KUPONYA KWA IMANI

Tumaini la Saba

Kutoka katika Ujumbe kwa Wazee          

Wakati mmoja mwanzoni mwa uzee wangu pindi kicheko cha Said wa zamani kilipokuwa kikibadilika kuwa uliaji wa Said mpya, kwa kuchukulia kuwa mimi bado ni Said wa zamani, watu wa dunia Ankara waliniita pale, nami nikaenda. Mwishoni mwa majira ya kupukutika majani nilipanda mpaka juu ya ngome, ambapo ilikuwa na umri mkubwa mno, chakavu na kuchoka kuliko mimi. Ilionekana kwangu kuwa imetokana na matukio ya kutisha ya kihistoria. Uzee wa msimu wa mwaka pamoja na uzee wangu, uzee wa ngome, uzee wa mtu, uzee wa Dola tukufu ya Uthman na kifo cha utawala wa Khalifa, na uzee wa dunia yamenisababishia kuangalia katika hali ya kusikitisha, ya kuhurumia na yenye huzuni katika ngome ile ya juu zaidi katika mabonde ya wakati uliopita na milima ya wakati ujao. Nilipopatwa na hali nyeusi kabisa ya akili Ankara iliyozungukwa na matabaka manne au matano ya weusi wa uzee, mmoja ndani ya mwingine,

Hali yangu ya akili katika wakati huo ilinifanya niandike dua kwa lugha ya Kiajemi. Ilichapishwa Ankara, katika maandiko yaliyoitwa, Hubab.

nilitafuta nuru, faraja, tumaini.          

Nilitafuta faraja kwa kuangalia upande wa kuume, yaani, kwenye wakati uliopita, baba yangu na wahenga wangu na mbari ya kibinaadamu ilitokeza katika namna ya kaburi kubwa na kunijaza huzuni badala ya kunifariji. Katika kutafuta tiba, niliangalia mustakabali, uliyokuwa upande wangu wa kushoto. Niliona kuwa ulijitokeza kama kaburi kubwa lenye giza kwa ajili yangu, watu wa wakati wangu, na vizazi vijavyo; ikaleta kitisho katika nafasi ya mazoea. Katika hali ya kujihisi ukiwa upande wa kushoto na kuume, nikaangalia wakati wa sasa. Ukatokezea katika kughafilika kwangu na jicho la kihistoria kama jeneza likiwa na nusu yangu ikiwa maiti, maumivu na mwili unaohangaika kwa kukata tamaa. Kisha, katika hali ya kukatia tamaa mwelekeo huo pia, nilikiinua kichwa changu na kuangalia juu ya mti wa uhai wangu, na kuona kuwa mti huo ulizaa tunda moja tu, na kuwa lilikuwa mwili wangu; lilikuwa juu ya mti na lilikuwa likiniangalia. Katika hali ya kutishika katika mwelekeo huo pia, niliinamisha kichwa changu. Nikaangalia chini ya mti wa uhai wangu, mizizi yake, na kuona udongo wake wa hapo, mchanga uliokuwa chanzo cha kuumbwa kwangu na vumbi la mifupa yangu likichanganyika pamoja, lilikanyagwa kanyagwa chini ya mguu. Hiyo haikuwa tiba, badala yake hilo lilizidisha maumivu katika mateso yangu.

Halafu nikalazimishwa niangalie nyuma yangu. Nikaona kuwa dunia hii isiyo imara, ya mpito ilikuwa ikiporomoka, kupotelea katika mabonde ya kutokuwepo na giza la kupotea. Huku nikitafuta kitulizo cha maumivu, iliongeza sumu tu. Kwa kuwa sikuona jema katika upande huo nikaangalia mbele yangu, nikatazama ili kuona mustakabali. Nikaona kuwa mlango wa kaburi ulikuwa wazi katikati kabisa ya njia yangu, ulikuwa ukiniangalia mimi huku mdomo wake ukiwa wazi. Barabara kuu nyuma yake ilielekea kwenye umilele, na misafara iliyokuwa katika barabara hiyo ilionwa na jicho langu kwa mbali. Na mbali ya uwezo finyu, mdogo wa hiari kama msaada wangu na silaha ya kujilinda mbele ya vitisho vilivyokuja kutoka katika pande sita, sikuwa na kingine.

Kwa kuwa uwezo mdogo wa hiari, silaha pekee ya mwanaadamu dhidi ya maadui hao wengi na mambo ya madhara yasiyo na ukomo, ni pungufu na dhaifu, na inakosa uwezo wa kuumba, mwanaadamu hawezi kitu zaidi ya kuchuma. Haikuweza kwenda katika wakati uliopita ili kuondoa huzuni zilizonijia kutoka huko, wala haikuweza kupenya katika mustakabali ili kuzuia hofu iliyokuja kutoka huko. Niliona kuwa haikuwa na manufaa katika matumaini na maumivu yangu kuhusu wakati uliopita na mustakabali.

