USO WA NDANI WA ULIMWENGU

Tumaini la Nane

Kutoka katika Ujumbe kwa Wazee

Katika wakati ambapo mvi, alama ya uzee, zilipoanza kujitokeza katika nywele zangu, msukosuko wa Vita vya Kwanza vya Dunia uliyozidisha usingizi wa ujana, mageuzi ya kukamatwa kwangu kama mfungwa wa kivita, nafasi ya umashuhuri mkubwa na heshima kunijia katika kurejea kwangu Istanbul na kufanyiwa vyema na kuzingatiwa zaidi ya ninavyostahili kutoka kwa kila mmoja, kutoka kwa Khalifa, hata, sheikhul-Islam, na kamanda mkuu wa jeshi mpaka wanafunzi wa elimu ya dini,  kulevya kwa ujana, na hali ya kiakili iliyosababishwa na nafasi yangu ilifanya usingizi wa ujana uzidi sana kiasi kwamba niliona dunia kama ya kudumu na mimi mwenyewe kuwa katika hali nzuri sana isiyokwisha iliyogandamana nayo.          

Kisha, siku moja katika Ramadhan, nilikwenda katika Msikiti wa Bayazid kusikiliza wasomaji Qur’an. Kwa kupitia ndimi za wasomaji hao Qur’an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza ilikuwa ikitangaza kwa anuani yake tukufu kabisa ya mbinguni aya isemayo:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ Qur’an, 3:185

ambayo inatoa habari kuhusu mauti ya mwanaadamu na viumbe wote wenye roho. Iliingia sikioni mwangu, ikapenya mpaka ndani kabisa ya moyo wangu na kukaa humo; ilivunja usingizi ule uliojikita na kutokujali kule. Nikatoka msikitini. Kwa sababu ya mzubao wa usingizi ambao kwa muda mrefu ulikaa kichwani kwangu, kwa siku nyingi tufani sasa lilikuwa likifanya ghadhabu ndani mwake, na mwenyewe niliona kama ngalawa yenye kutoa moshi na dira yenye kuzunguka. Kila nilipoziangalia nywele zangu kwenye kioo, mvi ziliniambia: “Tuzingatie!” na kwa hivyo hali ikawa dhahiri kwa maonyo ya mvi zangu.          

Nikaangalia na kuona kuwa ujana wangu uliyoniteka sana kwa starehe zake ambazo nilizitumainia sana zikiniaga, na kuwa maisha ya kidunia niliyoyapenda sana na niliyojihusisha nayo sana yalikuwa yakianza kuzimika, na kuwa dunia niliyoungana nayo sana na kuipenda ilikuwa ikiniambia: “Safari njema”, na ilikuwa ikinionya kuwa nitatoka katika nyumba hii ya wageni. Yenyewe, pia, ilikuwa ikisema “Kwaheri”, na ilikuwa ikijiandaa kuondoka. Kutokana na ishara za aya ya Qur’an ya Ufafanuzi wa Kimiujiza,

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ

maana ifuatayo ilikuwa ikijikunjua moyoni mwangu: mbari ya kibinaadamu ni kiumbe hai; itakufa ili ifufuliwe. Na tufe la dunia ni kiumbe hai; pia itakufa ili iwe na umbo la milele. Na dunia, pia, ni kiumbe hai; itakufa ili iwe na umbo la Akhera.

Hivyo, nikiwa katika hali hii, niliitafakari hali yangu. Niliona kuwa ujana, ambao ni chanzo cha furaha, ulikuwa ukiondoka, na uzee, ambao ni chanzo cha huzuni, ulikuwa unakuja, kwamba uhai, uliokuwa uking’aa sana, ulikuwa unaanza kuondoka, ilhali kifo, ambacho kinatisha na giza dhahiri kilikuwa kikijitayarisha kuwasili, na kuwa dunia inayopendwa, iliyodhaniwa kuwa ya kudumu na ya kupendwa na wasio na mazingatio, ilikuwa ikiharakishia katika kifo chake.

