JELA KAMA FAIDA

Kwa Jina Lake, (s.w)

Ndugu zangu wapendwa na waaminifu!

Nitaeleza kitulizo muwafaka katika ‘Nukta’ tatu kwa wenye kupata taabu jela, na kwa wenye kuwasaidia kwa wema na kiimani wanaosimamia chakula chao, kinachowajia kutoka nje.

Nukta ya kwanza:

Kila siku inayopita katika jela inaweza kuleta mpaka siku kumi za ibada, na, kwa kuangalia matunda yake, inaweza kugeuza saa zile fupi na kuwa saa za kudumu, na adhabu ya miaka mitano au kumi inaweza kuwa njia ya kumwokoa mtu kwa mamilioni ya miaka ya kifungo cha milele. Kwa waumini, hali ya kupata faida hii muhimu na yenye thamani kubwa ni kuswali swala tano za faradhi, kutubu madhambi yaliyokuwa sababu ya kufungwa, na kuwa na shukurani katika subira. Kwa hakika, gereza ni kizuizi cha madhambi mengi: Haiwapi fursa.

Nukta ya Pili:

kama ambavyo kukoma kwa starehe kunasababisha maumivu, ndivyo pia kukoma kwa maumivu kunavyoleta starehe. Kwa hakika, katika kuifikiria furaha iliyopita, siku za raha, kila mmoja anahisi maumivu ya majuto na shauku, na kusema: “Basi!”, na kukumbuka siku za nyuma za majanga, zisizo za furaha, wanapata namna ya furaha kwa kuwa yameshapita, na anasema: “Sifa njema na shukurani ni kwa Allah, balaa lile limeacha zawadi nyuma yake na limeshaondoka.” Anatoa pumzi ya faraja. Maana yake, maumivu mafupi na ya huzuni huacha nyuma namna ya furaha rohoni, ilhali saa ya furaha huacha maumivu.

Kwa kuwa ukweli ni hivyo; na kwa kuwa balaa zilizopita pamoja na maumivu yake hayapo, na siku zijazo za dhiki kwa sasa hazipo, na hakuna maumivu yanayoletwa kutokana na kisichokuwepo, kuendelea kula mkate na kunywa maji leo, mathalani, kwa sababu ya uwezekano wa kusikia njaa na kiu kwa siku kadhaa zijazo, ni upumbavu mkubwa. Na kwa namna hiyo hiyo, kwa sasa kufikiria saa za huzuni zilizopita na zijazo, ambazo kwa sasa hazipo, na kukosa subira, na mtu kusahau makosa yake, kunong’ona kama vile kumlalamikia Allah ni pia upumbavu mkubwa. Kwa kuwa nguvu ya subira haijasambazwa kwenda kushoto na kuume, yaani, katika wakati uliopita na ujao, na imeimarishwa katika kukabili saa ya sasa na siku, kunatosha. Huzuni inaporomoka kutoka kumi hadi moja.

Kwa hakika, lakini isiwe malalamiko, upendeleo wa kiungu umeashiria ukweli wa hapo juu kwangu ilhali nikiwa katika siku chache za maumivu ya kimwili na kiroho, maradhi, na majaribu ambayo mfano wake sikuwahi kuyapata kabla maishani mwangu, nilikandamizwa hususani kwa kukata tamaa na huzuni, niliyohisi katika moyo na roho kwa kushindwa kwangu kuihudumia Qur’an na imani kwa Risale-i Nur. Basi nikawa nimeridhika na maradhi ya kuhuzunisha na kifungo cha jela. Kwa kusema: “Ni faida kubwa kwa mwenye mkosi kama mimi anayengojea katika mlango wa kaburi ili kufanya saa moja inayoweza kupitishwa katika upuuzi na kutozingatia saa kumi za ibada”, nikashukuru.

Nukta ya Tatu:

kuna faida kubwa katika kuwasaidia wafungwa kwa huruma, katika kuwapa mahitaji yao, na katika kutuliza vidonda vyao vya kiroho kwa kuwafariji. Na kuwapa chakula chao kinachokuja kutoka nje ni kama zaka ambayo, ni kwa kiasi hasa cha chakula, imeandikwa katika kitabu cha amali njema kwa hao, wa nje na ndani, wanaofanya haya, pamoja na waangalizi wanaohusika. Na hususani kama mfungwa asiye na furaha ni mzee, mgonjwa, masikini, au mgeni, basi malipo ya zaka hii yanazidi kwa mara nyingi.

Hivyo faida hii ya thamani kubwa sharti lake ni kuswali swala tano za faradhi, ili huduma hiyo iwe ni kwa ajili ya Allah. Na hali nyingine ni kuharakisha kuwasaidia kwa ikhlasi, huruma na furaha, na katika namna ya kutowafanya wao kuhisi kuwa wenye kulazimishwa.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.