MWALE WA ISHIRINI NA TANO

[Tasnifu hii imebeba tiba ishirini na tano. Iliandikwa kama kitulizo, faraja na ponyo kwa wagonjwa, na ili kuwatembelea na kuwatakia ponyo la haraka.]

Tanbihi na Kuomba Radhi

Maelekezo haya ya kitiba ya kimaanawi yaliandikwa kwa haraka kubwa kuliko maandiko yangu mengine,

{Waraka huu uliandikwa ndani ya saa nne na nusu. Imesainiwa, Rüştü, Re’fet, Hüsrev, Said} 

na kwa kuwa sikupata muda wa kutosha kufanya masahihisho na kuudurusu, niliusoma mara moja tu tofauti na maandiko yangu mengine. Hii ina maana kwamba, waraka huu umebaki katika hali ya muswada bila kupangiliwa. Sikuona haja ya kuudurusu upya, kwa sababu mawazo yanayokuja moyoni moja kwa moja kwa silika ya kimaumbile hayatakiwi kuharibiwa kwa kuyapamba sana kwa maneno na ufundi uliokithiri. Hivyo, ninawaomba wasomaji, hasa wagonjwa, wasihisi huzuni au kuumizwa na maneno yasiyoliwaza na sentensi ngumu; na wasinisahau katika dua zao.

بِسْمِ اللّٰهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ

اَلَّذِينَ اِذَا اَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّا اِلَيْهِ رَاجِعُونَ ٭ {Qur’an, 2:156}

وَالَّذِى هُوَ يُطْعِمُنِى وَيَسْقِينِ وَاِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ{Qur’an 26: 79-80}

Katika Mwanga huu wa Nuru, tumeelezea kwa ufupi dawa na tiba ishirini na tano ambazo zinaweza kuwa kitulizo na tiba yenye manufaa kwa wagonjwa na wale waliokwama katika masaibu, ambao wanaunda moja ya kumi ya wanadamu.

DAWA YA KWANZA

Ewe mgonjwa uliyenyongeka! Usiwe na wasiwasi, ishikilie subira! Kwa sababu maradhi yako sio kilema kwako; bali ni aina ya ponyo. Kwa maana umri ni rasilimali inayopita; isipozaa matunda inakuwa imepotea bure; na ikitumika kwa mghafala hupotea haraka. Maradhi huifanya rasilimali yako hiyo kuzalisha faida kubwa. Aidha, inafanya umri wako usiondoke kwa haraka, huuzuia na kuuongeza, ili upate kuondoka baada ya kuzalisha matunda. Ishara kwamba umri wako unarefushwa kupitia maradhi ni methali ifuatayo ambayo husemwa mara nyingi: “Muda wa janga ni mrefu, muda wa furaha na raha ni mfupi.”

DAWA YA PILI

Ewe mgonjwa uliyekosa subira! Shikamana na subira, na ushukuru! Maradhi yako yanaweza kuigeuza kila dakika ya umri wako kuwa sawa na saa moja ya ibada. Kwa maana kuna aina mbili za ibada. Ya kwanza ni chanya kama ibada maarufu ya dua na sala. Ya pili ni hasi kama vile maradhi na majanga. Kupitia aina hii ya pili, wale waliopatwa na maswaibu hutambua udhaifu na unyonge wao; hujinyenyekeza kwa Muumba wao Mwenye kurehemu na kukimbilia Kwake; hudhihirisha ibada ya kweli na isiyokuwa na unafiki. Naam, kuna riwaya ya Hadith sahihi inayoeleza kuwa muumini anapokuwa katika maradhi huhesabika kuwa yuko katika ibada kwa sharti kuwa asilalamike kuhusu Mwenyezi Mungu.

{Al-Albani, Sahih Jami’ al-Saghir, 256.}

Imethibiti pia katika riwaya mbalimbali na kutoka kwa watambuzi kuwa dakika moja ya maradhi ya baadhi ya watu wenye kusubiri na kushukuru kikamilifu huwa sawa na saa moja ya ibada na dakika moja ya maradhi ya watambuzi ni sawa na ibada ya siku nzima. Hivyo, usilalame kuhusu maradhi ambayo huigeuza dakika moja ya umri wako kuwa dakika elfu moja na kuurefusha umri wako; yakupasa kushukuru.

 DAWA YA TATU

Ewe mgonjwa usiye na subira! Ukweli kwamba watu wanaokuja duniani huondoka, vijana kuzeeka, na mwanadamu kuzunguka katika hali ya kifo na utengano ni uthibitisho kwamba hakuja duniani kwa lengo la kustarehe na kupata raha.

Aidha, wakati mwanadamu ndiye kiumbe bora, aliyenyanyuliwa daraja ya juu kuliko viumbe hai vingine na aliyejaaliwa vipawa tofauti vingi, anaishi katikati ya furaha zenye kupita na mabalaa yajayo, na hivyo huumaliza umri wake akiwa ndani ya maisha yenye uchungu, tabu na kujishusha kwenye udhalili mbaya zaidi ya udhalili wa wanyama. Hii ina maana kwamba mwanadamu hakuja duniani kwa lengo la kuishi maisha ya raha na starehe. Bali, ana rasilimali kubwa, na amekuja hapa kufanya kazi na kuchuma kwa ajili ya maisha ya milele na yenye kudumu.

Rasilimali aliyopewa mwanadamu ni umri wake. Kama kusingekuwepo na maradhi, afya njema na ustawi vingemfanya aghafilike, kwa maana vinaonesha kwamba dunia ina raha na kuifanya akhera isahaulike. Vitu hivyo havitaki kuona kifo na kaburi; vinaifanya rasilimali ya umri kupotea bure. Maradhi yanapofungua macho ya mja, huuambia mwili: “Wewe si mwenye kudumu milele. Hujaachwa bure, una majukumu ya kutekeleza. Acha kiburi, mkumbuke aliyekuumba. Tambua kwamba utaingia kaburini, hivyo jiandae kwa ajili ya hilo!”

Kwa muktadha huu, maradhi ni mshauri na muongozaji mwaminifu asiyekuhadaa. Hivyo, sio kitu cha kulalamikiwa, bali ni kitu cha kushukuriwa. Na iwapo maradhi hayo ni makali sana, basi omba subira kwa Allah Mtukufu.

DAWA YA NNE

Ewe mgonjwa mwenye kulalamika! Huna haki ya kulalama; bali yakupasa kushukuru na kufanya subira. Kwa maana mwili, viungo na vipawa vyako sio mali yako. Hukuviumba wala hukuvinunua dukani. Hii ina maana kwamba ni milki ya mwingine, na mmiliki huyo ana haki ya kutumia mali yake apendavyo.

Kama ilivyosimuliwa katika tasnifu ya Neno la Ishirini na Sita, kwa mfano, iwapo fundistadi tajiri na mtaalamu sana akimuajiri mtu maskini kama muonesha mitindo kwa ajili ya kuonesha mavazi na mali yake; akamlipa ujira wa nusu saa atakayovaa mavazi ya thamani. Ili kuonesha ubora na wingi wa ustadi wake akawa anakata ile nguo, anaibadilisha, anairefusha na kuipunguza. Je, mwajiriwa huyo atakuwa na haki ya kumwabia tajiri yule: “Unanipa tabu, unanisababisha msongo kwa muundo wa nguo uliouandaa na kunifanya niiname na kusimama?” Je, ana haki ya kumwambia kuwa anamharibia muonekano wake mzuri kwa kurefusha na kupunguza nguo inayomfanya aonekane mzuri? Je, anaweza kumwambia kuwa si mtu mwema na mtenda haki?

