NAMNA YA KUNUFAIKA NA GEREZA

Wale walio jela wana haja kubwa ya faraja ya kweli ya Risale-i Nur. Hususani wale waliopata maumivu ya vipigo vya ujana, wanaopitisha ujana wao, maisha matamu jela; wana haja na Risale-i Nur kama wanavyohitaji mkate.          

Kwa hakika, ujana unazingatia hisia badala ya sababu, na hisia na utashi ni upofu; hawafikirii athari zake; Wanapendelea wakia moja ya furaha ya papo hapo badala ya tani za furaha za baadaye. Wao huua kwa ajili ya furaha ya dakika moja ili kufurahia ulipizaji kisasi, halafu wanapata maumivu kwa saa elfu themanini ya maumivu ya jela. Na starehe potovu ya saa moja katika masuala ya heshima inaweza kupelekea furaha ya maisha kuteketezwa kabisa kwa kuhofia jela na maadui. Na kuna mifano mingi mingine, hatari nyingi zisizoonekana kwa vijana wenye mikosi kwa sababu ambayo wanabadili maisha yao matamu sana kuwa machungu sana na maisha ya hatari.

Fikiria hali kubwa ya kaskazini; imepata umiliki wa tamaa za vijana wake na inatikisa karne hii yote kwa dhoruba zake. Kwani imehalalisha kwa vijana wake mabinti wazuri na wake wa watu walionyooka, na vijana hawa wanatenda kwa kufuata hisia zao tu, ambazo hazioni athari zote. Kwa hakika, kwa kuruhusu wanaume na wanawake kwenda pamoja katika bafu za umma, wanahamasisha ukosefu wa maadili. Na wanachukulia kuwa ni halali kwa wahuni na masikini kupora mali za matajiri. Watu wote wanatetemeka katika kukabili balaa hili.

Na kwa hivyo ni lazima sana katika karne hii kwa vijana wote wa Kiislamu kufanya ushujaa, na kujibu mashambulizi haya mawili yanayouma kwa mapanga ya ari kama Matunda ya Imani na Mwongozo kwa Kijana kutoka Risale-i Nur. Vinginevyo vijana wasiobahatika watavunja yote mawili, mustakabali wao duniani, na maisha yao yenye kukubalika, na starehe yao ya Akhera, na maisha yao ya milele, na kuyageuza kuwa adhabu na taabu. Na ubadhirifu wao na ufisadi, wataishia mahospitalini, na kwa kukithirisha maishani mwao, katika magereza. Uzeeni kwao, watalia sana huku wakiwa na majuto mengi.

Kama, kwa upande mwingine, watajihifadhi kwa mafunzo ya Qur’an, na kwa ukweli wa Risale-i Nur, watakuwa vijana shujaa kikweli kweli, watu wenye sifa nzuri, waislamu wenye mafanikio, na kwa namna nyingine watawala kwa viumbe hai na wanyama wote.

Kwa hakika, kijana anapopitisha saa moja jela kati ya ishirini na nne kila siku katika swala za faradhi, na akajutia makosa yaliyokuwa sababu ya balaa lake, na akajizuia dhidi ya maovu mengine, madhambi, hilo litamnufaisha sana maishani mwake, na mustakabali wake, na nchi yake, na taifa lake, na nduguze, ndivyo pia atanufaika katika ujana wake wa mpito kwa miaka kumi mpaka kumi na mitano ya ujana wa kudumu na mzuri sana. Kwanza kabisa Qur’an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza, na maandiko yote yaliyoteremshwa, yametoa bishara hii ya uhakika.

Kama kijana wa aina hiyo anashukuru neema nzuri ya ujana kwa wastani na utii, itauzidisha, na kuufanya wa milele, na kuufanya starehe. Vinginevyo utakuwa balaa, na kuwa wenye maumivu, na jinamizi, na kisha utaondoka. Itamsababisha awe kama mzururaji, mwenye kuwakosea ndugu na jamaa zake, nchi na taifa lake.

