SWALI MUHIMU

Mnasema:Hakika mapenzi si jambo la hiari halipo katika matakwa yetu, mimi kwa mujibu wa haja yangu ya kimaumbile ninapenda vyakula vitamu, na matunda mazuri, na ninawapenda wazazi wangu wawili na watoto wangu na mke wangu ambaye ni mwenza wa maisha yangu, na nawapenda manabii watukufu, na mawalii wema, na ninapenda ujana wangu, na uhai wangu, na ninapenda majira ya machipuo na kila kitu kizuri, na kwa maelezo ya ufupi mimi naipenda dunia. Na kwanini nisipende vitu vyote hivi? : Lakini vipi nitaweza kuwasilisha aina zote hizi za mapenzi kwa Mwenyezi Mungu, na kujaalia mapenzi yangu kwa majina yake mazuri na sifa zake tukufu na dhati yake takatifu (s.w)? Hii ina maana gani?

Jawabu:

Unapaswa kusikiliza nukta nne zifuatazo:

Nukta Ya Kwanza:

Hakika mapenzi hata kama sio ya kihiari, isipokuwa yanaweza kugeuzwa muelekeo wake kwa matakwa kutoka mpendwa mmoja kwenda mwingine; mathalani kama vile kudhihiri ubaya wa anaependwa na uhakika wake, au kujulikana kwamba ni kizuizi na pazia kwa mpendwa wa hakika anaestahiki mapenzi, au kioo chenye kuakisi uzuri wa huyo mpendwa wa hakika, basi hapo inawezekana kugeuzwa sura ya mapenzi kutoka mpenzi asie wa hakika na kwenda kwa mpenzi wa hakika.

Nukta Ya Pili

Sisi hatukuambii: Usibebe mapenzi kwa kila ulichotaja hapo nyuma. Lakini tunakwambia jaalia mapenzi yako kwa hivyo ulivyovitaja yawe kwa ajili ya Allah na kwa dhati yake tukufu.

Kuburudika na vyakula vyenye ladha na kuonja matunda mazuri pamoja na kukumbuka kuwa hiyo ni hisani kutoka kwa Allah (s.w), na ni neema kutoka kwa Mwingi wa rehma, mwenye kurehemu, inamaanisha mapenzi kwa jina la (Al-rahmaan) na jina la (Al-muniimu) katika majina mazuri zaidi, isitoshe hiyo ni shukrani ya kimaanawi. Na ambayo inatujulisha kuwa mapenzi haya hayakuwa kwa ajili ya nafsi na matashi yake bali kwa ajili ya jina la (Al-rahman) ni kutafuta riziki ya halali pamoja na kukinai kikamilifu ndani ya duara la halali kisheria na kutumia kwa kutafakari kuwa hiyo ni neema kutoka kwa Allah (s.w), pamoja na kumshukuru.

Kisha mapenzi yako kwa wazazi wawili na kuwaheshimu kunarejea katika kumpenda Allah (s.w); kwani yeye ndiye aliyepandikiza kwao upole na huruma hata wakakulea kwa huruma na hekima zote. Na alama ya kuwa ni mahaba kwa ajili ya Allah (s.w), kuzidisha kuwapenda na kuwaheshimu wanapofikia uzee, na hakubakiii tamaa yoyote ndani  yako kupata chochote kutoka kwao, ukawa unaongeza huruma kwao pamoja na kuwa wanakushughulisha na matatizo na kukuzidishia uzito wa mashaka. Basi aya tukufu:

إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلاَهُمَا فَلاَ تَقُل لَّهُمَآ أُفٍّ وَلاَ تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلاً كَرِيمًا ۞ وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا Qur’an, 17:23-24

Zinalingania watoto kuchunga haki za wazazi wawili katika ngazi tano, na zinabainisha umuhimu wa kuwafanyia wema na ubaya wa kuwaudhi, kwani mzazi hakubali kutanguliwa na yoyote isipokuwa mwanawe kwani habebi katika maumbile yake hasadi yoyote dhidi yake jambo ambalo huziba njia kwa mtoto kudai haki yake kutoka kwa mzazi, kwani uhasama ima unatokana na hasadi na kushindana kati ya wawili au hutokana na kudharau haki, mzazi yuko salama amenusuriwa na hayo kimaumbile, kwa hiyo si halali kwa mtoto kuleta madai dhidi ya mzazi wake, hata kama ataona kwake uovu hana haki ya kumuasi na kumuudhi. Kwa maana anaewaasi na kuwaudhi wazazi wake wawili huyo hawi vimginevo ila ni Mwanaadamu aliyegeuzwa umbo na kuwa mnyama mshambuliaji . Ama kuwapenda watoto ni kumpenda Allah (s.w) vilevile na kunarejea kwake. Na hii ni kwa kutekeleza matunzo yao kwa upole na huruma kamili kwa kuwa wao ni hiba kutoka kwa Al-rahiim Al-kariim, na ama alama ya kuwa mapenzi hayo ni kwa ajili ya Allah (s.w), na kwa ajili yake ni kule kusubiri pamoja na kushukuru wakati wa kupatwa na mtihani na hasa wakati wa kifo, na kujiepusha na kukata tamaa na kupuuzia dua, bali inapasa kusalimu amri mbele ya majaaliwa kwa kushukuru. kama kusema: Hakika kiumbe huyu ni mwenye kupendwa mbele ya mola Muumba Mkarimu na mwenye kumililkiwa naye, na amenikabidhi akiwa ni amana kwa muda fulani, na sasa imeamua hekima yake (s.w), kumchukuwa kutoka kwangu kumpeleka mahali pa salama na bora zaidi. Ikiwa nina hisa moja tu ya dhahiri, basi yeye (s.w), ana hisa elfu moja za hakika. Hakuna pa kukimbilia kutokana kujisalimisha na hukumu ya Allah (s.w).

Ama kuwapenda masahiba, wakiwa ni katika watu wa Imani na uchamungu basi kuwapenda hao ni katika njia ya Allah (s.w), na kunarejea kwa (s.w) kwa mujibu wa (kupenda kwa ajili ya Allah (s.w))

Ama kumpenda mke naye ni mwenza wa maisha yako ni juu yako kumpenda akiwa ni zawadi maliwazo nzuri katika zawadi za rehema za kiungu. Na ole wako ufungamanishe na uzuri wa nje ambao huondoka haraka bali ufunge kwa umadhubuti na uzuri usiotoweka wenye kuzidi kung’ara siku baada ya siku nao ni uzuri wa tabia na mwenendo mzuri ulojikita kwenye uwanajike wake na upole wake. Na hakika kilicho kizuri mno kwake katika urembo na kikuu Zaidi, ni katika huruma yake ya dhati yenye nuru. Huu uzuri wa huruma na mwenendo mwema hudumu na kuongezeka hadi mwishoni mwa umri, na kwa kuvipenda viwili hivyo ndipo haki za kiumbe huyu mpole mnyonge huweza kulindwa, na kama sivyo, haki zake huzikosa wakati ambapo yeye huzihitajia mno, kwa sababu ya kuondoka uzuri wa nje. 

