NENO LA KWANZA

Kwa Jina la Allah,

Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Na kutoka Kwake tunataka msaada.

Kila sifa njema ni kwa Allah,

Mola Mlezi wa ulimwengu,

na rehema na amani zimfikie mkuu wetu,

Muhammad, na aali na Sahaba zake wote.

NENO LA KWANZA

Bismillah, “Kwa jina la Allah”, ni mwanzo wa mambo yote mema. Sisi pia, tunaanza kwa jina hilo. Tambua, ewe roho yangu! Kama maneno hayo matukufu yalivyo alama ya Uislamu, ndivyo pia husomwa mara zote na viumbe wote kwa ndimi zao za silika. Kama unataka kujua namna nguvu ilivyo kubwa, namna gani Bismillah ilivyo chanzo cha baraka isiyokoma, sikiliza kisa kifuatacho kilicho katika namna ya mlinganisho. Kinaenda kama hivi:

Mtu anayesafiri katika majangwa ya Uarabuni anapaswa asafiri kwa jina la mkuu wa kikabila na kuwa chini ya hifadhi yake, kwa njia hii angeweza kunusurika dhidi ya kuvamiwa na majambazi na kulinda haja zake. Peke yake, anaweza kupotelea mbele ya maadui wengi na mahitaji. Na kwa hivyo, watu wawili walikwenda safarini na kuingia katika jangwa. Mmoja alikuwa mwenye haya na mnyenyekevu, mwingine alikuwa na kiburi na mwenye majivuno. Yule mnyenyekevu alitumia jina la mkuu wa kabila, ilhali mwenye kiburi hakutumia. Wa kwanza alisafiri kwa usalama popote alipokwenda. Alipokutana na majambazi, alisema: “Ninasafiri kwa jina la fulani bin fulani, kiongozi wa kabila,” na hawakumsumbua. Alipofika katika baadhi ya mahema, aliheshimiwa kwa sababu ya jina hilo. Ama mwenye kiburi alipata majanga katika safari yake yote ambayo hayaelezeki. Alitetemeka mbele ya kila kitu na kuwa mwombaji kutoka kwa kila mtu. Alidhalilika na akawa mwenye kudhihakiwa.

Na kwa hivyo, ewe roho yangu jeuri! Wewe ni msafiri, na dunia hii ni jangwa. Udhaifu na umasikini wako havina ukomo, na maadui zako na haja zako havina mwisho. Kwa kuwa ni hivyo, chukua jina la Mtawala wa Tangu hapo kale na Mola Mlezi wa Milele wa jangwa na unusurike dhidi ya kuombaomba ulimwenguni kote na kutetemekea kila jambo.

Kwa hakika, fungu hili la maneno ni hazina iliyobarikiwa sana ambayo ufukara, na udhaifu wako usio na ukomo hukuunganisha na uwezo na rehema isiyo na ukomo; inafanya udhaifu na uhitaji huo uwe mwombezi wa kukubalika katika Mahakama ya Mmoja Mweza wa Yote na Mwenye Rehema. Mtu anayetenda jambo kwa kusema, “Kwa Jina la Allah,” anafanana na anayejiandikisha jeshini. Anatenda kwa jina la serikali; hamwogopi yeyote; anazungumza, anafanya kila jambo, na anahimili kila kitu kwa jina la sheria na jina la serikali.

Mwanzoni tulisema kuwa viumbe wote husema, “Kwa jina la Allah” kwa ndimi za silika. Sivyo?

Kwa hakika, ndivyo. Kama ungeona kuwa mtu mmoja amekuja na kuwaondoa wakazi wote wa mji kwenda sehemu nyingine kwa nguvu na kuwashurutisha kufanya kazi, ungekuwa na uhakika kuwa hakufanya hivyo kwa jina lake na kwa nguvu zake mwenyewe, bali alikuwa askari, anayetenda kwa jina la serikali na kutumainia nguvu ya mfalme.

