MADA YA SITA

Kutoka matunda ya imani          

Huko Kastamonu,

Ni mji uliyopo kaskazini mwa Uturuki. Ustadh Said Nursi alihamishiwa huko mwaka 1936 na alibakia hapo akiishi kwa lazima mpaka alipoondolewa mwaka 1943 kwa ajili ya kuhukumiwa katika mahakama kuu ya haki ndani ya mji wa Denizli.

kikundi cha wanafunzi wa shule za juu, waliniijia, wakisema: “Tuambie kuhusu Muumba wetu, walimu wetu hawazungumzi kuhusu Mwenyezi Mungu.” Nikawaambia: “Sayansi zote mnazojifunza zinaendelea kila mara kumzungumzia Mwenyezi Mungu na kufanya Muumbaji atambulike, kila moja katika lugha yake. Msiwasikilize walimu, zisikilizeni hizo.”

Mathalani, duka la madawa lililosheheni vyema huku likiwa na dawa zenye kuleta uhai na inatibu kwa kila chupa iliyopimwa kwa vipimo sahihi inaonesha mfamasia hodari asiyetiliwa shaka, mwenye uzoefu sana mwenye hekima. Vivyo hivyo, kwa kiasi kikubwa na kamilifu zaidi na bora lililosheheni kuliko duka lile la dawa la sokoni, duka la dawa la tufe la dunia likiwa na dawa za uzima katika chupa ambazo ni aina mia nne elfu za mimea na wanyama linaonesha na kumtambulisha katika macho yasiyoona hata – kwa kipimo cha sayansi ya tiba mnayosoma – Mwingi wa Hekima kuliko wote, (s.w), Ambaye ndiye Mfamasia wa duka kuu la madawa duniani.

Ama mfano mwingine; kiwanda cha ajabu kinachoshona maelfu ya aina za nguo kutokana na malighafi za kawaida, bila ya shaka kinamtambulisha mtengenezaji na fundi hodari. Aina hiyo hiyo, kwa kiwango chochote, ni kikubwa na kikamilifu zaidi kuliko kiwanda cha kibinaadamu, mashine hii yenye kusafiri inayojulikana kama tufe la dunia pamoja na maelfu ya vichwa na ndani ya kila kimoja kuna mamia ya maelfu ya viwanda, inaonesha na kumtambulisha – kwa kipimo cha sayansi ya uhandisi mnayosoma – Mtengenezaji wake na Mmiliki.

Na, mathalani, ghala, stoo, au duka lililokusanywa ndani yake na kuhifadhiwa katika mtindo na mpangilio mzuri aina elfu na moja za ruzuku, pasi na shaka, linamtambulisha mmiliki na msimamizi wa ruzuku na vyakula, wa kustaajabisha. Pia ni vivyo hivyo, kwa kiwango chochote, ni kubwa na kamilifu zaidi kuliko stoo au kiwanda, ghala hili la chakula la Mwingi wa Rehema, linalojulikana kama tufe la dunia, meli hii ya Kiungu, ghala hili, na duka lenye bidhaa, vifaa na chakula kilichohifadhiwa, ambalo kwa mwaka mmoja, husafiri kwa kawaida katika njia ya miaka elfu ishirini na nne, na inabeba makundi ya viumbe wenye kuhitaji vyakula tofauti na kupitia katika majira katika safari yake na kuyajaza majira ya kuchipua majani kwa maelfu ya ruzuku mbalimbali kama gari kubwa, linawaletea wanyama hai walemavu, ambao chakula chao kilishamalizika katika majira ya baridi kwa kipimo cha sayansi ya uchumi mnayosoma – ghala la dunia linamtambulisha na kumfanya meneja wake, mratibu na mmiliki apendwe.