Ama kuwapenda manabii (a.s), na mawalii wema nako pia ni kwa ajili ya Allah (s.w) na katika njia yake kwa kuwa wao ni waja wa Allah (s.w), wateule wenye kukubalika mbele ya Allah (s.w) kwa upande huu mapenzi hayo yanakuwa ni kwa ajili ya Allah (s.w).

Pia maisha ambayo Allah (s.w) amekutunukia na kwa Mwanaadamu, ni rasilimali adhimu unayoweza kuitumia kuvuna maisha ya akhera ya kubakia milele, nayo ni hazina adhimu yenye kubeba ala na makamilisho ya kudumu. Kwa ajili hii kuyahifadhi na kuyapenda ni kutokana na upande huu, na kuyatumia kwa ajili ya Mola mlezi (s.w), hurejea kwa Allah (s.w).

Kadhalika kuupenda ujana, uzuri, na kupendeza kwake na kuuthamini kwa kuwa ni neema nzuri kutoka kwa Bwana Mlezi, kisha kuutumia vema, hayo ni mapenzi ya kisheria na bali ni yenye kushukuriwa.

Halafu kupenda majira ya machipuo na kuwa na shauku nayo kwa ajili ya Allah (s.w), na yenye kuelekea katika majina yake mazuri, kwa kuwa kwake ni ubao mzuri wa kuonekana michoro ya majina mazuri yenye nuru na maonyesho makuu zaidi kwa ajili ya kuonesha ufundi makini maridadi wa Mola Mlezi. Hivyo kutafakari majira ya machipuo kwa upande huu ni mapenzi yanayoelekea kwenye majina mazuri.

Hata kupenda dunia hugeuka kuwa ni mapenzi kwa ajili ya dhati ya Allah (s.w), pale inapokuwa kuitazama hiyo dunia ni kwa upande wa kuwa ni shamba la Akhera, na kioo cha majina ya Allah (s.w), mazuri, na ni barua za Bwana Mlezi katika Uwepo (ulimwengu na kila kilichomo) na nyumba ya ugeni kwa muda na kwa sharti la kutoingilia nafsi yenye kuamrisha maovu ndani ya mapenzi hayo.

Muhtasari:

Jaalia kupenda kwako dunia na vilivyomo miongoni mwa viumbe kwa maana (ya kiherufi) na siyo kwa maana (ya kijina) yaani kwa maana ya yaliyomo na sio dhati yake yenyewe. Wala usiseme kwa kitu: “uzuri ulioje wa kitu hiki!” bali sema: “uzuri ulioje wa umbo la kitu hiki!” au “umbo lake ni zuri namna gani!” Na tahadhari usije ukaacha mwanya wa kumpenda asiyekuwa Allah (s.w), ndani ya moyo wako, kwani ndani yake ni kioo cha Al-swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote), na ni mahsusi na maalum kwa ajili yake Allah (s.w), na useme: Ee Allah! Turuzuku kukupenda na kupenda yanayotukurubisha kwenye kukupenda wewe. 

Kama hivyo, yote tuliyoyataja katika aina za mapenzi endapo yataelekezwa upande sahihi kwa sura iliyotajwa huko nyuma, yaani yanapokuwa kwa ajili ya Allah (s.w), na kwa njia yake, basi yataleta ladha ya ukweli bila ya machungu na itakuwa ni muunganiko wa kweli pasina kutoweka bali yatazidisha mapenzi ya Allah (s.w), ukiachilia mbali kule kuwa hayo ni mapenzi ya kisheria na yanakuwa ni shukurani kwa Allah (s.w), katika ladha hiyo hiyo na kutafakari juu ya neema zake ndani ya hayo hayo mapenzi.

Mfano:

Ikiwa mfalme mkubwa amekuzawadia

Tukio hili lilitokea kwa hakika hapo zamani, wakati viongozi wa koo mbili walipoingia kwa Sultani mkuu na wakatimiza mfano wa yaliyoelezwa hapo juu. (Mtunzi)

tufaha -mathalan- hakika utalipa aina mbili ya mapenzi na utaburudika nalo kwa ladha za aina mbili:

Ya kwanaza:

Mapenzi ambayo yanarejea kwenye tufaha, kwa kuwa ni tunda zuri lina ladha kiasi cha sifa maalum zilizomo ndani yake, mapenzi haya hayarejei kwa mfalme. Bali anayelila kwa kupupia mbele yake huonesha mapenzi yake kwa hilo tunda na sio kwa mfalme, na pengine mfalme asifurahishwe na kitendo hicho, na akachukia mapenzi hayo makubwa kwa nafsi yake. Zaidi ya kuwa ladha ya tufaha ni ndogo nayo ni yenye kutoweka kwani mara tu baada ya kumaliza kula tufaha hilo ladha huondoka na kusababisha majuto.

Ama mapenzi ya pili:

Ni kwa ajili ya takrima ya kifalme na kuzingatia kwake kwema ambako kumeonekana kwa tufaha, kana kwamba tufaha lile ni kielelezo cha heshima ya kifalme, au ni sifa iliyobeba umbo kutokana na tufaha. Anayepokea zawadi ya mfalme kwa mapenzi na takrima, anaonesha mapenzi yake kwa yule mfalme na sio kwa lile tufaha, hali ya kujua kwamba katika tufaha lile ambalo limekuwa ni maonesho ya takrima, lina ladha ya juu mno zaidi ya matufaha elfu moja mengine kwa thamani ladha hii yenyewe ni shukrani, na mapenzi haya ni mapenzi yenye heshima na utukuzo unaoendana na hadhi ya mfalme.

Hivyohivyo Mwanaadamu akielekeza mapenzi yake kwenda kwenye neema na matunda hasa, na akastaraehe hali ya kughafilika kwa ladha zake za kimaada tu, hayo ni mapenzi ya kinafsi yanarejea kwenye matashi ya nafsi, na ladha hizo ni zenye kutoweka na kuumiza. Ama mapenzi yakiwa ni kwa upande wa takrima ya kiungu na upande wa mazuri ya huruma zake (s.w), na matunda ya hisani yake, kwa kuthamini viwango vya hisani na upole hali ya kupata ladha yake kwa hamu kamili, hiyo inakuwa ni shukurani ya kimaanawi, na hiyo ni ladha isiyosababisha maumivu.

Nukta Ya Tatu:

Hakika mapenzi yanayoelekea kwenye majina mazuri yana tabaka kadhaa: Unaweza kuelekeza mapenzi kwa majina mzuri ya Allah (s.w) kwa kupenda athari za kiungu zilizozagaa ulimwenguni –kama tulivyobainisha huko nyuma- na unaweza kuelekeza mapenzi kwa majina mazuri ya Allah (s.w), kwa kuwa ni anuani ya kamilifu za kiungu zilizotukufu, na Mwanaadamu anaweza kuwa na shauku ya majina mazuri ya Allah (s.w), kwa haja zake kubwa na hii ni kwa wasifu wake jumuishi na mahitajio yake yasiyo na mipaka, yaani anayapenda majina hayo kwa msukumo wa mahitajio yake kwa majina hayo.