Ewe mgonjwa! Kama ilivyo katika mfano huu, ili kuonesha vazi la mwili wake alilokuvika, akakupamba kwa viungo mbalimbali kama vile macho, masikio, akili na moyo, na nakshi za majina Yake mazuri, Muumba huyo Mtukufu hukufanya uzunguke katika hali mbalimbali na kukubadilisha katika mazingira mengi. Kama unavyolijua jina Lake la Mwenye kuruzuku wakati wa njaa, basi lijue pia jina Lake la Mponyaji wakati wa maradhi yako. Kwa kuwa masaibu huonesha kiwango cha ukuu wa baadhi ya majina Yake, kuna vielelezo vingi vya kheri ndani ya miali hiyo ya hekma na rehma. Iwapo pazia ya maradhi unayoyaogopa ikiondolewa, nyuma yake utakuta manufaa mengi mazuri na yaliyo maridhawa.

 DAWA YA TANO

Ewe uliyepatwa na maradhi! Kupitia uzoefu, nimebaini kuwa katika kipindi hiki maradhi ni neema na tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa baadhi ya watu. Ingawa sikubahatika kuipata neema hiyo, kwa kipindi cha miaka nane au tisa iliyopita vijana kadhaa wamekuwa wakinijia kuhusu maradhi yao na kunitaka niwaombee dua. Nimetambua kwamba wote wameanza kufikiria zaidi kuhusu akhera kuliko vijana wengine. Wameacha ulevi wa ujana, wakayakandamiza matamanio ya kihayawani na mghafala kwa kiasi kikubwa. Hivyo, nimekuwa nikiwakumbusha kwamba maradhi yao ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo wanaweza kuistahamili. Nilikuwa nikiwaambia: “Ndugu zangu! Mimi sipingani na maradhi yenu haya. Siwaonei huruma kwa sababu ya kiasi cha kuwaombea dua. Jaribuni kuwa na subira mpaka maradhi yenu yatakapowaamsha kikamilifu kutoka kwenye mghafala, na yakishatimiza wajibu wake, Allah Mwenye kurehemu atairejesha afya yenu, inshaAllah.”

Pia niliwaambia: “Kutokana na janga la afya njema, baadhi ya wenzenu wamekuwa wenye kughafilika, wanaacha swala tano, hawafikirii kuhusu kaburi, na wanamsahau Mwenyezi Mungu Mtukufu. Furaha ya juu juu ya umri mfupi wa duniani umewafanya watikisike na kuyaharibu maisha yao ya milele, na hata kuyaangamiza. Kwa sababu ya maradhi, mnaweza kuliona kaburi, ambalo mtaliingia siku yoyote, na baada ya hapo kwenda akhera, na mkishaona hivyo mnaishi katika njia sahihi. Hivyo kwenu nyinyi, maradhi ni afya, ilhali kwa wenzenu afya inawapa maradhi”.

DAWA YA SITA

Ewe mgonjwa unayelalama kwa masumbuko! Ninakwambia: fikiria kuhusu umri wako uliopita na ukumbuke kuhusu siku za furaha, raha na nyakati za tabu na shida, hakika utasema: “Oh!” au “Ah!” Yaani, moyo na ulimi wako vitasema: “Himidi na shukrani ziende kwa Mwenyezi Mungu”, au “hasara iliyoje na masikitiko yaliyoje!” Kumbuka, kinachokufanya useme “Himidi na shukrani ziende kwa Mwenyezi Mungu” ni pale unapofikiria maumivu na majanga yaliyokusibu; husababisha aina ya furaha kiasi kwamba moyo wako hutoa shukrani, kwa maana baada ya dhiki ni faraja. Maumivu na majanga yanapopita, huacha athari ya furaha ndani ya moyo wako, ambayo ikiamshwa kwa tafakuri, humwaga shukrani kutoka kinywani mwako.

Kinachokufanya useme “hasara iliyoje na masikitiko yaliyoje” ni pale unapokumbuka nyakati za raha na furaha ambazo uliwahi kukutana nazo, ambapo zinapopita huacha athari ya maumivu endelevu ndani ya moyo wako. Unapozikumbuka na kuzifikiria, maumivu huibuka tena, yakasababisha majuto na huzuni kumiminika.

Kwa kuwa raha ya haramu ya siku moja huweza kusababisha masumbuko ya mwaka mzima moyoni, na kwa kuwa maumivu ya maradhi ya siku moja yenye kupita husababisha furaha na jazaa ya siku nyingi pamoja raha ya faraja ya kuondokewa na masumbuko, fikiria kuhusu matokeo ya maradhi haya yaliyokusibu kwa muda mfupi, na ubora wake wa ndani. Sema: “Yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu! Hili pia litapita”, na shukuru badala ya kulalama.

DAWA YA SITA

{Mwanga huu ulinijia ghafla moyoni, na tiba mbili zimewekwa pamoja katika Dawa ya Sita. Tumeiacha kama ilivyo ili kutoharibu uasili wake; hakika, hatukuibadilisha kwa kufikiria kuwa inaweza ikawa imebeba siri ndani yake.}

za dunia na kupatwa na huzuni kwa sababu ya kuumwa! Kama dunia hii ingekuwa yenye kudumu, na kama tusingekuwa na siku ya kufa, na kama upepo wa mtengano na kifo usingevuma, na kama roho zisingekuwa na msimu wa baridi ndani ya mustakabali wenye majanga na kimbunga, ningekuonea huruma. Lakini kwa kuwa siku moja dunia itatufukuza na kutosikiliza vilio vyetu, tunapaswa kutoipenda sasa kupitia maonyo ya maradhi haya, kabla haijatufukuza. Hatuna budi kufanya juhudi za kuitelekeza kabla haijatutelekeza.

Naam, maradhi hutupatia onyo hili: “Mwili wako haukuundwa kwa mawe na chuma, bali umeundwa kwa maada mbalimbali ambazo lazima zitaondoka. Jivue kiburi chako, tambua udhaifu wako, mtambue Mmiliki wako, yajue majukumu yako, jua kwa nini ulikuja hapa duniani!” Huyatangaza haya kwa siri ndani ya sikio la moyo.

Aidha, kwa kuwa raha na furaha za dunia hii sio endelevu, na hususan kama ni za haramu zinapita zikiwa zimetuachia maumivu na dhambi, basi usilie kwa kisingizio cha maradhi kwa kuzipoteza raha hizo. Badala yake, fikiria kuhusu vipengele vya ibada na thawabu za akhera zinazopatikana ndani ya maradhi, na ujaribu kupokea furaha kutoka humo.

DAWA YA SABA

Ewe mgonjwa uliyekosa raha ya afya! Maradhi yako hayaziharibu raha za neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kinyume chake, huzifanya ziwepo na kuongezeka. Kwa maana, kama kitu fulani ni chenye kuendelea, hupoteza athari yake. Watu wa haki wamekubaliana katika msemo kuwa

اِنَّمَا اْلاَشْيَاءُ تُعْرَفُ بِاَضْدَادِهَا

“Kitu hujulikana kupitia kinyume chake.” Kwa mfano, kama kusingekuwepo na giza, nuru isingejulikana na kusingekuwa na furaha. Kusingekuwepo na baridi, joto lisingejulikana, lisingekubalika. Kusingekuwa na njaa, chakula kisingekuwa na thamani. Kusingekuwa na kiu, kusingekuwa na raha ya kunywa maji. Kusingekuwa na maradhi, afya njema isingekuwa na raha.

Muumba Mwenye hekma amemjaalia mwanadamu aina mbalimbali za viungo na vipawa ili aweze kuhisi na kuzitambua neema mbalimbali zilizopo ulimwenguni. Hii inaonesha kuwa anataka kumfanya atambue kila aina ya neema Zake zitakazomfanya aendelee kumshukuru. Kwa hali hiyo, atampa maradhi, magonjwa, na masaibu, kama ampavyo siha na afya njema.

