UJUMBE KWA MAGONJWA

DIBAJI

Maradhi, mateso na majanga ni mambo halisi katika maisha ambayo yanamsibu kila mtu. Kwa kiasi kikubwa huonekana kama ubaya usioepukika katika maisha yetu, licha ya maendeleo katika tiba, sayansi na teknolojia katika zama za sasa. Kama ambavyo maendeleo haya makubwa hayajafuta maradhi na majanga, huku ikiwa hakuna nafuu ya kupungua, vivyo hivyo hayajatoa tiba yoyote kwa maradhi na masumbuko yasiyokuwa ya kimwili ambayo hutokana nayo, na kuyazidisha. Hali iko hivyo hivyo kwa nyanja zote za ustaarabu wa kisasa. Ingawa maendeleo yake ya kimaada yameboresha sana maisha ya kimaada ya baadhi ya vipengele vya mwanadamu, hayajaleta furaha na ukamilifu kwa vipengele vyote.

Nukta hii imechambuliwa kwa undani na Bediuzzaman Said Nursi katika Risale-i Nur katika ulinganishaji baina ya njia ambazo Qur’an imempatia mwanadamu, kwa upande mmoja, na falsafa kwa upande mwingine; kati ya imani na ukafiri, kati ya wongofu na upotofu. Amethibitisha na kuonesha kuwa furaha na maendeleo ya kweli ya mwanadamu yanapatikana ndani ya njia ya mwanzo pekee, yaani kutambua na kukiri uwepo na umoja wa Muumba wa ulimwengu, kuwatambua mitume na vitabu vitukufu alivyoviteremsha, na hususan ufunuo wa mwisho, yaani Qur’an, na dini kamili iliyoletwa kwa ajili ya wanadamu, yaani Uislamu, na Mtume Muhammad (s.a.w) aliyeviwasilisha. Kwa maana, ni kutokana na hayo tu ndipo mwanadamu anapoweza kulijua lengo na maana ya uwepo wake mwenyewe na uwepo wa ulimwengu, na lengo la uhai na kifo, maradhi, mateso na masaibu.

‘Dawa’ ishirini na tano zinazowasilishwa na Bediuzzaman katika kitabu hiki ni chemichemi kutoka ndani ya Qur’an na zinawasilisha mtazamo tofauti kabisa kuhusu maradhi na masaibu. Kupitia nuru ya Qur’an na jicho la imani, maradhi yanaonekana kuwa na faida, manufaa na mifano mingi ya hekma ambazo zinayafanya yasiwe kitu cha kuogopwa na kulalamikiwa, bali kitu ambacho kinapaswa kupokelewa kwa shukrani na subira.

Bediuzzaman sio mpinzani wa tiba za kisasa na maendeleo yake, bali ameandika kuwa katika “famasia ya ardhi” kuna tiba kwa kila maradhi, na tiba hizo zinatakiwa kutumiwa. Lakini mja anatakiwa kutambua kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anayejaalia dawa hizo kufanya kazi.

Aidha, kwa kuwa maradhi ya kweli ya mwanadamu hutokana na kutokuwa na imani, na maradhi ya kimwili yenyewe mara nyingi ni matokeo ya “matumizi mabaya” na “israfu”, yaani kwa sababu ya kutofuata mafundisho ya dini, Bediuzzaman anashauri kuwa ili kupata tiba, kimbilio linapaswa kuwa kwa madaktari waumini na washika dini, na kwamba “madaktari wa kimaada na wenye mghafala” wao wenyewe wanatakiwa “kupata tiba ya imani kutoka kwenye famasia tukufu ya Qur’an” kama kweli wanataka kuwatibu wengine.

Kwa umaizi wake usiomithilika juu ya nafsi ya mwanadamu na maarifa yake adhimu juu ya Qur’an, Bediuzzaman anatoa dawa maridhawa na mujarabu kabisa ambayo ni faraja na tiba kwa wale wenye maradhi ya kimwili na wale walioumizwa na kutokuwa na Imani na upotofu.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.