Kubainisha hayo kwa mfano:

Jenga picha hali ya kuwa unaleta hisia ya udhaifu wako na uhitaji wako mkubwa kwa ambaye atakusaidia kuwaokowa wale unaowahurumia katika hali zao miongoni mwa jamaa wa karibu na mafukara na hata viumbe dhaifu wenye haja, tahamaki mmoja wao anatokeza katika medani, na anafanya wema, ufadhili juu yao na kuwaenezea neema zake kwa namna utakavyo, basi kiasi gani nafsi yako huwa vizuri na kustarehe kwa jina lake (Al-munim) na (Al-kariim ) na kiasi gani nafsini mwako hufurahika na kukunjuka kutokana na mjina haya mawili. Bali ni kiasi gani mtu huyo atapata pendo na thamani kutoka kwako, na kiasi gani unavyomuelekea kwa mapenzi kwa majina na anuani hizo mbili!

Kwa mwanga wa mfano huu zingatia majina mawili tu katika majina mazuri nayo: Ni (Al-rahman) na (Al-rahiim) utaona kuwa waumini wote miongoni mwa kinababa na mababu waliopita na wapenzi wote na marafiki, hawa ambao unawapenda na kuwaweka moyoni sana na kuwahurumia, wananeemeshwa duniani kwa aina za neema zenye ladha, kisha watafurahishwa huko Akhera, kwa kupewa neema zenye ladha na kupendeza, bali Mwenyezi Mungu atawazidishia naye ni Mwingi wa rehema mwenye kurehemu kuwapa furaha na neema ya kukutana wao kwa wao na kuona uzuri wa kudumu milele huko Akhera, basi kiasi gani yanakuwa majina mawili ya (Al-Rahman) na (Al-rahiim) yenye kustahiki upendo? na kiasi gani roho ya Mwanaadamu inakuwa na shauku kubwa kwa majina hayo? Pima mwenyewe hayo ili uone kiasi cha usahihi wa kauli yetu: ‘Alhamdulillah kwa sifa yake ya wingi warehema na mwenye kurehemu.’

Kisha hakika wewe unaambatana na viumbe vilivyotawanywa ardhini, na unapata uchungu kwa taabu zake, mpaka inakuwa kana kwamba ardhi yote ni makazi yako mazuri na nyumba yako uliyoizowea, basi kama utachunguza kwa makini utakuta rohoni mwako kunashauku kubwa na haja kubwa ya jina la Al-hakiim (Mwingi wa hekima) na anuani ya Al-murabbi (mlezi) kwa ambaye anapangilia viumbe hivi vyote kwa hekima kamili nidhamu madhubuti na usimamizi wa hali ya juu na malezi yenye huruma.

Kisha kama utatazama kwa makini katika jinsi ya Mwanaadamu utajikuta unaambatana nao na kuumia kwa ajili ya hali zao mbaya na unaumia sana kwa kutoweka kwao na kufariki kwao, tahamaki roho yako inapata shauku ya jina la Al-waarithu, Al-baaithu (mrithi wa kila kitu na mwenye kufufua wafu) na unahitajia anuani ya Al-baaqy (mwenye kubakia daima) Al-kariim (karimu sana), Al-muhyi (muhuishaji), Al-muhsin (Mwingi wa hisani) ya Muumba karimu sana ambaye anawaokoa kutoka kwenye giza nene la kutokuwepo na kuwapa makazi mazuri na bora zaidi kuliko dunia.

Na kama hivi na kwa kuwa haiba ya mwanaadamu ni ya juu na umbo lake ni jumuishi, hivyo yeye ni muhitaji wa haja elfu moja na moja majina elfu moja na moja katika majina yake Allah (s.w) yaliyo mazuri na nyingi mno ya ngazi za kila jina. Basi haja yenye kuongezeka ni shauku, na shauku yenye kuongezeka ndiyo mahaba na mahaba yenye kuongezeka ndiyo ashiki, kwa mujibu wa ukamilifu wa roho ya mwanaadamu hufunuka ngazi za mahaba kulingana na ngazi za majina, na mahaba ya majina yote vilevile hugeuka kuwa mahaba ya dhati yake tukufu (s.w) kwani majina hayo ni anuani na udhihirisho wa dhati yake mtukufu na wa sifa za juu.

Na sasa tutabainisha kati ya majina elfu moja na moja kati ya majina mazuri, ngazi moja tu na kwa njia ya mfano kati ya ngazi elfu moja na moja, ya jina la (Al-Adli, Al-Hakamu, Al-Haqq, Al-Rahiim) kwa mfano ufuatao:

Ikiwa unataka kushuhudia yaliyo ndani ya hekima na uadilifu kutokana na jina (Al-Rahmanirrahiim, Al-Haqq) jumla ya duara pana kubwa basi zingatia mfano huu:

Jeshi linalojumuisha vikosi mia nne tofauti katika askari, kila kimoja ni tofauti na kingine katika mavazi yanayowapendeza na kutofautiana katika vyakula wavipendavyo, na kuwa mbali mbali katika silaha wazitumiazo kwa wepesi, na kuwa aina tofauti katika matibabu wayatumiayo. Basi pamoja na kuwa na tofauti hizo na kuhitilafiana katika kila kitu, hakika vikosi hivyo mia nne havitengani katika matapo na makundi makundi, bali yanashikana pamoja pasi na kubaguka.

Kama pakiwepo mfalme mmoja anayelipa kila kundi mavazi yanayowiana nalo, na riziki zinazoendana nalo na matibabu yanayonasibiana nalo, na silaha zinazoafikiana nalo, bila ya kusahau yeyote wala kuchanganya, na bila ya kuwa na msaidizi, bali anazigawa zote kwao kwa dhati yake, kwa sifa anazosifikana nazo ikiwemo rehema, upole, uweza, elimu yenye muujiza, na kuyazungukia kikamilifu mambo yote pamoja na uadilifu wa hali ya juu na hekima iliyotimia.

Naam, ikiwa atakuepo mfalme kama huyu asiye na kifani, na ukashuhudia kwa nafsi yako kazi zake muujiza dhahiri, wakati huo utaona kiasi cha uweza wake, upole wake na uadilifu wake, hiyo ni kwa sababu kuandaa kikosi kimoja chenye watu kumi tofauti kwa zana mbali mbali na mavazi anuwai ni jambo gumu sana hata inakimbiliwa katika kuandaa jeshi kwa namna maalumu iliyothibiti katika mavazi na zana vyovyote watakavyotofautiana watu na aina zao.

Ukitaka -katika mwanga wa mfano huu- kuona udhihirisho wa jina la Allah (Al-Haqq) na (Al-Rahmani Al-rahiim) ndani ya eneo la uadilifu na hekima, basi tembeza mtazamo wako kwenye majira ya machipuo katika mahema yale yaliyosimamishwa juu ya busati la ardhi la mataifa mia nne elfu mbali mbali na makundi tofauti ambayo yanawakilisha jeshi la mimea na wanyama, tazama kwa makini utakuta kwamba mataifa yote hayo na makundi yote hayo, pamoja na kuwa yameingiliana, na mavazi yao ni tofauti, na riziki zao ni tofauti na silaha zao ni anuwai na njia ya maisha yao ni tofauti na mazoezi yao tofauti na mafunzo yao tofauti.