Halikadhalika, mambo yote yanafanya kwa jina la Allah (s.w), kwa vitu vidogo, kama mbegu na nafaka zenye kubeba miti mikubwa vichwani mwao; zinabeba mizigo kama milima. Maana yake miti yote husema: “Kwa jina la Allah,” hujaza mikono yao kutoka hazina ya Rehema, na kutuletea. Mashamba yote husema: “Kwa jina la Allah,” na kuwa masufuria makubwa kutoka katika majiko ya Nguvu ya Kiungu ambamo hupikwa namna nyingi za vyakula. Wanyama wote wabarikiwa kama ng’ombe, ngamia, kondoo na mbuzi husema: “Kwa jina la Allah,” na kutoa chemchemi za maziwa kutoka katika wingi wa Rehema, na kutuletea chakula halisi kitamu kama maji ya uzima kwa jina la Mwenye Kuruzuku. Mizizi mikubwa na midogo, laini kama hariri, ya mimea yote, miti, na majani, husema: “Kwa jina la Allah,” na kupasua na kupenya katika mwamba mgumu na ardhi. Kwa kutaja jina la Allah, jina la Mwingi mno wa Rehema, kila kitu kinadhalilishwa kwao.

Kwa hakika, majani yanayoenea katika mwamba mgumu na ardhi na kuzalisha matunda kwa urahisi kama matawi yanavyotanda angani na kuzaa matunda, na majani laini ya kijani yenye kuhifadhi unyevunyevu kwa miezi mingi katika joto kali, hupiga kofi midomoni mwa wenye imani ya nguvu za Asili na kutia kidole katika macho yao mapofu huku yakisema: “Hata joto na ugumu, mnaoutumainia sana, viko chini ya amri. Kwa kuwa, kama Fimbo ya Musa, kila mzizi wa udogo wa hariri unafuata amri ya

 فَقُلْنَا اضْرِب بِّعَصَاكَ الْحَجَرَ Qur’an, 2:60

na jiwe likapasuka. Na majani laini na madogo kama karatasi ya sigara, yanasoma aya,

يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا Qur’an, 21:69

dhidi ya joto la moto, kila moja kama watu wa Ibrahim (a.s).

Kwa kuwa vitu vyote husema, “Kwa Jina la Allah” na kupata neema za Allah kwa jina la Allah na sisi kupewa hizo neema, basi sisi pia tunapaswa tuseme: “Kwa Jina la Allah.” Tunapaswa kutoa kwa Jina la Allah na kuchukua kwa Jina la Allah. Na tusichukue kutoka kwa watu wasio wasikivu wanaoacha kutoa kwa Jina la Allah.

Swali:

Huwa tunawapa watu thamani, ambao ni kama wenye kubeba chano. Basi ni thamani gani anayotaka Allah, ambaye ndiye mmiliki wa kweli?

Jibu:

Ndiyo, bei anayotaka Mkweli wa kuruzuku neema hizo za thamani kubwa na bidhaa ni mambo matatu: moja ni kumkumbuka, jingine kumshukuru, na jingine ni tafakuri. Kusema, “Kwa jina la Allah” mwanzoni mwa jambo ni kumkumbuka. Na “sifa zote njema ni kwa Allah” mwishoni mwa jambo ni Kumshukuru. Tafakuri ni kufahamu na kuzifikiria neema hizo, ambazo ni sanaa ya ajabu isiyowezekana kuipa thamani, miujiza ya uwezo wa Mmoja Mpweke Wa Milele Mwenye Kutegemewa na zawadi za rehema Yake. Ni upumbavu mkubwa mno kubusu mguu wa mtu duni anayekufikishia zawadi ya thamani kubwa ya mfalme na kuacha kumtambua mwenye kutoa zawadi, ni upumbavu uliokithiri mno kusifu na kupenda chanzo kinachoonekana cha neema na kumsahau Mkweli wa Kuruzuku.

Ewe roho yangu! Kama hutaki kuwa mpumbavu wa namna hiyo, toa kwa Jina la Allah, chukua kwa Jina la Allah, anza kwa jina la Allah, na utende kwa Jina la Allah. Hilo ndivyo jambo lilivyo kwa kifupi!

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.