Sasa ninakuuliza: Kama usingepatwa na maradhi haya kichwani, mkononi au tumboni mwako, ungetambuaje neema maridhawa ya afya njema ya kichwa, mkono, au tumbo lako na kumshukuru? Kwa hakika, usingelifikiria jambo hilo hata kidogo, achilia mbali kutoa shukrani! Ungeitumia afya yako hiyo katika mghafala na hata upotofu.

DAWA YA NANE

Ewe mgonjwa unayoifikiria akhera! Maradhi huondosha uchafu wa dhambi kama sabuni na kuusafisha. Imethibiti katika Hadith sahihi kuwa maradhi ni kafara ya dhambi. Hadith nyingine inasema: “Muumini anapopatwa na maradhi, Mwenyezi Mungu huyadondosha madhambi yake kama majani yanavyodondoka kutoka mtini.”

{ 6 Bukhari, Mardha 1, 2, 13, 16; Muslim, Birr 45; Darimi, Riqaq 57; Musnad i, 371, 441; ii, 303, 335; iii, 4, 18, 38, 48, 61, 81.}

Dhambi ni maradhi sugu ya maisha ya milele, na katika maisha haya ya kidunia husababisha maradhi ya moyo, nafsi na roho. Iwapo utafanya subira na kutolalama, ugonjwa wa muda mfupi utaweza kukuokoa dhidi ya magonjwa mbalimbali yenye usugu. Kama hufikirii dhambi zako, huijui akhera au humtambui Mwenyezi Mungu, basi unasumbuliwa na maradhi mabaya sana ambayo ni zaidi ya maradhi yako madogo ya sasa kwa mara milioni moja. Yakimbie na upige kelele, kwa sababu kila kitu duniani kina uhusiano na moyo, nafsi na roho yako. Uhusiano huu huendelea kukatwa na panga la utengano, na kufungua majeraha mbalimbali. Hasa kwa kuwa huijui akhera na kudhani kuwa kifo ni jambo lisilokuwepo, utakuwa umejeruhiwa na kuvilia vibaya sana.

Hivyo, jambo la kwanza unalopaswa kulifanya ni kutafuta tiba ya imani, ambayo ni tiba ya uhakika kwa maradhi mengi yanayowasibu majeruhi na wagonjwa; unapaswa kuhakikisha kuwa imani yako ni sahihi. Njia fupi kabisa ya kuipata tiba hiyo ni kuitambua nguvu na rehma ya Utukufu wa Mwenyezi Mungu Muweza kupitia dirisha la udhaifu na unyonge wako uliooneshwa nyuma ya pazia la mghafala, uliyopewa na maradhi yako ya kimwili.

Naam, yule asiyemtambua Mwenyezi Mungu abeba kichwani mwake mabalaa yaliyo na uzito kama dunia. Wakati ulimwengu wa yule anayemtambua umejaa nuru na furaha ya kimaanawi; huyaona hayo kulingana na uimara wa imani yake. Masumbuko yatokanayo na maradhi ya kimwili huondoshwa na furaha, tiba na raha ya kimaanawi inayotokana na imani; masumbuko hayo huyeyuka.

DAWA YA TISA

Ewe mgonjwa unayemtambua Muumba wako! Maradhi huibua maumivu, hofu, na wasiwasi kwa sababu wakati mwingine husababisha kifo. Kwa kuwa kifo cha juu juu na cha mghafala kinaogofya, maradhi yanayokisababisha huibua hofu na wasiwasi.

Hivyo, kwanza tambua na kuamini kwa dhati kuwa saa ya kufa imeshapangwa na haibadiliki. Wale wanaolia kwa uchungu pembezoni mwa mgonjwa na ambao ni wazima kiafya hufariki dunia, ilhali wagonjwa wenyewe wakipona na kuendelea kuishi.

Pili: Kifo si chenye kuogofya kama inavyoonekana kwa nje. Kupitia nuru ya Qur’an Tukufu, katika maeneo mbalimbali ya Risale-i Nur tumethibitisha kikamilifu na pasina shaka kwamba kwa waumini kifo ni kuwaondoshea mzigo wa majukumu ya maisha. Kwao, kifo ni mapumziko dhidi ya ibada, ambayo ni maelekezo na mafunzo katika medani ya mitihani ya dunia hii. Pia ni njia ya wao kuungana tena na marafiki na jamaa, ambao tisini na tisa kati ya mia wameshaondoka kuelekea akhera. Ni njia ya kuingia makazi na makao ya kweli yaliyojaa furaha ya milele na yenye kudumu. Pia ni mwaliko wa kutoka kwenye korokoro za dunia kwenda kwenye mabustani ya Pepo. Na ni fursa ya kupokea malipo kutoka kwa Muumba Mwenye kurehemu kwa kazi waliyoifanya. Kwa kuwa huu ndio uhalisia wa kifo, hakipaswi kuchukuliwa kuwa kitu cha kuogofya, bali kinyume chake, kinatakiwa kuchukuliwa kama utangulizi wa rehma na furaha.

Aidha, baadhi ya waja wa Mwenyezi Mungu huogopa kifo, sio kwa sababu kinaogofya bali kwa sababu walitarajia kupata fursa zaidi ya kuendelea kufanya mambo mema iwapo wangepewa fursa ya kuendelea kuishi.

Naam, kwa waumini, kifo ni mlango wa rehma, ilhali kwa wale waliopotea, ni shimo la giza la milele.

DAWA YA KUMI

Ewe mgonjwa mwenye wasiwasi wa bure! Unahofia ukali wa maradhi yako na wasiwasi unaotokana nayo. Ikiwa wataka ukali wa maradhi yako upungue, jaribu kutokuwa na hofu. Yaani, fikiria kuhusu faida za maradhi yako, manufaa yake, na kwamba yataondoka haraka; hiyo itakuondolea wasiwasi na kuling’oa shina la maradhi.

Kwa kweli wasiwasi huzidisha maradhi, kwa maana husababisha maradhi ya kimaanawi katika moyo ambao hufanya maradhi ya kimwili kuwa maradufu; maradhi ya kimwili huendelea kudumu kupitia hilo. Iwapo wasiwasi utakoma kwa kujisalimisha, na kutambua sababu ya maradhi, sehemu kubwa ya maradhi hayo huondoka; ukali wake hupungua na sehemu kubwa kutoweka. Wakati mwingine maradhi kidogo ya kimwili huongezeka maradufu kutokana na wasiwasi. Wasiwasi ukikoma, tisa ya kumi ya ugonjwa husika hutoweka.

Kama ambavyo wasiwasi huzidisha maradhi, vivyo hivyo humfanya mgonjwa kana kwamba anaituhumu hekma ya Mwenyezi Mungu, kuikosoa rehma yake na kumlaumu. Kwa sababu hiyo, mtu mwenye wasiwasi huadabishwa na maradhi yake kuongezeka kinyume na makusudio yake. Naam, shukrani huongeza neema, hivyo malalamiko huongeza maradhi na mashaka.

Aidha, wasiwasi wenyewe ni maradhi. Tiba yake ni kutambua hekma inayopatikana ndani ya maradhi na malengo yake. Kwa kuwa sasa umeyajua hayo, yatumie kuondosha wasiwasi na kupata faraja! Sema “Namhimidi Mwenyezi Mungu kwa kila hali” badala ya kulalama na kulalamika.