Nao hawamiliki ndimi waweze kutafuta uhakika wa haja zao na kujibu matakwa yao. Pamoja na yote haya kila moja kati yao, huongozwa na kulelewa na kuchungwa kwa jina la (Al-Haqq, Al-Rahman, Al-Razzaq, Al-Rahiim na Al-kariim) pasi na  kuchanganya wala kusahau ndani ya eneo la hekima na uadilifu kwa mizani madhubuti na mpangilio wa hali ya juu, shuhudia udhihirisho huu na uzingatie;

Je, inawezekana kuingilia yeyote asiyekuwa Allah katika kazi hii ambayo inaendeshwa kwa mfano wa mpangilio huu wa ajabu na mizani madhubuti? na je, inawezekana kwa sababu yoyote vyovyote iwavyo kunyoosha mkono wake ili kuingilia katika ufundi huu wa kushangaza na uendeshaji wenye busara na ulezi wenye rehema na uongozi wenye kuenea ila mmoja wa pekee Mwingi wa hekima (Al-Hakiim), Muweza (Al-Qadir) juu ya kila kitu?

Nukta Ya Nne

Unasema mimi ninabeba aina mbali mbali ya mahaba ndani ya nafsi yangu, yenye kuambatana na vyakula vitamu, nafsi yangu, mke wangu watoto wangu, wazazi wangu, wapenzi wangu, marafiki zangu, mawalii wema, na manabii watukufu, bali mapenzi yangu yanaambatana na kila kilichokuwa kizuri, na kwa majira ya machipuo yenye kupambika maalumu na dunia kwa ujumla. Aina hizi tofauti za mapenzi ikiwa zitakwenda kulingana na vile ambavyo Qur’an’an tukufu inaamrisha, matokeo yake yatakuwaje na faida zake ni zipi?

Jibu:

Kubainisha matokeo hayo na kufafanua faida hizo zote, inahitaji utunzi wa kitabu kikubwa katika jambo hili,kwa hiyo hapa tutaashiria matokeo mamoja au mawili kati yake kwa ujumla. Na kwanza tutabainisha matokeo ambayo yatadhihiri duniani, kisha baada ya hapo matokeo yatakayodhihiri Akhera, nayo ni kama yafuatayo:

Tumekwisha taja huko nyuma: Kwamba aina za mahaba ambayo yapo kwa watu wenye kughafilika na watu wa dunia na ambayo hayatokani ila kwa ajili ya kushibisha raghba za nafsi, zina matokeo machungu na hatima mbaya katika tabu na mashaka, pamoja na yaliyomo katika furaha ndogo sana na raha ndogo, basi mathalan: Huruma hugeuka kuwa ni balaa yenye kuumiza kwa sababu ya kushindwa, na mahaba hugeuka kuwa ni kuunguza kwa hatari kwasababu ya utengano, na ladha hugeuka kuwa ni kinywaji cha sumu kwa sababu ya kutoweka. Ama akhera zitabaki bila ya mafanikio wala manufaa, kwa sababu hazikuwa katika njia ya Allah (s.w) au zitakuwa adhabu iumizayo ikiwa zitapelekea katika haramu.

Swali:

Vipi yanakuwa mapenzi ya manabii watukufu na mawalii wema, bila ya manufaa au faida yoyote?

Jibu:

Ni kama manasara wenye kuitakidi utatu hawanufaiki na mapenzi yao kwa bwana Issa (a.s), na vilevile Al-rawafidh na mapenzi yao kwa Sayyidina Ali (r.a).

Ama ulichokieleza katika aina za mahaba yakiwa kulingana na maelekezo ya Qur’an tukufu na katika njia ya Allah (s.w) na mahaba ya Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, hakika matokeo mazuri huzaa matunda duniani, ukiachilia mbali matokeo mazuri ya kudumu milele Akhera.

Ama matokeo yake duniani:

Hakika kupenda kwako vyakula vitamu na matunda mazuri, hiyo ni neema ya kiungu haichanganyiki na maumivu, na ladha njema ndani ya shukrani yenyewe.

Ama kuipenda nafsi yako, yaani kuionea huruma, na kufanya jitihada ya kuilea na kuitakasa na kuizuia na matamanio mabaya, huifanya kuwa ni yenye kukutii, haikuendeshi wala haikufungi na matamanio yake, bali wewe unaiongoza kuelekea kwenye mwongozo na sio matamanio ya nafsi.

Ama kumpenda mkeo naye ni mwenza katika maisha yako, ni kwa sababu yamejengwa juu ya wema wa mwenendo wake na uzuri wa huruma yake, na kuwa kwake hiba kutoka katika rehema ya kiungu. Basi utampa mapenzi ya dhati na huruma ya kweli naye kwa upande wake atabadilishana na wewe mapenzi haya pamoja na heshima na unyenyekevu, na hali hii huongezeka kati yenu kila mnapoendelea mbele katika umri, mtaishi maisha mema ya raha mustarehe kwa idhini ya Allah (s.w). Lakini mapenzi hayo yangekuwa yamejengwa juu ya uzuri wa sura ambao unapendwa na nafsi, kwa hakika, haraka sana hunyauka na kufifia, na kuharibu maisha ya kindoa pia.

Ama mapenzi yako kwa baba na mama, hiyo ni ibada ambayo unalipwa thawabu madamu ni katika njia ya Allah (s.w), na hapana shaka kwamba utazidisha mapenzi na heshima kwao wanapofika uzeeni, na utavuna ladha ya kiroho iliyo safi na raha ya kimoyo timamu katika kutekeleza huduma kwao, kuwabusu mikono yao na kuwatukuza kwa dhati, na hivyo kuelekea kwa Mola Muweza hali ya kuwa unahisi hisia hii ya juu na hima ya kweli, kwamba umri wao urefuke ili upate ziada ya thawabu. Lakini mapenzi hayo na heshima hiyo yakiwa ni kwa ajili ya kuchuma makapi ya dunia, na yanatokana na matashi ya nafsi, hakika huzaa maumivu ya kiroho totoro hutokana na hisia duni iliyoporomoka na hisia ya chini sana, nayo ni kuwakimbia hao watukuzwa wawili ambao walikuwa ni sababu ya uhai wako wewe na kuwaona wazito hali ya kuwa wamefikia uzee na kuwa ni mzigo kwako, kisha la kutisha mno kuliko hilo kutamani umauti wao, na kungojea kutoweka kwao.!

Ama mapenzi yako kwa watoto wako, yaani kuwapenda kwako wale ambao Allah (s.w) amekupa amana, usimamie malezi yao, na kuwachunga. Basi mapenzi ya hao waliwazaji wapendwa katika viumbe wa Allah (s.w) hakika ni mapenzi yaliyovikwa taji la furaha na sherehe, na ni neema ya kiungu wakati huo huo, ukihisi hili, isikufunike huzuni juu ya msiba wao wala usipige kelele kwa majonzi juu ya kufa kwao. kwani -kama tulivyoeleza – hakika Muumba wao ni Mwingi wa rehema kwao, Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo yao, na hapo utasema, hakika umauti katika haki ya watu hawa, ni furaha kwao. Kwa jambo hili basi utaokoka kutokana na machungu ya utengano na utatafakari kumiminiwa juu yako rehema zake (s.w) Ama kuwapenda kwako marafiki na ndugu ni kwa ajili ya Allah (s.w), basi kutengana nao wala umauti wao havizuii kudumu kwa udugu wenu, mapenzi yenu, na kuliwazana kwenu, kwa sababu hudumu mafungamano hayo ya kiroho na mapenzi ya kimaanawi ya dhati, kwa duru yake basi hudumu pia ladha ya kukutana na utamu wa kuungana. Lakini mapenzi hayo yasipokuwa kwa ajili yake (s.w) wala katika njia yake, hakika ladha ya kukutana siku moja hurithisha maumivu ya kutengana kwa siku mia moja.