Na kwa mfano, hebu tufikirie jeshi kubwa la mataifa mia nne elfu, na kila taifa linahitaji chakula tofauti, linatumia silaha tofauti, linavaa sare tofauti, hufanya kwata tofauti, na hutumwa majukumu yake kwa aina tofauti. Kama jeshi hili na kambi lina kamanda mtenda muujiza ambaye yeye peke yake, anayapa mataifa hayo tofauti vyakula vyao tofauti, silaha zao tofauti, sare zao tofauti na vifaa bila ya kusahau au kuchanganya yeyote katika wao, basi kwa hakika, jeshi na kambi linamwonesha kamanda na kumfanya apendwe mno. Kadhalika vivyo hivyo, kambi ya majira ya kuchipua ya uso wa dunia ambamo katika kila majira ya kuchipua, jeshi jipya la Kiungu lililofundishwa la aina mia nne elfu za mimea na wanyama hupewa sare zao mbalimbali, vyakula, silaha, mafunzo na kuruhusiwa kuondoka katika aina kamilifu na ya kiada kwa amri ya Amiri Jeshi Mmoja tu asiyemsahau au kumchanganya yeyote katika wao – kwa ukubwa wowote ule, kambi ya dunia ya majira ya kuchipua ni kubwa sana na kamilifu zaidi kuliko ile ya jeshi la kibinaadamu, – kwa kipimo cha sayansi ya kijeshi mnayosoma – inamtambulisha kwao kwa daraja la ukamilifu, Mtawala wake, Mwendeshaji, na Kamanda Mtukufu zaidi, na kusababisha maajabu mshangao na shangwe, na kumfanya awe mwenye kupendwa na kusifiwa na kutukuzwa.

Mfano mwingine, mamilioni ya taa za umeme zinazokwenda na kusafiri katika jiji la ajabu, chanzo cha nishati yao na nguvu hakimaliziki kamwe, waziwazi hali hiyo inamtambulisha fundi stadi mtenda maajabu na fundi umeme wa ajabu mwenye ujuzi mkubwa anayesimamia umeme, anatengeneza taa ziwe zinatembea, anaunda chanzo cha umeme, na analeta nishati, vinasababisha wengine kumshukuru na kumpigia makofi, na kumpenda. Halikadhalika, ingawa baadhi ya taa za nyota katika dari ya kasri la dunia katika jiji la ulimwengu – kama zitafahamika kama unavyosema unajimu – ni kubwa mara elfu moja kuliko dunia na zinatembea haraka kiasi cha mara sabini kuliko tufe la mzinga, hazivurugi mpangilio wao, wala hazigongani, wala kuzimika wala nishati yao kuisha. Kwa mujibu wa elimu ya unajimu, mnayosoma, ili jua letu liendelee kuungua, ambalo ni kubwa mara milioni kuliko dunia na umri wake ni mara milioni na pia ni taa na jiko katika nyumba moja ya wageni ya Mwingi wa Rehema kuliko wote, kuwa na mafuta mengi kama bahari za dunia na makaa mengi ya mawe kama milima yake au kwa magogo na kuni nyingi za dunia zaidi ya kumi vinalazimika kuwepo ili lisizimike. Licha ya ukubwa huo na ukamilifu zaidi kuliko mfano huu ni taa za umeme za kasri la dunia katika jiji kubwa la ulimwengu, zinazoashiria kwa vidole vyao vya nuru kuelekea kwenye nguvu isiyo na ukomo na mamlaka yanayolitia nuru jua na nyota nyingine za juu kama jua lenyewe bila ya mafuta, kuni au makaa ya mawe bila hata kuziruhusu zizimike au kugongana, ingawa zinasafiri pamoja kwa kasi, kwa kiwango hicho – kwa kipimo cha sayansi ya umeme ambayo ama mnasoma au mtasoma – zinamshuhudia na kumtambulisha Mtawala Mkuu, Mletaji nuru, Mwongozaji na Mtengenezaji wa onyesho lenye nguvu la ulimwengu, zinamfanya apendwe na wote, kuabudiwa na kutukuzwa.

Na kwa mfano, kitabu ambacho katika kila mstari wake, kitabu chote kimeandikwa vizuri, na kwa kila neno lake kuna sura ya Qur’an imeandikwa kwa kalamu nzuri. Kwa kuwa ni cha maana pana mno masuala yake yote, baadhi yake yakithibitishana na mengine, na kwa hiyo kitabu hiki cha ajabu kinaonesha mwandishi na mtunzi wake kuwa ni mjuzi sana na mwenye uwezo, hilo bila ya shaka linamuonesha  mwandishi wake na mtunzi pamoja na ukamilifu wake wote na sanaa waziwazi kama mwangaza wa mchana, na kumfanya atambulike. Hilo linamfanya athaminiwe kwa maneno kama, “Namna gani ya maajabu aliyotaka Mwenyezi Mungu!” na “Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu!”. Na ni Vivyo hivyo kwa kitabu kikuu cha ulimwengu; tunaona kalamu kwa macho yetu, inayoandika katika uso wa dunia, ambayo ni mojawapo katika kurasa zake, na katika wakati wa majira ya kuchipua, ambayo ni ukurasa mmoja, aina mia tatu elfu za mimea na wanyama tofauti, ambazo ni kama vitabu tofauti mia tatu elfu, vyote, kimoja ndani ya kingine, bila ya kasoro au makosa, bila ya kuvichanganya, kwa ukamilifu na kwa utaratibu kamilifu, na wakati mwingine anaandika shairi katika neno kama vile mti, na muhtasari kamili wa kitabu katika mbegu iliyo kama nukta.