DAWA YA KUMI NA MOJA

Ewe ndugu usiyekuwa na subira! Japokuwa maradhi hukusababishia sumbuko la haraka, maradhi yako kuanzia zamani mpaka sasa yanazalisha raha na furaha ya kimaanawi inayotokana na thawabu unazozipata kwa kustahmili na kusubiri. Kuanzia leo, au hata kuanzia sasa, maradhi hayapo, na hakika hakuna maumivu katika kitu ambacho hakipo. Na ikiwa hakuna maumivu, hakuna wasiwasi. Unakosa subira kwa sababu unawaza vitu kimakosa. Maradhi ya kimwili uliyokuwa nayo kabla ya leo, na maumivu yake, vimeondoka; kilichobaki ni thawabu zake na raha inayopatikana baada ya kuondoka. Hili linapaswa kukupatia faida na furaha, hivyo fikiria kuhusu siku zilizopita na uone kwamba kuhuzunika na kukosa subira ni wendawazimu.

Siku za baadaye hazijafika; kuishi nazo sasa, na kujipa huzuni na kukosa subira kwa kuiwazia siku ambayo haipo na maradhi ambayo hayapo na wasiwasi ambao haupo, ni kupandikiza jambo katika jambo ambalo halipo kama huo si wendawazimu, ni nini basi?

Iwapo saa iliyopita ilikuwa ya maradhi, inazalisha furaha; na kwa kuwa muda wa baada ya sasa haupo, ambapo maradhi na wasiwasi havipo, usiitawanye nguvu ya subira uliyopewa na Mwenyezi Mungu kulia na kushoto, bali itumie kukabiliana na maumivu ya sasa; sema: “Ewe Mwingi wa Subira!” na usimame imara.

DAWA YA KUMI NA MBILI

Ewe mgonjwa uliyenyimwa ya ibada na nyiradi zake kwa sababu ya maradhi! Tambua kwamba imeelezwa katika Hadith kuwa: “Muumini mwenye kumcha Mwenyezi Mungu ambaye ameshindwa kutekeleza ibada na nyiradi zake kwa sababu ya maradhi, hupata thawabu ya ibada alizokuwa akizitekeleza (hata akiwa katika maradhi yake)”.

{Bukhari, Jihad 134; Musnad iv, 410, 418}

Iwapo mgonjwa atatekeleza ibada zake za faradhi, kwa kadiri iwezekanavyo, kwa subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu, maradhi yake yatachukua nafasi ya ibada za sunna katika kipindi cha ukali wa maradhi yake na kwa namna ya ikhlasi.

Aidha, maradhi humfanya mtu aelewe udhaifu na unyonge wake; humfanya aombe dua kwa kauli na kwa ulimi kutokana na udhaifu wake. Mwenyezi Mungu alimpa mwanadamu udhaifu na unyonge usiokuwa na mipaka ili aendelee kujisalimisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuendelea kumuomba.

قُلْ مَا يَعْبَؤُا بِكُمْ رَبِّى لَوْلاَ دُعَاؤُكُمْ{Qur’an, 25:77}

umuhimu gani kama hamswali na kuomba dua?” Kwa mujibu wa Ayah hii, swala na dua ndio sababu ya kuumbwa kwa mwanadamu na thamani yake. Kwa kuwa maradhi ni miongoni mwa haya, kwa muktadha huu, hayapaswi kulalamikiwa bali mja anapaswa kuwa mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu, na bomba la dua linalofunguliwa na maradhi halipaswi kufungwa baada ya kupona.

DAWA YA KUMI NA TATU

Ewe mgonjwa mwenye kulalamikia maradhi! Kwa baadhi ya watu maradhi ni hazina kubwa, ni tunu ya thamani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mgonjwa anaweza kuufikiria ugonjwa wake kwa njia hii.

Saa ya kifo haijulikani; hilo limefanywa ili kumuondosha mwanadamu katika hali ya kukata tamaa na mghafala, na kumuweka baina ya matarajio na hofu na hivyo kuilinda dunia yake na akhera yake, kwa hekma Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ameificha saa ya kifo, kinaweza kuja wakati wowote. Kikimkuta mwanadamu katika hali ya mghafala, itakuwa hasara kubwa kwenye maisha yake ya milele. Hata hivyo, maradhi humuondoa mja katika mghafala; humfanya afikirie kuhusu akhera; humkumbusha kuhusu kifo, ili apate kujiandaa. Baadhi ya maradhi ni yenye faida mno kiasi kwamba faida ambayo mtu anaweza kuipata ndani ya siku ishirini asingeweza kuipata ndani ya miaka ishirini.

Kwa mfano, miongoni mwa rafiki zangu kulikuwa na vijana wawili Mwenyezi Mungu awarehemu. Mmoja aliitwa Sabri kutoka kijiji cha Ilema, na mwingine Vezirzade Mustafa kutoka Islamkoy. Nilikuwa nikishangazwa kwamba japokuwa hawakuwa wakijua kuandika walikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mstari wa mbele kabisa katika usafi wa moyo na kuitumikia imani. Sikujua sababu ya hili. Baada ya vifo vyao nilibaini kuwa walikuwa wakisumbuliwa na maradhi makubwa. Kutokana na maradhi hayo, waliweza kupata kiwango kikubwa cha hofu ya Mwenyezi Mungu, wakatoa kiwango kikubwa sana cha huduma, na wakapata faida na manufaa makubwa ya akhera yao, tofauti na vijana wengine ambao waliacha kutekeleza ibada zao za lazima. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, mateso ya maradhi yao yaliyodumu kwa miaka miwili yaliwafanya wapate furaha ya mamilioni ya miaka katika maisha yao ya milele. Sasa nimeelewa kuwa dua ambazo wakati fulani nilikuwa nikiwaombea ili wapone zilikuwa kama laana kwa maisha yao ya duniani.

Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, ni matumaini yetu kuwa wamelipwa mema huko Akhera.

Hivyo, ninaamini kwamba, wawili hao walipata faida ya hofu ya Mwenyezi Mungu ambayo yumkini ingepatikana kwa kipindi cha miaka kumi. Kama wangeutegemea ujana na uzima wa afya yao kama wafanyavyo baadhi ya vijana  na kujitupa kwenye mghafala na uovu, kifo kikawanyemelea na kuwakuta wakiwa katikati ya uchafu wa dhambi zao, wangekuwa wameyafanya makaburi yao kuwa mashimo ya nge na nyoka, badala ya kuwa hazina ya nuru.

Kwa kuwa maradhi yana faida mbalimbali kama hizo, hayapaswi kulalamikiwa bali kustahmiliwa kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kumshukuru na kuwa na imani katika rehma Yake.

DAWA YA KUMI NA NNE

Ewe mgonjwa uliyepoteza uwezo wa kuona! Kama ungeijua nuru na jicho la kimaanawi linalopatikana kama ukipoteza uwezo wa kuona yanayolifunika jicho la muumini, ungesema: “Shukrani mara laki moja kwa Mola wangu Mwingi wa rehma!” Nitasimulia tukio fulani kuifafanua dawa hii. Tukio hilo ni hili lifuatalo:

Wakati mmoja shangazi wa Suleyman kutoka Barla, ambaye alinihudumia kwa miaka minane kwa uaminifu na utayari, alipatwa na upofu. Kutokana na dhana yake nzuri kwangu, ambayo ilikuwa kubwa mara mia moja kuliko nilivyostahiki, mwanamke huyo alinijia na kuniomba nimuombee dua ili macho yake yapate uoni. Hivyo, niliutumia unyoofu wa mwanamke huyo aliyebarikiwa kuwa nyenzo ya dua yangu, na katika kumsihi Mwenyezi Mungu Mtukufu, niliomba: “Mola wangu! Mrejeshee uoni wake kwa heshima ya unyoofu wake.” Siku mbili baadaye, mtaalamu wa macho kutoka Burdur aliwasili na kumfanyia tiba ya mtoto wa jicho. Siku arobaini baadaye, mama huyo alipoteza tena uoni wake. Nilisikitika sana na kuendelea kumuombea. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, dua yake ilipokubaliwa kwa ajili ya maisha yake ya akhera, vinginevyo dua yangu hiyo ingekuwa laana ya kimakosa kwake. Kwa maana zilikuwa zimebaki siku arobaini za uhai wake; siku arobaini baadaye akafariki dunia Mwenyezi Mungu amrehemu.

