Barua ya Kumi na Saba Barua ya Rambirambi kwa Kifo cha Mtoto

بِاسْمِهِ وَاِنْ مِنْ شَيْءٍ اِلاَّ يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ

Ndugu yangu wa akhera, Hafiz Halid Efendi!

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ اِذَا اَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّا اِلَيْهِ رَاجِعُونَ {Qur’an 2: 155-156)

Ndugu Yangu! Kifo cha mwanao kimenihuzunisha, lakini,

اَلْحُكْمُ لِلّٰه{Qur’an 40:12}

Hivyo, kuridhia uamuzi Wake na kusalimu amri mbele ya qadari Yake, ni alama miongoni mwa alama za Uislamu. Ninamuomba Mwenyezi Mungu awape subira njema, na amfanye marehemu kuwa msaada na muombezi wenu siku ya Qiyama.

Nitakubainisha nukta tano ambazo ni bishara njema na faraja ya kweli kwako na kwa waumini kama wewe wenye kumcha Mwenyezi Mungu:

Nukta ya Kwanza: 

Hakika siri na maana yakauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo vildenun muhalledun…

{ Qur’an, 56:17 ; Qur’an, 76:19}

ndani ya Qur’an Tukufu ni hii: Watoto wa waumini wanaokufa kabla ya umri wa baleghe wataendelea kuwa watoto wasiopevuka, wenye ujana wa milele, wenye kupendwa kwa namna inayoendana na Pepo; kwamba wataendelea kuwa chanzo cha milele cha furaha ya wazazi wao watakaoingia Peponi; na watahakikisha kuwa wazazi wao wanapata furaha maridhawa kabisa, upendo na papaso la watoto; na kwamba kila kitu chenye kuburudisha kitapatikana Peponi; kwamba wale wanaosema kwamba kwa kuwa Pepo sio mahala pa kuzaliana hapatakuwa na upendo na papaso la watoto, kauli yao sio sahihi; na kwamba kupata mamilioni ya miaka ya upendo safi, usiokuwa na maumivu na papaso la watoto watakaodumu milele badala ya miaka kumi au mfano wake ya upendo wao uliochanganyika na huzuni za dunia hii, ni chanzo cha furaha kuu kwa waumini.

Nukta ya Pili:

Wakati fulani alikuwepo mtummoja aliyekuwa gerezani akaletewa mmoja wa wanaye aliyekuwa akimpenda sana. Mfungwa huyo aliyekosa furaha aliumizwa na hali yake mwenyewe na kushindwa kwake kumpa furaha mwanaye. Mtawala aliyekuwa na huruma akamtumia ujumbe kupitia kwa mtu aliyesema: “Hakika mtoto huyu ni wako, lakini ni raia wangu na ni mmoja wa wananchi wangu. Nitamchukua kumpeleka kwenye kasri zuri na kumpa matunzo mazuri huko.” Bwana yule alilia sana kwa uchungu. Akasema: “Sitakupatia mwanangu, yeye ndiye faraja yangu!” Wenzake wakamwambia: “Huzuni zako hazina maana. Iwapo wamhurumia mwanao, atakwenda kwenye kasri zuri na lililojaa furaha badala ya gereza hili chafu na lililojaa dhiki. Iwapo waionea uchungu nafsi yako na kutaka manufaa yako binafsi, akibaki hapa atapata mashaka, dhiki na maumivu makubwa kwa manufaa yako ya muda! Lakini akienda huko atakuwa chanzo cha manufaa na faida nyingi kwako, kwa sababu atakuwa sababu ya mtawala kukuonea huruma, na hivyo atakuwa kama muombezi kwako. Bila shaka siku moja hakimu atataka kukutana nawe, utatolewa gerezani na kupata bahati ya kwenda kwenye kasri hilo kukutana na mwanao. Lakini kwa sharti umuamini na kumtii mfalme.”

Ndugu yangu mpendwa! Waumini kama wewe wanapaswa kuutafakari mfano huu kwa namna hii pindi watoto wao wanapofariki dunia na kusema: Mtoto huyu hana hatia na Muumba wake ni Mwenye kurehemu, Mwenye ukarimu. Amemchukua kumpeleka kwenye uangalizi na rehma Yake kamili badala ya malezi na huruma yangu yenye upungufu. Amemtoa katika jela ya dunia hii yenye maumivu na masaibu na kumpeleka kwenye mabustani ya Pepo Yake. Furaha iliyoje kwa mtoto huyo! Nani ajuaye angekuwa nani na angefanya nini kama angebaki katika dunia hii? Hivyo, siumii, na ninajua kuwa amekuwa mwenye bahati. Ama hakika maumivu yangu ni kwa ajili ya nafsi yangu, hivyo siumii sana kwamba nimeikosa furaha yangu binafsi. Kwa maana, kama angebaki duniani, angekuwa na miaka kumi ya upendo wa mpito uliochanganyika na maumivu. Kisha kama angekuwa mwema na kama angekuwa na uwezo katika masuala ya kidunia, yumkini angenisaidia. Lakini kwa kifo chake, amekuwa aina ya muombezi ambaye atanipatia mamilioni ya miaka ya upendo katika Pepo ya milele na furaha ya kudumu.