Ili nijidanganye na kutumbukiza kichwa changu tena katika kutokujali nilitafakari furaha za msimamo wa kijamii niliofurahia katika Istanbul, uliyokuwa wa juu zaidi kuliko nilivyostahiki, lakini hakukuwa na faida yoyote katika hilo. Fikra, mtizamo, na faraja ingeweza tu kuja mpaka katika mlango wa kaburi; hapo ingezimika. Na kwa kuwa niliiona kama unafiki wa kutaabisha, taabu baridi, na fadhaa ya muda mfupi chini ya stara ya pambo la utukufu na umashuhuri, ambao ni kusudio la kufikirika la wenye kuabudu umashuhuri, nilifahamu kuwa mambo haya yaliyonihadaa tangu wakati huo yasingeweza kunifariji, hakukuwa na nuru yoyote katika hayo.          

Nikaanza tena kuwasikiliza wasomaji katika Msikiti wa Bayazid ili nisikie mafunzo ya mbinguni ya Qur’an, na kupata uamsho zaidi. Basi kutokana na maelekezo hayo adhimu nilisikia habari njema kwa kudura tukufu za namna yake,

 وَبَشِّرِ الَّذِين آمَنُواْ Qur’an, 2:25, n.k.

Kwa mng’ao wa Qur’an, nilitafuta faraja, matumaini, na nuru, si nje yake, lakini ndani ya nukta nilizotishika, kuhuzunika na kukata tamaa. Shukurani nyingi sana ni kwa Allah (s.w), nikapata tiba ndani ya maradhi yenyewe. Nikapata nuru katika giza lenyewe. Nikapata faraja katika kitisho chenyewe.

Mosi, niliangalia katika mkabala wa kifo, ambacho nilidhani ndiyo jambo la kutisha zaidi, na kinamtisha kila mmoja. Kwa nuru ya Qur’an Niliona kuwa ingawa stara ya kifo ni nyeusi, yenye kiza na mbaya, kwa waumini sura yake halisi, ni mwanga na nzuri. Na tumethibitisha ukweli huu kimkataa katika sehemu nyingi za Risale-i Nur. Mathalani, kama tulivyoeleza katika Neno la Nane na Barua ya Ishirini kifo si maangamizi, si utengano, badala yake ni mwanzo wa uzima wa milele. Ni mwanzo wake. Ni pumziko kutokana na taabu za majukumu ya maisha, ni ruhusa ya kwenda nyumbani. Ni kubadilisha makazi. Ni kukutana na msafara wa rafiki mmojawapo ambao tayari wamehamia kwenye Dunia ya Kati na Kati; na kuendelea. Niliona ukweli wa kifo, na uso wake mzuri kwa ukweli kama huu. Niliuangalia uso wa kifo si kwa hofu bali kwa shauku. Nilifahamu maana moja ya Kisufi ya ‘tafakuri ya mauti’.

Halafu nikauangalia ujana – ujana unaoondoka, unaomliza kila mmoja kwa kuondoka kwake, unaowapumbaza na kuwajaza hamu, na kuwasababishia kuutumia katika dhambi na kutokujali. Niliona kuwa pamoja na vazi lake zuri lililotariziwa ulikuwa una sura mbaya, uliyolewa na uso uliopigwa bumbuwazi. Kama sikujua hali yake halisi, basi ungenifanya nilie kwa miaka mia moja kama ningebakia duniani muda huo, baada ya kunilewesha na kunikejeli kwa miaka kadhaa.  Kama mtu mmoja alivyolalamika:

“Laiti siku moja tu, ujana wangu ungerejea, nikaueleza majonzi niliyoletewa na uzee.”

Ni sehemu ya shairi la Abulataahiya.

Kwa hakika, wazee kama huyo hapo juu wasiojua hali halisi ya ujana, hufikiria ujana wao wenyewe, na kulia kwa majuto na shauku. Lakini ujana unapokuwa kwa waumini wenye akili nzuri na nyoyo, ni njia ya nguvu zaidi, yenye kukubalika na nzuri ya kufanya kazi njema, na biashara kwa ajili ya Akhera, maadamu wanautumia katika ibada, biashara hiyo na kazi hizo njema. Na kwa wenye kujua majukumu yao ya kidini, na hawautumii vibaya ujana wao, ni neema yenye thamani kubwa sana ya kiungu na ya furaha. Usipotumika katika ustawi, unyoofu, na kumcha Allah, una hatari nyingi, unaharibu furaha ya milele na maisha ya hapa duniani. Kwa hakika, badala ya furaha ya ujana wa mwaka mmoja au miwili, husababisha miaka mingi ya masikitiko na huzuni uzeeni.