Hivyo, badala ya kuyatazama kwa huzuni mabustani ya Barla kwa macho ya uzee wake, alipata faida ya kuyatazama mabustani ya peponi kwa siku elfu arobaini. Kwa maana imani yake ilikuwa imara na alikuwa mnyoofu kikamilifu.

Naam, muumini akipoteza uoni wake na kuingia kaburini akiwa na upofu, kulingana na kiwango cha imani yake anaweza kuuona ulimwengu wa nuru kwa kiwango kikubwa kabisa kuliko wafu wengine. Kama ambavyo hapa duniani tunaona vitu ambavyo waumini wenye upofu wa macho hawawezi kuviona, iwapo kipofu akifariki akiwa muumini wa kweli, anaweza kuona kwa kiwango kikubwa kabisa zaidi ya wafu wengine. Waumini hao wenye upofu wa macho wanaweza kuyatazama mabustani ya peponi na kuyaona kama sinema kana kwamba wanatazama kupitia darubini yenye nguvu kubwa, kulingana na kiwango cha imani yao.

Hivyo, kupitia shukran na ustahmilivu, nyuma ya pazia la jicho lako la sasa unaweza kukuta jicho lililojazwa nuru, na ambalo ukiwa duniani unaweza kuitazama na kuiona Pepo (kupitia jicho hilo la kiroho). Atakayeondosha pazia hilo machoni mwako, daktari wa macho atakayekufanya utazame kwa macho hayo, ni Qur’an Tukufu.

DAWA YA KUMI NA TANO

Ewe mgonjwa unayeugulia na kulalama! Usitazame hali ya nje ya maradhi yako na kulalama, bali fikiria faida na maana ya maradhi hayo uridhike. Kama ndani ya maradhi isingekuwepo faida yoyote, Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma asingewapa maradhi waja Wake anaowapenda mno. Kwa maana, kuna Hadith isemayo kuwa,

اَشَدُّ النَّاسِ بَلاَءً َاْلاَنْبِيَاءُ ثُمَّ اْلاَوْلِيَاءُ َاْلاَمْثَلُ فَاْلاَمْثَلُ{Al-Munawi, Fayd al-Qadir, i, 519, na: 1056; al-Hakim, al-Mustadrak, iii, 343; Bukhari, Marda, 3; Tirmidhi, Zuhd, 57; Ibn Majah, Fitan, 23; Darimi, Riqaq, 67; Musnad, i, 174, 180, 185; vi, 369.}

kishahidi; humpa kiwango na daraja iliyo sawa na uwalii. Kwa mfano, watu wanaokufa kishahidi kutokana na maradhi yanayoambatana na uzazi

{Kipindi ambacho daraja ya shahada inapatikana kupitia maradhi ni takriban siku arobaini za ‘nifasi’.}

na maumivu, kwa kuzama katika maji, kuungua moto na ugonjwa wa tauni. Kuna maradhi mengine pia ambayo humpatia mtu anayekufa daraja ya uwalii. Aidha, kwa kuwa maradhi humpunguzia mtu upendo wa kupenda na kushikamana na dunia, humuangazia njia ya kuiacha dunia kupitia kifo, ambacho kwa maisha ya kidunia ni chenye kuhuzunisha na kuumiza, na wakati mwingine hukifanya kuwa chenye kutamaniwa.

DAWA YA KUMI NA SITA

Ewe mgonjwa unayelalamikia mateso! Maradhi huchochea heshima na huruma, ambayo ni mambo muhimu na mazuri kabisa katika maisha ya kijamii. Kwa maana humuokoa mwanadamu dhidi ya kupanda kiburi kunakomfanya kutoshirikiana na wengine na kutokuwa mwema. Kwa siri iliyopo

اِنَّ اْلاِنْسَانَ لَيَطْغَى اَنْ رَآهُ اسْتَغْنَى{Qur’an 96: 6,7}

na kuhisi kuwa ni yenye kujitosheleza kutokana na afya njema na ustawi, humfanya mtu kutokuwa na heshima kwa ndugu zake ambao wanastahiki kuheshimika. Na hahisi kuwahurumia wagonjwa na wale waliokumbwa na majanga, ingawa wanastahiki kutendewa wema na kuhurumiwa. Anapoumwa, hutambua unyonge na uhitaji wake mwenyewe na huwaheshimu ndugu zake ambao wanastahiki heshima. Huwathamini ndugu zake waumini ambao humzuru au kumsaidia. Huingiwa na hisia ya wema wa kibinadamu, ambayo hutokana na hisia za wenzake, na huruma kwa wale wanaokumbwa na majanga, jambo ambalo ni tabia muhimu sana ya Kiislamu. Na anapojilinganisha nao, huingiwa na huruma ya dhati. Hufanya analoweza ili kuwasaidia, huwaombea dua na kuwazuru kwa lengo la kuwajulia hali, jambo ambalo ni Sunna kwa mujibu wa Shari’a na hivyo hupata thawabu.

DAWA YA KUMI NA SABA

Ewe mgonjwa unayelalama kwa kushindwa kufanya amali njema kutokana na maradhi! Toa shukrani! Maradhi ndiyo yanayokufungulia mlango wa amali njema zilizojaa ikhlasi ya hali ya juu kabisa. Sambamba na mgonjwa na wale wanaomhudumia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kuendelea kupata thawabu, maradhi ni njia muhimu sana ya kukubaliwa dua mbalimbali.

Hakika, kuna thawabu kubwa kwa waumini wanaowahudumia wagonjwa. Kuulizia hali zao na kuwazuru kwa sharti ziara husika isiwe yenye kuwasumbua ni Sunna

{ Al-Munawi, Fayd al-Qadir ii, 45, Na: 1285.} na pia ni kafara ya dhambi. Kuna Hadith isemayo: “Pokeeni dua za wagonjwa, kwa maana ni zenye kujibiwa.” { Ibn Majah, Janaiz 1; Daylami, Musnad al-Firdaws, i, 280.}

Kuwahudumia wagonjwa, kama ni ndugu, au hasa wazazi, ni ibada muhimu yenye thawabu nyingi. Kuufurahisha moyo wa mgonjwa na kumfariji, ni aina ya sadaka. Mwenye bahati ni yule anayezifariji nyoyo laini za wazazi wakati wa maradhi na kupokea dua zao. Hata malaika hushangilia na kusema: “Maashallah” “Baarakallah!” mbele ya mandhari maridhawa ya watoto wanaoitikia kwa heshima kubwa na upendo wakati wa maradhi ya wazazi wao na kuonyesha kiwango cha juu kabisa cha utu kwa maana wao ndio wanaostahiki zaidi heshima katika maisha ya kijamii.

