UTAMBULISHO WA KITABU “ISHARA KUU”

ISHARA KUU

Kitabu hiki ni katika jumla ya vitabu vya Risale-i Nur ambavyo Ustadhi Said Nursi ameviandika vikiwa na ujumbe mkubwa wa Imani ya uhakika juu ya kuwepo kwa Allah (s.w) kwa hoja mbalimbali. Kitabu pamoja na kugawika katika sehemu za tanbihi, utangulizi na maelezo ya kuelezea utambulisho wa Risale-i Nur na wasifu wa Ustadhi Said Nursi mwishoni, kina sehemu kuu mbili; mlango wa kwanza na mlango wa pili.

Katika mlango wa kwanza; kunaelezwa kwa namna ya hekaya ya mfano ambapo mtalii anataka kumjua Muumba, na anachunguza kila kitu kinachomzunguka. Mtalii ameangalia pamoja na vingine mbingu, ardhi na vilivyomo, ametafakari ulimwengu wa wanadamu, wanazuoni, mawalii, mitume na kadhalika, vilevile ameangalia ulimwengu wa ghaibu na kubaini kuwa yupo mmiliki wa Ulimwengu.

Kwa mfano: Kwa kuangalia mbingu na vilivyomo, anabaini kuwa kuna kuendesha, kutiisha, kunadhimu, kusafisha na kukabidhi majukumu kwa kila kilichopo. Na kwa kugeukia ardhi mathalani anabaini kwamba kuna kupamba, kupambanua, kupanga, kufungua sura za mimea na wanyama na kadhalika. Hii inamtambulisha kuwa kila kitu kimewekwa kwa Hekima, Elimu, na Utashi na ni muhali kutokuwepo mmiliki wa vitu hivyo.

Mlango wa pili: Mlango huu unathibitisha Tawhidi na kwamba hakika kadhaa zinaonesha huyo mmiliki wa kila kitu ni mmoja tu. Kwa mfano hakika ya nidhamu na mpangilio kamili, inaonyesha wazi kuwa Ulimwengu umo katika mpangilio na kufuata kanuni. Na jambo hili haliwezi kuwa kama hakuna chanzo kimoja cha uendeshaji na upangaji kinachotiiwa na kila kitu. Vinginevyo pangeshuhudiwa fujo na vurugu katika kila kitu na maisha yasingewezekana kabisa. Kungekuwa na Miungu wengine pamoja na huyu basi mambo yangeharibika.

Msomaji wetu mwema tumekupa muhtasari sana ama kionjo tu, nawe unaweza kufaidi mwenyewe utakaposoma kwa undani zaidi kitabu hiki.

Allah ndiye mjuzi.

Jopo la wafasiri wa Risale-i Nur Tanzania.

You May Also Like

Leave a Reply

Your email address will not be published.