Hakika sekunde moja ya kukutana katika njia ya Allah (s.w) inahesabiwa mwaka katika umri. Wakati mwaka wa kukutana kwa ajili ya dunia yenye kutoweka hailingani na sekunde.

Ama kuwapenda kwako manabii (a.s) na mawalii wema, hakika ulimwengu wa barzakh ambao ni ulimwengu wa giza unatisha katika mtazamo wa watu wa upotevu na kughafilika, utaona kuwa ni nyumba za nuru zilizonawirishwa na hao wenye nuru, na wakati huo hautoogopa kukutana nao, wala huhofii ulimwengu wa barzakh, bali utakuwa na shauku nao, na kuupenda bila hilo kutibua kustarehe kwako na maisha ya dunia. Lakini mapenzi yao yakiwa yanashabihiana na yale ya watu wa ustaarabu kuwapenda watu mashuhuri wa ubinaadamu, basi kule kutafakari tu kuhusu kutoweka kwa mawalii hao wakamilifu, na kuoza mifupa yao katika makaburi ya zamani makubwa, huzidisha maumivu juu ya maumivu ya maisha, na humsukuma mtu kupata picha ya umauti wake na kutoweka kwake ambapo atasema: Siku moja nitaingia makaburi haya ambayo huozesha mifupa ya wakubwa.! atasema hayo kwa machungu yote na majuto yote na hofu, wakati ambapo katika mtazamo wa awali anawaona wanaishi kwa raha na starehe katika ulimwengu wa barzakh ambao ni ukumbi wa mustakbali na baraza zake, baada ya kuwa wameacha mavazi yao ya kimwili katika zama zilizopita, na anatazama makaburi mtazamo wa shauku na maliwazo.

Kisha mapenzi yako kwa vitu vizuri na mambo mazuri yakiwa ni mahaba katika njia ya Allah (s.w) na katika njia ya kumjua mtengezaji wake mtukufu, kiasi inakufanya useme: Uzuri ulioje wa uumbaji wake! mapenzi haya yenyewe kwa dhati yake ni tafakuri yenye ladha na burudiko, ukiachilia mbali kuwa inafungua njia mbele ya vionjo vya kupenda uzuri na shauku ya uzuri ili kuchungulia ngazi za viojo vya juu zaidi na kuonesha kuwa kuna hazina za thamani basi huisubiria mja kwa furaha ya hali ya juu; kwa sababu mahaba haya hufungua anga mbele ya moyo ili kugeuza mtazamo wake kutoka athari za fundi mtukufu kuelekea uzuri wa matendo yake ya ajabu, na kutoka uzuri wa matendo kuelekea katika uzuri wa majina yake mazuri, na kutoka katika majina yake mazuri kwenda katika uzuri wa sifa zake tukufu, na kutoka katika uzuri wa sifa zake tukufu kuelekea katika uzuri wa dhati yake takatifu. Basi mahaba haya na kwa njia hii hakika ni ibada yenye ladha na tafakuri ya juu ya kuburudisha wakati huo huo.

Ama kupenda kwako ujana, ni kwa sababu ulipenda enzi za ujana wako kwa kuwa kwake ni neema nzuri ya Allah (s.w), bila shaka utautumia katika kumuabudu yeye (s.w) wala hutouua kwa kuzama kwenye upumbavu na kudondokea katika upotevu, kwani ibada ambazo unazivuna wakati wa ujana hakika ni matunda yenye kustawi ya kubaki milele yamezalishwa na enzi hizo zenye kutoweka. Basi kila unapovuka enzi hiyo na kuongezeka katika umri unapata ziada ya matunda yake ya kudumu, na unaokoka kidogo kidogo kutokana na maafa ya nafsi yenye kuamrisha maovu na maovu ya babaiko la ujana. Basi unataraji kutoka kwa mola Muweza akuwafikishe kuvuna ziada ya ibada uzeeni, ili uwe mwenye kustahiki rehema zake kunjufu. Na kuendeleza nafsi yako na kuepuka kuwa miongoni mwa mfano wa wenye kughafilika ambao wanatumia miaka hamsini katika umri wa uzee wao na ukongwe wao kwa masikitiko na majuto kwa walichokikosa katika starehe za ujana ndani ya miaka mitano au kumi. Hata mmoja wa washairi akaeleza kuhusu majuto na masikitiko hayo kwa kauli yake:

Laiti ujana ungerudi siku moja,nikaupa habari namna uzee ulivyofanya.

Ni shairi la Abu al-Ataahiya. Aljahidh, Al-bayaan wa al-tabyiin 1/429.

Ama mapenzi yako kwa mandhari za kupendeza na hasa mandhari za majira ya machipuo, na kwa kuwa ni kushuhudia maajabu ya ufundi wa Allah (s.w) na kuutazama, basi kuondoka kwa majira hayo ya machipuo hakuondoshi ladha ya kushuhudia na starehe ya kutazama, kwani huacha maana yake nzuri nyuma yake, kwa kuwa majira ya machipuo inafanana sana ilivyo na risala ya kiungu yenye kupendeza inayofunguliwa kwa ajili ya viumbe. Taswira yako na muda ni vyenye kufanana na mkanda wa sinema vinakudumishia ladha ya kushuhudia huku, na daima vinafanya upya maana yake yanayobeba ujumbe wa majira ya machipuo, hivyo mapenzi yako kwa hiyo hayawi ya muda mfupi wala kufunikwa na masikitiko na majonzi, bali safi yametakata  matamu yenye kuleta raha.

Ama kupenda kwako dunia, ni kwa kuwa ni mapenzi kwa ajili ya Allah (s.w), hakika vilivyomo ndani yake vyenye kusisimua, kuamsha hofu, na mshangao hugeuka kuwa ni marafiki zako waliwazaji, na kwa kuwa unavielekea kwa mahaba kwa kuwa kwake ni shamba la akhera, unaweza kuvuna kutokana na kila kitu ndani yake kinachoweza kuwa tunda katika matunda ya akhera, au utavuna kutokana nayo kinachoweza kuwa ni rasilimali ya akhera, misiba yake hivyo haikuhofishi na kutoweka kwake na kwisha kwake hakukupi tabu. Na namna hivi utatumia muda wa kuishi kwako humo hali ya kuwa wewe ni mgeni mheshimiwa. Lakini kama mapenzi yako kwa dunia ni sawa na yale ya watu wa mghafala, tumekwisha kukuambia mara kwa mara: Utaizamisha nafsi yako na kuiteketeza kwa mapenzi yenye kusaga, kukaba, yenye kutoweka hakuna faida wala manufaa yanayobakia nyuma yake.!