Kwa namna iliyo pana, kamilifu zaidi, na yenye maana kuliko kitabu katika mfano uliotajwa hapo juu, ni huu muhtasari wa ulimwengu na Qur’an kubwa iliyopata mwili duniani ambayo kila neno lake lina maana na kuna mifano mingi ya hekima, kwa kiwango cha juu mno – kwa mujibu wa kipimo kipana na muono unaoangalia mbali wa sayansi ya asili mnayosoma na sayansi ya kusoma na kuandika mliyoifanya huko shuleni – inamtambulisha mwandishi na mtunzi wa kitabu cha ulimwengu pamoja na ukamilifu wake usiopimika.

Kutamka “Mwenyezi Mungu ni Mkubwa Zaidi!” inamtambulisha. Kusema maneno kama “Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu!” inampendezesha. Kwa kusema, “Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu!” inamfanya apendwe.

Hivyo, mamia ya sayansi nyingine kama hizi humtambulisha (s.w) Muumbaji wa ulimwengu pamoja na Majina Yake, kila moja kwa kipimo chake kikubwa, kioo chake mahususi, macho yake yanayoona mbali, na uangaliaji wa kutafuta, zinatambulisha sifa Zake na Makamilifu Yake.

“Ni kwa ajili ya kutoa maelekezo katika suala hili, ambalo ni ushahidi adhimu wa tawhidi ya Kiungu, kuwa Qur’an yenye maelezo ya kimiujiza, inatufundisha kuhusu Muumba wetu mara kwa mara kwa aya,

 خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ Qur’an, 6:1

na

ربُّ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ Qur’an, 13:16

“Niliwaambia haya vijana wa shule, na wao waliyakubali kikamilifu kwa kusema: “Shukurani zisizo na mwisho ni za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa tumepata ukweli kabisa na somo tukufu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awe radhi nawe!” Mimi nikasema: Mwanaadamu ni mashine iliyo hai ambaye hupata maelfu ya huzuni tofauti na hupata furaha katika maelfu ya njia tofauti. Licha ya udhaifu wake, ana maadui wasiohesabika, wa kuonekana na wa kiroho, na licha ya umasikini wake mkubwa, ana haja zisizo na idadi, za nje na za ndani, na pia ni kiumbe dhaifu anayedumu katika kuumizwa na misiba ya vifo na utengano. Lakini bado, kwa njia ya imani na ibada, mara moja anaungana na Mtawala (s.w), anapata mahali pa msaada dhidi ya maadui wake wote na chanzo cha msaada kwa ajili ya haja zake zote, na kama kila mmoja, anapata fahari kwa heshima na hadhi ya bwana aliyejishikiza kwake, mnaweza kuangalia wenyewe namna gani mtu anavyokuwa radhi mwenye shukurani na mwenye fahari baada ya kuunganishwa kwa njia ya imani kwa Mtawala Mwenye nguvu na Mwenye huruma, wakati wa kuanza kumtumikia kwa njia ya ibada, na kujibadilishia tangazo la utekelezaji wa saa iliyopangwa na kuwa nyaraka zenye kumwacha huru kutokana na majukumu.”

Ninakariri kwa wafungwa waliopatwa na janga, yale niliyowaambia vijana wa shule: “Mtu anayemtambua Yeye na kumtii ana bahati hata kama yuko jela. Ilhali anayemsahau Yeye ni fidhuli na mfungwa hata kama anakuwa mkazi wa kwenye kasri la kifalme.”

Hata mtu aliyekosewa lakini mwenye bahati aliwaambia madhalimu fidhuli waliokuwa wakimnyonga: “Mimi sinyongwi, bali ninapewa ruhusa na kuondoka kwenda mahali nitakapopata furaha ya milele.

Lakini naona nyinyi mtahukumiwa kunyongwa kwa milele na mimi ninakulipizieni kisasi stahiki. Na ninatangaza: “Hapana wa haki kuabudiwa isipokuwa Allah!” Akasalimisha roho yake kwa furaha.

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَناَ إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ العَلِيْمُ الحَكِيْمُ

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.