Wakati nilipokuwa nikipambana katika kitisho, ukiwa, giza na ukataji tamaa unaokuja kutoka pande sita hizo, nuru ya imani inayong’aa katika anga ya Qur’an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza ghafla ilikuja kunisaidia. Ziliwaka na kuziangaza pande hizo sita kiasi kwamba kama vitisho na giza nililoona lingezidi mara mia moja, bado mwangaza ungenitosha. Ilibadili vitisho vyote hivyo kimoja baada ya kingine katika liwazo na ukiwa kwendea katika mazoea. Ilikuwa kama ifuatavyo:

Imani imepasua pasua mtizamo wa ukiwa wa wakati uliopita kama kaburi kubwa, na ilionesha kwa uhakika kabisa kuwa ni jambo lililozoeleka  na ni mkusanyiko angavu wa marafiki.

Na imani imeonesha mustakabali, uliojitokeza katika umbo la kaburi kubwa kwa macho yangu yasiyozingatia, kuwa kwa hakika zaidi dhifa ya Mwingi wa Rehema katika makasri ya upeo wa furaha.

Na imani imechana chana mtizamo wa wakati wa sasa kama jeneza, kama ilivyojitokeza kwenye nadharia yangu isiyozingatia, na kuionesha kwa uhakika kuwa  sehemu ya biashara kwa ajili ya Akhera na nyumba ya wageni ing’aayo ya Mwingi wa Rehema.

Na imani imeonesha kwa uhakika kabisa kuwa tunda pekee juu ya mti wa uhai halikuwa mwili wa maiti kama ilivyojitokeza katika jicho langu lisilozingatia, badala yake, roho yangu, ambayo ingedhihirisha uzima wa milele na iliyoumbwa kwa ajili ya furaha ya milele, ingeacha nyumba yake iliyochakaa na kusafiri baina ya nyota.

Na imani imeonesha kwa muujiza wa imani kuwa mifupa yangu na udongo uliokuwa chanzo cha kuumbwa kwangu haikuwa mifupa isiyo na thamani iliyosagwa na kukanyagwa miguuni, bali udongo ulikuwa mlango wa kuingia kwenye Rehema ya Kiungu na pazia mbele ya jengo la Pepo.

Na imani imeonesha kupitia siri za Qur’an kuwa dunia iliyojitokeza katika jicho langu lisilozingatia nyuma yangu kama kuangukia kwenye kutokuwepo na kupotea kuwa inajumuisha barua za anayeombwa Milele na kurasa za mapambo na nakshi zenye kumtukuza Allah ambazo zimekamilisha majukumu yao, zimefafanua maana zake, na zimeacha matokeo yake katika kuwepo mahali pake. Ilijulisha kwa uhakika kabisa namna hasa dunia ilivyo.

Na imani imeonesha kwa nuru ya Qur’an kuwa kaburi litakalofumbua macho yake na kuniangalia hapo baadaye halikuwa mlango wa kisima, badala yake, ulikuwa mlango wa kuingia kwenye dunia ya nuru, na kuwa barabara iliyoelekea kwenye umilele nyuma ya kaburi haikuelekea kwenye kutokuwepo, bali kwenye kuwepo, mahali pa nuru, na upeo wa furaha ya milele. Kwa kuwa imani imeonesha hilo mpaka kwa kiwango cha kusadiki kabisa, imekuwa ni tiba na kitulizo cha maumivu yangu.

Na katika nafasi ya uwezo mdogo sana wa kupokea, imani inaweka waraka mkononi mwa uwezo finyu na mdogo wa hiari ili iweze kutumainia uwezo usio na ukomo na kuunganishwa katika Rehema isiyohesabika mbele ya maadui hao wasiohesabika na tabaka za giza. Kwa hakika, imani ni waraka mkononi mwa uwezo mdogo wa hiari. Na ingawa silaha hii ya kibinaadamu ya hiari ya kupendelea, yenyewe ina mapungufu, na haina uwezo, na ina kasoro, kama vile wakati mwanajeshi anatumia nguvu zake ndogo kwa niaba ya dola, anafanya kazi zaidi ya nguvu zake, ndivyo pia kupitia siri ya imani, kama uwezo finyu na mdogo wa hiari unapotumika kwa jina la Allah (s.w) na katika njia Yake, unaweza pia kupata Pepo upana wake kama upana wa miaka mia tano.

Na imani huchukua kutoka mikononi mwa mwili hatamu za uwezo mdogo wa hiari, ambao hauwezi kupenya kwenye wakati uliopita na mustakabali, na kukabidhi hayo kwenye moyo na roho. Kwa kuwa wigo wa uzima wa roho na moyo haujabanwa katika wakati wa sasa kama mwili, na imejumuishwa humo miaka mingi sana kutokea wakati uliopita na miaka mingi kutoka katika mustakabali, uwezo mdogo unaacha kuwa mdogo na unapata uenevu. Kama vile kwa uimara wa imani inaweza kuingia katika vina vya mabonde ya wakati uliopita na kuondoa giza la huzuni yake, ndivyo pia kwa nuru ya imani inaweza kupanda juu sana kama milima mirefu ya mustakabali, na kuondoa hofu zake.

Na kwa hivyo ndugu zangu wazee wa kike na kiume mnaotaabika na uzee kama mimi! Kwa kuwa, alhamdulillahi, sisi ni waumini, na katika imani kuna hazina hii yenye kung’aa, ya kufurahisha, ya kukubalika, na ya kupendeza; na kwa kuwa uzee wetu unatusukumia hata zaidi kwenye yaliyo kwenye hazina, kwa hakika, badala ya kulalamikia uzee ulioambatana na imani, tunapaswa tutoe shukurani zisizo na ukomo.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.