Na kama hivi hakika tumejitahidi kuonesha jambo jema moja kati ya mamia ya mema yanayorejea kwa yote uliyoyaeleza. Pale ambapo mapenzi yako kwake ni kwa mujibu wa maelekezo ya Qur’an tukufu, na katika wakati huo huo tumeashiria mojawapo kati ya mamai ya madhara ya mapenzi hayo kama hayakuwa kwa mujibu wa namna Qur’an tukufu inavyoamuru. Ukiwa unataka kudiriki matokeo ya aina hizi tofauti za mahaba katika mji wa kudumu na ulimwengu wa akhera, kama namna ambavyo aya za waziwazi za Qur’an zimeashiria, tutakubainishia ubainifu wa jumla faida moja ya kiakhera katika faida za hizo aina za kihalali miongoni mwa mapenzi, na hii ni katika ishara tisa, baada ya kutanguliza utangulizi kabla yake. 

UTANGULIZI

Hakika Allah (s.w) -kwa uungu wake mtukufu, na rehema yake kubwa na ulezi wake mkubwa, na upole wake mwema, na uweza wake mkuu, na hekima yake njema,- amempamba huyu mtu mdogo kwa milango ya fahamu na hisia nyingi sana, na kumfanya kuwa mzuri kwa viungo na zana na viungo mbali mbali vingi, ili amjulishe tabaka za rehema yake yenye kuenea na amuonjeshe aina za neema zake zisizohesabika, na amtambulishe vigawanyo vya hisani zake visivyodhibitika kwa hesabu, na amuoneshe kupitia vifaa na viungo hivyo vingi juu ya aina za madhihirisho yake yasiyo na mpaka ya majina elfu moja na moja katika majina yake mazuri, na kuyapendezesha kwake, na kumfanya anayapa hadhi vyema haki ya hadhi yake.

Basi kila kiungo miongoni mwa hivyo viungo vingi, na kila kifaa na zana miongoni mwake, kina kazi zake anuwai na ibada zake tofauti kama ilivyo ladha zake mbali mbali na maumivu yake ni tofauti na thawabu yake ni yenye kupambanuka.

Basi mathalani: Jicho hushuhudia uzuri katika picha, na linaona miujiza ya qudra ya kiungu nzuri katika ulimwengu wa kuonekana hivyo hutimiza kazi yake kwa kuleta shukrani kwa Allah (s.w) kupitia mtazamo wake wenye mazingatio. Na haifichikani kwa yeyote kiasi cha yaliyomo katika mtazamo huu katika ladha, na maumivu yapatikanayo kutokana na kutoweka kwake. Kwa hivyo hakuna haja ya utambulisho wa ladha ya kuona na maumivu ya kukosa kuona.

Na mathalani: Sikio huhisi uzuri wa rehema ya kiungu inayoenda katika ulimwengu wa vyenye kusikilizwa, kwa kusikia kwake aina za sauti na viimbo vyake vizuri tofauti. Basi lina ibada maalumu kwake, na ladha inayoihusu, na thawabu inayorejea kwake.

Na mathalani: Mlango wa fahamu wa kunusa ambao unahisi rehema ya kiungu yenye kunukia vema kutokana na manukio ya aina za uturi na manukato, hakika ina ladha yake maalumu miongoni mwa kutekeleza kwake shukrani yake maalumu na hapana shaka kwamba inathawabu maalumu kwake.

Na mathalani: Mlango wa fahamu wa kuonja ambao umo kinywani, unatimiza kazi yake na unaleta shukrani yake ya kimaanawi kwa aina mbali mbali kupitia utambuzi wake vionjo vya aina za vyakula na ladha zake.

Na kama hivi, kila chombo katika vyombo vya mwanaadamu na kila mlango wa fahamu na kiungo, na kila kilicho laini katika laini zake muhimu -kama moyo, roho, akili n.k- kina kazi zake mbali mbali, na ladha zake anuwai zilizo mahususi kwake, basi katika yasiyo na shaka ndani yake kwamba Muumba Mwingi wa hekima ambaye ametiisha vyombo hivi kwa kazi hizo atalipa kwa kila mojawapo kwa namna inayoafiki na kustahiki katika malipo.

Hakika matokeo ya haraka ya aina nyingi ya mapenzi -yaliyotajwa hapo nyuma- kila mwanaadamu anahisi kwayo hisia ya ndani na kuthibitisha hisia yake hii na kuwa na yakini nayo kwa bunio la kweli. Ama matokeo yake ya kiakhera yamethibitishwa na hakika kumi na mbili katika hakika zenye kung’ara ya neno la kumi na misingi sita ya dhahiri ya neno la ishirini na tisa.

Ama upambanuzi wake umethibiti kwa mkato kwa Qur’an tukufu ambayo ni maneno ya kweli zaidi na nidhamu fasaha zaidi nayo ni maneno ya Allah mfalme, mwenye enzi, mjuzi wa kila kitu, katika kueleza aya zake za bayana na ishara zake na alama zake.

Kwa hiyo hatuoni haja ya kuleta hoja za kurefushwa katika jambo hili, kwa kujua kwamba sisi tumehudhurisha haja nyingi sana katika (Maneno) mengine na katika kituo cha pili cha kiarabu cha (Neno la ishirini na nane) linalohusu pepo na katika (Neno la ishirini na tisa).

Ishara Ya Kwanza:

Hakika matokeo ya kiakhera ya mapenzi yaliyo halali yaliyotunukiwa taji la shukrani kwa Allah (s.w), kwa vyakula vitamu na matunda mazuri duniani, ni vile vyakula na matunda mazuri vinavyoafikiana na pepo ya kudumu, kama inavyoeleza hilo Qur’an tukufu. Mapenzi haya, ni mapenzi yenye shauku na kutamani pepo hiyo na matunda yake. Hata hakika tunda unalokula duniani na kulitamkia

  الحَمْدُ للهِ

litafanyika mwili peponi kuwa tunda lake maalumu na wewe kupewa uzuri katika mazuri ya pepo. Hapa wewe unakula tunda, na huko

الحَمْدُ للهِ

ikiwa imeundika mwili kuwa tunda katika matunda ya peponi. Na kwakuwa wewe unaleta shukrani ya kimaanawi iliyo tamu kwa kuona kwako neema za kiungu na kukengeuka kwa kiungu katika vyakula na matunda ambayo unayala hapa, utapewa huko peponi zikiwa ni vyakula vitamu na matunda mazuri, kama ilivyothibiti katika hadithi na kwa ishara za Qur’an tukufu, na kwa muktadha wa hekima ya kiungu na rehema yake enevu.

Ishara Ya Pili:

Hakika ya matokeo ya mapenzi halali upande wa nafsi, yaani mapenzi yake yaliyojengwa duniani kwa kuona mapungufu yake kinyume cha mazuri yake, na kujaribu kuyakamilisha, kuyatakasa, kuyachunga kwa huruma na upole na kuyasukuma katika njia ya kheri, ni kipawa cha muumba (s.w) kwa wapendwa wenye kulingana nayo na pepo.