Naam, kuna furaha inayopatikana wakati wa maradhi kutokana na wema, huruma na upendo wa wale wanaomzunguka mhusika; ni furaha kubwa, inayofariji na kupunguza maumivu ya maradhi. Kukubaliwa kwa dua za mgonjwa ni jambo muhimu. Kwa muda wa miaka thelathini au arobaini iliyopita, mimi mwenyewe nimekuwa nikiomba dua nipone maradhi ya maumivu ya mgongo ninayoumwa. Lakini, nilielewa kuwa maradhi hayo yameletwa kwa ajili ya dua. Kwa kuwa dua haiwezi kuondolewa na dua; yaani, kwa kuwa dua haiwezi kujiondoa yenyewe, nilielewa kuwa matokeo ya dua hiyo yamefungamana na Akhera,

{14 Naam, wakati baadhi ya maradhi ni sababu ya uwepo wa dua, iwapo dua hiyo ni chanzo cha kutokuwepo kwa maradhi, uwepo wa dua utakuwa chanzo cha yenyewe kutokuwepo, na hiyo itakuwa kadhia tofauti.}

na hiyo ni aina ya ibada, kwa maana kupitia maradhi mtu anaweza kutambua udhaifu wake na kutafuta hifadhi kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo, japokuwa kwa miaka thelathini nimekuwa nikiomba dua ili nipate kupona na dua zangu hazikujibiwa, sijawahi kuwa na wazo la kukata tamaa. Kwa maana kipindi cha maradhi ni kipindi cha kujinyenyekeza kwa kuomba dua. Kupona sio matokeo ya dua. Ikiwa Mwenyezi Mungu Mwenye hekma na Mwenye rehma akitoa ponyo, hufanya hivyo kutokana na rehma Yake isiyokuwa na kikomo.

Aidha, iwapo dua hazijapokelewa kwa namna tunavyotaka, haipaswi kusemwa kuwa hazikupokelewa. Muumba wetu Mwenye hekma anajua zaidi kuliko sisi; anatupatia kile chenye maslahi na manufaa kwetu. Wakati mwingine huyaweka akiba maombi yetu ya duniani ili yatufae Akhera, na kuyapokea kwa namna hiyo. Kwa vyovyote vile, dua yenye ikhlasi kutokana na maradhi, udhaifu, unyonge, unyenyekevu na uhitaji, huwa karibu sana na kukubaliwa. Maradhi huifanya dua kujawa na ikhlasi. Hivyo, mgonjwa mshika dini na waumini wanaomhudumia wanapaswa kufaidika na fursa ya dua hii.

DAWA YA KUMI NA NANE

Ewe mgonjwa unayeacha kushukuru na kuchukuliwa na malalamiko!

Malalamiko hutokana na uwepo wa haki, lakini hakuna haki yako yoyote iliyopotea kiasi cha kukufanya ulalamike. Hakika, kuna shukrani nyingi ambazo ulipaswa kuzitekeleza, hujazitekeleza. Pasipo kumpatia Allah haki zake, unalalamika kwa njia ambayo si sahihi. Hutakiwi kuwaangalia waliokuzidi siha, na kulalamika. Bali unatakiwa kuwatazama wagonjwa ambao kwa mtazamo wa kiafya umewazidi na utoe shukrani. Iwapo mkono wako umevunjika, itazame mikono yao iliyokatwa. Ukiwa una jicho moja, mtazame kipofu ambaye hana macho yote mawili, na umshukuru Mwenyezi Mungu!

Kwa  hakika,  hakuna  mwenye  haki  ya kuwatazama waliomzidi kwa neema na kuanza kulalamika. Ama kuhusu masaibu, ni haki ya kila mtu kuwatazama wale waliowazidi, ili wapate kushukuru. Siri hii imefafanuliwa katika maeneo mbalimbali katika Risale-i Nur kwa mfano, ambao mukhtasari wake ni huu ufuatao:

Mtu mmoja anamchukua masikini kuelekea kwenye kilele cha mnara. Wanapofika kwenye kila ngazi, anampatia zawadi, tunu tofauti. Wanapofika kileleni anampatia zawadi kubwa kabisa. Japokuwa anataka kushukuriwa na kutambuliwa kwa kila zawadi aliyoitoa, masikini huyo anazisahau zawadi alizopewa kwenye kila ngazi, au anaona kuwa hazina umuhimu wowote, akaacha kushukuru, akatazama juu na kuanza kulalamika akisema, “Lau kama mnara ungekuwa mrefu zaidi, ningeweza kwenda mbali zaidi. Kwa nini si mrefu kama mlima au mnara ule?” Utovu wa shukurani ulioje kwa kuanza kulalama kwa namna hiyo!

Kwa namna hiyo hiyo, mwanadamu huja duniani kutoka katika hali ya kutokuwa chochote, sio kama jiwe, mti au mnyama, bali kama mwanadamu na kama Muislamu, na mara nyingi akiwa mwenye afya na kupata neema za hali ya juu. Licha ya hayo yote, kulalama na kutokuwa na subira kwa sababu hajapewa baadhi ya neema, au kwa sababu amezipoteza kupitia machaguo mabaya au matumizi mabaya, au kwa sababu hakuzifikia, na kumkosa Mwenyezi Mungu kwa kusema “Nimefanya nini mpaka haya yanifike?”, ni hali ya maradhi ya kiakili na kimaanawi ambayo ni hatari zaidi kuliko maradhi ya kimwili. Malalamiko hayo huyafanya maradhi yake kuwa mabaya zaidi mfano wa mtu anayepigana hali ya kuwa mkono wake umevunjika. Mtu mwenye utambuzi ni yule anayekumbuka maana

لِكُلِّ مُصِيبَةٍ اِنَّا لِلّٰهِ وَاِنَّا اِلَيْهِ رَاجِعُونَ{ Qur’an, 2:156}

husalimu amri na kuwa mwenye subira, ili maradhi hayo yakamilishe jukumu lake na kisha yaondoke.

DAWA YA KUMI NA TISA

Majina yote ya Mwenyezi Mungu Mkusudiwa kupewa sifa ya “Majina Mazuri”, inaonesha kuwa majina yote ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mazuri. Miongoni mwa viumbe, uhai ndio kioo kizuri, maridhawa na kikuu cha sifa ya Mwenyezi Mungu Samadaniya. {Mwenyezi Mungu Mwenye kukusudiwa peke yake katika haja zote, na yote yanayo takikana.} Kioo cha uzuri huwa kizuri pia. Kioo kinachoakisi sifa nzuri huwa kizuri. Kama ambavyo kila kinachoakisiwa na uzuri huo kwenye kioo hicho ni chema na kizuri, basi kila kinachoakisiwa katika uhai pia, kwa uhalisia, ni kizuri. Kwa maana huonesha mvuto wa majina mazuri kabisa, ambayo ni mema na mazuri.

Maisha huwa kama kioo chenye nakisi kama yakipita kwenye afya na siha ya kudumu bila hali ya mabadiliko. Kwa upande mmoja, inaweza kumfanya ahisi hali ya kutokuwa chochote, upuuzaji na kusababisha uchakavu. Inaweza kupunguza thamani ya uhai na kuzigeuza furaha kuwa dhiki. Kwa kudhani kuwa muda wake utapita haraka, kutokana na uchoshi, mtu anaweza kujitupa kwenye uchafu au anasa. Huyachukia maisha yake yenye thamani na kutaka kuyaangamiza na kuyafanya yapite kwa haraka kana kwamba ni adhabu ya jela. Lakini iwapo uhai wake unapitia katika mabadiliko na hali mbalimbali, thamani, umuhimu na raha yake huonekana. Mtu huyo hapendi umri wake upite haraka, hata kama ni katika tabu na masaibu. Halalamiki kwa kusema, “kwa nini jua halijazama,” au “kwa nini jua halijachomoza.”

Naam, muulize mtu mwenye utajiri na anayeishi katika dimbwi la starehe, “Vipi hali yako?” Lazima utasikia jibu la kusikitisha kama vile: “Muda hauendi mbio. Njoo tucheze kete. Au tutafute kiburudisho ili tupoteze muda.” Au utasikia malalamiko yanayotokana na matamanio ya kihayawani, kama vile: “Sijapata hiki na kile; natamani ningekuwa nimefanya hiki na kile.”