Kwa kuwa kwa watu wengi, ujana una madhara, sisi wazee tunapaswa kumshukuru Allah kuwa tumenusuriwa dhidi ya hatari na madhara yake. Kama kila kitu kingine, furaha za ujana huondoka. Kama umetumika katika ibada na kazi njema, matunda ya ujana wa aina hiyo huendelea kubakia katika mahali pao na ni njia za kupata ujana katika maisha ya milele.

Baada ya hapo, niliitafakari dunia, ambayo watu wengi wamepumbazika nayo na wameshikamana nayo. Kwa nuru ya Qur’an, niliona kuwa dunia ina nyuso tatu, moja ndani ya mwingine:

Kwanza:

Hii inaangalia Majina ya Kiungu; ni kioo cha majina hayo.

Uso wake wa pili:

Hii inaangalia Akhera, na ni shamba lake.

Uso wake wa tatu:

Hii inaangalia watu wa kidunia; ni uwanja wa michezo wa wasiozingatia.

Kwa kuongezea, kila mmoja ana dunia yake pana humu duniani. Kwa wepesi, zipo dunia nyingi mojawapo ndani ya nyingine kwa idadi ya wanaadamu. Nguzo ya dunia binafsi ya kila mmoja ni maisha yake mwenyewe. Wakati wowote mwili wake unapoondoka, dunia yake inaangamia kichwani mwake, huwa ni kiama chake. Kwa kuwa wasiozingatia na wenye kupuuzia hawatambui kuwa dunia yao itaangamia kwa haraka, wanaidhania kuwa ya milele kama dunia ya jumla na wanaiabudu. Nilijifikiria mwenyewe: “Mimi, pia, nina dunia yangu itakayoangamia taratibu na kuvunjika kama dunia za watu wengine. Kuna thamani gani katika dunia hii binafsi, maisha yangu haya mafupi?”

Halafu, kwa nuru ya Qur’an niliona kuwa kwa ajili yangu na kila mwingine, dunia ni sehemu ya biashara ya muda mfupi, nyumba ya wageni ambayo kila siku hujaa na kubakia tupu, soko lililo njiani kwa ajili ya wapita njia kuja kununua, daftari lenye kufanywa upya la Mwandishi wa Tangu linaloendelea kuandikwa na kufutwa, na kila majira ya kuchipua huandikwa herufi za dhahabu, na kila kiangazi kimesheheni vyema, chenye namna ya vioo vyenye kuakisi na kuhuisha udhihirisho wa Majina ya Muumbaji (s.w), ni kitalu cha Akhera, kitalu cha maua ya Rehema ya Kiungu, na karakana maalumu ya muda mfupi ya kutengeneza mabango yatakayooneshwa katika dunia ya Umilele.

Nilimshukuru sana Muumbaji (s.w) aliyeiumba dunia kwa namna hii. Na ninafahamu kuwa ilhali kupenda sura nzuri za ndani za dunia zinazoangalia Akhera na Majina ya Kiungu kapewa mwanaadamu, kwa kuwa wanaitumia katika uso wake wa mpito, mbaya, wa dhambi na usiozingatia, wanadhihirisha maana ya Hadithi: (Kuipenda dunia ni chanzo cha uchupaji mipaka wote).

Sahihul-Bukhari.

Na kwa hivyo, enyi wazee! Ninautambua ukweli huu kwa nuru ya Qur’an yenye hekima na maonyo ya uzee na imani kufumbua macho yangu. Na nimeionesha kwa shuhuda mkataa katika sehemu nyingi ndani ya Risale-i Nur. Nikapata faraja ya kweli, matumaini yenye nguvu, na nuru yenye kung’aa. Niliushukuru uzee wangu, na niliufurahi kuwa ujana wangu umeondoka. Nyinyi, pia, msilie, bali mtoe shukurani. Kwa kuwa kuna imani na huo ndiyo ukweli, waache wasiozingatia walie, waache wapotevu walalamike.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.