Basi nafsi ambayo iliyoacha duniani matashi na matamanio yake na ikaacha raghba zake katika njia ya Allah (s.w), na kutumia yaliyo ndani yake miongoni mwa zana anuwai kwa njia bora zaidi na timamu zaidi, Muumba mtukufu (s.w) ataitunuku malipo kwa ajili ya mapenzi haya ya halali yaliyovikwa taji la uja kwa Allah (s.w), mahuruaini wenye kujipamba kwa mapambo sabini katika mapambo ya peponi mbali mbali kwa aina ya mazuri na mapambo yake, na waliyojiremba kwa aina sabini za uzuri na urembo, hata wanakuwa kana kwamba wao ni pepo ndogo iliyoundika inayotweta kwa roho na uhai, ili jicho la nafsi ile iliyomtii Allah (s.w) litue na hisia zilizotulia katika amri za Allah (s.w) zipate kutulia. Matokeo hayo hakuna shaka ndani yake kwani aya tukufu zinasema wazi hivyo kwa yakini.

Kisha matokeo ya mapenzi yenye kuelekea upande wa ujana duniani yaani kutumia nguvu ya ujana na umaridadi wake katika ibada na uchamungu, ni ujana wa kudumu milele katika mji wa kubakia na neema za kudumu.

Ishara Ya Tatu

Ama matokeo ya kiakhera kwa mapenzi ya mke yaliyo asisiwa juu ya uzuri wa mwenendo wake na uzuri wa tabia yake na ulaini wa huruma zake, na ambayo yanamlinda na kuasi na kumuepusha na makosa na madhambi, ni kumfanya mke huyo mwenye kupendwa na mpenzi na rafiki mkweli na mwenza mliwazaji peponi. Uzuri wake unang’ara mno kuliko hurul-aini, mapambo yake yanavutia kuliko mapambo yao, uzuri wake unavuka uzuri wao, anabadilishana mazungumzo na mumewe, wanakumbushana matukio ya siku zilizopita, kama hivi ameahidi Mwingi wa rehema Mkarimu sana, basi kwa kuwa ameahidi atatimiza ahadi yake kwa hakika.

Ishara Ya Nne

Ama matokeo ya kuwapenda wazazi wawili na watoto ni kuwa Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu (s.w), anatenda wema kwa familia hiyo njema yenye bahati, licha ya kutofautina ngazi zao huko peponi kwa kukutana wao kwa wao, kuchanganyikana, kukaa pamoja, na kuongea pamoja kati yao kwa hali ambayo inakubaliana na pepo na maisha ya kudumu milele, kama jambo hili lilivyothibiti katika Qur’an tukufu. Na wazazi hao wataneemeshwa kwa kucheza na watoto wao ambao wamefariki katika maisha ya dunia kabla ya umri wa kubaleghe, na kuwafanya kwa ajili yao kuwa ni watoto “Weldanun mokhalladun” katika hali ya upole zaidi na inayopendeza zaidi nafsini mwao, na kwa hivi hutuliza raghba ya dekezo la watoto katika maumbile ya mwanaadamu, na wastarehe kwa starehe ya kudumu na onjo la kudumu huko peponi, ambapo wamewekwa milele wana wao wadogo -ambao hawajafikia umri wa kukalifishwa- na ilikuwa inadhaniwa kwamba peponi hakuna dekezo la watoto, kwa sababu si mahali pa kuzaana, lakini pepo kwa kuwa inakusanya ladha bora zaidi kuliko dunia na uzuri zaidi, basi kuwafanyia dekezo watoto na kucheza nao hapana budi hilo lipo huko kwa sura zake zilizo bora na maumbo yake mazuri zaidi.

Al-Tirmidhiy, sifat al-Jannah 23. Ahmad ibn Hanbal, Al-Musnad 3/80.

Basi furaha iliyoje ya hao wazazi ambao wamewapoteza watoto wao katika maisha ya dunia.

Ishara Ya Tano

Hakika matokeo ya mapenzi yako kwa ajili ya marafiki na jamaa wa karibu ambayo yanahitajia (mapenzi katika Allah), hakika hiyo ni katika vikazi vyenu kwenye makochi yenye kuelekeana na kuliwazana kwenu kwa kumbukumbu nzuri, kumbukumbu za masiku ya duniani na matukio yake mazuri, na kuishi wakati wa raha na mzuri kwa mazungumzo haya na kukaa pamoja, kama hili lilivyokuwa ni thabiti kwa maelezo ya Qur’an tukufu.

Ishara Ya Sita

Ama matokeo ya kuwapenda mitume na mawalii wema kulingana na Qur’an tukufu iliyobainisha, ni kuvuna uombezi wa hao manabii wema na mawalii wema katika ulimwengu wa barzakh, na katika mkusanyiko mkubwa, ukiacha kutafuta kumiminiwa –kwa mapenzi hayo– katika mimiminiko ya makamo yao ya juu, na ngazi zao zilizonyanyuka zinazolingana nao. Naam, hakika hadithi tukufu inaeleza kuwa “Mtu ni pamoja na yule ampendaye”.

Al-Bukhary, Al-Adab 96. Muslim, Al-birr 165.

Kwa hiyo mwanaadamu anaweza kuinuka kwenda makamo ya juu na yaliyonyanyuka zaidi, kwa vile alivyofuma na sahiba yake katika mafungamano ya mapenzi na kwa kunasibiana naye na kumfuata.

Ishara Ya Saba

Hakika kupenda kwako vitu vizuri, na majira ya machipuo, yaani kuyatazama katika pembe ya kauli yako: “Uzuri uliyoje wa umbo lake!” na kuelekeza mapenzi yako nyuma ya kitu hicho kizuri katika uzuri wa matendo na mpangilio wake, na nyuma ya matendo hayo yaliyoratibika katika uzuri wa madhihirisho ya majina mazuri, na nyuma ya majina hayo mazuri katika madhihirisho ya sifa tukufu.

Na kam hivi, hakika matokeo ya mapenzi haya ya halali ni kushuhudia uzuri mkuu kuliko uzuri huo ambao umeshuhudia katika vilivyotengenezwa kwa maelfu na maelfu ya mara. Yaani kushuhudia madhihirisho ya majina mazuri na uzuri wa sifa tukufu kwa namna inayoendana na pepo na maisha ya kudumu milele, hata akasema Imamu Al-rabbani Al-sirhandi (r.a): “Hakika mazuri ya peponi ni mifano ya majina mazuri” Basi zingatia!.