Kisha muulize mtu aliyekumbwa na masaibu, kibarua au masikini anayeishi katika ufukara: “Vipi hali yako?” Kama ni mwenye kujitambua, atajibu: “Namshukuru Mwenyezi Mungu, ninafanya kazi. Kama jioni isingeingia haraka, ningekuwa nimemaliza hii kazi! Muda unakwenda haraka sana, na umri nao hivyo hivyo; huponyoka haraka. Kwa hakika mambo ni magumu kwangu, lakini hilo nalo litapita. Kila kitu hupita kwa haraka.” Kiuhalisia anaonesha namna umri ulivyo na thamani na anavyosikitika kwa umri huo kwenda mbio. Hii ina maana kwamba anaitambua furaha na thamani ya umri kupitia tabu na ugumu wa kazi. Ama kuhusu raha na siha, huyafanya maisha kuwa machungu na kumfanya mtu awe na matarajio ya kwamba yanapita haraka.

Ewe ndugu yangu mgonjwa! Tambua kwamba hali ya kutokuwepo ndio asili ya masaibu na shari, na hata dhambi, kama ilivyothibitishwa na kuelezwa kwa undani katika maeneo mengine ya Risale-i Nur. Kwa maana, hali ya kutokuwepo ni mbaya, ni giza.

Hali zisizobadilika kama vile furaha, ukimya, utuvu na utulivu zinakaribia sana kuwa hali ya kutokuwepo na kutokuwa chochote, na hivyo kusababisha hisia ya giza la hali ya kutokuwepo na kusababisha dhiki. Ama kuhusu matendo na mabadiliko, vipo na uwepo wake unahisika. Na uwepo ni kheri na nuru halisi.

Kwa kuwa ukweli uko hivi, maradhi uliyo nayo ni mgeni aliyetumwa kwako kuja kutekeleza majukumu yake mengi kama vile kuyatakasa maisha yako yenye thamani, kuyapa nguvu, kuyaendeleza, na kuamsha vipawa vingine vya kibinadamu ulivyo navyo vipate kukisaidia kiungo chako kinachoumwa, na kuonesha uzuri mbalimbali wa majina ya Muumba Mwenye hekma. In sha Allah, maradhi hayo yatatekeleza majukumu yake kwa haraka na kuondoka, na yataiambia siha yako njema: “Njoo ukae mahala pangu daima, na utekeleze majukumu yako. Haya ni maskani yako. Kaa hapa kwa furaha na raha.”

DAWA YA ISHIRINI

Ewe mgonjwa unayetafuta tiba! Maradhi ni ya aina mbili: aina ya kwanza ni halisi, na nyingine ni ya kufikirika. Ama kuhusu aina halisi, Mwenyezi Mungu Mwenye Hekma na Mponyaji Mwenye ukuu amejaalia kila ugonjwa kuwa na dawa, na kuiweka katika famasia Yake kuu ambayo ni ardhi. Kwa tiba hizo, zinahitaji maradhi. Allah ametengeneza tiba kwa kila maradhi. Ni halali kuzitafuta na kuzitumia kama tiba, lakini yakupasa kutambua kuwa ufanyaji kazi na uponyaji wake hutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Yeye ndiye anayetoa maradhi na kujaalia ponyo.

Kufuata maelekezo ya madaktari mahiri na wachaMungu ni ponyo muhimu. Kwa sababu maradhi mengi hutokana na matumizi mabaya, kutojizuia, kupuuza maelekezo, israfu, dhambi, kutojali na kutochukua tahadhari. Daktari mshika dini atatoa ushauri na maelekezo yaliyo ndani ya mipaka ya uhalali. Atakataza matumizi mabaya na israfu, na kuingiza faraja na matumaini ndani ya moyo wa mgonjwa. Mgonjwa atakuwa na imani na ushauri na faraja yake, na maradhi yake yatapungua; hutengeneza furaha badala ya dhiki na malalamiko.

Ama inapokuwa ni maradhi ya kufikirika, dawa nzuri kabisa ni kutoyapa umuhimu. Kadiri maradhi yanapopewa uzito, ndivyo yanavyozidi kupanda na kukua. Yakipuuzwa, hupungua na kutoweka. Kama ambavyo manyigu yanapochokozwa ndivyo yanavyozidi kutengeneza kivuli juu ya kichwa cha mtu, iwapo yakipuuzwa hutawanyika. Kadhalika, kadiri mtu anavyoipa umuhimu kamba iliyolala mbele yake gizani na kumsababishia kihoro, ndivyo inavyomzidi kumfanya akimbie kama mwendawazimu. Ilhali kama hatoipa umuhimu, ataona kuwa ni kipande cha kamba na sio nyoka, na atamcheka yule atakayekhofu na kuwa na wasiwasi.

Kama unyong’onyevu na ulegevu wa moyo (wa kuona mashaka juu ya afya) ukiwa sugu, hubadilika kuwa uhalisia. Ni maradhi mabaya yanayowasibu wenye wasiwasi na wale wanaosalimu amri mbele ya mambo yenye kufikirika; watu hao hutengeneza milima kwa vichuguu na hamasa yao huharibika. Kisha, wanapokutana na daktari asiye mjuzi au asiye mwadilifu, ulegevu wao huzidi kuchochewa. Iwapo ni matajiri, hupoteza utajiri wao, au siha na afya zao.

DAWA YA ISHIRINI NA MOJA

Ewe ndugu yangu mgonjwa! Maradhi yako yanaandamana na maumivu ya kimwili. Lakini, umezungukwa na kiwango kikubwa cha furaha ya kimaanawi kitakachoondosha athari za maumivu hayo. Kwa maana, ikiwa baba yako, mama yako, na ndugu zako wako pamoja nawe, usuhuba wao mtamu uliousahau tangu utotoni utaamshwa na kwa mara nyingine utaweza kuuona muamala maridhawa ulioupata ulipokuwa mtoto. Aidha, urafiki uliokuwa wa siri na wenye kujificha hupata kukuzunguka; yote hayo hukumiminikia wewe kwa upendo kupitia mvuto wa maradhi. Kutokana na hayo, maumivu yako ya kimwili hupungua. Vilevile, maradhi hukufanya uwe bwana kwa sababu wale uliokuwa ukiwahudumia kwa upendo nao sasa wanakuhudumia kutokana na maradhi hayo. Kadhalika, umevutia kwako hisia za usuhuba na wema wa watu, na hivyo umepata marafiki kadhaa na maswahiba wema. Maradhi yako yamekupa amri ya kupumzika dhidi ya majukumu na kazi nyingi.

Hakika, mbele ya furaha hizi za kimaanawi, maumivu yako madogo yanapaswa kukufanya uwe mwenye kushukuru, badala ya kulalama.

DAWA YA ISHIRINI NA MBILI

Ewe ndugu yangu unayesumbuliwa na maradhi mabaya kama kiharusi! Kwanza ninakupa habari njema kuwa kwa waumini kiharusi huhesabiwa kuwa ni baraka. Muda mrefu uliopita nilikuwa nikilisikia hili kutoka kwa watu wema na sikujua sababu. Sasa, sababu yake moja iliyonitokea ni hii ifuatayo:

Ili kupata ukaribu na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuokolewa dhidi ya hatari za kimaanawi za  dunia hii, na kupata furaha ya milele, marafiki wa Mwenyezi Mungu walichagua kufuata kanuni mbili zifuatazo:

Ya Kwanza:

ni tafakuri juu ya kifo. Kwa kufikiri kuwa dunia ni makazi ya mpito, na wao wenyewe ni wageni wa mpito wenye majukumu, wanafanya kazi kwa ajili ya maisha ya milele.