Kama mfungwa amefungwa kwa dhuluma, kwa sharti kuwa anaswali swala tano, kila saa moja italingana na ibada ya siku nzima, na jela itakuwa kama chumba cha mtu anayeishi peke yake. Atahesabiwa miongoni mwa watawa wachamungu wa hapo zamani waliokimbilia mapangoni kwa ajili ya kujiweka katika ibada. Kama ni masikini, mwenye umri mkubwa, na mgonjwa, na anayetaka ukweli wa imani, kwa sharti kuwa anaswali swala tano za faradhi na anatubu, kila saa italingana na saa ishirini za ibada, na jela itakuwa kama nyumba yake ya mapumziko, na kwa sababu ya marafiki zake humo wanaompenda, nafasi ya upendo, mafunzo, na elimu. Huenda akawa mwenye furaha zaidi kukaa jela kuliko kuachiliwa huru, kwa kuwa nje anachanganyikiwa na anapata mashambulizi ya madhambi kutoka kila upande. Anaweza kupata elimu kamili kutoka jela. Siku ya kuachiliwa, haitakuwa kama muuaji, au kuwa na kiu ya ulipizaji kisasi, bali mtu mwenye subira, aliyethibitishwa na majaribu, mwenye tabia njema, na mwenye manufaa kwa taifa lake. Kwa hakika, wafungwa wa Denizli kwa hivyo wamekuwa na maadili mema ajabu baada ya kusoma Risale-i Nur kwa muda mfupi tu ambao baadhi ya waliohusika walisema: “Kusoma Risale-i Nur kwa wiki kumi na tano kuna athari zaidi katika kuwabadili wao kuliko kuwaweka gerezani kwa miaka kumi na mitano.”

Kwa kuwa kifo hakifi na saa iliyopangwa haijulikani, kinaweza kuja katika wakati wowote; na kwa kuwa kaburi haliwezi kufungwa, na kikundi baada ya kikundi huingia na kupotea; na kwa kuwa imeoneshwa katika ukweli wa Qur’an kuwa kifo kwa waumini kimebadilika kuwa nyaraka za kuruhusiwa watoke katika ukandamizwaji wa kudumu, ilhali kwa wakorofi na mafisadi ni kupotelea milele katika maangamizi ya milele, na pia ni utenganishwaji usio na kikomo baina yao na wapenzi wao na viumbe wote, lililo na hakika na bila ya shaka yoyote, mtu mwenye bahati sana ni aliye mvumilivu na anashukuru kikamilifu manufaa tangu wakati wake wa jela, na kusoma Risale-i Nur kwa ajili ya kuitumikia Qur’an na imani yake katika njia iliyonyooka.

Ewe mtu uliyezoea furaha na starehe! Mimi nina umri wa miaka sabini na tano, na ninajua kwa hakika kutokana na wingi wa uzoefu, shuhuda, na matukio kuwa furaha ya kweli, starehe isiyo na maumivu, isiyo na masikitiko, na furaha ya maisha inaweza tu kupatikana katika imani na katika wigo wa ukweli wa imani. Starehe moja ya kidunia hata hivyo, huleta maumivu mengi. Kama vile kupigwa makofi kumi kwa ajili ya tunda moja la zabibu, huondoa starehe zote za maisha.

Enyi watu msiobahatika wanaopata janga ndani ya jela! Kwa kuwa dunia yenu inalia na maisha yenu ni machungu, fanyeni jitihada ili Akhera yenu pia isilie, na maisha yenu ya milele yafurahi na kuwa matamu! Nufaikeni na jela! Kama ambavyo wakati mwingine katika hali iliyoshitadi katika kumkabili adui, uangalizi wa saa moja unaweza kulingana na ibada ya mwaka mmoja, ndivyo pia katika hali iliyoshitadi unayoweza kuwepo, ugumu wa kila saa iliyotumika katika ibada inakuwa yenye kulingana na saa nyingi, hubadili ugumu huo na kuwa rehema.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.