Ishara Ya Nane

Ama kuipenda kwako dunia mapenzi ya halali, yaani kuipenda kwako pamoja na kuzingatia na kutafakari katika sura zake mbili nzuri ambazo ni shamba la akhera, na kioo cha madhihirisho ya majina mazuri ya Allah (s.w), hakika matokeo yake ya kiakhera ni kuwa utapewa pepo inayotosha dunia yote, lakini haiondoki kama hiyo dunia bali ni yenye kudumu milele daima. Na itadhihirishwa kwako katika vioo vya pepo hiyo, madhihirisho ya majina mazuri kwa mng’aro mkubwa mno wa memetuko lake na utukufu wake, ambazo umeona baadhi ya vivuli vyake dhaifu duniani. Kisha kuipenda dunia katika sura yake kuwa ni shamba la akhera, yaani kuzingatia kuwa dunia ni bustani ndogo sana ya kuotesha mbegu ili ifanye mashuke akhera na izae matunda huko, hakika matokeo yake ni matunda ya pepo pana inayotosha dunia yote, hufunuka humo milango yote ya fahamu na hisia za kibinaadamu anazobeba mwanaadamu duniani kama vijimbegu vidogo, kufunuka kitimilifu na ukuaji kamili na vijimbegu vya maandalizi ya kimaumbile kufanya mashuke ndani yake vikibeba aina zote za ladha na makamilifu, matokeo haya ni yenye kuthibiti kwa muktadha wa rehema ya Allah iliyoenea na hekima yake isiyo na ukomo, na matokeo hayo ni yenye kuthibiti kwa kauli ya hadithi

Al-Bukhary, bad’u al-khalq 8. Muslim, al-Iman 312.

tukufu na ishara za Qur’an tukufu.

Na kwa kuwa kuipenda kwako dunia sio kwa sura ile mbaya ambayo ndio kichwa cha kila kosa, bali ni mapenzi yenye kuelekea katika sura zake mbili, yaani katika majina mazuri na akhera, na umekwishafunga kwa ajili ya mawili hayo mafungamano ya mapenzi pamoja nayo na ukaimarisha sura hizo mbili kwa nia ya ibada, hata kana kwamba umetekeleza ibada kwa dunia yako yote. Basi hapana budi kwamba thawabu ipatikanayo kutokana na kupenda huku itakuwa thawabu kunjufu mno kuliko dunia yote. Na hili ndilo hukumio la rehema ya kiungu na hekima yake.

Kisha kwa kuwa mapenzi hayo yamepatikana kwa kuipenda akhera na kuwa kwake ni shamba lake, na kwa kumpenda Allah (s.w), na kuwa kwake kioo cha kudhihirisha majina yake mazuri, hapana shaka kwamba hukabiliwa na kipendwa chenye upana zaidi kuliko dunia nacho sio kingine isipokuwa ni pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi.

Swali:

Nini faida ya pepo pana sawa na upana wa dunia?

Jibu:

Ingekuwa yawezekana ukatembea kwa kasi ya kufikiria katika pande zote za dunia, na ukazuru nyota karibu zote zilizomo mbinguni, ungesema wakati huo: Hakika ulimwengu wote ni wangu. Uwepo wa malaika, watu wengine na wanyama pamoja nawe hausongamani na hukumu yako hii wala haukanushi katika ulimwengu huu mpana.

Na vilevile unaweza kusema: Hakika pepo hiyo ni yangu hata ingekuwa imejaa waendao humo. Na tumebainisha katika risala ya (Pepo) -nayo ni (Neno la ishirini na nane)- maana ya hadithi iliyopatikana kuwa watapewa baadhi ya watu wa peponi pepo upana wake ni miaka mia tano,

Al-Baghawy, sharhu al-sunan 15/232. Al-Suyuuti, Al-fathu al-kabir 1/62.

na vile vile tumebainisha katika raisala ya (Ikhlasi).

Ishara Ya Tisa

Hakika matokeo ya kumuamini Allah (s.w) na kumpenda (s.w) ni kuona uzuri mtakatifu na ukamilifu mtakatifu wa dhati tukufu (s.w), kama ilivyothibiti kwa hadithi sahihi

Kutoka kwa Abu Hurayra r.a kwamba watu walisema: “Ewe mjumbe wa Allah je, tutamuona mola wetu mlezi siku ya kiama? Akasema mjumbe wa Allah (s.a.w): “Je, mnadhuriwa katika kuona mwezi usiku wa badri? Wakasema : “Hapana ewe mjumbe wa Allah s.w Akasema: “Je mnadhuriwa katika jua lisilokuwa nyuma yake mawingu?” Wakasema: hapana. Akasema: “Basi hakika nyinyi, mtamuona kama hivyo” na hadithi kwa urefu wake ameipokea Bukhari, al-mawaakiit 16, 26.

na Qur’an tukufu. Kuona huku ambako saa moja yake ni sawa na miaka elfu elfu ya neema za peponi, neema hiyo ambayo saa yake moja inavuka miaka elfu elfu ya maisha mazuri ya dunia,

Imepatikana katika hadithi tukufu:  “…Amesema: Basi atafunua Allah (s.w) pazia na atawadhihirikia na kuwafunika kwa nuru yake, lau asinge wahukumia wasiungue wangeungua kutokana na nuru yake aliyowafunika. Akasema: Kisha wataambiwa: Rejeeni majumbani kwenu. Amesema: Watarejea majumbani kwao wakiwa wamefichikana kwa wake zao na wao wamefichikana kwa waume zao kutokana na nuru yake (s.w) iliyowafunika, wanapokuwa kwenye nyumba zao hurejeshwa nuru na kujizuia mpaka warejee katika sura zao walizokuwa nazo. Amesema: wake zao watawaambia: Hakika mmetoka kwetu katika sura na mmerejea katika sura nyingine? Akasema: hapo basi watasema: Hivyo ni kwa sababu Allah (s.w) ametudhihirikia tukatazama kwake ambacho kimetuficha kwenu. Ameipokea Al-Bazzar, Al-Targhib Wa Al-Tarhiib cha Al-hafidh Al-Mundhir 4/556.

kama ilivyothibiti mbele ya watu wa elimu na kufunuliwa kwa kuafikiana.

Na tunaweza kupima kiasi cha shauku na kutamani yanayo kuwamo kwenye maumbile ya mwanaadamu ili kuona uzuri huo mtakatifu na ukamilifu mtakasifu, na kiasi cha yaliyoma katika raghba kali na matamanio makali na kuvutiwa kuviona kwa mfano ufuatao:

Kila mtu anahisi ndani mwake uhitaji mkubwa wa kumuona sayyidina Suleiman (a.s) ambaye amepewa ukamilifu, na anahisi vilevile shauku kubwa katika kumuona sayyidina Yusuf (a.s) ambaye amepewa nusu ya uzuri. Basi ni kiasi gani cha shauku na uhitaji kwa mwanaadamu ili kuona uzuri mtakatifu na ukamilifu uliotakasika na kasoro zote, ambao katika madhihirisho ya uzuri huo na ukamilifu ni pepo ya kudumu kwa mazuri yake yote na neema na makamilifu yake yote ambayo yanavuka kwa kiasi kisicho na mpaka cha mara mazuri yote ya dunia na makamilifu yake.

اَللَّهمَّ ارزُقنَا حُبَّك وَحُبَّ مَا يُقَرِّبُنَا إِلَيْكَ وَالإِسْتِقَامَة كَمَا أَمَرْتَ وَفِي الآخِرَةِ رَحْمَتِك وَرُؤْيَتِك

سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَناَ إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ العَلِيْمُ الحَكِيْمُ

اللَّهُم ّصَلّ وَسَلِّم عَلَي مَن أَرْسَلتَه رَحْمَةً للعَالَمِينَ وَعَلَي آلِه وَصَحْبِه أَجْمَعِين. آمِين

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.