Hakika, mtu anayepoteza faida moja yenye shaka, ya muda huo na kupata faida elfu za uhakika zilizocheleweshwa halii na kulalama, wala halii kwa kukata tamaa.

Nukta ya Tatu:

Mtoto aliyefariki dunia, yeye navipawa vyake vyote, alikuwa kiumbe, milki na mja wa Muumba Mwenye kurehemu; alikuwa milki Yake na alikuwa rafiki yake, aliyewekwa chini ya usimamizi wao wa muda. Muumba aliwafanya wazazi kuwa wahudumu wa mtoto huyo. Aliwapa huruma maridhawa kama malipo ya huduma wanayoifanya.

Na sasa, Muumba huyo Mwenye kurehemu ambaye ndiye Mmiliki halisi wa mtoto huyo na ambaye ana hisa tisini na tisa huku wazazi wakiwa na hisa moja tu kwa mtoto huyo akimchukua mtoto huyo, kutokana na hekma na rehma Zake, akakatisha huduma yenu kwake, haitawafaa waumini kuhuzunika kwa kukata tamaa na kulia kwa sauti kuonesha kuwa wanamlalamikia Mmiliki wa haki mwenye hisa elfu, kwa hisa yao moja. Hakika hilo hufanywa na watu walioghafilika na kupotea.

Nukta ya Nne:

Lau kama dunia ingekuwa yenyekubaki milele, mwanadamu angekuwa mwenye kubaki humo milele, na kama utengano usingekuwa na mwisho; huzuni, maumivu na masikitiko vingekuwa na maana. Lakini hii dunia ni makazi ya wageni, mahali ambapo mtoto huyo amekwenda, wewe na sisi pia tutakwenda huko. Aidha, yeye siye pekee aliyekufa, bali ni njia ya kila mtu. Na kwa kuwa utengano huu sio wa milele, utakutana naye mbeleni, katika ulimwengu wa kaburini na Peponi.

Hivyo tunapaswa kusema: “Hukmu ni ya Mwenyezi Mungu. Ni vyake anavyovitoa na kuvichukua”; na “Himidi ni za Mwenyezi Mungu kwa kila hali”, na kushukuru kwa kufanya subira.

Nukta ya Tano:

Huruma, ambayo ni kielelezomaridhawa, kizuri na kitamu cha ishara za rehma ya Mwenyezi Mungu, ni kioevu chenye nuru. Ni wenye uwezo wa kupenya zaidi ya shauku ya upendo, na nyenzo yenye kasi zaidi katika kumtafuta Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Upendo wa kufikirika wa kidunia hubadilika kuwa upendo wa kweli ambapo mwenye nao humpata Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa tabu kubwa, lakini huruma huunganisha moyo na Mwenyezi Mungu kwa namna safi na ya moja kwa moja na bila tabu.

Baba na mama humpenda mtoto wao kuliko chochote duniani. Iwapo watakuwa ni waumini wa kweli, wanaponyang’anywa mtoto huyo huzigeuza nyuso zao kutoka kwenye dunia hii na kumuelekea Mneemeshaji wa Kweli. Husema: “Dunia ni yenye kupita na hivyo haifai kwa moyo kushikamana nayo.” Hushikamana na kule alikokwenda mtoto wao, na hili huwapatia daraja kubwa ya kimaanawi.

Watu wa mghafala na upotofu ni wenye kunyima furaha na bishara njema za nukta hizi tano.

Unaweza kuona kutokana na yafuatayo namna hali yao inavyosikitisha na kuumiza: wanapomuona mtoto wao wa pekee akikaribia kukata roho, na kwa sababu wanadhani kuwa dunia ni kitu cha milele kutokana na mghafala na upotofu wao, hudhani kuwa kifo ni kitu kisichokuwepo na ni utengano wa milele. Wanafikiria anavyoliacha godoro lake laini na kulala katika udongo wa kaburi lake, na kutokana na mghafala au upotofu wao, wanasahau kabisa Pepo yenye baraka na neema za Muumba Mwenye kurehemu. Unaweza kuona kwa kulinganisha huzuni na maumivu wanayoyapata. Ama imani na Uislamu humwambia muumini: Muumba Mwenye kurehemu atamchukua mwanao huyu anayekaribia kukata roho kutoka katika dunia hii dhalili na kumpeleka Peponi. Atamfanya kuwa muombezi wako na mtoto atakayedumu milele. Usiwe na wasiwasi, utengano ni wa muda! Sema:

اَلْحُكْمُ لِلّٰهِ ٭ اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّا اِلَيْهِ رَاجِعُونَ{Qur’an 2:152, Qur’an 40:12}

kisha vumilia kwa subira.

Mwenye kubaki, Ndiye Mwenye kubaki! Said Nursi

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.