Ya Pili:

kwa kufunga, mazoezi na amali za kidini, hujaribu kuiua nafsi yenye kuamrisha maovu na hivyo kuokolewa dhidi ya hatari zake na dhidi ya upofu wa kimaanawi.

Na wewe, ewe ndugu yangu ambaye umepoteza siha ya nusu ya mwili wako! Bila kuwa na hiari, umepewa kanuni hizi mbili, ambazo ni fupi, rahisi na ni chanzo cha furaha. Hivyo, hali ya afya yako inaendelea kukuonya juu ya uhalisia wa dunia yenye kuhadaa na kwamba mwanadamu ni mwenye kupita tu. Dunia haiwezi tena kukuzamisha, wala mghafala hauwezi kukufumba macho. Na kwa hakika, nafsi yenye kuamrisha maovu haiwezi kumlaghai kwa kutumia matamanio ya kihayawani mtu ambaye yuko katika hali ya nusu-mtu; hivyo anakuwa ameokolewa haraka sana dhidi ya majaribu ya nafsi.

Kwa hivyo, kupitia siri ya imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu, kujisalimisha Kwake na kumtegemea Yeye, kwa muda mfupi muumini anaweza kunufaika kutokana na maradhi mabaya kama kiharusi, ambayo yanashabihi majaribu makubwa wanayoyapata mawalii wa Mwenyezi Mungu. Hivyo, maradhi makubwa kama hayo hupata kuwa na wepesi sana.

DAWA YA ISHIRINI NA TATU

Ewe mgonjwa usiye na furaha na mpweke! Hata kama upweke wako na kutengwa pamoja na ugonjwa wako huibua huruma ndani ya nyoyo ngumu na kuvutia wema na huruma kwako. Hakika pia vitavutia kwako huruma ya Muumba Mwenye Huruma yote, ambayo kwa hakika ni mbadala wa wema na huruma ya kila kitu kingine. Kwa maana, Yeye amejidhihirisha kwetu mwanzoni mwa kila surah ya Qur’an Tukufu kwa sifa za “Mwingi wa rehma na Mwenye kurehemu,” na kwa nuru moja ya huruma Yake amewafanya wazazi wote kuwalea watoto wao kwa huruma ya ajabu, na kwa ishara moja ya rehma Zake kila msimu wa machipuo huujaza wajihi wa ardhi kwa neema mbalimbali. Maisha ya milele Peponi pamoja na maajabu yake ni ishara moja tu ya rehma Zake. Hivyo basi, hakika uhusiano wake Naye kupitia imani, kumtambua kwako na kumuomba kupitia ulimi wa unyonge wako, kupona kwako dhidi ya maradhi na masaibu ya upweke na ukiwa, vitamfanya akutazame kwa jicho la rehma Zake, ambazo zinapatikana katika kila kitu. Kwa kuwa Yupo na Anakuona, kila kitu kitakuwepo kwa ajili yako. Wale ambao wana upweke na ukiwa wa kweli ni wale ambao hawajaungana Naye kwa imani na kujisalimisha Kwake, au wanapuuza uhusiano huo.

DAWA YA ISHIRINI NA NNE

Ewe unayewahudumia watoto wagonjwa au wazee, ambao ni kama watoto wasiokuwa na hatia! Mbele yako kuna biashara muhimu ya akhera. Hivyo, ifanye kwa hamasa na juhudi yako! Inafahamika na watu wa ukweli kwamba maradhi ya watoto wadogo wasio na hatia ni kama mafunzo kwa ajili ya miili yao, chanjo na matayarisho ya kimaanawi yanayowaandaa kukabiliana na ghasia za dunia; kwamba pamoja na mifano mingi ya hekma kuhusu maisha ya mtoto duniani, kafara ya dhambi kwa maisha ya mtu mzima yanaonekana kama ni nyenzo ya utakaso wa maisha, maradhi ni kama chanjo zinazotoa uhakika wa maendeleo ya baadaye ya maisha ya kiroho kwa mtoto; na kwamba fadhila zinazopatikana kutokana na maradhi hayo hupelekwa kwenye kitabu cha matendo mema ya wazazi, na hususan mama ambaye kwa sababu ya huruma yake hujali afya ya mwanaye kuliko afya yake.

Ama kuhusu kuwahudumia wazee, Inafahamika katika Hadith sahihi na matukio mengi ya kihistoria kwamba pamoja na kupata thawabu nyingi, kupokea dua za wazee na hususan wazazi, kuzifurahisha nyoyo zao na kuwahudumia kwa moyo wote, humpa mhusika furaha ya duniani na akhera. Na imethibitishwa na matukio mengi kwamba mtoto mwenye bahati anayewatii wazazi wake atapata muamala huo huo kutoka kwa watoto wake, lakini kama mtoto muovu akiwaumiza wazazi wake ataadhibiwa kwa majanga mbalimbali hapa duniani na huko akhera. Naam, Uislamu unamtaka mtu awahudumie sio tu ndugu zake wazee au watoto, bali pia wazee wengine waumini kupitia kamba ya udugu wa imani, na awahudumie kwa uwezo wake wote wazee wanaoumwa iwapo watahitajia huduma yake.

DAWA YA ISHIRINI NA TANO

Ndugu zangu wagonjwa! Iwapo mnahitajia ponyo tukufu yenye manufaa na dawa ya kila ugonjwa yenye ladha ya kweli, imarisheni na mstawishe imani yenu! Yaani, tumieni imani, ambayo ni ponyo tukufu, na dawa itokanayo na imani hiyo kwa kufanya toba, kuomba maghfira, kuswali swala tano na kufanya ibada mbalimbali.

Naam, wale walioghafilika,  kwa  sababu ya kuipenda na kushikamana sana na dunia, wamejikuta kana kwamba wamebeba maradhi ya kimaanawi yenye uzito sawa na ukubwa wa dunia. Tumethibitisha katika maeneo mbalimbali ya Risale-i Nur kwamba imani huondoa mara moja maradhi hayo na kuyasambaratisha kwa pigo la kifo na mtengano. Lakini, ninaishia hapa ili nisikuchoshe kwa mazungumzo yangu.

Ama kuhusu tiba ya imani, hufanya kazi unapotekeleza wajibu wako wa kidini kadiri iwezekanavyo. Mghafala, uovu, matamanio ya nafsi, starehe za haramu hupunguza utendaji kazi wake.

Maradhi huondosha mghafala, hukata matamanio, na ni kizuizi cha starehe za haramu, hivyo jitahidi kufaidika nayo. Nufaika na ponyo tukufu na nuru ya imani kwa kufanya toba na kuomba maghfira, kuswali na kuomba dua.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu ayafanye maradhi yako kuwa kafara ya dhambi zako. Amiin. Amiin. Amiin.

اَلْحَمْدُ لِلّٰهِ الَّذِى هَدَينَا لِهذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِىَ لَوْلاَ اَنْ هَدَينَا اللّٰهُ لَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ{Qur’an 7:43}

سُبْحَانَكَ لاَ عِلْمَ لَنَا اِلاَّ مَا عَلَّمْتَنَا اِنَّكَ اَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ{Qur’an 2:32}

اَللّٰهُمَّ صَلِّ عَلَى سَيِّدِنَا مُحَمَّدٍ طِبِّ الْقُلُوبِ وَ دَوَائِهَا وَ عَافِيَةِ اْلاَبْدَانِ وَ شِفَائِهَا وَ نُورِ اْلاَبْصَارِ وَ ضِيَائِهَا وَ عَلَى آلِهِ وَ صَحْبِهِ وَ سَلِّمْ

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.