Anasa kubwa za muda mfupi za maisha ya kidunia zinawasababisha watikise na kuharibu maisha ya milele, na hata kuyaangamiza kabisa. Ilhali, kutokana na maradhi yenu, mnaliona kaburi, ambalo kwa namna yoyote mtaingia na makazi ya Akhera baada yake, na mtatenda kulingana nayo. Kwa hivyo, kwenu nyinyi ugonjwa ni afya njema, ilhali kwa baadhi yenu, afya njema ni ugonjwa.”

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.